Header Ads

Mrithi wa mikoba ya Kitwanga huyu hapa


WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ni moja ya wizara ambazo kwa miaka 55 tangu nchi ipate uhuru, imeongoza kwa kupukutisha mawaziri.
 


RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AKIFANYAKAZI OFISINI KWAKE IKULU JIJINI DAR ES SALAAM.PICHA: NA MAKTABA

Baadhi ya sababu za kuondolewa kwao ni pamoja na matukio ya mauaji ya raia, askari kutesa watu, wafungwa kutoroka gerezani, ujambazi, uzembe na kashfa binafsi za waziri husika.
Tangu mwaka 1961 mpaka sasa, wizara hiyo imeongozwa na mawaziri 26 huku wengine wakimaliza muda wao ama kubadilishwa kwa sababu za kawaida au wengine kufukuzwa kwa sababu mbalimbali.
Miongoni mwa kashfa ni kama iliyomkumba Waziri Charles Kitwanga, aliyedumu kwa miezi sita, kabla ya kufukuzwa kwa sababu ya ulevi na Rais John Magufuli, wiki iliyopita.
Kutokana na kufukuzwa kwake, ambako lugha ya kisiasa inaitwa ‘kutengua uteuzi’, Rais Magufuli sasa anasubiriwa kuteua mtu atakayechukua nafasi ya Kitwanga na tayari kumeanza tetesi na mazungumzo ya sifa za mtu anayefaa kushika wadhifa huo.
SIFA ZA MRITHI WA KITWANGA
Hata hivyo, ili kupata waziri atakayeweza kudumu katika wizara hiyo, baadhi ya wabunge na wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa wanashauri ni vizuri sasa Rais Magufuli akaangalia uwezekano wa kuteua mtu ambaye siye mbunge na kumpa nafasi hiyo na sifa nyingine awe anatoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.
Wamesema ni vizuri nafasi hiyo ikakamatwa na mtu anayejua vizuri mifumo ya vyombo vya ulinzi na usalama inavyofanya kazi.
Kutokana na ukweli kuwa taifa linakabiliwa na changamoto nyingi na hasa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu.
Uhalifu umeshika kasi nchini kutokana na kuongezeka kwa ujambazi, biashara ya dawa za kulevya, utoroshaji wa wanyama hai na nyara za serikali, mauaji ya raia na matukio mengine.
Pia waziri anayekuja anatakiwa kutokuwa mtu mwenye maslahi ya kibiashara na hasa na taasisi za ulinzi na usalama.
Ili kuepusha vyombo vya ulinzi kuingia katika kashfa za rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma na uhalifu.
Pia waziri anayekuja anatakiwa kuwa mwelewa wa historia na siasa ya nchi yetu ili kusimamia amani na utulivu katika nchi yetu na kutojihusisha na mambo yatakayopanda mbegu za hisia za ubaguzi wa dini, rangi, ukabila na itikadi za vyama.
WABUNGE: ANAYEFAA KUONGOZA
Wakihojiwa na Nipashe kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa jana, wabunge wa vyama mbalimbali walitaja sifa ambazo wangependa mrithi wa Kitwanga awe nazo.
PETER MSIGWA
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, alisema atafurahi kuona mrithi wa Kitwanga anateuliwa kutoka nje ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walioko bungeni kwa sasa kwa madai kuwa chama hicho hakina viongozi bora.
"Nafikiri itakuwa vyema atoke nje ya wabunge wa CCM waliopo hapa bungeni. Litakuwa jambo jema ikiwa Rais (John) Magufuli atateua waziri kutoka upinzani kuchukua nafasi ya Kitwanga. Upinzani kuna watu wazuri kama kina (Godbless) Lema," alisema Mchungaji Msigwa.
JOSEPH KAKUNDA
Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, alisema: "Rais ateue mtu yeyote anayekidhi matakwa ya kisheria. Si lazima awe Mbunge wa CCM. Anaweza kutoka hata upinzani, kwa makubalino maalum anaweza kumteua kuwa waziri. Anaweza kuchukua mtu kutoka Chuo Kikuu maana bado anazo nafasi za kuteua wabunge."
JUMA HAMAD OMAR
Mbunge wa Ole (CUF), Juma Hamad Omar, alisema anatarajia kuona mrithi wa Kitwanga anakuwa waziri anayetenda haki kwa wananchi wote bila kuwa na upendeleo kwa baadhi ya makundi, hasa vyama vya siasa.
"Tunatarajia waziri wetu asiwe na upande. Sheria haibagui, tumeshuhudia hivi karibuni vyombo vya dola vimekuwa vikinyanyasa watu ambao ni 'innocent' (hawana hatia)," alisema Omar.
KANGI LUGOLA
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema mrithi wa Kitwanga anapaswa kumsoma Rais Magufuli’ na afuate kasi yake katika kuwahudumia wananchi.
"Awe na moyo wa dhati wa kupambana na wahalifu kwa maana ya majambazi, watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za ulevya.
Pia amsome Rais wetu ni wa aina gani. Awe mtu makini na hodari, asiyeyumba katika kufanya uamuzi. Katika kutumbua majipu, asiwe mwoga na asiyejali cheo wala sifa ya mtu aliyeharibu kazi," alisema.
ESTER BULAYA
Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, alisema mrithi wa Kitwanga ni lazima asiwe mlevi ili kulinda hadhi yake, serikali na Bunge.
ZAINABU MWAMWINDI
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa (CCM), Zainabu Mwamwindi, alisema mrithi wa Kitwanga anapaswa kuwa mwadilifu na anayejiheshimu.
"Tukio lililotokea kwa Kitwanga ni fedheha na aibu si kwa CCM tu, bali kwa taifa zima. Si jambo zuri kwa Mheshimiwa Rais aliyemteua, hivyo mrithi wake lazima azingatie maadili ya kazi yake na awe mtu anayejitambua," alissema Mwamwindi.
UPENDO PENEZA
Mbunge huyu wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza, alisema waziri atakayevaa viatu vya Kitwanga anapaswa kutambua kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni nyeti, hivyo ni lazima awe na mtazamo wa kufanya kitu bora kwa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo likiwamo Jeshi la Polisi na Magereza.
JOSEPH MBILINYI 'SUGU'
Mbunge huyu wa Mbeya Mjini (Chadema), alisema mrithi wa Kitwanga anapaswa kupitia kwenye mchujo wa vyombo vya usalama.
KHATIB SAID HAJI
Mbunge wa Konde, Kaskazini Pemba (CUF), Khatib Said Haji, alisema mrithi wa Kitwanga lazima awe mtu anayejituma na anayeelewa mazingira ya kutunza usalama wa nchi.
"Awe mtu asiyeogopa katika kufanya uamuzi muhimu kwa nchini na mwenye weledi," alisema Haji.
SUSAN LYIMO
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Lyimo, alisema mrithi wa Kitwanga anapaswa kuwa mbunifu na mchapakazi na asiwe na tabia za kupokea na kutoa rushwa.
Mbali na Kitwanga aliyeteuliwa Desemba 10, mwaka jana na uteuzi wake kutenguliwa Mei 20, mwaka huu, mawaziri wengine ambao walihudumu kwa mwaka mmoja ama chini yake nao pia, walitolewa katika nafasi hiyo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mauaji ama kashfa mbalimbali zilizohusu wizara hiyo.
Kutokana na sababu mbalimbali za kubadilishwa kwa mawaziri hao, katika kipindi cha miaka 25 ya Mwalimu Julius Nyerere, wizara hiyo iliongozwa na mawaziri 11, huku watangulizi wake waliomfuata ambao waliongoza kwa miaka 10 kila mmoja, pia walikuwa wakibadilisha mawaziri wa wizara hiyo mara kwa mara.
Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia aliwahi kuhudumu kama waziri wa wizara hiyo kwa mwaka mmoja, katika awamu yake alikuwa na mawaziri watano wa wizara hiyo, Benjamin Mkapa katika awamu tatu alikuwa na mawaziri watatu, Rais Jakaya Kikwete alikuwa wa pili kutoka kwa Nyerere kwa kuwa na mawaziri wengi ambapo alikuwa nao sita.
Safari ya Kikwete ya miaka 10 huenda ikawa kama ya Rais Magufuli ambaye mpaka sasa ikiwa ni miezi saba tangu kuapishwa kwake Novemba 5, mwaka jana, ameshamfuta kazi waziri aliyemteua kuongoza wizara hiyo.
Mbali na Kitwanga, mawaziri wengine ambao wamehudumu kwa mwaka mmoja ama chini ya hapo ni pamoja na Sir George Kahama aliyekuwa waziri wa kwanza wa wizara hiyo chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere mwaka 1961.
Baada ya Kahama, mwaka 1962 Oscar Kambona aliongoza wizara hiyo, Job Lusinde (1966), huku Mwinyi akiongoza kuanzia 1975 hadi 1976, Nalaila Kiula (1990), Ernest Nyanda (1995) na John Chiligati (2006) .
WALIOONGOZA WIZARA HIYO CHINI YA NYERERE
Katika serikali ya awamu ya kwanza, mawaziri walioshika wadhifa wa kuongoza wizara hiyo ni pamoja na Kahama (1961), Kambona (1962), Lawi Sijaona (1963-1965), huku mwaka 1966 akiwa Job Lusinde na mwaka 1967- 1973 ikionozwa na Said Maswanya.
Mwaka 1973-1974, wizara hiyo iliongozwa na Omar Muhaji, Mwinyi (1975-1976) , Hassan Moyo (1977- 1978) , Salim Amor Juma (1979- 1980) , Abdala Natete (1980- 1983) huku mwaka 1983-1985 ikiongozwa na Muhidin Kimario.
CHINI YA MWINYI
Mwinyi aliposhika wizara hiyo aliendelea na Muhidin Kimario kuanzia 1985-1989 na ilipofika 1990, akateuliwa Nalaila Kiula na baadaye mwaka huo huo akateuliwa Augustino Mrema kuiongoza wizara hiyo mpaka 1994 na kumaliza na Ernest Nyanda mpaka 1995 alipong’atuka.
MKAPA
Kuanzia mwaka 1995-1999, wizara hiyo iliongozwa na Ali Ameir Mohamed, Mohamed Seif Hatibu (2000-2002) huku 2003-2005 ikiongozwa na Ramadhan Omar Mapuri
KIKWETE
Rais Kikwete alianza na John Chiligati 2006, na mwaka huo huo wa 2006 mpaka 2008 ikaongozwa na Joseph Mungai, huku Lawrance Masha akiiongoza kuanzia 2008-2010, akafuata Shamsi Vuai Nahonda (2010-2012), kabla ya Emanuel Nchimbi kuiongoza kuanzia 2012-2013 na baadaye Matias Chikawe kushika usukani 2014-2015.
Rais Magufuli tayari amemfukuza kazi waziri wake wa kwanza kwenye wizara hiyo na katika baraza lake la mawaziri, swali linaloumiza wengi kwa sasa ni mtu mwenye sifa gani atashika nafasi hiyo? Je, mpaka anamaliza miaka 10 ni wangapi watakuwa wamepita wizara hiyo?
Kabla ya kashfa ya kuingia bungeni akiwa amelewa, Kitwanga alikuwa akiandamwa na kashfa ya Kampuni ya Infosys ambayo anadaiwa ni mbia wake kuingia mkataba na ile ya Lugumi Enterprises ya kufunga vifaa maalumu vya kuchukua alama za vidole kwenye vituo 108 vya polisi nchini.
Katika mkataba huo wa Sh. bilioni 37, taarifa ya CAG inaonyesha kuwa tayari wabia hao wameshalipwa Sh. bilioni 34, huku ikiwa ni vituo 14 tu ndivyo ambavyo mashine hizo zinafanya kazi na maeneo mengine vikiwa havijafungwa.

CHANZO: NIPASHE

No comments