Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 26


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Mama Colin aliyekuwa mbali kidogo mazungumzo yale yalimtia moyo na kuamini mpango wake umeweza kufanikiwa kwa kuamini Mage ndiye chaguo lake la awali kabla Cecy kuingilia penzi lile. Taarifa ya kurudishwa Cecy kutoka India hakutaka kumweleza haraka mwanaye mpaka akapotua nchini kwani kwa taarifa siku inayofuata ndiyo aliyokuwa akiwasilia nchini.
SASA ENDELEA...
Alipanga kuonesha ushirikiano mkubwa lakini alibakia na siri yake juu ya Cecy na ugonjwa wake ambao kama ulishindikana India basi Tanzania ilikuwa ni kusubiri kifo. Kumweka Mage karibu na Colin kungemsaidia kumweka karibu kimapenzi hata akifa Cecy basi Mage achukue nafasi ile.
Baada ya mazoezi walirudi nyumbani huku kila mmoja akiwa na furaha moyoni mwake japokuwa furaha ya Colin ilikuwa usoni na mdomoni lakini moyoni bado halikosa raha kushindwa kupata mawasiliano ya kujua hali ya mpenzi wake Cecy. Lakini aliamini baada ya muda hali yake itatengemaa na yeye mwenyewe kwenda India kumuona Cecy.
Siku ile Mage alishinda pale na kufanya kila kitu kwa ajili ya Colin, kuanzia usafi wa chumba chakula cha mchana vyote alifanya yeye na muda mwingi alikuwa karibu yake ili kuhakikisha anairudisha nafasi iliyoipoteza kupitia matatizo ya Cecy. Kitu kile kilimfurahisha sana mama Colin na kuuona mpango wake taratibu utafanikiwa.
Siku ile taarifa ilifika kwa Cecy anawasili toka India, mama Colin hakutaka kumwambia mwanaye ila saa sita usiku alikwenda kuwapokea pekle yake. Baada ya ndege tukutua abiria waliteremka na kutoka nje.
Alisimama macho yakiwa ndani huku akijiuliza Cecy atarudi katika hali gani, akiwa mapokezi alikiona kitanda kikisukumwa nyuma yake alikuwepo daktari aliyeondoka naye na nyuma ya daktari alikuwepo mama Cecy ambaye alionekana amepururuka mwili kutokana na matatizo ya mwanaye.
Mama Colin alijitokeza kuwapokea kwa kumkumbatia mama Cecy.
“Jamani dada karibuni, poleni na safari.”
“Mungu ni mwema.”
“Karibuni,” alikwenda kitandani kumwangalia Cecy ambaye muda huo alikuwa amepitiwa usingizi.
“Vipi anaendeleaje?”
“Tutazungumza nyumbani, vipi Colin naye anaendeleaje?”
“Kweli Mungu ni mwema anaendelea vizuri.”
Kwa vile alikuwa amekuja na gari aina ya Toyota Noah aliyeelezwa ndiyo inayotakiwa kumpokelea mgonjwa, walimweka kwenye gari na kuelekea nyumbani kwa mama Cecy ambako siku ile kulifanyika usafi na kuiweka nyumba katika hali nzuri. Hivyo walikuta nyumba ipo vizuri pamoja na msichana wa kazi aliyeachwa kwa ajili ya kuangali nyumba kwa muda wote ambao hakuwepo.
Baada ya kufikishwa nyumbani aliingizwa chumbani na kulazwa kitandani, muda wote mama Colin alimfuatilia Cecy na kuonesha hakuwa na dalili zozote za kupona. Pamoja na huruma kumjia lakini bado aliamini kama Cecy atakufa basi Mage ndiye mbadala wake.
Baada ya kumlaza kitandani daktari aliyekwenda na Cecy India alikaa na wazazi wawili na kuwaeleza:
“Jamani nina imani maelezo tulipewa India unayakumbuka, lakini kwa kuongezea ninataka kuwaeleza, mgonjwa hali yake bado japo kuna mabadiliko makubwa sana tofauti na alivyokwenda. Ugonjwa wa Cecy umekuwa tofauti na ugonjwa mwingine ambao madaktari bingwa wamekutana nayo huu kidogo umewala akili.
“Inaonekana mwili wa Cecy anajenga mawasiliano taratibu sana inaweza chukua muda mrefu sana kunyanyuka kitandani. Hivyo anatakiwa uangalizi wa karibu sana, kama kuna uwezekano aajiliwe mtu kwa kazi hii ili kumpumzisha mama yangu hapa kwani namhurumia amefanya kazi kubwa usiku na mchana kwa ajili ya kumwangalia mwanaye japo nilimsaidia bado muda wote alikuwa halali.
“Mgonjwa ataendelea kupata huduma ya kuchuliwa kila siku mwili mzima ili kusisimua misuli ya mwili. Nina imani kwa uwezo wa Mungu anaweza kupata nafuu upesi kwa vile mwisho wa akili ya mwanadamu ndipo uwezo wa Mungu huchukua nafasi yake,” dakta Mariamu Shaka aliwapa moyo kwa maneno ya hekima.
