Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 25


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Moyoni mwake alikuwa tayari kumsubiri Hans hata miaka kumi ili waoane lakini kifungo cha maisha kilimvunja nguvu na kuamini mtu sahihi kwake alikuwa Colin. Aliapa kumpigania Colin kwa nguvu zote kumrudisha mikononi mwake hata kwa kutoa uhai wa mtu. Alipofika nyumbani kwao alimweleza mama yake kilichotokea na kumshtua sana.
SASA ENDELEA...
“Mmh! Yamekuwa hayo unafikiri utafanyaje naona kila kitu kimevurugika.”
“Lakini mama Colin kasema kesho niende nikampeleke Colin hospitali.”
“Utampeleka vipi ikiwa hataki hata kukuona?”
“Mama yake kasema yeye anajua kila kitu kinachotakiwa kufanyika na ameniahidi lazima nitaolewa na mwanaye.”
“Mmh! Sawa kwa vile kasema mama yake lakini maneno ya Colin yamenitisha kusema, eti yupo tayari kufunga ndoa na maiti ya Cecy kuliko kuoa mwanamke mwingine.”
“Mama au akili ya Colin imepata tatizo baada ya kujigonga kwenye ajali?”
“Inawezekana maana ajali haikuwa ya kawaida.”
“Mmh! Inawezekana maana alivyonigeuka si kawaida yake, mama naamini Colin ananipenda.”
“Au yule mtoto alimwendea Colin kwa Karumanzila?”
“Inawezekana kabisa si bure ana urembo gani wa kumfanya Colin atake kufunga ndoa na maiti yake.”
“Hata mimi naona, lazima nasi tuhangaike ili kuhakikisha nafasi hiyo unaipata wewe.”
“Yaani huwezi kuamini sara zangu zote namuomba Ziraili amtokee Cecy na kummaliza kabisa tufikirie mambo mengine.”
“Duh! Kweli wewe kiboko, wenzio dua zao wanaomba amani wewe shari.”
“Siku zote adui yako muombee matatizo.”
“Mmh! Haya.”
MUMBAY INDIA
Katika hospitali ya Apolo katika mji wa Mumbay nchini India madaktari waliendelea kuumiza kichwa kutokana na ugonjwa wa Cecy ambao uliwachanganya akili baada ya kuweza kufumbua macho lakini mwili bado haukuwa na mawasiliano kwa asilimia zote.
Waliufanyia vipimo vyote na kukaa jopo la madaktari mabingwa kuchunguza Cecy ana tatizo gani lililopelekea kuwa katika hali ile. Hali iliyojitokeza ilikuwa tofauti na maelezo ya ajali yake, walijikuta wakifikia uamuzi wa kumrudisha Tanzania kwani waliamini hakutaka na mabadiliko yoyote kwa muda mfupi.
Matumaini ya kupata nafuu yalikuwa asilimia ndogo sana kuliko kupoteza maisha. Uhai wake waliamini hautachukua muda mrefu kwa vile mawasiliano hayakuwepo zaidi ya mapigo ya moyo yalienda kawaida pia hata mapafu yalifanya kazi vizuri.
Kilichowashangaza kuweza kupita kwa chakula laini na kufanyiwa kazi na kutoka kinyesi chepesi ambacho alisaidia bila habari. Mama yake alikuwa na kazi ya kumgeuza na kumsafisha anapojisaidia pia kumbadili ubavu ili kutoweka vidonda kwa kulalia upande mmoja kwa muda mrefu.
Mama Cecy naye alikata tamaa ya mwanaye kupona kutokana na kutotokea mabadiliko yoyote makubwa zaidi ya kuweza kutazama na kula kitu kilichokuwa kikitia matumaini kidogo.
Baada ya jopo la madaktari kukubaliana kumrudisha Tanzania, kwa kuamini kwa kuwa Tanzania ataweza kupata vitu viwili, moja kulikava taratibu akiwa nyumbani hivyo kupunguza gharama. Pili hata akifa wasipate gharama za kuusafirisha mwili wa marehemu.
