Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 9


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Cecy nitakutafuta tuzungumze akili yako ikitulia.”
“Usijisumbue.”
“Lazima nijisumbue kwako kwa vile kuna kitu ndani yako nilichokiona.”
“Colin niache nirudi nyumbani.”
“Unakaa wapi nikupeleke.”
“Colin unataka mama yako aje kuchoka pagala letu, aliona picha ikawa vile vipi anione kwenye gari lako?”
“Hawezi, na ungeniambia alichokifanya ningempa ukweli, tabu ya kina mama wa kiswahili wazungu hawajali vitu vya kijingakijinga.”
“We nenda tu.”
SASA ENDELEA...
Colin alimbembeleza sana Cecy, kwa vile naye alikuwa akimpenda akiingia kwenye gari na kurudishwa nyumbani kwao. Walipomfikisha Colin naye aliteremka na kuongozana hadi kwa kina Cecy ambako kulikuwa na nyumba ya vyumba viwili na sebule. Lakini nyumba ilikuwa ya hali ya chini bati zake zilikuwa na kutu na juu waliweka mawe ili kuzuia bati lisiezuliwe na upepo.
Cecy baada ya kufika eneo la kwao alishukuru na kuanza kuelekea nyumbani, lakini Colin alimsemesha.
“Cecy mbona unaniacha mgeni?”
“Colin nashukuru umenileta, lakini naomba usifike nyumbani.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Nimekueleza mara ngapi kuhusu mama yangu, unataka mama yako aje akitie moto kibanda chetu.”
“Cecy suala la kuhusu mama yangu niachenie mimi, naomba nimsalimie mama mara moja.”
“Mmh! Sawa.”
Waliongozana Cecy na Colin hadi nyumbani kwao ambako alitambulishwa kwa mama yake na kumfanya mama Cecy ashtuke.
“Ha! Wewe ndiye unayenyanyasa mwanangu?”
“Kumnyanyasa kivipi mama?”
Mama Cecy alimweleza mateso yote ya mwanaye juu yake na jinsi mama yake alivyokwenda kuwatukana huku akitishia maisha ya Cecy kama ataharibu ndoa yake na Mage. Colin baada ya kusikilia maneno yale aliyarudia maneno ya Cecy juu ya mapenzi yake kwake.
Ashangaa kuona penzi la Cecy kwake lilikuwa wazi kwa mama yake lakini mhusika mkuu alikuwa hajui kitu zaidi ya kumuona Cecy kama msichana mzuri lakini hakuwa na uwezo wa kumtamkia chochote kutokana na mama yake kumtafutia mwanamke aoe ambaye kwa upande wake aliungana na uchaguzi wa mama yake.
“Mzazi wangu, kwanza niwaombeni radhi kwa yote yaliyotokea kwa mama yangu kuja kuwatukana bila sababu. Naweza kusema labda makosa nimefanya mimi kwa kutomjulisha nini nilichotaka kukifanya na Cecy.
“Najua mama yangu alimpenda Cecy lakini si kuwa mke wa mwanaye bali msichana mzuri anayejiheshimu. Inawezekana kigezo cha elimu ndicho kilichomfanya mama yangu amtafute Mage, nina imani kama Cecy angekuwa na elimu kama ya Mage basi angekuwa chaguo la kwanza la mama.
“ Wasiwasi mkubwa wa mama ilianzia siku alipomuona Cecy kapendeza naweza kusema aliwashinda wote waliokuwa kwenye sherehe yangu. Kilichomshtua mama yangu kunikuta na picha ya Cecy aliyokuwa amependeza sana. Aliamini kabisa ni mpenzi wangu hivyo kujihami kabla mambo hayajaharibika kutokana na harusi yetu kuandaliwa kwa fedha nyingi sana.
