Header Ads

Upinzani wanusa ufisadi mabilioni ya maliasili Uingereza, Marekani


KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imehoji taratibu za manunuzi zilizotumika katika kutoa zabuni mbili za jumla ya Sh. bilioni 2.8 kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utali vya nyumbani katika nchi za Uingereza na Marekani mwaka 2014.
 


WAZIRI WA MALIAASILI PROFESA JUMANNE MAGHEMBE

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii bungeni mjini hapa jana, Msemaji wa kambi hiyo katika wizara hiyo, Esther Matiko, alisema hawana uhakika kama matangazo hayo yalikuwa katika mpango wa Bodi ya Utalii nchini (TTB).
Matiko alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kuwa mwaka 2013/14, TTB ilitoa zabuni namba PA/036/2013-14/NC/05 yenye thamani ya Sh. bilioni 1.2 ya kufanya matangazo ya utalii kwa timu ya Sunderland ya Uingereza.
Aidha, alisema Matiko, katika mwaka huo wa fedha, TTB pia ilitoa zabuni namba PA/036/2013-14/NC/06 yenye thamani ya Sh. bilioni 1.59 kwa timu ya Seatle Sounders ya Marekani.
"Je, serikali ilitumia utaratibu gani kutoa zabuni hizo?" Aliuliza Msemaji huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kuhoji:
"Je, kulikuwa na ushindani katika utangazaji wa zabuni hiyo? Je, kufanyika kwa matangazo ya utalii kwa kupitia timu hizo, kulikuwa kwenye mpango wa Bodi ya Utalii?"
 

KAMPUNI YA GREEN MILES
Aidha, Matiko alisema kampuni ya Green Miles Limited ilibainisha kufanya uwindajhi haramu na kunyang'anywa leseni ya biashara ya uwindaji nchini lakini Waziri Profesa Jumanne Maghembe ameirudishia tena kampuni hiyo kibali cha uwindaji.
Alisema kuwa katika barua yake ya Mei 9, 2016, yenye kumbukumbu namba SEC.315/563/01C/7 inaonekana kuwa serikali imeipatia tena kampuni hiyo kitalu cha uwindaji.
 

VIGOGO WA UJANGILI
Mbunge huyo wa Tarime Mjini (Chadema), alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya Operesheni Tokomeza kwa kuwa tume iliyokuwa inaongozwa na Jaji Msumi, ilikamilisha kazi na kuwasilisha ripoti kwa Rais.
"Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangaa kuwaona wahusika wakubwa wa biashara ya ujangili bado wapo na wanaendelea na biashara hizo," alisema.
 

UJENZI JENGO LA UTALII
Matiko alisema mwaka 2015/16 serikali iliidhinishiwa Sh. bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la utalii 'Phase II', lakini hadi sasa fedha hizo hazijatolewa ili kumalizia jengo hilo lililoanza kujengwa na Wamarekani.
"Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali ikamilishe jengo hilo kwa wakati ili kuondoa tabia ya serikali kuacha viporo ambavyo vimekuwa vikisabisha hasara," alisema.
 

MALI KALE
Matiko alisema kuwa kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia, mabaki ya mjusi mkubwa ajulikanaye kama dinosari mwenye urefu wa mita za mraba 22 yalipatikana eneo la Tendaguru mkoani Lindi, na yalichukuliwa na serikali ya Ujerumani kwenda mjini Berlin mwaka 1918.
Alisema kwa mujibu wa ripoti ya DW ya Januari mwaka huu, watalii 542,000 kwa mwaka 2015 walitembelea makumbusho ya mabaki ya mifupa ya mjusi huyo mrefu zaidi duniani ikilinganishwa na watalii 463,000 waliotembelea makumbusha hayo 2014.
"Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali itoe majibu ya kina ni kwanini mpaka leo mjusi huyo hajarudishwa nchini," alisema.
VIUMBE HAI NA WANYAMAPORI
Matiko aliitaka serikali kutoa kama imewarejesha nchini vura wote wa Kihansi iliyowapeleka kwenye Chuo Kikuu cha Colorado nchini Marekani mwaka 2009.
"Vyura hawa ni wa kipekee duniani, Wanazaa na kunyonyesha vitoto vyao tofauti na amphibia wengine na wanapatikana kwenye maporomoko ya Udizungwa," alisema.
 

MALIPO VIWANJA VYA NDEGE
Matiko alisema katika viwanja vya ndege na hata mahoteli ya kitalii bado malipo yanafanyika kwa fedha taslimu badala ya kulipwa kielektroniki.
Kutokana na changamoto hiyo, wageni wengi hupata usumbufu mkubwa na kuiona Tanzania kuwa ni nchi iliyojaa urasimu.
Aidha, Matiko alisema viwanja vingi vya ndege, mfano KIA, vina hali mbaya na kwamva changamoto hiyo imekuwa ikiathiri mapato yatonakayo na utalii.
 

