Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 23


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
“Basi wazazi wangu ajali waliyopata ilikuwa mbaya sana, majeraha si makubwa sana lakini inaonesha wamejigonga kwenye kitu kigumu wakati gari likipata ajali hivyo kusababisha mtikisiko wa ubongo uliopelekea kupoteza fahamu. Lakini tunahangaika ili kurudisha fahamu zao.”
SASA ENDELEA...
“Zitachukua muda gani kurudi?” mama Cecy aliuliza.
“Hatuwezi kujua ubongo umecheza kiasi gani, lakini msiwe na wasiwasi hii ni hali ya kawaida kwenye ajali za namna hii,” dokta aliwapa moyo.
“Tunaweza kwenda kuwaona?” aliuliza mama Cecy.
“Kwa leo bado kuna baadhi ya mambo tunashughulika nayo kuanzia kesho mna nafasi ya kuja kuwaona.”
“Sawa.”
Mama Colin na mama Cecy walitoka ofisini kwa mganga mkuu na kukutana na Mage na mama yake wakiwasubiri, walipotoka waliwauliza.
“Vipi wanasemaje?” Mage alikuwa wa kwanza kuuliza.
“Bado wapo chini ya uangalizi maalumu,” alijibu mama Colin.
“Hatuwezi kuwaona?” mama Mage aliuliza.
“Kwa leo haiwezekani.”
“Mmh! Basi watakuwa wana hali mbaya sana,” Mage alisema.
“Anayejua ni dokta, sisi hatujui kwa vile hatujawaona,” alijibu mama Colin ambaye alionesha kuchoshwa na maswali ya Mage.
“Jamani hatuna cha kufanya maombi yetu yote yawe kwa watoto wetu ili Mungu awaepushe na matatizo yaliyo mbele yao,” alisema mama Mage.
“Ni kweli dada yangu,” alisema mama Cecy ambaye muda wote alikuwa kimya kutokana na mshtuko alioupaka kwa ajali ya watoto wao.
Walikubaliana kurudi nyumbani mpaka kesho ambayo wangerudi kuwaona, mama Mage aliwashauri wote waongozane nyumbani kwa mama Colin kufanya maombi ya pamoja ili Mungu awaepushe na matatizo yale. Waliongozana wote hadi nyumbani kwa mama Colin ambako walifanya maombi ya pamoja yaliyoongozwa na mama Mage.
Walipiga magoti na kushikana mikono kisha mama Mage alishusha maombi.
“Baba Mungu tumepiga magoti mbele yako tunajua hakuna chochote chini na juu ya jua kiwezacho kufanyika bali kwa idhini yako. Baba Mungu lisilowezekana kwa mwanadamu kwake linawezekana, lililo zito kwa mwadamu wako ni jepesi. Eeh, Baba tunaomba uwaepushe watoto wetu na matatizo mazito kama ulivyoweza kumuepusha mwanao mpendwa pale msalabani.
Kama ulivyoweza kumponya Ayubu na maradhi ya ajabu ambayo alipona kupitia kwa uweza wako. Baba Mungu unaweza kumponya aliye mahututi unaweza kumfufua aliyekufa kwako wewe hakuna kinachoshindikana baba waponye wenetu ambao hatujui hali zao ni wewe pekee mwenye kuugeuza usiku ukawa mchana basi yaondoe maradhi miilini mwao wape afya njema.
Baba vunja pepo wa maumivu vunja pepo wa mauti vunja pepo wa maradhi kwa jina la mwanao Yesu Kristo aliyehai Amen.”
“Ameni,” waliitikia pamoja.
Baada ya maombi walinyanyuka na kukaa kwenye makochi, kwa vile hawakuwa na la kuzungumza mpaka siku ya pili watakapokwenda kuwaona wagonjwa wao. Mama Mage na mwanaye waliaga na kuondoka kurudi nyumbani na kuwaacha mama Colin na Cecy wakiwa wamekaa kila mmoja akiwaza lake.
***
Siku ya pili alfajiri walikutana wote hospitali ya Muhimbili , kwa vile daktari alikuwa hajafika ilibidi wamsubiri mpaka saa moja asubuhi alipofika, alipowaona aliwaeleza wasubiri ili afike wodini kwanza. Dokta Bukos baada ya kuwazungukia wagonjwa wote na kuchukuwa taarifa kutoka kwa daktari wa zamu aliwafuata kwenda kuwaona wagonjwa wao.