“Lakini hakutakiwa kuchukua uamuzi aliochukua bila kuniuliza mimi japokuwa nilimweleza sababu ya kuwa na picha ile. Ila napenda kuwaeleza kitu kimoja kuwa sitauacha upendo wa Cecy upitee hivihivi najitolea kumsomesha ili aongeze elimu na ujuzi.
Baada ya elimu hiyo nitafanya naye kazi ndani na nje ya nchi ambayo naamini itamweka katika maisha mazuri na ramani ya dunia. Pia nitahakikisha naijenga nyumba yenu katika hadhi ya kisasa pia mama nitakufungulia mradi ili muendeshe maisha yenu,” Colin alieleza nia yake nzuri kwa Cecy na mama yake.
“Asante bab..”
“Mama nani kamwambia sisi tuna shida ya vitu hivyo? Kama kilichonitesa nimekikosa, sihitaji kitu kingine toka kwako,” Cecy alimkatisha mama yake na kumjia juu Colin kwa kauli yake.
“Cecy mimi na wewe nani mwenye kosa, ulilolisema leo ungelisema mapema situngefika huku,” Colin alijitetea.
“Muongo! Colin hata ningesema ingekuwa sawa na kazi bure kwa vile tayari mama yako aliisha kuchagulia mwanamke,” Cecy alisema kwa hisia kali.
“Kabla ya kutoa uamuzi ningechagua.”
“Mimi na Mage unampenda nani?”
“Nawapenda wote, ila kwa sasa Mage kwa vile ndiye tupo katika mipango ya ndoa.”
“Kwa kauli hiyo naomba tukomane kila mtu ashike hamsini zake ukinikuta njiani nipite kama nguzo ya umeme,” Cecy alisema kwa hasira.
“Cecy kuwa na adabu, heshimu anachokisema mwenzako...Baba kama una nia hiyo ifanye faida hataiona leo, lakini baadaye atakushukuru.”
“Sawa mama nimekuelewa, Cecy punguza hasira nina nia nzuri na wewe, uzuri wako nitaulinda na baadaye utakuingia fedha nyingi na kumsaidia mama. Utauza ndizi mpaka lini?”
Cecy hakujibu kitu aliinama chini, Colin alimsogelea na kumbembeleza kitu kilichomfanya Cecy aangue kilio na kusema:
“Colin nisamehe kwa yote, hujui kiasi gani penzi lako lilivyouathiri moyo wangu, najua nilikupenda bila kushauriana na moyo wangu. Mnaweza kuniona mdogo lakini nami nina hisia za mapenzi kama wengine,” Cecy alisema huku akimtazama Colin kwa macho yaliyojaa machozi.
“Najua Cecy, isingekuwa mipango ya harusi ningeza kufanya chochote ili ujue nauthamini upendo wako.”
“Sawa Colin nimekuelewa.”
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda Colin aliaga kuwahi nyumbani baada ya kuondoka bila kuaga. Alikwenda kwenye gari na kuwaletea laki moja, walimshukuru naye aliondoka kuelekea nyumbani. Njiani alijikuta akimuwaza Cecy msichana mdogo lakini alikuwa jasiri kuzielezea hisia zake japo aliamini mama yake asingemkubali kutokana na uduni wa maisha na kukosa elimu.
Kwa upande mwingine aliamini kabisa kutokana na kasi ya mabadiliko duniani Mage ndiye mwanamke sahihi kwake. Kwani aliamini maisha ni zaidi ya mapenzi kwa vile maisha yakiwa vizuri kila kitu kinakwenda. Aliamini kwa umbile adimu la Cecy angeweza kuifanya kazi yake vizuri ya maonesho ya mavazi.
Kitu kikubwa aliamini Cecy kama atapata twisheni ya kingereza ataweza kuongeza uwezo wake hata kusafiri nchi za nje kufanya kazi ya maonesho ya mavazi pia kupata tenda ya kupamba majarida. Aliamini akimtumia vizuri Cecy kampuni yake itafika mbali na yeye kujitengezea kipato kikubwa.
Alipanga kuwekeza fedha nyingi kwa Cecy baadaye angevuna fedha nyingi kwa kuamini alikuwa na kitu cha ziada ambacho wasichana wengi hawakuwa nacho. Japokuwa alikuwa na wasiwasi na kikwazo cha mama yake, lakini kwa vile yupo kikazi alijua mama yake angemuelewa tu.
Alipanga ndani ya wiki mbili nyumba ya kisasa ya kina Cecy iwe imesimama huku akimtafutia twisheni nzuri ili kuijua lugha haraka. Alipanga kufungua duka mbele ya nyumba yao ambalo litawafanya waingize kipato kila siku. Kutokana na kuzama kwenye mawazo ya kumuwaza Cecy alijikuta akimsahau Mage mpaka alipofika kwao.
***
Alipoingia ndani alikutana na mama yake ambaye alishangaa kumuona mwanaye akiteremka kwenye gari.
“Colin unatoka wapi?”
Colin ilibidi amweleze mama yake kilichotokea, baada ya kumsikiliza alimuuliza:
“Colin mwanangu umemfanya nini mtoto wa watu?”
“Mama sijamfanya kitu chochote kama nilivyokueleza.”
“Mage si mjinga kulia tu na kukataa kuzungumza na wewe wakati mlikuwa pamoja?”
“Yaani sijui kitu labda uulize wewe utapata jibu.”
“Nitauliza, lakini Colin kuna kitu unanificha haiwezekani Mage aondoke bila kukuaga kisha akatae kuzungumza na wewe wakati usiku mmelala pamoja?”
“Mama piga simu uulize labda utagundua kitu.”
“Mmh! Sasa nimepata jibu,” mama Colin alisema huku akitikisa kichwa kama kakumbuka kitu.
“Jibu gani?”
“Colin lazima kuna kitu Mage amegundua kuhusu wewe na Cecy, nasema hivi ndoa ikivunjika Cecy atanitambua.”
“Mama unamuonea bure mtoto wa watu, toka siku ile ya sherehe sijaonana na Cecy,” Colin alidanganya.
“Muongo umemkataza asilete ndizi ili mkutane sehemu nyingine. Colin Mage akinieleza kuwa amegundua una uhusiano na msichana mwingine pagala lao nakwenda kulitia moto sasa hivi.”
“Mama kwa nini unanihukumu kwa kosa nisilofanya, nimekueleza piga simu uulize unaanza kutengeneza mawazo yako. Cecy amekukosea nini mpaka kumchukuia hivyo, ni wewe ndiye uliyekuwa naye karibu?”
Mama Colin hakusema kitu aliingia ndani kuchukua simu ili ampigie Mage kujua amepatwa na nini.
***
Baada ya Colin kuondoka mama Mage alimfuata mwanaye chumbani aliyekuwa amezama kwenye dimbwi la mawazo juu ya hali ya Hans na familia yake ilivyomtenga na kumuona kama kinyesi. Moyo ulimuuma na kujua hakukuwa na haja ya yeye kwenda hospitali pia kumuacha mchumba wake mumewe mtarajiwa akiwa amelala na kuondoka bila kumuaga.
Alijilaumu kwa kitendo chake cha kumpita Colin bila kumsemesha, alijiuliza atamfikiliaje. Alijiuliza ndoa yake ikivunjia na ijulikane sababu ya Hans mwanaume asiye na mapenzi naye ataiweka wapi sura yake. Lakini alijiuliza angesimama na kuzungumza na Colin angemwambia anatoka wapi na kwa nini hakumuaga?
Akiwa katika dimbwi la mawazo mama yake aliingia na kumkuta amezilaza chali huku ameukumbatia mto wake na wacho yake alikuwa akiangalia darini.
“Mage..Mage.”
“A..a..bee.”
“Mbona sikuelewi mwanangu?”
“Mama nahitaji msaada wako najua nimechanganya madawa.”
