Header Ads

Maneno mabaya, makali ni sumu kwenye Mapenzi!

 ASANTE Mungu kwa kunipigania na kunipa uhai mimi na wasomaji wangu. Pole kwa wale wote waliokutana na misukosuko ya kimaisha kwa wiki iliyopita. Mada ya leo hapa jamvini inahusu maneno ambayo ni makali, mabaya na ya kudhalilisha ambayo matumizi yake ni sumu kali kwenye uhusiano wowote wa kimapenzi, iwe kwa wapenzi, wachumba na hasa wanandoa. 

Mara nyingi wapenzi wamekuwa wakiyaona maneno hayo ni ya kawaida bila kujua au wengine wakijua kuwa ni sumu katika mapenzi. Mara nyingi maneno haya hutolewa wakati wapenzi wanapokuwa wamechukizana au kukwaruzana ndiyo maana nakushauri usifanye uamuzi wowote ukiwa na hasira kwani hasira ni hasara.

NIANZE NA WANAUME 

Katika utamaduni wa jamii nyingi za Kiafrika, mwanaume ndiye hupaswa kumuomba uhusiano wa kimapenzi mwanamke na kama wataridhiana basi mwanamke hana budi kuwaacha wazazi wake na kuambatana na mwanaume. Inapotokea hivyo ni dhahiri kabisa kuwa mwanamke ataondoka na vitu vichache kutoka kwao, mathalan begi au mabegi ya nguo na si rahisi kuondoka na vitu vingine kwa sababu anakwenda kuanza maisha mapya. Maisha ambayo yanamtenga na familia au ukoo wake kwa muda hadi pale tu atakapopata ridhaa ya mumewe kwenda kusalimia kwao.

NILICHOKIGUNDUA 

Katika maisha ya wawili waliopendana, wakaamua kuwa kitu kimoja na kuishi pamoja, kila wanapokwazana maneno anayoyatoa mwanaume ni yenye karaha, dhihaka na manyanyaso ndani yake. Si ajabu ukasikia mwanaume anamwambia mkewe ‘hapa ni kwangu hukuja na kitu hata kimoja kutoka kwenu, ni hako kabegi kako tu ulikokuja nako’. Ni maneno ambayo mwanaume anamwambia mkewe ambaye alimpenda ndiyo maana akamchagua kuishi naye, mwanamke aliyemnyima usingizi na kumtesa kutokana na misimamo yake, leo anamnyanyasa na kumtupia nguo nje.

 Kweli hii ni haki? Kwa nini unamshusha thamani mke au mpenzi wako uliyempenda mwenyewe? Unamzalisha na kila mkikwaruzana unamtimua. Nini faida yake kama mwanamke, iwapo utamtusi kwa maneno yenye shombo, haipendezi kiukweli. Kimsingi ni maneno hayo ya kuwa ‘hapa huna kitu au hukuja na kitu’ huwatia uchungu wanawake wengi kwani ni maneno yanayowanyong’onyesha na kuwafanya wajione wao ni kama tu viwanda vya kuzalisha watoto, jambo ambalo si sawa. Kikubwa mwanaume anapaswa kuwa mstaarabu hasa anapokosana na mwenza wake. 

Ni lazima awe na uwezo wa kujichunga kutumia maneno ambayo hapaswi kumwambia kwani yanaweza kumkaa kwenye mtima wake kwa muda mrefu na pengine yakatengeneza ufa mkubwa ndani ya moyo wake, ufa ambao ni vigumu wewe kuuona kwa macho lakini ni wenye kuteteresha kwa kiasi fulani sehemu ya uhusiano au familia yako kwani mwenzako unakuwa umempa shaka ndani yake. Anaanza kupoteza imani na wewe. 

Anaanza kuona huthamini uwepo wake. Mpenzi msomaji tukutane wiki ijayo kwa sehemu ya pili ya mada hii ambapo nitazungumzia maneno makali ya mwanamke kwa mwanaume ambayo yanaweza kuvunja ndoa, uchumba na hata kusababisha mauaji na kadhalika. Kwa elimu na mjadala zaidi usikose kutembea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mitandao ya Kijamii ya Facebook na Insta:mimi_na_ uhusiano.

GABRIEL NG’OSHA +255 657 486745

No comments