Header Ads

WAKILI WA MOYO - 01


SEHEMU: 01
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
WAKILI WA MOYO
Maumivu ya moyo hayana msaidizi na moyo wa kupenda hauna subira, kilichojificha moyoni huwa sawa na mfungwa asiye na kosa lakini hajui kujitetea. Siku zote anayependa kama mhusika hajui kama anapendwa huwa mateso ya kujitakia. Cecilia msichana alinayetoka katika familia ya maskini anampenda Colin mvulana aliye katika familia ya kitajiri mwenye mchumba anayetaka kufunga naye ndoa. Anajikuta akiumia kila akimuona, pamoja na kuonekana jambo hilo kama maji kupanda mlima lakini msichana Cecy anauapia moyo wake kuwa atauwekea wakili na kuweza kushinda kesi ya maumivu ya mapenzi.
Je, atafanikiwa? Kuyajua yote ungana tena na mtunzi mahiri katika hadithi tamu ya mapenzi ili upate uhondo mwanzo mwisho.
TWENDE KAZI.....
Mama Cecy alishangaa kumuona mwanaye amerudi mapema huku sinia likiwa limejaa ndizi, alimalizia kupuliza moto wa kuni kisha alitoka jikoni huku akifuta machozi kwa upande wa khanga kutokana na moshi wa kuni kumuingia machoni. Alimtazama binti yake aliyekuwa amekaa chini huku ameshika tamaa na machozi kumtoka.
“Cecy nini tena mama?” alimuuliza huku akimsogelea.
“Mama hata nashindwa kujielewa sijui ni kwa nini inakuwa hivi?” alisema huku akiondoka mkono shavuni bila kufuta machozi.
“Una lingine au ni lilelile za siku zote?”
“Kuna lingine lipi mama yangu! Hata sijui kwa nini nimejiingiza kwenye mateso ya kumpenda Colin mtu ambaye hayajui mapenzi yangu kwake.”
“Lakini kwa nini mwanangu unapenda kuota ndoto za mchana, wewe na Colin wapi na wapi kama mbigu na ardhi.”
“Najua mama utasema hivyo lakini katika mapenzi hakuna kitu kama hivyo, nakuapia kwa Mungu Colin atakuwa mume wangu wa ndoa.”
“Cecy mwanangu hebu achana na kujishugulisha na masuala ya mapenzi, hebu jiangalie ulivyo na alivyo Colin. Kwanza mwenzako hand same.”
“Hata mimi beutiful girl,” Cecy alijibu kwa kujiamini huku akinyanyuka na kujishika mkono kiunoni kujionesha kuwa ni mrembo.
“Mwenzio ana elimu ya chuo kikuu wewe darasa la saba la kufeli, mwenzako anatoka kwenye familia ya kitajiri wewe pangu pakavu tia mchuzi. Kingine ambacho kinafanya usiweze kabisa kumpa ni kuwa Colin ana mchumba na mipango ya harusi ipo karibuni sasa huyo Colin yupi wa kukuona?”
“Mama nina uhakika kwa asilimia mia Colin kunioa,” Cecy alisema kwa kujiamini.
“Wee mtoto una wazimu? Au kuna mganga kakudanganya, maana siku hizi ushirikina hauna mtoto wala mzee.”
“Mama katu mapenzi sitayaendelea kwa mganga, ila nitayapigania kwa nguvu zote.”
“Kipi hasa kinakupa jeuri ya kusema hivyo?”
“Ipo siku nitakwambia lakini amini ndoa ya Colin na Mage haipo ila mimi ndiye mke wake.”
“He he he heee, usinichekeshe miye, kwa nini unasema hivyo?” mama Cecy alicheka mpaka machozi yakamtoka.
“Mage hampenzi Colin.”
“We umejuaje?”
“Ni historia ndefu mama.”
Cecy alianza kumhadithia mama yake sababu ya kuamini siku moja Colin atakuwa mpenzi japokuwa hajawahi kumtamkia kitu kama hicho hata siku moja.
Alianza toka siku ya kwanza kumuona Colin, Mage msichana aliyetoka katika familia ya kimaskini elimu yake ya darasa la saba shuleni alikuwa mmoja wa wasichana waburuza mkia.
