Header Ads

KABLA SIJAFA, DUNIA INISAMEHE-7


Taarifa za kifo cha chifu Onuku kwa ajali ya gari kilichotokea nchini Cambodia kiliwasikitisha watu wengi sana na masikini wengi nchini humo walishindwa kuelewa kama kweli angepatikana mtu mwingine ambaye angewajali wananchi wa Nigeria kama alivyokuwa chifu Onuku, Nigeria nzima ililia na hata viongozi wa serikali walisikitika nchi hiyo ilikuwa imepoteza mtu mashuhuri kwa maendeleo ya nchi hiyo.
Kitu kingine kilichowasikitisha zaidi wananchi wa Nigeria ambacho kiliwafanya baadhi yao kuhisi ajali iliyotokea ilikuwa ya kupangwa ni taarifa za kusakwa kwa chifu Onuku aliyekuwa akitakiwa nchini Uingereza kujibu mashtaka ya mauaji ya halaiki, walishindwa kuelewa ni lini chifu aliua watu mpaka asakwe ili kufikishwa mbele ya sheria.
Watu wengi walihisi zilikuwa ni njama za maadui wake kibiashara waliokuwa na nia ya kumnyang’anya visima vyake vya mafuta.
Mengi yalisema lakini hakuna aliyekuwa na jibu sahihi la maswali yao na walipojaribu kumuuliza mkewe juu ya ajali ya mumewe, alilia ili kuudanganya umma wa wananigeria kuwa chifu Onuku hakuwa hai na ndiye mtu aliyekuwa akiishi naye ndani kwa wakati huo akiwa amebadili sura yake.
Pamoja na kuujua ukweli kuwa mume wake hakufa kila siku ya jumapili asubuhi, alikuchukua maua na kwenda nayo kaburini kulipamba kaburi ambalo watu wengi waliamini lilikuwa la mumewe! Hakutaka mtu mwingine ajue kuwa mwanaume alikuwepo ndani ya nyumba yake alikuwa Chifu Onuku katika sura na sauti tofuati.
Chifu alikuwa amejibadili kiasi cha kutosha na haikuwa rahisi hata kidogo kuamini alikuwa ni chifu Onuku! Kuna kipindi hata yeye mkewe alimtilia mashaka lakini alama pekee ya kovu kubwa lililokuwa kwenye paja la mguu wake wa kulia lilimsaidia kuwa na imani kuwa yule alikuwa mume wake!
*****
Kilichowashangaza wengi nchini Nigeria ni uelewanao ulitokea kati ya mke wa chifu Onuku na mume aliyekuja baada ya kifo cha mumewe! Ingawa mwanamke huyo tayari alikuwa mzee walitembea pamoja, walikula na kulala pamoja na haikuwepo tofauti yoyote na kipindi alipokuwepo mumewe!
Watu wengi na hata ndugu wa chifu Onuku walichukizwa sana na kitendo hicho cha mke wa marehemu na wengi walikitafsiri kama umalaya uliokithiri isingewezekana mwanamke wa Kinigeria kufanya hivyo hata siku moja tena muda mfupi baada ya kifo cha mume! Ilibidi wamsamehe mke wa profesa kwa sababu alikuwa mzungu.
Alishindwa kuwaeleza ukweli kuwa aliyekuwa akiishi naye ndani alikuwa ndiye chifu, alijibadilisha sura ili kujiepusha na maaskari waliokuja nchini Nigeria kumsaka ili akamatwe na kupelekwa Uingereza ambako angeshtakiwa na hatimaye kuuawa! Ili kumlinda mumewe mama huyo alilazimika kuyakubali manyanyaso yote kutoka kwa ndugu na marafiki wa familia yake.
Kwa miezi karibu miwili wapelelezi wa Scortland Yard waliendelea kumtafuta profesa Owo nchini Nigeria bila mafanikio yoyote! Hawakujua mahali alipokuwa akiishi katika jiji la Lagos na hawakujua kama alibadilisha jina! Ingawa walijua ni lazima alikuwemo katika jiji hilo, hakuna mtu hata mmoja kati yao aliyehisi profesa Owo ndiye aliyeitwa chifu Onuku kwa wakati huo, hata waliposoma katika magazeti kuwa tajiri huyo alipata ajali na kufa nchini Cambodia wala hawakutilia mashaka waliendelea na msako wao kama kawaida.
****
Pamoja na utajiri mkubwa aliokuwa nao chifu Onuku kabla ya matatizo kuanza kumpata, unene mkubwa wa mwili wake ulimfanya ashindwe mambo mengi sana, si kukimbia tu bali hata uwezo wake wa kufanya tendo la ndoa pia ulipungua!
Lakini wakati chifu Onuku alinenepa sana, mkewe aliyemzidi umri kwa sababu ya kutumia pombe kali alizidi kukondeana na hivyo kuendelea kuonekana mama wa makamo ingawa alikuwa mzee sana na alijipamba kama wasichana wadogo.
Tofauti yao ya uzito ndiyo iliyopelekea kutoka kwa matatizo katika ndoa yao, wakati chifu Onuku alikuwa mzito mkewe alikuwa mwepesi akitaka tendo la ndoa karibu kila siku, jambo ambalo chifu Onuku hakuliweza kabisa hivyo mkewe pamoja na uzee wake akawa haridhishwi!
Zaidi ya uzito wa mwili wake pia chifu Onuku alifikiria sana biashara zake na kumsahau mke wake, kuna wakati alikesha nyuma ya kompyuta chumbani kwao akihangaika na mahesabu ya biashara zake, huku mke wake akiwa amelala kitandani akijiridhisha mwenyewe na Chifu Onuku hakujali hata kidogo.
Yalikuwa mateso makubwa sana kwa mke wake lakini alishindwa kuondoka kurudi kwao Uingereza, sababu walishazeeshana na mumewe na isitoshe kurudi Uingereza kwa hali aliyokuwa nayo nchini Nigeria ilikuwa ni sawa na kukimbia utajiri!
Hivyo alilazimika kuvumilia na kuendelea kuishi na mumewe lakini kama ilivyo kawaida binadamu wote ambao akikosa jambo Fulani karibu yake hulazimika kulitafutia mahali pengine, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mama yule! Alilazimika kuitafuta raha ya tendo la ndoa nje na kwa sababu ya umri wake mkubwa alizimika kutumia pesa nyingi kuwalaghai vijana wadogo kufanya nao tendo la ndoa, alichagua vijana wenye sura nzuri za kuvutia.
*****
Harrison Kabuye alikuwa ni mfanyabiashara maafuru wa gesi kutoka Uganda na alifuata gesi hiyo nchini Nigeria, alikuwa ni kijana aliyefanikiwa kupata nyingi katika umri mdogo na ni pesa hiyo ndiyo iliyomkutanisha na mke wake Diana mjini Kampala ambaye alikuwa miongoni mwa vijana waliochanjwa na chanjo ya polio miaka mingi kabla.
Harrison na Diana walipendana na kufikia uamuzi wa kufunga ndoa na baadaye kubahatika kupata mtoto mmoja!
Miaka mitatu baada ya ndoa yao Diana aliugua sana na hatimaye kufariki dunia, alikonda sana kabla ya kifo chake jambo lililofanya watu wahisi alikuwa na virusi vya Ukimwi ingawa hakupimwa!
Muda mfupi baada ya kifo cha mkewe Harrison alilazimika kupima afya yake na mwanae, Joe! Wote walikutwa wana vizuri vya Ukimwi na miezi michache baadaye mtoto wake alikufa kwa ugonjwa wa kuharisha, Harrison alibaki peke yake bila mke wala mtoto! Alichanganyikiwa kiasi cha kutosha lakini kwa sababu alikuwa na pesa za kutosha aliamua kuusambaza ugonjwa huo hatari watu wengine hakujali wala kumwogopa Mungu!
Kwa jinsi Harrison alivyokuwa maarufu hapa Tanzania zoezi la kuwaambukiza wengine lilikuwa gumu kwa sababu kila mtu alifahamu kuwa mke wake alikufa kwa ugonjwa huo hivyo alikosa kabisa mtu wa kumuambukiza ikabidi ahamishie ufuska wake Nigeria alikonunua gesi! Huko aliishi hoteli akibadilisha wanawake kama nguo kwa sababu alishakata tamaa ya maisha.
Harrison alikuwa muathirika mwenye afya njema na sura yake ilikuwa nzuri na ya kuvutia kama ilivyokuwa awali! Harrison alikuwa ni miongoni mwa wavulana wenye sura nzuri duniani, hakuna mwanamke ambaye angemwona Harrison na kusema hakumpenda, alikuwa na rangi nzuri ya ngozi na alikuwa mrefu mwenye mwanya, hakuna binadamu yeyote mwenye macho mawili ambaye angeweza kuhisi Harrison alikuwa na virusi vya Ukimwi!
Biashara ya gesi ilizidi kumpa pesa nyingi na kumfanya awe maarufu zaidi nchini Tanzania na Nigeria, lakini watu walimwogopa na jambo hilo lilifanya muda mwingi wa maisha yake awe Nigeria ambako hakufahamika kama Tanzania.
Ni huko Nigeria ndiko alikokutana na mke wa profesa Owo ambaye pamoja na umri wake mkubwa hakupenda kabisa mvulana mzuri apite mbele yake, ili kumtongoza Harrison aliyekuwa mteja wake wa gesi, alimpakilia kontena zima la gesi akauze na kupata pesa.
Aliyafanya yote hayo akitaka kumteka Harrison na kumfanya awe wake siku zote! Kwa sababu ya pesa Harrison hakuwa na kipingamizi, alikubali na baadaye kupangishiwa nyumba nzuri kaskazini mwa jiji la Lagos na mara nyingi chifu mwenye sura ya bandia akiwa safarini mkewe alikwenda kulala kwa Harrison na kufanya naye mapenzi usiku mzima.
Na mume aliporudi kutoka safari walishirikiana nae kama mtu na mke wake ingawa kidogo sana, hatimaye virusi vikawa vimeingia ndani ya nyumba ya profesa Owo au chifu Onuku mtengenezaji wa virusi vya Ukimwi.
*****
Wapelelezi wa Scortland Yard walikaa nchini Nigeria kwa mwaka mzima bila mafanikio ya kumpata profesa Owo, ndipo wakuu wao wa kazi walipoamua kuwarudisha nchini mwao Uingereza, roho iliwauma sana kwa kutotimiza kazi waliyokuwa wamepewa lakini hapakuwa na kitu cha kufanya!
Si kwamba profesa Owo hakuwepo Lagos, alikuwepo na walikutana naye njiani lakini hawakufanikiwa kumgundua kwa sababu alishajibadilisha sura na wao walimtafuta kwa sura ya zamani!
Je nini kitaendelea?
Tutaonana.

No comments