Header Ads

Mwinyi: Hali ya ulinzi ni shwari

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imebainisha kuwa hali ya ulinzi na usalama wa mipaka yote nchini ikiwemo na ya nchi za jirani ni shwari, lakini kuna tatizo la wizara hiyo kupatiwa fedha pungufu za bajeti.


Aidha, imesema imejizatiti na kuweka mikakati thabiti ya kukabiliana na tatizo la matukio ya ugaidi yanayoendelea katika nchi za jirani, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inadhibiti itikadi zenye misimamo mikali nchini.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2016/17, Waziri Dk Hussein Mwinyi alisema katika mwaka huu wa fedha wa 2015/16, wizara hiyo iliomba kuidhinishiwa Sh trilioni 1.6 kwa ajili ya fedha za matumizi ya kawaida na maendeleo.

Alisema hadi kufikia Machi mwaka huu, wizara hiyo ilipokea jumla ya Sh trilioni moja sawa na asilimia 63.7 ya bajeti na kati ya fedha hizo asilimia 71 ilikwenda kwenye fedha za matumizi ya kawaida na asilimia 18.1 pekee ndio ilikwenda kwenye shughuli za maendeleo.
Alisema katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha wa 2015/16 utekelezaji wa shughuli za maendeleo haukuwa wa kuridhisha kwa baadhi ya mafungu ya maendeleo kwani Wizara ilipata kiasi cha Sh bilioni 41, Ngome ilipata Sh bilioni moja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) halikupata fedha yoyote.

“Hali ya kutengewa bajeti ndogo na kupatiwa fedha pungufu imekuwa ikiathiri utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya jeshi na kusababisha ulimbikizwaji wa madeni hususan ya kimikataba...,” alisisitiza Dk Mwinyi.
Hata hivyo, alisema pamoja na changamoto hiyo, jeshi hilo limeendelea kujizatiti na kulinda mipaka ya nchi ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukabiliana na matukio ya uhalifu yanayotokana na viashiria vya machafuko kutoka nchi jirani.

Alisema hali ya mipaka inayopakana na Tanzania ambayo ni ya Kaskazini, Mashariki, Magharibi na Kusini ni shwari isipokuwa katika mpaka wa Magharibi ambao kutokana na machafuko ya kisiasa katika nchi za jirani, yamesababisha wimbi la wakimbizi kuingia nchini.
Alikiri kuwa hali ni tete katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na matukio ya kigaidi yanayofanywa na vikundi vya kigaidi vya al-Shabaab na kusisitiza kuwa jeshi hilo limejipanga kufuatilia mienendo ya makundi hayo.

Alisema jambo linalofanyiwa kazi kwa kina ni kitendo cha baadhi ya Watanzania kudaiwa kujiingiza katika makundi hayo jambo linaloiweka nchi hatarini. “Ndio maana moja ya mkakati wetu ni kudhibiti kuenea kwa itikadi zenye misimamo mikali,” alifafanua.
Naye Menyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu alisema kitendo cha Wizara hiyo kutopatiwa fedha kulingana na bajeti kimesababisha miradi mingi kushindwa kuendelea.

Naye Msemaji wa Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga la taifa Juma Hamad Omar (CUF), pamoja na kupongeza utendaji na weledi wa jeshi hilo alisema kambi hiyo inasikitishwa na kitendo cha bajeti ya wizara hiyo kutotekelezwa ipasavyo.
“Tunataka serikali itambue kwamba, kuchelewesha au kutopeleka kabisa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwenye Wizara hii ni kuuweka rehani ulinzi na usalama wa taifa hili. Tunaitaka serikali isifanyie mzaha bajeti hii kwani jeshi hili ni muhimu kwa usalama wa nchi yetu,” alisisitiza.

Chanzo: Habari Leo Imeandikwa na Halima Mlacha, Dodoma

No comments