Header Ads

Snura aeleza alivyoteswa na Chura

Msanii wa Mduara, Snura Moshi ambaye video ya wimbo wake wa Chura ilizua gumzo mitaani na kwenye mitandao ya kijamii,  ameeleza namna alivyoteswa na wimbo huo kabla ya kufungiwa na serikali.
Akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa Habari Maelezo ulipo Posta jijini Dar, Alhamisi iliyopita, Snura aliomba radhi kwa serikali na Watanzania wote waliochefuliwa na wimbo huo huku akisisitiza kuwa hakuna wimbo uliomtesa kama Chura.

“Naomba radhi Watanzania wenzangu, sitarudia. Lakini hata hivyo muelewe tu huu wimbo wa Chura ulinitesa sana kuliko hata Majanga na Nimevurugwa. Nisemwa sana na watu mbalimbali na kuniita mimi mhuni niliyepitiliza kwa ajili ya Chura tu.

“Watu walifikiri mimi nilikuwa na dhamira mbaya ya kupotosha jamii na hadi kufikia hatua ya kunitamkia maneno mabaya. Hata hivyo nimejifunza mambo mengi sana kutokana na Chura na ninaahidi kuwa balozi wa maadili kwa wasanii wengine,” alisema Snura. Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Snura  alifafanua kuwa wimbo huo ulisimamishwa na serikali kwa kukiuka maadili sambamba na yeye kutojisajiri katika Baraza la Sanaa na Taifa (Basata) lakini siku hiyohiyo (Mei 4) aliyosimamishwa, alikwenda kusajili Basata na kukamilisha taratibu zote hivyo yupo huru kufanya sanaa na ataurekebisha wimbo huo na ataendelea kuutumia.

No comments