HASARA YA MABILIONI
Matiko alisema serikali imepata hasara ya Sh. bilioni 3.076 kutokana na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuhusu kutangaza tozo mpya zitakazotumika katika mahoteli yaliyo ndani ya hifadhi ya taifa ya Ngorongoro.
Katika kesi hiyo, wamiliki wa hoteli zilizopo bungani na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro walikuwa wakivutana kuhusu ukwepaji wa kulipa tozo zilizowekwa na mamlaka hizo.
Matiko alisema wamiliki hao walishindwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilimtaka Waziri wa Maliasili na Utalii atangaze katika gazeti tozo mpya zitakazotumika katika mahoteli yaliyomo ndani ya hifadhi hizo mara moja, lakini hakufanya hivyo.
 

PROFESA MAGHEMBE
Awali akiwasilisha hotuba yake kuhusu makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 bungeni mjini hapa jana, Profesa Maghembe, alisema katika mwaka wa fedha 2016/17, Sh. bilioni 118.051 zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati Sh. bilioni 17.746 ni za miradi ya maendeleo.
Katika mwaka 2015/16, Wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni 66 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na hadi Machi mwaka huu, ilikuwa imepokea Sh. bilioni 43.487.
Aidha, Sh. bilioni 7.709 ziliidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara hiyo mwaka 2015/16, lakini hadi kufikia Machi mwaka huu, walikuwa wamepewa Sh. bilioni moja tu (asilimia 12.9 ya bajeti ya maendeleo).
Profesa Maghembe alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2016/17, wizara yake itapambana na majangili na biashara haramu ya nyara za serikali na kutatua migogoro ya mipaka kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi.
Vipaumbele vingine vya Wizara, kwa mujibu wa Waziri huyo ni kufanya doria ndani ya nje ya mapori ya akiba na kukusanya nyara za serikali zilizopo kwenye vituo vya polisi, halmashauri za wilaya na hifadhi za taifa.
Alisema wizara yake pia itaimarisha ulinzi wa maisha na mali za wananchi dhidi ya wanyamapori, kusimika mfumo wa kisasa wa ukaguzi ili kuimarisha udhibiti wa mapato na matumizi, kudhibiti maambukizi ya magonjwa kati ya wanyama na mifugo pamoja na magonjwa kati ya binadamu na wanyamapori na kukarabati miundombinu ndani ya hifadhi.
 

KAMATI YA BUNGE
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Utalii imenusa harufu ya ufisadi wa fedha za miradi ya maendeleo Sh. bilioni moja uliofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii, huku ikigiza ukaguzi maalum ufanyike katika miradi iliyotengewa fedha hizo.
Kadhalika, Kamati hiyo imeishauri serikali kuimarisha kitengo cha intelijensia cha kupambana na ujangili kwa kukipatia vifaa vya kisasa ikiwa ni pamoja na kutumia ndege zisizoendeshwa na rubani.
Mjumbe wa kamati hiyo, Sebastian Kapufu, wakati akiwasilisha taarifa ya kanmatio hiyo bungeni kuhusu makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, alisema Bunge lilidhinisha Sh. bilioni 7.7 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wizara hiyo mwaka huu.
Alisema kuwa hadi Machi, mwaka huu, wizara ilikuwa imepokea Sh. bilioni moja kwa ajili ya kutekeleza mradi namba 4646 wa Participatory Forestry Management Programme REDD na CCIP
Alisema fedha hizo zilitumika kutoa mafunzo kwa wananchi wa wilaya zilizoteuliwa, kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa wakutubi wa Chuo cha Misitu Olmotonyi, kufanya ukarabati wa nyumba saba za chuo pamoja na kununua vifaa mbalimbali vya kusaidia kuhifadhi na kuendeleza misitu.
Hata hivyo, alisema kamati haikulidhishwa na taarifa iliyowasilishwa kuhusiana na matumizi ya fedha hizo za mradi.
“Kamati imeilekeza wizara kufanya ukaguzi maalum katika mradi ili kubaini kama kuna ubadhirifu wowote na kuwasilisha taarifa ya ukaguzi kwa kamati,” alisema Kapufu.
Mjumbe huyo pia alisema serikali inapaswa kuajiri askari wa wanyamapori wa kutosha, kununua silaha za kisasa pamoja na magari ya doria, pamoja na kuweka wazi takwimu za idadi ya Tembo nchini ili watanzania kwa pamoja waamue ni jinsi gani wataokoa na kulinda rasilimali.
Imeandikwa na Sanula Athanas na Gwamaka Alipipi


CHANZO: NIPASHE

No comments