Walimwita mama Cecy kumpa taarifa zile walizokubaliana kuhusu mwanaye kurudishwa Tanzania. Baada ya kuingia kwenye ofisi ya madaktari bingwa alikaa kitini huku akiwa na mkalimani daktari aliyeongozana naye.
“Mama Cecy, tumekuita hapa ili kukujulisha hatua tuliyofikia, inaonesha ugonjwa wa mwanao utachukua muda mrefu kupona. Hivyo tumeamua kumrudisha Tanzania ili uweze kumhudumia nyumbani pia kupata msaada wa matibabu ya kusaidia kuusisimua mwili.”
“Mmh! Sasa itakuwaje ikiwa hospitali inayotegemewa mmeshindwa, mwanangu si ndiyo anakwenda kufa?”
“Hapana si kufa bali huduma za muhimu tumejitahidi kadri ya uwezo wetu, hatuwezi kuendelea kumweka hospitali na kuongeza gharama wakati huduma zingine anaweza kuzipata akiwa hukohuko Tanzania. Sisi kazi yetu kubwa tumemaliza kilichobakia na kazi ya Mungu.”
“Mmh! Sawa.”
Mama Cecy alikubali kwa sauti ya kukata tamaa kwani siku zote watu waliokwenda India hurudi wamepona na ikishindikana basi mtu huyo huwa wa kumzika. Aliamini ile ilikuwa kauli ya kumpa moyo lakini siku za kuishi mwanaye zilikuwa zinahesabika.
Iliandaliwa mipango yote ikiwa pamoja na tiketi ya kurudi Tanzania na kupangiwa siku ya kurudi. Habari zile zilikuwa pigo mujarabu moyoni kwa mama Cecy mwanaye mmoja kama mboni ya jicho lake alimuona akitoweka katika sura ya dunia. Lakini yote alimuachi Mungu kwa vile muweza wa kila kitu.
Taarifa za kurudishwa Tanzania Cecy baada ya ugonjwa wake kuonekana utachukua muda mrefu kupata nafuu. Zilimfikia mama Colin na kuamini ile ndiyo nafasi ya pekee kwa Mage kuichukua nafasi ile baada ya kupata uhakika hali ile inaweza kuchukua muda mrefu kupata nafuu au maisha yake yote yawe ya kitandani alijua ilikuwa kuwapa moyo lakini Cecy alikuwa maiti mtalajiwa.
Kwa taarifa ile aliamini mwanaye pamoja na msimamo lazima atabadilika na kukubali kumuoa Mage huku akijitolea kumsaidia Cecy kwa kumwekea mtu wa kumhudumia na kumlipa kwa maisha yake yote ili tu kumfurahisha mwanaye.
Alitamani siku moja aitwe bibi na hakuwa na mtoto mwingine zaidi ya Colin ambaye ndiye aliyemtegemea kumleta mjukuu. Ugonjwa wa Cecy ulionesha hakukuwa na dalili zozote kuweza kubeba ujauzito na yeye kupata mjukuu. Moyoni alijikuta akipata mawazo mabaya ya kumuua Cecy kama mwanaye atasimamia msimamo wake wa kutotaka kuoa mwanamke mwingine.
Lakini kuna kitu kilimtisha baada ya kukumbuka kauli ya mwanaye kufunga ndoa hata na maiti ya Cecy. Hiyo ilimpa wakati mgumu. Lakini alipanga kumtumia Mage kuyabadili mawazo yake na kukubali kumuoa. Siku ya pili Mage alifika kama alivyoelekezwa na mama Colin lakini hakutakiwa kuonana na Colin mpaka mpango wake autekeleze.
Baada ya Mage kufika alifikia chumba cha msichana wa kazi na mama Colin alikwenda chumbani kwa Colin kumwamsha ili ajiandae kwenda hospitali.
“Jiandae basi ukafanye mazoezi.”
“Sawa mama.”
Colin aliingia bafuni kuoga baada ya kuoga alibadili nguo na kutoka chumbani kwake na kwenda kukaa sebuleni kumsubiri mama yake ili waende kwenye mazoezi ya viungo (Physiotherapy). Mama Colin alitoka chumbani kwake akiwa tayari kwa safari begi lake begani. Colin alipomuona mama yake alinyanyuka ili waondoke.
Lakini ghafla alishtuka kumwona mama yake akiweka mkono kichwani katika paji la uso huku amekunja uso.
“Nini mama?” Colin alishtuka.
“Kichwa,” mama alisema kwa sauti ya kujilazimisha.
“Mungu wangu! Kimefanya nini tena mama yangu?” Colin alishtuka na kujitahidi kumfuata mama yake ili amshike.
“Hapana baba , niache nitakaa mwenyewe,” mama Colin alisema huku akisogea kwenye kochi na kukaa.
“Nipe maji,” alisema akiwa ameinama mkono kichwani.
Colin alipotaka kwenda kumchukulia maji alimkataza na kutaka amwambie msichana wa kazi. Baada ya kuitwa alileta maji kwenye glasi na kumpa mama Colin aliyeyanywa yote na kupumua pumzi nyingi kisha alisema.
“Duh! Afadhali kidogo.”
“Sasa itakuwaje maana kwa hali hiyo huwezi kuendesha gari?”
“Na kweli siwezi kuendesha gari, nimekumbuka Mage alisema atakuja kukuona asubuhi.”
“Mage gani?”
“Si aliyekuwa mchumba wako.”
“Mama niseme mara ngapi kuwa sitaki kumuona yule shetani wa kike,” Colin alisema kwa hasira kidogo.
“Mwanangu wewe ndiye uliyekuwa ukinieleza siku zote nisikae na jambo baya moyoni muda mrefu naweza kupata matatizo. Kwa nini unamchukia hivyo Mage? Hata kama alifanya kosa lililosababisha ajali bado alitakiwa kusamehewa. Humtaki kuwa mpenzi wako lakini bado ni mwanadamu anayetakiwa kusamehewa na kumwona rafiki, hujui adui wa leo ni rafiki wa kesho.”
“Ni kweli mama, najitahidi kumsamehe lakini moyo wangu umekuwa mzito.”
“Huyo ni pepo mchafu tunatakiwa kumkemea.”
“Sawa mama nitajitahidi.”
“Kwa vile siwezi kuendesha gari leo basi naomba Mage atatupeleka hospitali.”
“Sawa mama,” Colin hakutaka kukataa kwani angemuudhi mama yake.
“Ngoja nimpigie simu.”
Mama Colin alijifanya kipiga simu na kujizungumzisha peke yake:
“Eeh! Umekaribia... tena umefanya vizuri... wahi basi utupeleke hospitali...haya tunakusubiri... Umekaribia... sawa... hakuna tatizo tupo tayari,” mama Colin alijifanya kukata simu.
“Kwani kafika wapi?” Colin aliuliza.
“Yupo nje ya geti.”
“Sawa.”
Mama Colin alijifanya kuelekea upande wa vyumbani na kwenda chumba cha msichana wa kazi na kwenda kuzungumza Mage.
“Mambo yamekwenda vizuri japokuwa imenibidi nilazimishe kwa cheo cha umama, sasa pitia mlango wa nyuma kisha ingilia mlango wa mbele kujifanya ndiyo unaingia.”
“Sawa mama.”
Mage alitokea mlango wa nyuma na kwenda kulichua gari alilokuwa amelipaki nje na kuingia nalo. Aliteremka kwenye gari na kuingia ndani.
“Karibu mama.”
“Asante, za hapa?”
“Nzuri.”
Mage alisogea kwa Colin na kumsalimia:
“Umeamkaje?”
“Namshukuru Mungu.”