“Nina imani mpaka leo yupo hivi lazima turudishe shukrani zangu kwa Mungu wetu,”mama Colin alisema.
“Kingine mama, huoni maajabu pamoja na mwili kukosa mawasiliano lakini vitu vyote vya ndani vinafanya kazi hata kuweza kula japo chakula laini kitu ambacho kimewashangaza hata madaktari bingwa.”
“Ni kweli tuna kila sababu ya kumshukuru alichotupa si haba, kama leo katupa kidogo na kurudisha shukurani kwake basi hatasita kutupa kikubwa nina imani mwanangu siku moja atasimama,” alisema mama Cecy kwa hisia kali.
“Amina, Mungu wetu ni msikivu,” alijibu dokta Mariamu.
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda mama Colin aliaga kurudi nyumbani na kumwacha mama Cecy mgonjwa na daktari ambaye alilala pale ili kesho yake baada ya kumpatia mgonjwa huduma arudi nyumbani kwake.
Kutokana na hali aliyomuona nayo Cecy hakutaka kumweleza mwanaye kwa kujua atamshtua hata kukosa raha na kumuongezea matatizo kwa vile alimpenda sana mchumba wake. Lakini alijiuliza mwanaye akijua lazima atamweleza vibaya, alipanga kumwambia baadaye kuwa Cecy amerudi.
Aliamua kukaa kimya huku wiki ilikatika bila kumweleza kitu chochote mwanaye juu ya Cecy kurudi toka India. Siku zote alitoka peke yake kwenda kumwona Cecy na kuonesha kugushwa na hali ile huku akimlipa daktari aliyekwenda naye India pesa nyingi ili kumpatia huduma ya kumchua na kumwangalia kila siku baada ya kazi.
Wema wake ulikuwa wa mamba wa kutoka machozi lakini alikuwa na siri moyoni mwake kujionesha anamjali mgonjwa. Lakini aliamini kupona kwa Cecy ni ndoto, kila alipoulizwa na mama Cecy kuhusu hali ya Colin alisema hajambo kiasi.
“Hawezi kutembea?”
“Mmh! Kwa sasa amekatazwa kutembea.”
“Kwa nini basi usimlete aje amwone mchumba wake?”
“Atakuja hali yake ikitulia.”
“Kwa hiyo hali yake inaonekana bado.”
“Ni kweli.”
“Mmh! Mpe pole isingekuwa hali ya Cecy ningekuja kumwona mkwe wangu.”
“Mungu atawapa afya na kuweza kunyanyuka.”
“Mungu atasikia dua zetu, kila jambo la heri Mungu ulishika mkono nina imani Cecy na Colin watasimama na siku moja kusherehekea harusi yao.”
“Amen,” mama Colin aliitikia huku moyoni akijisemea “Labda harusi aliyosema mwanaye ya kufunga ndoa na maiti ya Cecy, lakini harusi ya sherehe ukumbuni itakuwa muujiza.”
Mama Cecy aliamini hali ya Colin ni mbaya ila mama yake anampa moyo, alipanga siku akipata nafasi afike kumwona kwani haikuwa vizuri mzazi mwenzie kuja kumuona mwanaye na yeye kutokwenda kumuona Colin. Kwa vile hali ya mwanaye alijua alipanga siku moja baada ya kumpatia chakula akilala atoke mara moja kwenda kumwona Colin na kuwahi kurudi.
Siku ya tatu ambayo mama Colin alipiga simu kuwa hatakwenda kwa vile kuna sehemu ambapo angerudi usiku. Siku hiyo mama Cecy aliitumia kumwandaa Cecy ambaye alishangaa kuona mabadiliko madogo baadhi ya sehemu kupata joto kama miguuni ambako kulikuwa na ubalidi kwa muda mrefu.
Baada ya kumpatia chakula chepesi na dawa alimwacha apumzike na yeye kukodi gari mpaka kwa mama Colin kumjulia hali mgonjwa. Wakati huo Mage alikuwa akiendelea kuwa karibu na Colin ili kujivuta karibu kwa kuamini baada ya kifo cha Cecy basi nafasi ile ni yake.
“Colin nina imani sasa hivi afya yako ni nzuri unaweza hata kuendesha gari.”
“Namshukuru Mungu, pia nashukuru kwa msaada wako kwangu kwa muda wote wa kuniangalia.”
”Usijali nipo kwa ajili yako, nitapigania afya yako hata kwa gharama yoyote.”
“Usiwe na wasi nina imani sasa hivi sijambo na wiki ijayo nitakwenda India kumwangalia Cecy.”
“Lakini hali yako si bado kwa nini usisubiri upone kabisa.”
“Mage, mimi sijambo sasa hivi naweza kufanya lolote, lakini afya ya mpenzi wangu siijui. Mpaka leo bado yupo hospitali huenda yupo kwenye hali mbaya lazima niende nikajue hali yake.”
