Header Ads

Lissu ahisi cheo kinampwerepweta AG

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amemhenyesha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, bungeni mpaka kufikia hatua ya kuhoji endapo nafasi hiyo inamtosha ama inampwerepweta.

Hali hiyo ilitokea juzi jioni wakati wa kupitisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, ambapo Lissu alitaka taarifa juu ya Ripoti ya Tume ya Kijaji iliyochunguza majaji waliotuhumiwa kwenye sakata la Akauti ya Tegeta Escrow.
Wakati wa majibizano ya wawili hao, mara kadhaa Masaju alijikuta akishindwa kuzungumza na kiti cha Spika kama kanuni zinavyotaka na badala yake akawa anajibizana na Lissu na wakati mwingine kukatisha maelezo yake kutokana na kujibizana chini chini.
 

Hali hiyo ilifanya mara kadhaa, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson aliyekuwa akiendesha kikao hicho kumtaka Mwanasheria Mkuu kuzungumza na kiti.
Katika hoja yake hiyo, Lissu alisema Chande Othman, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema tume iliyochunguza majaji waliotuhumiwa kwenye sakata la Escrow imemaliza kazi yake na kilichobaki ni kuweka hadharani ripoti yake.
 

Alisema licha ya kauli hiyo, ambayo ilitolewa Desemba mwaka jana, mpaka leo hakuna kilichoonekana.
Wakati Bunge lilipokaa kama kamati, Lissu alipewa nafasi na kusema “Nataka kuzungumzia sera ya nidhamu ya majaji, katika mchango wangu na hotuba ya kambi ya upinzani tumezungumzia tatizo la nidhamu ya majaji.
 

“Tunautaratibu uliowekwa kwenye Katiba juu ya majaji ambao wanatuhumiwa kwa utovu wa maadili, Katiba imezungumzia ambao wanaweza kuondolewa kwa sababu wana tababia mbaya wanatakiwa kuondolewa kwa kuundiwa Tume ya Uchunguzi ya Kijaji.
 

“Tangu mwaka 1991 Jaji Mwakibete alivyoundiwa tume na kuondolewa wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, hakujawa na tume nyingine ya kijaji kuchunguza matatizo ya kinidhamu ya majaji wetu.
 

“Bunge hili limepitisha azimio kwamba majaji hawa ambao ushahidi uliletwa bungeni hapa waundiwe tume ya uchungizi, hatukusema wafukuzwe, hatukusema wafungwe.
 

“Tumesema waundiwe tume ya kijaji kuchunguza maadili yao, leo mwaka na nusu hakuna majibu, kwa hiyo Bunge tulikaa hapa kupoteza muda? Haiwezekani, kwa hiyo naomba na kama maelezo hayakutosheleza kwanini tume ya uchunguzi ya majaji wa ESCROW, Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa, haijaundwa, kama imeundwa ripoti iko wapi, lilikuwa ni azimio la Bunge.
 

“Kama hakuna maelezo ya kutosheleza nitashika shilingi kwenye mshahara wa waziri,” alisema Lissu.
 

Baada ya maelezi hayo, Mwanasheria Masaju alisimama ili kumjibu Lissu, ambapo alirudia baadhi ya maneno aliyozungumza awali wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia kwenye hoja ya wizara hiyo ambapo alitumia muda wote kujibu hozilizokuwa zimetolewa na Lissu asubuhi.
 

“Kwanza mambo haya tuweke wazi, Bunge hili siyo mamlaka ya kinidhamu ya majaji, Katiba iko wazi ibara ya 113, imelieleza vizuri hili, kuna Tume ya Mahakama kama kuna Jaji anatuhumiwa tume hiyo inafanya na kupendekeza kwa rais ndiyo aunde tume endapo ataridhika.
 

“Kwenye hili Bunge siyo mamlaka ya kinidhamu kwa majaji, kwenye maadhimio yale ilishauri tu serikali, sisi hatuwezi tukaa hapa tukajifanya ni majaji, siyo mamlaka sahihi ya majaji, hilo liko wazi lazima tuheshimu.
 

“Kwanza mambo mengine hata haya ya Escrow yapo mahakamani kwa hiyo naomba tufikie mwisho. Hakuna haja ya kuondoa shilingi kwenye mshahara,” alisema.

CHANZO; NIPASHE

No comments