Header Ads

Shetta aitambulisha ngoma mpya ‘Namjua’ na mtindo mpya wa kucheza ‘AdedeDance’


Shetta ni bingwa wa kuingiza maneno mapya ya Kiswahili mjini na yakateka maongezi ya vijana vijiweni na kwenye maeneo yao ya kazi kupitia nyimbo zake. Unakumbuka ‘Mdananda’, na ‘Shikorobo’ jinsi ambavyo hazikuishia kuwa nyimbo kali za kuchezeka tu na kuvuma kila kona, bali pia maneno hayo yakawa midomoni mwa watu.
Na sasa, Shetta amekuja na kitu kipya kinachotabiriwa kuhodhi mawimbi ya redio na TV pamoja na mtandaoni kwa muda mrefu. Ameachia single yake mpya ‘Namjua’ iliyomuunganisha tena na mtayarishaji raia wa Comoro, Jobanjo aliyeitayarisha ngoma yake ya mwanzo, Shikorobo kwa kushirikiana na studio za Wasafi Records.

Wimbo huo mkali unaoweza kukuingia kirahisi kichwani na kujikuta ukirudiarudia kionjo chake, umeachiwa rasmi Ijumaa hii. Pia umekuja na mtindo mpya wa uchezaji alioupa jina la ‘AdedeDance.’

Shetta anakukaribisha kuucheza mchezo huu na ukajirekodi ukijivinjari nao na kisha kuwaonesha washkaji kwenye Instagram au Facebook. Ukitisha zaidi, unaweza kupata fursa ya kuonekana kwenye video yake ijayo. Kumbuka kuambatanisha na hashtag #AdedeDance.  Changamka.

No comments