Header Ads

Manji hii kufuru...Yanga itakuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe FA, basi ishiriki michuano yote ya Caf


Saleh Ally,
Dar es Salaam
NAMNA hali inavyokwenda, hakuna ubishi Yanga itakuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara lakini mwenyekiti wake, Yusuf Mehbub Manji ameweka malengo yake na huenda ikawa rekodi mpya katika soka duniani.
 

Manji anataka kama Yanga itakuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara na bingwa wa Kombe FA, basi ishiriki michuano yote ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
 

Katika mahojiano maalum na Championi Jumamosi, Manji anasema wakiwa mabingwa wa Bara na FA, hawataiachia hata nafasi moja kwa kuwa wanataka kushiriki michuano yote miwili kwa kuwa uwezo wa kufanya hivyo wanao.
 

Manji amesema Yanga wamenuia kuweka rekodi mpya kwa kujifunza mengi. Hivyo wanapambana na Wanayanga wawaunge mkono na wapenda michezo washirikiane nao katika kuiwakilisha Tanzania vizuri.
 

Championi: Nafikiri ingekuwa vizuri kama ni mabingwa wa Bara na Kombe la FA mchague aina moja ya mashindano Afrika, unaonaje?
 

Manji: Kwa nini tuchague na tuna uwezo wa kushiriki yote!
Championi: Kushiriki michuano yote kwa wakati mmoja, huoni itakuwa tatizo kwenu?
 

Manji: Hakuna tatizo, tuna uwezo wa kusajili vizuri. Watakuwa wachezaji 30 imara na tutagawanya timu mbili. Mfano moja isafiri kwenda Ligi ya Mabingwa na nyingine inabaki kucheza Kombe la Shirikisho au inasafiri pia.
Championi: Lakini umesikia, kama ni bingwa Bara na FA, basi lazima mtoe nafasi kwa mshindi mwingine wa pili aende kuliwakilisha taifa.
 

Manji: Hakuna kanuni inayotulazimisha kufanya hivyo, hapa waangalie kama tuna uwezo au hatuna. Sisi tunajiamini na tunataka kushiriki michuano yote. 

Hivyo tukiwa mabingwa, watuamini na sisi tutaonyesha mfano na kuweka rekodi mpya na kuandika historia si Tanzania tu, bali barani Afrika.
 

Bado suala hilo linakuwa na ugumu kwa kuwa bingwa wa Ligi ya Mabingwa na wa Shirikisho hukutana kucheza Super Cup.
 

Ingawa hilo halijawahi kutokea, lakini bado inaonekana kutakuwa na ugumu kwa Caf kuiruhusu Yanga kufanya hivyo.
 

Kuhusu jambo hilo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lililazimika kutoa ufafanuzi kuwa iwapo bingwa wa Bara atashinda pia taji Kombe la FA, ndiye atayeiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2016/17.
 

“Kwa msingi huo, timu ambayo itafungwa katika fainali hizo za Kombe la FA, ndiyo itakayowakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho msimu wa 2016/17,” ilisema sehemu ya taarifa ya TFF jana.
Fainali ya Kombe la FA itachezwa baadaye mwezi ujao, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments