Header Ads

Magufuli kugawa bure sukari iliyofichwaWafanyabiashara wadogo na wananchi wakiwa kwenye foleni kusubiri kununua sukari katika dukla la jumla la Gulamali lililoko majengo mjini Dodoma kutokana na kuhadimika kwa bidhaa hiyo. PICHA: IBRAHIM JOSEPH.


•Kutaifisha sukari na kuigawa bure kwa wananchi haitakuwa mara ya kwanza kwa Rais kufanya jambo kama hilo.....
RAIS John Magufuli ametangaza kutaifisha tani zote za sukari zitakazokamatwa zikiwa zimefichwa na wafanyabishara kwenye maghala na kisha kuzigawa kwa wananchi bure.

Aidha, Rais Magufuli alisema sukari nyingi inayotoka nje ya nchi na kuuzwa kwa bei rahisi nchini, inakuwa imeisha muda wake.
Pamekuwa na uhaba mkubwa wa sukari wa ghafla nchini kiasi cha kuonekana kwa misururu mirefu ya wafanyabiashara wa rejareja wa bidhaa hiyo mjini Dodoma jana, na Kagera kupitisha uamuzi wa kuuza sukari katika madula maalumu tu.
Rais Magufuli alitoa tamko hilo jana, wakati akizungumza na wananchi wa Katesh, Mkoani Manyara alipokuwa safarini kuelekea mkoani Arusha kwa barabara, akitokea Dodoma.
Rais Magufuli alisema baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa ya utajiri wamekuwa wakienda kwenye nchi kama Brazil na kununua sukari kwa bei rahisi na kuja kuilangua.
Kutaifisha sukari na kuigawa bure kwa wananchi haitakuwa mara ya kwanza kwa Rais kufanya jambo kama hilo.
Wakati akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi mwaka 2009, Dk. Magufuli alikamata meli ya Tawaliq 1 ya China ikifanya uvuvi haramu kwenye pwani ya nchi ambapo samaki waliokuwa mwaevuliwa waligawanywa bure kwa taasisi zenye mahitaji.
“Tayari nimeshaagiza vyombo vya dola viwafuatilie wale wote walioficha sukari, hawa ni waujumu uchumi," alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wananchi hao.
"Tutachukua sukari waliyoficha na kuigawa bure maana hawa ni sawa na wahujumu uchumi.”
Rais Magufuli alisema “Kumukewa na tabia ya ajabu ya wafanyabishara kwenda kununua sukari ambayo imeshaisha muda wake wa matumizi kwenye nchi nyingine na kuja kuziuza kwetu.
"Badhi ya nchi humwaga sukari iliyoharibika baharini lakini wafanyabiashara wamekuwa wakichukua na kuiuza nchini kwa bei rahisi na matokeo yake kuwasababishia wananchi kuugua magonjwa mbalimbali.”
Alisema wafanyabishara hao walioficha sukari katika maeneo mbalimbali pia watafungiwa leseni za kufanya biashara nchini.
“Wafanyabiashara wanaocheza na serikali hii, wanacheza na maisha yao. Watoe sukari hiyo waiuze kwa wananchi kama ambavyo walikuwa wamepanga,” alisema Magufuli na kuongeza:
“Kuficha sukari si sawa na kuficha sindano maana tutawabaini tu, Serikali ya Magufuli haiwezi kushindwa kununua sukari hata kama ni mabehewa mangapi.
"Nimeshaongea na Waziri Mkuu, tutaagiza sukari na kuuza kwa bei rahisi na tatizo hili litakwisha.”
Alisema ana taarifa za wafanyabishara walionunua sukari maeneo ya Kilombero zaidi ya tani 3,000 na mwingine eneo la Mbagala tani 4,000 lakini wamezificha. Hakuwataja.
Alisema lengo la wafanyabishara hao ni kuikwamisha serikali na wananchi wakose huduma hiyo ili baadae wailangue kwa bei ya juu.
“Mlinichagua kwa moyo mmoja, endeleeni kuniombea na ninaahidi kuwa sitawaangusha.”
Kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na malalamiko ya sukari kupanda bei kwa kuuzwa kwa Sh. 2,500 hadi 2,800 kutoka kikomo cha bei elekezi ya Sh. 1,800.
Rais Magufuli alipiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi bila ya kuwa na kibali cha serikali mapema mwaka huu ili kuondoa ushindani usio rafiki kwa viwanda vya ndani vya bidhaa hiyo.
Akilihutubia Bunge la 11, April Mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema nchi inahitaji tani 420,000 za sukari kwa mwaka na kwamba uwezo wa viwanda vya ndani umekuwa ni tani 320,000 na hivyo kufanya kuwepo kwa nakisi ya tani 100,000.
Alisema pamoja na mpango huo wa kuagiza sukari kutoka nje, serikali itakuwa macho katika kuhakikisha kuwa sukari inayoruhusiwa kuingia ni ile inayotakiwa na si zaidi.
Lengo la mkakati wa serikali ni kuvifanya viwanda vya ndani kuendelea na uzalishaji hadi kuviwezesha kufikia uwezo wa juu wa kukidhi mahitaji ya nchi, alisema.
Alisema pamoja na upungufu uliopo, serikali inazo taarifa kwamba sukari iliyopo nchini hivi sasa inafikia tani 37,000, lakini baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakificha waliyonayo ili kusubiri kupanda kwa bei kutokana na upungufu uliopo

No comments