Waliingia mmojammoja kutokana na taratibu za kuingia chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Colin alikuwa akipumulia mashine akiwa amelala bila kutikisika. Lakini dokta Bukos aliwaeleza kuwa kidogo ameanza kupata fahamu kwa misuli ya mwili kuanza kufanya kazi taratibu japo hakuonesha mabadiliko yoyote zaidi ya kulala vilevile walivyomkuta.
Katika chumba kingine Cecy naye alikuwa vilevile amejilaza akitumia mashine kupumua, yeye alionekana ufahamu bado kabisa japokuwa mapigo ya moyo dokta alisema yapo mbali sana. Lakini aliwaomba wazidishe kumuomba Mungu na si kulia.
WIKI MOJA BAADAYE
Baada ya wiki moja hali ya Colin ilimalika kidogo kwa kuweza kutambua watu japo bado alikuwa hawezi kuzungumza kwa haraka kwa kutafuta maneno. Cecy hali yake ilikuwa bado mbaya pamoja na mwili kuanza kurudisha hisia bado alikuwa akiendelea kutumia mashine za kumsaidia kupumua.
Walijikuta katika wakati mgumu baada ya hali ya Cecy kuonekana kuchelewa kuimalika. Mganga mkuu aliomba kama wana uwezo basi Cecy apelekwe India kwa ajili ya matubabu zaidi baada ya kuamini uwezo wa madaktari wa Tanzania uliishia pale kuweza kuuamsha mwili lakini hali ilikuwa bado tofauti na Colin ambaye aliweza kula hata kufanyishwa mazoezi japokuwa alikuwa akizungumza kwa shida.
Madaktari waliwahakikisha ndani ya wiki nyingine hali itaimalika zaidi na kuweza kuanza mazoezi ya peke yake. Fedha iliyokuwa ikitakiwa kwa ajili ya matibabu na nauri ya Cecy na msaidizi wake ilikuwa kubwa ambayo mama Cecy hakuwa nayo. Kwa hali ya mgonjwa ilivyokuwa ikionekana mama Colin aliamini kabisa Cecy hawezi kupona hivyo kutoa kiasi hicho cha fedha ni sawa na kuzitupa.
Mama Cecy alikuwa radhi kuuza nyumba ili tu mwanaye akatibiwe, lakini mama Colin alimshauri asisumbuke kwa vile wagonjwa wa aina ile huwa hawaponi heri asiipoteze nyumba kwani Cecy akifa atakuwa na sehemu ya kukaa.
Mama Cecy alikuwa radhi kulala nje lakini ajue hatima ya hali ya mwanaye, ili kujitoa kwenye lawama alichangia milioni tano katika milioni ishrini na tano zilizotakiwa. Mama Cecy alitafuta dalali wa kuiuza nyumba kwa bei ya kutupa ili tu mwanaye akatibiwe India kama kufa basi afe akijua alikuwa akipigania maisha yake.
Wiki ile ndiyo ilikuwa wiki ya malipo ya Cecy kutoka katika kampuni ya jarida la Ebony ambayo iliijngiza kwenye akaunti ya Cecy pia walifunga safari mpaka Tanzania kuonana na Cecy kwa ajili ya kumpiga picha zingine kwa ajili ya matoleo mengine. Jarida lililotoka na picha ya Cecy ilivunja rekodi ya mauzo ya kampuni ile toka ianzishwe.
Uongozi wa kampuni ile ulipanga kumpa mkataba mnono wa muda mrefu zaidi pia kumfunga asitumike kwenye majarida mengine. Walipofika walitaka kuonana na meneja wake ambaye ni mchumba wake Colin mmiliki wa kampuni ya Urembo. Taarifa walizopata ziliwashtuka kusikia Cecy na mchumba wake walipata ajali mbaya sana. Walikwenda mpaka hospitali na kuwaona wagonjwa.
Colin alionekana hajambo lakini Cecy bado hali yake ilikuwa tata, walionana na mganga mkuu na kutaka kujua nini hatma ya mgonjwa kwa siku alizokaa hospitali. Aliwaeleza hatua walizochukua tokea mwanzo kwa wagonjwa wote na kufanikiwa kwa mmoja na sehemu walipokwama na kuhitaji msaada wa matibabu zaidi nje ya nchi.
Waliulizia kama kuna uwezekana wa mgonjwa kupona, walijibu upo wa hamsini kwa hamsini. Waliuliza gharama ya matibabu yote walielezwa milioni ishirini na tano kwa awali kama itazidi watajulishwa kwa vile mgonjwa hakuwa wa kutoka mapema. Walikubali kugharamia matibabu ya Cecy mpaka hatua ya mwisho. Baada ya makubaliano zilifanywa taratibu zote za kumsafirisha mgonjwa na mtu wake wa karibu.
Siku ya tatu Cecy alisafirishwa pamoja na mama yake kwenda India kwa matibabu ambayo wengi waliamini madaktari wa Tanzania waliona aibu kusema ukweli kuwa Cecy ameisha kufa anachosubiri kupoa tu. Baada ya safari ya angani Cecy alitua katika jiji la Mumbay na kupelekwa katika hospitali ya Apolo.
Alipokelewa mara moja alianza kupatiwa matibabu kwa kuchukuliwa vipimo vyote ili kuangalia tatizo lipo wapi. Baada kurudi majibu ya vipimo ilionesha Cecy atapona lakini itachukua muda kurudi katika hali ya kawaida kutokana na kupoteza kumbukumbu na ubongo wake kucheza kidogo, lakini alikuwa na bahari nzuri ubongo haukuvia damu.
TANZANIA
Hali ya Colin iliendelea vizuri kwa kuimalika kwa kasi kubwa tofauti na walivyotegemea. Baada ya wiki aliweza kuzungumza vizuri na kuanza kumkumbuka mpenzi wake Cecy. Wakiwa wamekaa kitandani Colin alimuuliza mama yake.
“Mama mbona simuoni Cecy wala mama yake leo siku ya tatu?”
“Cecy alisafiri walifiwa na bibi yao kabla hujapata ajali.”
“Mama ina maana nilipata ajali peke yangu?”
Swali lile lilimchanganya sana mama yake aliyeamini mwanaye baada ya ajali alipoteza kumbukumbu na hakutaka kumshtua kutokana na hali na mchumba wake ambaye aliamini aliondoka mfu kwa asilimia tisini na tano.
“Kwani unakumbuka nini?”
“Unajua mama nakumbuka wakati napata ajali nilikuwa na Cecy tukitoka mazoezini na sababu ya ajali ni Mage.”
“Mage?” mama yake alishtuka.
“Ndiyo mama.”
“Mage kasababisha kivipi?”
Colin alimweleza tukio zima la ajali ilivyotokea mpaka kupata ajali, baada ya kumsikiliza aliguna na kusema:
“Kwani Mage aliandika ujumbe gani?”
“Kwa kweli sikuuona bali usomaji wa Cecy ulionesha ujumbe siyo mzuri.”
“Sasa wewe nini kilikupelekea kupata ajali.”
“Mama baada ya kumwangalia Cecy usoni moyo ulishtuka na kujua hakuna tena usalama kwa vile aliisha mshutumu Mage mapema baada ya hukumu ya mchumba wake kabla ya simu na kutishia kusitisha mkataba. Mage alinipigia simu na kuzungumza maneno ambayo ni uchokonozi kwa vile anajua kabisa nipo na nani.”
“Inaonekana alikuacha bado anakupenda ulikuwa una hiyari kukubali au kukataa au hata kumfanya spea taili.”
“Mama Cecy ni kila kitu kwangu ndiye mwanamke wa pekee moyoni mwangu sina nafasi nyingine.”
“Lakini ulitakiwa kujua ameandika ujumbe gani kabla ya kupagawa na kusababisha ajali mbaya.”
“Kwani gari limeharibika sana?”
“Limeungua lote na moto.”
“Mungu wangu na..na Cecy?”
“Naye alipata majeraha kama yako.”
“Yupo hapa hospitali?”
“Hapana yeye inaonekana alipata matatizo makubwa na kukimbizwa India.”
“Maskini mpenzi wangu,” Colin alishika kichwa kwa mshtuko.
“Lakini taarifa zinasema anaendelea vizuri,” mama yake alimpa moyo.
“Hospitali natoka lini?”
“Wiki hii lakini utatakiwa kuja kila siku asubuhi kufanya mazoezi ya viungo ili kuurudisha mwili katika hali ya kawaida.”
“Nikijisikia vizuri kidogo nakwenda India kumwona mpenzi wangu.”
“Hakuna tatizo tutakwenda wote,” mama Colin alimkubalia mwanaye kumpa moyo lakini aliamini kabisa Cecy hakuna kitu siku zake zilikuwa zikihesabika walichosubiri taarifa za msiba wake.
Itaendelea

2 comments:

  1. Story nzur sana kaka na lazima tukuchangie k2 kwa uwezo huu Mungu aliokujalia namba yng in 0656411621 naomba uniunge na mm na utujulishe garama

    ReplyDelete
  2. Story nzur sana kaka na lazima tukuchangie k2 kwa uwezo huu Mungu aliokujalia namba yng in 0656411621 naomba uniunge na mm na utujulishe garama

    ReplyDelete