Baada ya kufeli kwenye mtihani wa mwisho aliamua kufanya biashara ya ndizi kwa kupita mtaani kuuza. Japokuwa alikuwa maskini lakini alijipenda sana.
Baada ya kuuza ndizi siku za mwanzo alinunua nguo nzuri ambazo alizivaa kila alipozunguka mkaani kuuza ndizi zake.
Kitu kilichopelekea apendwe na wateja wengi kutokana na umaridadi wake na heshima kwa wote akiwemo mama Colin ambaye alikuwa mnunuzi wake mkubwa.
Nyumba ya mama Colin ilikuwa ndiyo iliyokuwa ikinunua ndizi nyingi kitu kilichomfanya Cecy aongeze mtaji. Mama Colin alitokea kumpenda sana na kumwita mkwe.
Siku moja alipitisha ndizi kama kawaida bila kujua kama nyumba ile ina kijana mzuri aliyekuwa nje amerudi baada ya kumaliza masomo yake. Baada ya kufika nje ya geti alibonyeza kengele na mlinzi alimfungulia mlango na kuingia ndani.
“Mwambie mama mkwe leo nimeleta ndizi za ukweli,” alimwambia mlinzi aliyekuwa amemzoea sana.
“Mamkweee,” Cecy alipaza sauti kama kawaida yake kila alipofika.
Mara alitoka mama Colin akiwa katika muonekano wa mtoko.
“Ha! Ma mkwe safari ya wapi tena?”
“Nampeleka mchumba wako mjini.”
“Muongo, yupo wapi?”
“Yupo ndani anakuja.”
“Amekuja lini?”
Siku zote Cecy alipokuwa akipeleka ndizi alitaniwa na mama Colin kwa kuitwa mkwe japokuwa hakuwahi kumuona huyo mwanaume. Kila siku alikuwa na hamu ya kumuona japokuwa alikuwa akitaniwa.
“Jana usiku na ndege.”
“Waawooo,” Cecy aliruka juu kama anamfahamu.
Ghafla alinyamaza baada ya kumuona mvulana mzuri tena mtanashati akitoka ndani. Alibakia kama kapigwa shoti ya umeme kwa jinsi alivyosimama kwa mshangao kidole mdomoni.
“Colin umemuona mchumba wako niliyekuandalia?” mama Colin alitania.
“Nimemuona mzuri tena mrembo,” Colin alisema huku akimtazama Cecy aliyekuwa bado amesimama.
“Cecy umemuona Colin?”
“Ndi..ndi..yo,” Cecy alipatwa na aibu na kushindwa kuzungumza.
“Sasa mkwe, msichana wa kazi atachukua ndizi sisi tuna safari ya mjini.”
“Sawa mkwe.”
Mama Colin alifungua pochi na kutoa noti ya elfu tano na kumpatia Cecy, wakati huo Colin alikuwa akilisimamisha gari pembeni ya mama yake. Mama Colin alifungua mlango wa gari wa nyuma na kuingia.
“Bai mchumba,” Colin alimuaga Cecy aliyekuwa ameingiwa aibu.
“Bai,” Cecy alisema huku akiangalia pembeni kwa aibu.
Geti lilifunguliwa na gari lilitoka nje kuelekea mjini na kumuacha Cecy akitoa ndizi kwa msichana wa kazi kisha alitoka na kuendelea kufanya biashara kama kawaida.
****
Safari ya mama Colin na mwanaye ilikuwa kwenda nyumbani kwao Mage msichana aliyemchagua kuwa mke wa mwanaye. Alimuona siku moja alipokuwa na mama yake walipokutana na shoga yake Super Market, wakati akiwa katika manunuzi ya bidhaa muhimu.
“Ha! Shoga za siku?” Mama Colin alimsemesha mama Mage.
“Nzuri shoga, za kupotezana?”
“Mmh! Nzuri, vipi Colin bado hajarudi?”
“Anarudi mwezi kesho mwishoni.”
“Shikamoo,” Mage alimwamkia mama Colin.
“Marahaba, hujambo mama?”
“Sijambo.”
“Monika, binti yako?” mama Colin alimuuliza shoga yake.
