Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 24


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Wiki hii lakini utatakiwa kuja kila siku asubuhi kufanya mazoezi ya viungo ili kuurudisha mwili katika hali ya kawaida.”
“Nikijisikia vizuri kidogo nakwenda India kumwona mpenzi wangu.”
“Hakuna tatizo tutakwenda wote,” mama Colin alimkubalia mwanaye kumpa moyo lakini aliamini kabisa Cecy hakuna kitu siku zake zilikuwa zikihesabika walichosubiri taarifa za msiba wake.
SASA ENDELEA...
***
Mama Mage na mwanaye walikuwa wakizungumza kuhusiana na hali ya Colin na mchumba wake.
“Mama unafikiri mchumba wa Colin anaweza kupona?”
“Mmh! Kwa kweli ni Mungu tu mwenye uwezo wa kumponya, taarifa nilizopata kutoka kwenye hospitali aliyokuwa anatibiwa kupona ni asilimia ndogo na hata akipona bado hata kuwa sawa.”
“Kwa hiyo mama nina imani hii ni nafasi yangu ya kurudi kwa Colin?”
“Ni nafasi yako kama ukiifanyia kazi bila hivyo itakupita huku unaiona.”
“Sasa mama niifanyie kazi ipi au niende wa Karumanzila?”
“Si kwenda kwa Karumanzila bali kujipendekeza muda huu wa matatizo kuonesha unamjali sana Colin kwa kwenda asubuhi unarudi usiku ikiwezekana ulale hukohuko.”
“Mama tena naondoka muda huu.”
“Mwanangu kijua ndicho hiki lazima uuanike sasa, huenda Mungu alikuwa na kusudio lake la kuirudisha ndoa yetu iliyoyeyuka kwa kifungo cha Hans na kufa kwa Cecy.”
“Umeona eeh, mama utakuwa nabii kwa kuiona hilo, japo siwezi kufurahi kwa matatizo ya Cecy lakini kila kitu hupangwa na Mungu.”
“Halafu nimeambiwa Colin atatakiwa kila siku asubuhi apelekwe hospitali kwa mazoezi, nataka kazi hiyo uifanye wewe tena utachukua gari la kifahari la kumpelekea hospitali.”
“Mama hilo si la kusema mbona kikohozi kimepata mkohoaji nitahakikisha mahaba ninayo mpa anamsahau marehemu wake(Cecy).”
Baada ya mazungumzo Mage alimuaga mama yake kwenda kumwona Colin nyumbani kwao ili aurudishe ukaribu wao kutokana na matatizo ya mchumba wake Cecy. Mage maombi yake alitaka Cecy afie India, Tanzania urudi mwili tu usio na uhai, aliendesha gari hadi nyumbani.
Mama Colin alimpokea Mage aliyejionesha mwenye huzuni kutokana ugonjwa Colin.
“Karibu mkwe.”
“Asante mama, mume wangu anaendeleaje?”
“Mmh! Kiasi hajambo vipi nyumbani hamjambo.”
“Hatujambo kiasi.”
“Kuna anayeumwa?”
“Hapana ila huwezi kuamini toka Colin apate matatizo nimekuwa sili wala silali vizuri utafikiri naumwa mimi.”
“Pole, la muhimu kumuomba atapona tu.”
“Mama maombi yangu yote kila dakika ni kwa Colin.”
“Mama yako hajambo?”
“Hajambo, mume wangu yupo wapi?” Mage alijifanya ana shauku ya kumuona Colin.
“Yupo chumbani kwake amepumzika.”
Kwa vile chumba cha Colin alikuwa akikijua alikwenda moja kwa moja na kuingia ndani bila hodi. Alimkuta amesinzia aliinama na kumpiga busu la shavu lililomfanya Colin afumbue macho. Alishtuka kukutana na Mage aliyekuwa amemchanulia tabasamu pana amesimama pembeni ya kitanda.
“Colin mpenzi wangu pole sana,” Mage alisema huku akikaa kitandani, lakini Colin hakumjibu alikuwa kama anamshangaa.
“Vipi inaendeleaje mpenzi?” alimuuliza tena.
“Mage unatafuta nini hapa?” Colin alimuuliza akiwa amemkunjia uso.
“Colin mpenzi wangu maswali gani hayo wakati unajua wewe ni mgonjwa?”
“Hata kama mgonjwa sikukuita uje unione labda ungekuja kuona jeneza langu na si mwili wangu.”
“Kwa nini unasema hivyo mpenzi wangu?” majibu la Colin yalimshtua Mage.
“Kwanza naomba jina la mpenzi lifutike mdomoni na moyoni mpenzi wako, mpenzi wangu ni mmoja tu Cecy.”
“Kumbuka kabla ya Cecy nilikuwepo miye.”
“Kuna mtu aliye mpenzi wa moyo wako si mwingine bali Hans si Colin.”
“Colin, Hans amefungwa si mpenzi wangu mwenye nafasi hiyo ulibakia wewe peke yako.”
“Mimi ulinipenda lakini Hans ulimpenda zaidi kwa hiyo ndiye chaguo sahihi la moyo wako si mimi. Nami wewe nilikupenda lakini Cecy nilimpenda zaidi naye ndiye aliyenipenda kuliko kiumbe chochote kilichopo chini ya jua. Malaika sijawaona nina amini hata wao ningewaona wasingeuzidi uzuri wa Cecy.”
“Wewe Colin acha kukufuru Cecy ana uzuri gani kumshinda malaika?”
“Malaika uliisha muona?”
“Sijamuona lakini nasikia mzuri sana.”
“Basi uzuri wao haufiki kwa Cecy, kwa vile ulichokitaka kimefanikiwa naomba uachane na mimi.”
“Colin nimefanya nini?” Mage aliuliza huku akilia.
“Unajua umeniumiza mara ya kwanza hukutosheka umeniumiza kwa mara ya pili bado hujaridhika naona kimebakia roho yangu tu.”
“Colin usiseme hivyo unaniumiza?”
“Ulitaka tufe sote lakini nakuhakikishia Cecy atapona na atarudi tufunge ndoa hata kama Cecy atakufa nitafunga ndoa na maiti ya Cecy si mwanamke mwingine.”
“Colin usiseme hivyo, Cecy akifariki siyo mwisho wa dunia maisha yataendelea, nina imani hakutakuwa na mwanamke mwingine atakayechukua nafasi ya Cecy bali mimi.”
“Ninacho kisema hakitafutika moyoni mwangu Cecy ndiye mwanamke wangu wa maisha nawe msubiri Hans mfunge ndoa au nenda mkafungie ndoa gerezani.”
“Kwa nini Colin unanichukia hivyo?”
“Sitakusamehe mpaka nakufa naomba utoke nje,” Colin alisema kwa sauti ya juu.
“Colin ukikataa najiua.”
“Kajiue kwani ukifa mimi napungukiwa nini labda muuaji mwezio Hans.”
Maneno yale yaliuchoma moyo wa Mage ambaye alikuwa na matumaini ya kuchukua nafasi ya Cecy ambaye aliamini kupona kwake ni asilimia ndogo sana na hata kipona hataweza kuwa sawa. Kutokana na maelezo ya kidaktari aliyemfuata baada ya Cecy kupelekwa India.
Alimweleza kuwa kama atapona angeweza kuwa na tatizo la kusahau au kupoteza kumbukumbu ambacho huwa sawa na kichaa cha kipindi kama maji kupwa maji kujaa kuna wakati inakaa sawa kuna wakati inahama.
Baada ya kuumizwa na maneno ya Colin yaliyomkatisha tamaa alitoka nje akilia kilio cha kwikwi kitu kilichomshtua mama Colin aliyekuwa amekaa sebuleni akisoma Biblia.
“We, Mage unalia nini, Colin kazidiwa?”
“Ha..ha..pana mama, Colin kanifukuza eti hataki kunioa.”
“He! Kwa sababu gani?”