“Mmh! Sawa,” Mage aliogopa kutia neno kwa kuhofia kukorofishana na Colin ambaye alionekana bado ana mapenzi mazito na Cecy. Alijua msimamo wake ni kwa vile hajamwona lakini akimwona hali yake aliamini lazima angebadili mawazo na nafasi ile kumpa yeye.
Wakiwa katika ya mazungumzo walishtuliwa na hodi, waliponyanyua macho Colin hakuamini kumwona mama Cecy aliyejua yupo India na mpenzi wake, lakini afya yake ilioneka imedhoofu sana.
“Ha! Mama ni wewe?” Colin alisema huku akinyanyuka na kwenda kumpokea mama mkwe.
“Ni mimi mwanangu, unaendeleaje na wewe?”
“Namshukuru Mungu, hali yangu sijambo. Sasa hivi nilikuwa nasema wiki ijayo nakuja India kumwona mchumba wangu. Ha..ha..lafu mbona uko huku Cecy umemwacha na nani hospitali?”
“Kwani mama yako hajakwambia?”
“Kuhusu nini?”
“Kurudi kwetu, nimemuulizia ameniambia hali yako bado si nzuri, hivyo nikaona nije nikujulie hali baba yangu na kumwacha mchumba wako na msichana wa kazi.”
“Mama unataka kuniambia Cecy yupo Tanzania?” Colin alishtuka huku macho yamemtoka pima.
“Colin unauliza ukweli au unatania?”
“Mama mimi na wewe hutujawahi kutaniana, hata muulize Mage muda si mrefu nilikuwa namwambia lazima nije India kumjulia mchumba wangu hali yake baada ya mimi kuamini nimepona.”
“Siamini unachokisema najua unaumwa hivyo hukuwa na uwezo wa kuja kumpokea mchumba wako, lakini sikubali kauli yako kuwa huna taarifa yoyote kuwa mimi na Cecy tupo nchini kwa wiki sasa.”
“Wiki!?” Colin alishtuka.
“Colin hebu acha kujitoa akili, ina maana mama yako hajakwambia?”
“Hajaniambia, ina maana mama anajua?”
“Mbona ndiye aliyetupokea na kila siku lazima afike kumuona mgonjwa kasoro leo.”
“Mmh! Una maanisha mama yangu, mama Colin?”
“Ndiye huyohuyo, ina maana hajakwambia?”
“Haki ya Mungu sijui kitu, sikuwa ugonjwa wa kushindwa kuja kumpokea mpenzi wangu, kwa nini mama kanificha hivi, Cecy mpenzi wangu atanielewa vipi?” Colin alisema kwa uchungu.
“Sijui, labda muda wake wa kukueleza bado, lakini namshukuru sana amejitolea kwa hali na mali ili kuhakikisha afya ya mpenzi wako inatengemaa.”
“Vipi hali ya mpenzi wangu?”
“Bado, lakini ana afadhali kwa mbali sana.”
Colin alinyanyuka na kumwomba mama Cecy aende akamwone mpenzi wake.
“Mama naomba nikamwone mpenzi wangu.”
“Colin pumzika kwanza hujapona vizuri, nilikuja kukuona tu.”
“Hapana...kama Cecy ana wiki hapa mama kanitendea unyama mkubwa sana,” Colin alisema huku akionekana kuchanganywa na taarifa zile ambazo hakutegemea kusikia kwa kuamini Cecy bado yupo India.
Colin hakusema kitu alikwenda ndani na kuchukua ufunguo wa gari na kutoka.
“Mama naomba twende,” Colin alipagawa na kusahau muda mfupi alikuwa na Mage alitoka bila hata kumuaga na kumfanya Mage aumie moyoni kuona ana kazi kubwa ya kuubadili moyo wa Colin. Lakini aliamini kifo cha Cecy ndiyo tiketi yake ya kuwa na Colin, aliendeleza dua za kuomba kifo cha Cecy.
Colin japo alikuwa hajaruhusiwa kuendesha gari alikwenda kuchukua gari na kumwomba mama Cecy waondoke. Waliongozana hadi kwenye gari na kuondoka kuelekea kwa Cecy. Wakiwa ndani ya gari Colin alimdodosa mama Cecy.
“Mama kwanza vipi hali ya mchumba wangu?”
“Hajambo, lakini bado.”
“Bado nini kinamsubua?”
“Siwezi kukueleza kwa vile unakwenda mwenyewe kila kitu utakiona.”
“Mmh! Sawa.”
Colin aliendesha gari huku akiwa na mawazo mengi juu ya mama yake kukaa kimya huku kila siku anakwenda kumwona mgonjwa bila kumwambia aljiuliza alikuwa na maana gani na mchumba wake angemwelewa vipi kama amerudi bila kwenda kumwona.
Walipofika walikwenda hadi ndani, Colin alionekana mwenye kimuhemuhe cha kumwona mpenzi wake. Kwa vile alikuwa akikijua chumba cha Cecy aliingia moja kwa moja. Lakini chumbani kwake hakuwemo alitoka na kukutana na mama Cecy.
“Mama mpenzi wangu yupo wapi?” Colin aliuliza macho yamemtoka pima na presha juu.
Itaendelea

No comments