“Nikusaidie nini?”
“Sijui Colin atanielewaje maana nilichomfanyia si kitu kizuri.”
“Kwa kweli hatua tuliyofikia huku vikao vikienda vizuri halafu mwenzako abadili uamuzi sijui sura zetu tutaziweka wapi?”
“Hapo ndipo ninapochanganyikiwa, mama kitendo walionifanyia familia ya kina Hans sitawasahau.”
“Umeona eeh, nilikueleza toka zamani familia ile ilikuwa haikupendi kama ungeolewa na Hans ndoa yako isingedumu. Mungu amekuletea mwanaume wa maisha yako unamchanganya.”
“Mama nimeisha fanya kosa naomba msaada wako, nitamweleza nini Colin anielewe.”
“Wala usiwe na wasi kamwambie kuwa ulimtuma Brenda cheni ambayo ulipanga kumpatia kama surprise umekuta hajaitengeneza na kujikuta umekasirika na kuanza kulia.”
“Mmh! Atanielewa? Naona kama utetezi mwepesi.”
“Walaa, ye anajua ulikuwa kwa Brenda, nilimwambia kuna kitu mmeshindwa kuelewana ndiyo maana ulirudi katika hali ile.”
“Mmh! Basi ngoja nifanye hivyo.”
Wakiwa katikati ya mazungumzo simu ya iliita ilikuwa ikitoka kwa mama Colin.
“Mkweo,” mama Mage alisema.
“Mmh! Lazima ataulizia kilichotokea.”
“Ngoja nimsikilize,” alisema huku akibofya cha kupolelea na kuweka simu sauti ya nje.
“Haloo mama Colin.”
“Eeh! Dada kuna nini huko?”
“Kwani vipi?”
“Naona Colin ananichanyanyia maneno wala simuelewi.”
“Wala hakuna kitu cha kutisha bali mkweo aliudhiwa na shoga yake, lakini kwa sasa yupo sawa na wakati wowote atakuja huko.”
“Mmh! Afadhali maana nilikuwa na wasiwasi.”
“Wa nini?”
“Nilijua Colin kisha mtibua mkwe wangu.”
“Walaa, sema mkweo ana hasira za kitoto kitu kidogo analia kama kafiwa.”
“Basi nikuacheni muendelee na mambo mengine.”
Baada ya simu kukatwa mama Mage alimgeukia mwanaye na kumwambia.
“Unaona ulivyotaka kumsababishia matatizo mwenzako?”
“Mama lazima niende sasa hivi najua mpenzi wangu hayupo kwenye hali nzuri.”
“Fanya hivyo na...” mama Mage alinyamaza baada ya mlango kugongwa.
“Unasemaje?” aliuliza kwa sauti.
“Kuna wageni.”
“Nakuja,” mama Mage alitoka nje kwenda kumsikiliza mgeni.
Alitoka hadi getini na kukutana wa wanaume wawili na mwanamke mmoja, aliwatazama walikuwa wageni kwake.
“Karibuni.”
“Asante.”
Aliwakaribisha hadi sebuleni, baada ya kuketi mama Mage alitaka kujua wana shida gani.
“Ndiyo jamani mna shida gani?”
“Sisi ni maafisa wa polisi,” walitoa vitambulisho vyao.
“Ndiyo, mna shida gani?”
“Tuna imani hapa ndipo anaishi Magreth Chogo.”
“Ndiyo.”
“Yupo?”
“Mna shida gani?”
Kabla hajajibu Mage alitoka chumbani ili awaone wageni ni kina nani, askari mmoja baada ya kumuona alijua ni Mage alibahatisha kwa kumwita jina.
“Mage.”
“Abee.”
“Upo chini ya ulinzi,” alisema askari wa kike.
“He! Kwa kosa gani?” Mage alishtuka.
“Kutokana na tukio lililomtokea mpenzi wako wa zamani.”
INAENDELEA HAPA

No comments