“Hata sijui, yaani anasema yupo radhi kufunga ndoa na maiti ya Cecy kuliko kunioa mimi. Eti mama, siombi ila kwa bahati mbaya Cecy amekufa mwanamke wa kuolewa na Colin kuna mwingine zaidi yangu?”
“Hakuna.”
“Sasa kwa nini ananidhalilisha kwa maneno makali?”
“Labda umemkuta leo hayupo vizuri.”
“Mama naomba kama Cecy atakufa basi nafasi yake nipewe mimi kwa vile tunajuana vizuri, inawezekana kufungwa kwa Hans na hii ajali ilikuwa mpango wa Mungu kuirudisha harusi yetu iliyofungwa mbinguni.”
“Mmh! Makubwa,” mama Colin aliguna maneno ya Mage.
“Mama naomba ukazungumze na Colin, si ulisema anatakiwa kupelekwa hospitali kila asubuhi, kazi hiyo nitaifanya mimi hata kumpikia chakula kumfulia kipindi chote nitafanya nini. Nipo tayari kuhamia hapa kuhakikisha Colin hapati tatizo lolote.”
“Basi tulia nitazungumza na Colin.”
Mama Colin alikwenda chumbani kwa Colin ili ajue kimetokea nini mpaka apishane kauli na mpenzi wake wa zamani. Alimkuta Colin amejilaza macho kaangalia juu, mlango ulipofunguliwa aligeuza shingo kuangalia nani anayeingia alimkuta ni mama yake.
“Vipi baba?” mama yake alimuuliza.
“Safi tu,” alijibu akiwa bado ameangalia juu.
“Upo sawa baba?”
“Sipo sawa,” alijibu akiwa bado macho yake yakiangalia darini.
“Kwa nini tena mwanangu?”
“Nani kampa ruhusa huyu shetani kuingia ndani?” aliuliza huku akigeuka kumtazama mama yake.
“Colin! Shetani nani?”
“Mage, sitaki kumuona machoni mwangu,” alisema kwa sauti ya juu kidogo.
“Kwa nini baba?”
“Aliyonifanyia madogo, leo ni Mungu tu nipo hai lakini kifo changu angechangia yeye hata mateso ya mpenzi wangu chanzo ni yeye. Kaniumiza mara ya kwanza hajafurahi karudia mara ya pili kaniumiza na mpenzi wangu bado tu ananifuata anataka nini kama siyo uhai wangu?”
“Lakini kwa nini unamhukumu bila kujua ujumbe alioandika umeandikwaje?”
“Mama, ulikuwa mbaya, Cecy hawezi kulia kwa ujumbe wa kawaida.”
“Colin bado hutakiwi kumhukumu kwa kitu usichojua, inawezekana ulikuwa wa kawaida lakini kwa vile mpenzi wako aliisha jenga chuki kwa Mage huenda hakufurahia ujumbe ule.”
“Lakini mama hata kama, ni haki mtu kutuma ujumbe au kupiga simu akijua kabisa mimi ni mchumba wa mtu na tupo katika hatua gani?”
“Hapo anaweza kuwa amefanya makosa lakini hakuna adui wa maisha, adui wa leo rafiki wa kesho, msamehe mwenzio nimemwacha analia kwa maneno yako makali.”
“Mama nitamsamehe Mage labda Cecy apone asipopona sitamsamehe mpaka nakufa.”
“Sikiliza mwanangu, ni wazi Mage anakupenda sana hujui tu, kama Mungu anapitisha uamuzi wake, Cecy anafariki Mage ndiye mwenye nafasi ya kuwa mkeo.”
“Mama kwa nini unakimbilia kufa mpenzi wangu, nataka nikuambie kitu. Cecy akifanya nitafunga naye ndoa kabla ya kuzikwa.”
“We’ Colin umerogwa yaani ufungwe ndoa na maiti ili iwe nini?”
“Kutimiza ahadi niliyomuahidi Cecy ambayo ndiyo ndoto yake kubwa kwangu ya kuwa mke na mume. Mama Cecy nampenda lakini yeye ni mwalimu wangu wa mapenzi ndiye wakili wa moyo wangu kanipigania wakati wote kuonesha ana mapenzi ya kweli kwangu Cecy hanipendei kitu bali mimi kama mimi.”
“Mmh! Na ukiisha muoa?”
“Nitaendelea kuwa muaminifu katika ndoa yangu mpaka mauti yatakaponichukua.”
“Kwa hiyo huoi tena?”
“Mama ndoa ipo moja tu dunia ikiisha fungwa duniani mpaka mbinguni haitafunguliwa.”
“Sasa kama amekufa si ndiyo mwisho wa ndoa yenu.”
“Kwangu itakuwa mwanzo kwa vile sijaitumikia ndoa yetu.”
“Colin mwanangu upo sawa?”
“Tena akili zangu zipo timamu.”
“Hebu pumzika naona kama haupo sawa.”
“Mama wala usisumbuke kufikiria unavyotaka kufikiria sina jibu zaidi hilo nililokupa.”
“Kwa mfano Cecy atarudi hayupo sawa na ugonjwa wake hauponi au amepooza utafanya nini?”
“Kama nitaweza kufunga ndoa na mwili wake usio na pumzi sitabadilika nitafunga ndoa na Cecy katika hali yoyote.”
”Mmh! Sawa.”
Mama Colin alitoka bila kuongeza neno huku akijiuliza Mage kamfanya nini Colin mpaka kufikia uamuzi mzito kama ule. Lakini aliamini zile ni hasira za kumwona Mage lakini baadaye zitashuka na kuelewana. Aliamini kabisa ugonjwa wa Cecy si wa kupona na kama akipona hata kuwa sawa hivyo mwanamke aliyeona anamfaa mwanaye ni Mage kwa vile tayari waliisha kuwa wapenzi kabla ya hapo.
Mage baada ya kutokeza mama Colin alikaa mkao wa kutaka kujua amezungumza nini na mwanaye.
“Vipi mama, Colin kasemaje?”
“Hii kazi niachie mimi, najua bado ana hasira zikipoa atanielewa tu.”
“Yaani mama siamini maneno anataka kuoa maiti ya Cecy kwani wanawake wamekwisha? Hata kama hanitaki mimi lakini bado wapo wazuri na wenye tabia nzuri kuliko Cecy.”
“Hilo lisikutie presha, nammudu kwa vile ni mwanangu na wala hataoa mwanamke mwingine zaidi yako. Ninyi mnafahamiana na vile mlikuwa mnapendana hivyo mtaendelea uliposimamia.”
“Umeona eeh mama, yaani Colin namshangaa kweli.”
“Sasa sikiliza kesho anatakiwa kupelekwa hospitali kwa mazoezi njoo asubuhi umpeleke.”
“Mamaa! Kwa hali hii atakubali?” Mage aliishangaa kauli ya mama Colin.
“Mage we njoo mimi nitajua nitafanya nini, nakuhakikishia lazima ataolewa na mwanangu.”
“Mmh! Mama nitafurahi, bado naona kama nipo ndotoni.”
“Wala si ndotoni, amini Colin wewe ndiye mkewe.”
“Nashukuru sana mama, basi nikuache niwahi nyumbani.”
“Hakuna tatizo msalimie mama yako.”
“Salamu zimefika.”
Mage aliagana na mama Colin na kurudi nyumbani kwao huku dua lake likiwa kwa Cecy asirudi hai ili aichukue nafasi ambayo aliamini ilikuwa yake hapo awali. Hakutaka kuyajutia maamuzi yake ya kuachana na Colin na kurudiana na Hans kwani kwake ulikuwa uamuzi sahihi ilitokea bahati mbaya ya kufungwa maisha.
Moyoni mwake alikuwa tayari kumsubiri Hans hata miaka kumi ili waoane lakini kifungo cha maisha kilimvunja nguvu na kuamini mtu sahihi kwake alikuwa Colin. Aliapa kumpigania Colin kwa nguvu zote kumrudisha mikononi mwake hata kwa kutoa uhai wa mtu. Alipofika nyumbani kwao alimweleza mama yake kilichotokea na kumshtua sana.
Itaendelea

No comments