Header Ads

MASTAA WALIOIBUKA NA MOTO WAO!


Na Gladness Mallya
KILA jambo lina wakati na majira yake, hivyo hata katika ulimwengu wa mastaa mbalimbali kuna wakati wanapanda na kuwa gumzo kila kona na kuna wakati mwingine wanashuka na kusahaulika kabisa kwenye midomo na akili za watu.
Kwenye ulimwengu wa sanaa Bongo, mastaa kama Wema Sepetu, Elizabeth Michael, Aunt Ezekiel na wengine wengi walikuwa gumzo kila kona miaka michache iliyopita, lakini kwa sasa nyota zao zimeanza kupoa na watu kuwazoea, maana hawana jipya.

Katika makala haya, tunakuletea orodha ya chipukizi wa kike ambao wameonekana kuja vizuri katika kazi zao.
GIGY MONEY
Gift Stanford ‘Gigy Money’ ni msanii chipukizi anayetumika kama video queen wa muziki wa kizazi kipya, aliyeibuka na kibao cha Lela na Majojorijo.
Mwanadada huyu ameonekana kuwa ni kiboko ya video queen maarufu Bongo, Agnes Gerald ‘Masogange’ kwani ameshirikishwa kwenye video za mastaa mbalimbali wa muziki kwa nyimbo kama Nasema Nawe wa Diamond, Kipi Sijasikia wa Profesa Jay, Shika Adabu Yako wa Nay wa Mitego, Get High wa Godzillah na nyingine nyingi na kumfanya kuwa gumzo kila kona.
Pamoja na hayo, pia ni muigizaji mzuri na amekuwa akishirikishwa kwenye filamu mbalimbali ambazo bado hazijatoka.

LULU DIVA
Video Queen huyu ambaye jina lake halisi ni Lulu Abbas amekuwa gumzo baada ya kufanya vizuri kwenye video ya Ngoma ya Naogopa aliyoimba Barakah Da Prince akishirikiana na Mirror.
Kuanzia hapo mwanadada huyu amekuwa akiitwa na wasanii mbalimbali kwa ajili ya kucheza kwenye video zao ambazo nyingi bado hazijatoka kama ya Christian Bella na nyinginezo.


KIDOA
Ni kama zali hivi kwa video queen huyu anayefahamika kwa jina halisi alilopewa na wazazi wake kama Asha Salum ‘Kidoa’ kwani baada ya kufanya vizuri kwenye video mbalimbali za wasanii wa Bongo Fleva kama Akadumba ya Nay wa Mitego na Shori ya Cyril Kamikaze, alijikuta akishinda taji la Ijumaa Sexiest Girl, linaloendeshwa na Gazeti la Ijumaa mwaka jana na kuongeza umaarufu zaidi.
Licha ya kuwa video queen, pia amecheza filamu mbalimbali ambazo bado hazijaingia sokoni na hivi karibuni alikuwa akicheza filamu za kampuni ya Five Effect, ambayo mkurugenzi wake ni msanii mkongwe nchini, William Mtitu.

MAUA SAMA
Maua Saleh Sama ‘Maua Sama’ ni mmoja kati ya wasanii wa kike wachache sana Bongo wanaofanya muziki wa Reggae/Dance Hall.
Msanii huyu amekuwa gumzo kwa mashabiki na wadau mbalimbali wa muziki kutokana na uwezo wake wa kuimba kuwa juu. Maua anashikilia tuzo ya Kili 2015 aliyoipata kupitia ngoma yake ya Let Them Know.
Maua ambaye alianza kutambulika kupitia Ngoma ya So Crazy akimshirikisha MwanaFA, kwa sasa anatikisa vilivyo kwenye redio na televisheni kupitia ngoma yake ya Mahaba Niue.

 Mwanadada Diana Exavery ‘Malaika’.

MALAIKA
Mwanadada Diana Exavery ‘Malaika’ ambaye anafanya vizuri kwenye muziki wa Bongo Fleva, ni mmoja wa wasanii wanaotikisa kila kona kupitia kazi zake.
Malaika alianza kutambulika kwa mara ya kwanza kupitia Wimbo wa Uswazi Take Away wa Chegge ambapo aliimba kiitikio.
Baada ya hapo aliamua kutoa wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama Mwamtumu kisha Saresare na Zogo ambazo zilidhihirisha uwezo wake.
Malaika ambaye kwa sasa anatamba na Wimbo wa Raruararua ni mmoja wa wasanii wapya wanaofanya vizuri wakiwafunika wazoefu kama Linah, Mwasiti na wengineo.

PAM D
Pamela Daffa ‘Pam D’ ni msanii wa Bongo Fleva ambaye kila kukicha amekuwa akitamkwa midomoni mwa mashabiki wengi wa muziki.
Wimbo wa Nimempata akiwa amemshirikisha Mesen Selekta ndiyo ulimuingiza kwenye chati ya muziki kiasi cha wimbo huo kuwa gumzo katika kumbi mbalimbali za starehe.
Pam D ambaye kwa sasa anabamba na Ngoma ya Popolipopo yupo pia mbioni kuibuka na ujio mpya na Nay wa Mitego.

No comments