“Nina imani hali yako itatengemaa muda si mrefu ili urudi katika majukumu yako, sara zangu zote hukutanguliza mbele nina imani Mungu ataipokea.”
“Amina.”
“Mage tunaweza kwenda.”
Mage alimshika mkono Colin na kunyanyua, alitoka naye hadi nje na kuingia kwenye gari la Mage ambalo aliomba walitumie kwa siku ile. Colin muda wote alikuwa kimya hakutaka kutia neno kwa kuhofia kumuudhi mama yake ambaye muda huo aliamini kabisa hali yake siyo nzuri hakutaka kuharibu kote kwani bado hali ya mpenzi wake Cecy ilibakia kitandawili.
Walikwenda mpaka kwenye kitengo cha mazoezi ya viungo (Physiotherapy), walipofika mama Colin alikaa pembeni na Mage alimsaidia Colin kufanya mazoezi kwa kumshikilia sehemu zingine ambazo alihitaji msaada. Kila dakika Mage alikuwa akitokwa na machozi kitu kilichomshtua Colin.
“Mage unalia nini?”
“Sijui moyoni mwako una hasira kiasi gani juu yangu.”
“Sina hasira yoyote.”
“Hapana Colin una kitu kizito juu yangu kutokana na yaliyotokea, ile ni mipango ya Mungu tu, naomba Colin unisamehe najutia kilichotokea ni mapenzi ndiyo yaliyonisukuma kufanya vile. Hata kama hutaki kuwa na mimi naomba unione rafiki na si adui.”
“Mage ningekuwa sijakusamehe tusingekuwa karibu hivi na kuweza kukusikiliza.”
“Nashukuru Colin kwa kunisamehe, naamini wewe ni mume mwema hakika Cecy kapata lulu kwenye chaza.”
“Nashukuru.”
“Vipi hali ya Cecy?”
“Kwa kweli mpaka sasa sijajua, mama amekuwa akinificha japo walinieleza inaendelea vizuri.”
“Mungu atamsaidi siku moja atasimama na kufanikisha mlichokipanga,” Mage alimpa moyo kinafiki.
“Amina.”
“Colin.”
“Naam.”
“Baada ya Cecy moyoni mwako yupo nani?”
“Bado sijamuona labda mwenetu atakaye zaliwa.”
“Basi naomba baada ya mwenenu nafasi inayofuata nipe mimi, naomba usiniweke mbali na mawazo yako.”
“Hakuna tatizo.”
“Naomba niwasiliane na wewe wakati Cecy yupo mbali.”
“Mage, suala la mawasiliano naomba tuliweke pembeni kwanza.”
“Kwa nini Colin, kukujulia hali tu.”
“Ukitaka kuwasiliana na mimi tumia simu ya mama lakini kwa sasa sitatumia simu kwa vile ndiyo iliyoleta yote haya.”
“Colin basi hujanisamehe.”
“Kukusamehe si kunilazimisha kufanya vitu nisivyo vitaka, nimekueleza sitaki kutumia simu unanilazimisha kwa kisingizio cha kutokusame. Kumbuka ubishi huo ndiyo uliosababisha yote haya.”
“Nimekuelewa Colin, nisamehe sana, nitajitahidi kukuelewa ili tusije kosana tena.”
“Itakuwa vizuri.”
“Colin nashukuru kunisamehe moyo wangu sasa mwepesi nilikuwa kama nimebeba mawe.”
“Kawaida katika maisha kuna kukosana na kupatana.”
“Nashukuru sana.”
Mama Colin aliyekuwa mbali kidogo mazungumzo yale yalimtia moyo na kuamini mpango wake umeweza kufanikiwa kwa kuamini Mage ndiye chaguo lake la awali kabla Cecy kuingilia penzi lile. Taarifa ya kurudishwa Cecy kutoka India hakutaka kumweleza haraka mwanaye mpaka akapotua nchini kwani kwa taarifa siku inayofuata ndiyo aliyokuwa akiwasilia nchini.
ITAENDELEA

No comments