Header Ads

Ngoma, Tambwe wapata dili England, Pluijm acharuka, atoa msimamo

AMISSI-TAMBWE-001-768x707
Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe.
HUENDA siku za mastraika Donald Ngoma na Amissi Tambwe zikaanza kuhesabika kwani Derby County FC ya England imeonyesha nia ya kuwasajili.
Derby County ya Ligi Daraja la Kwanza England, imetuma watu ambao sasa wapo katika harakati za kupata video za Ngoma na Tambwe za mechi za nyuma kwani tayari wameshaona uwezo wao katika michezo ya karibuni.
Klabu hiyo iliyoanzishwa Februari 5, 1884 na William Morley sasa inatumia Uwanja wa Pride Park unaochukua watazamaji 33,597, inamilikiwa na Mel Morris, kocha wake ni Darren Wassall.
Tayari Burnley na Middlesbrough zimeshapanda kucheza Ligi Kuu England msimu ujao, lakini Derby County iliyoshika nafasi ya tano, itacheza mtoano na Brighton & Hove Albion, Hull City na Sheffield Wednesday ili kupata timu moja itakapanda ligi kuu pia.
Kamusoko & Ngoma (15)Wachezaji wa Yanga wakipongezana.
Habari za uhakika ambazo Championi Jumamosi imezipata ni kwamba, klabu hiyo imetuma watu wake wawili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata video za Ngoma na Tambwe pia kufanya mazungumzo ya awali ya kufanikisha uhamisho wao.
“Watu wawili walifika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo na akina Ngoma na Tambwe, watu hao walipata taarifa za wachezaji hao wakiwa huko kwao.
“Walijiridhisha uwezo wa wachezaji hao kwa kuwafuatilia zaidi katika mechi zao ikiwemo dhidi ya Al Ahly waliyorudiana Misri, ndipo wakafika nchini kwa ajili ya mazungumzo zaidi na kutaka baadhi ya video za mechi zao walizozicheza,” kilisema chanzo chetu.
Alipotafutwa Tambwe kuzungumzia hilo, alishangaa kisha akasema; “Mmepata wapi habari hizo? Akili zetu sasa zipo katika Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ila ni kweli kwamba watu hao walifika hapa Dar na kututafuta lakini walifanya mazungumzo na meneja wangu ila wameshaondoka nchini wamerudi kwao.
“Kikubwa walichofuata ni video za mechi ambazo tumezicheza ili kuona mabao tuliyofunga na uwezo wetu wa kutengeneza mabao, nasikia wamepewa kwa ajili ya kwenda kuziangalia,” alisema Tambwe.
Kwa upande wake, Ngoma alisema: “Ningependa kupata ruhusa ya kocha kwanza ili kuzungumzia hilo.”
Alipotafutwa Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm alisema: “Hata aje nani, kwa sasa hivi siwezi kumruhusu mchezaji yeyote kuondoka kwenye timu yangu kwani tuna mechi za kimataifa mbele yetu.”
Ngoma ana mkataba wa mwaka mmoja na Yanga wakati Tambwe amebakiza miezi sita. Bado gazeti hili linafuatilia kwa karibu kuhusu dili hilo jipya, kwani viongozi wa Yanga hawakupatikana jana kutoa ufafanuzi.
Kama mambo yakienda sawa, kuna uwezekano mkubwa wa Ngoma na Tambwe kucheza Ligi Kuu England msimu ujao, endapo Derby Country itafuzu. Moja kati ya nyota waliochezea Derby Country ni kipa maarufu wa zamani wa Uingereza, Peter Shilton, 66, ambaye alicheza mechi 175 kati ya mwaka 1987-1992.

No comments