“Ndiyo amemaliza chuo kikuu Mlimani anasubiri ajira.”
“Nimempenda sana, unafaa kuwa mke wa Colin.”
“Tena wataendana wasomi kwa wasomi,” mama Mage aliunga mkono.
“Anaitwa nani?”
“Mage,” Mage alijibu mwenyewe.
Tokea siku ile wakawa wakiwasiliana hata kutembelea huku wakisubiri muda wa Colin kurudi toka masomoni ili wapange mipango ya ndoa. Mama Colin alimpenda sana Mage kwa umbile lake nzuri na heshima aliyoionesha siku zote kwake. Naye mama Mage alifurahi mwanaye kuolewa na Colin kutokana na kumfahamu vizuri.
Siku Colin aliyofika hakutaka kuwajulisha, kesho yake alimpeleka nyumbani kwao Mage bila taarifa ili wafanye surprise. Familia ya kina Mage ilikuwa ikikaa Kigamboni walikwenda hadi kwao na kupiga honi nje ya geti. Wakati wote huo Colin alikuwa hajui anakwenda wapi.
Baada ya geti kufunguliwa Colin aliliingiza gari ndani na kwenda kulipaki kwenye maegesho. Mama Mage alitoka nje baada ya kusikia gari likingia ndani na kujiuliza nani amekwenda kwake bila taarifa. Alishtuka kumuona mama Colin akiteremka kwenye gari.
“Waawooo jamani, ha! Colin siamini jamani karibu mwanangu,” alikuwa akimfuata mama Colin kumkumbatia lakini aligeuza baada ya kumuona Colin na kwenda kumkumbatia.
Colin alijikuta akishangaa baada ya kuteremka kwenye gari na kujiuliza pale ni wapi na yule aliye mfurahia na kumkumatia ni nani.
“Asante, shikamoo.”
“ Marahaba karibu sana mwanangu,” mama Mage alisema kwa furaha huku amemshika mabegani Colin na kumtazama.
Aliwapokea wageni na kuingia nao ndani kwenye sebuleni, baada ya kukaa alimwita Mage kwa sauti kubwa.
“Mageee.”
“Abee mama,” sauti ya Mage ilitoka chumbani.
“ Njoo mara moja.”
“Nakuja.”
Mage alikuja mbio bila kujua anaitiwa nini, alipofika alishtuka kumuona mama Colin.
“Ha! Mama mkwe.”
“Nimejaa tele,” mama Colin alijibu kwa tabasamu pana.
“Shikamoo.”
“Marahaba.”
“Mambo?” Mage alimsabahi Colin bila kumjua.
“Poa za hapa?”
“Nzuri,” Mage alijibu huku akishtuka na kujiuliza yule kama ndiye Colin, ili kupata uhakika aliomba msamaha na kutoka mara moja.
“Jamani samahanini nakuja mara moja.”
“Bila samahani,” alijibu mama Colin.
Alichepua mwendo na kwenda upande wa vyumba huku akimwambia mama yake.
“Mama njoo mara moja.”
“Jamani samahanini nakuja mara moja.”
“Hakuna tatizo,” mama Colin alijibu.
Baada ya mama Mage kuondoka kumufuata mwanaye, mama Colin alimsemesha mwanaye kwa sauti ya chini.
“Mchumba unamuonaje?”
“Yupo vizuri.”
“Umempenda?”
“Sana.”
“Nimefurahi kuona chaguo langu amelikubali.”
“Mama wee kiboko unajua kuchagua.”
Mama Mage baada ya kufika kwa mwanaye aliyekuwa amesimama upande wa vyumba.
“Vipi?” alimuuliza mwanaye.
“Safi, eti mama yule si Colin?”
“Ndiyo.”
“Mamaaa! Kwa nini hukuniambia mapema nijiandae anaweza kuniona sijipendi.”
“Walaa mbona umependeza, vipi umempenda?”
“Ndiyo,” Mage alikubali huku akinyanyua kichwa.
“Basi turudi.”
“Naona aibu ngoja nikaoge na kubadili nguo.”
Mama Mage aliwarudia wageni wake ili kuwapatia kinywaji kabla ya kuanza mazungumzo.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments