Header Ads

Kessy aivuruga YangaDar es Salaam
UJIO wa beki wa kulia wa Simba, Hassani Kessy ndani ya Yanga umekivuruga kikosi cha kwanza cha timu hiyo kinachonolewa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Kessy anaelezwa kukibadili kikosi hicho kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa watakayoshiriki.
 

Beki huyo, wiki iliyopita alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga akiwa amebakisha wiki mbili mkataba wake umalizike wa kuichezea timu hiyo iliyomsimamisha kwa utovu wa nidhamu baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Toto Africans, Christopher Edward.
Kusaini kwa Kessy Yanga kutaleta ushindani mkubwa kwenye nafasi ya beki wa kulia, kwani tayari yupo Juma Abdul aliye kwenye kiwango cha juu na Mbuyu Twite ambaye pia ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya mbili kikosini.
 

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya benchi la ufundi la Yanga, Pluijm ndiye aliyependekeza Kessy asajiliwe kwa ajili ya msimu ujao ili acheze nafasi ya Abdul beki ya kulia.
Chanzo hicho kilisema, wakati Kessy akicheza beki ya kulia, Abdul yeye atabadilishiwa nafasi na kucheza winga wa kulia inayochezwa na Simon Msuva kutokana na kasi yake ya ushambuliaji na uwezo wake wa kupiga krosi kwenye goli la timu pinzani.
Kiliongeza kuwa, Pluijm ameshawishika kumpendekeza Kessy kwenye usajili wake wa msimu ujao kutokana na ukabaji wa umakini timu inapokuwa haina mpira na uwezo wake wa kupeleka mashambulizi kwenye lango la wapinzani wao.
“Kikubwa benchi la ufundi limepanga kukipanua kikosi, wenyewe wanataka wawe na vikosi viwili vitakavyocheza kwa ushindani mkubwa, hiyo itasaidia kuepuka kumtegemea mchezaji mmoja ndani ya uwanja.
 

“Hivyo, kocha alipendekeza asajiliwe Kessy mara baada ya kupata taarifa kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu na ndiyo maana na mabosi haraka wakamalizana naye ili kuboresha kikosi.
“Kessy amesajiliwa kwa ajili ya kucheza namba mbili (beki ya kulia) na Abdul atahamishwa kucheza namba saba (winga ya kulia) inayochezwa na Msuva, anataka kumchezesha winga kwa ajili ya kuwatengenezea mabao ya vichwa Ngoma (Donald) na Tambwe (Amissi), hiyo ni baada ya kuonyesha kiwango,” kilisema chanzo hicho. 
 

Alipotafutwa Pluijm kuzungumzia hilo alisema: “Siwezi kuzungumzia suala hilo kwa hivi sasa, siwezi kumzungumzia mchezaji ambaye hayupo na sisi kwenye timu.”
 

Aidha alipotafutwa Kessy kuzungumzia hilo, alisema “Mimi ni mchezaji ninayetegemea kuendesha maisha yangu kwa ajili ya soka, kwa upande wangu mimi popote pale nikiambiwa nicheze nacheza wala sina hofu, pia unatakiwa kufahamu kuwa nipo tayari kwa ajili ya mapambano.”

No comments