Header Ads

WAKILI WA MOYO - 02

 
HADITHI: WAKILI WA MOYO
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Cecy alijiuliza kauli ile ya mama Colin ilikuwa na ukweli gani kutokana na kuona kuolewa na Colin sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano.
“Mbona sielewi, kweli Colin atanioa au ananitania, mbona hakukataa mbele ya mama yake, na kwa nini mama yake aendelee kuniita mkwe?”
Cecy alijiuliza bila kupata jibu la moja kwa moja. Lakini wasiwasi wake ikawa kwenye hali zao yeye muuza ndizi anazurura mitaani na mwenzake mtoto wa kitajiri.
“Watakuwa wananitania,” alisema kwa sauti ya kakata tamaa na kugeukia ukutani kuutafuta usingizi.
SASA ENDELEA...
Usiku ulikuwa mrefu kwake baada ya kushtuka katikati ya usiku kutokana na ndoto aliyoota akiwa na Colin ndani ya gari yeye akiwa anafundishwa na baada ya hapo walikwenda ufukweni kupumzika. Wakiwa wamejilaza ufukweni Cecy alitembeza mikono yake kwenye kifua cha Colin kilichojaa kimazoezi na vinyweleo vingi ‘garden love.’ Upepo mwanana wa bahari uliwapepea.
Aliposhtuka alijikuta yupo kitandani peke yake, mapigo ya moyo yalimwenda mbio na kijacho chembamba kilimtoka. Alikaa kitandani na kujiuliza ndoto ile ina maana gani.
Aliwasha taa na kukaa kitandani mkono shavuni akijitahidi kujua ndoto ile ilikuwa na maana gani. Mama yake aliyeshtuka usingizi alishtuka kuona taa inawaka, alijiuliza usiku ule Cecy alikuwa akifanya nini.
Alinyanyuka taratibu na kwenda chumbani kwa mwanaye. Kwa vile chumbani hakikuwa na mlango zaidi ya pazia la kitenge kichakavu. Alipofika alifunua taratibu na kuangalia ndani.
Alimkuta mwanaye amekaa kitandani mkono shavuni. Alitulia kwa muda bila kumsemesha na kutaka kujua mwisho wake nini. Baada ya muda kidogo Cecy alizima taa na kujilaza kitandani.
Mama yake aliendelea kusimama mlangoni kwa muda huku akiwa na maswahi na hali ya mwanaye toka jana yake. Aliamua kurudi chumbani kwake na kupanga kumuuliza siku ya pili kwa kumbana sana ili ajue sababu ya mwanaye kuwa katika hali ile ambayo kwake ilikuwa ngeni.
***
Colin akiwa chumbani kwake amejilaza kitandani aliukumbuka uzuri wa Mage msichana aliyeonekana mwelewa lakini mwenye jeraha la mapenzi. Sifa zake za elimu ya juu pia urembo na ucheshi ni vitu vilivyomteka kimwili na kiamili.
Moyoni alijiapiza kumpenda Mage kwa moyo wake wote, aliiona familia bora mbele yake yeye akiwa baba, Mage mama na watoto wao wawili wa kike na kiume.
Siku zote alipanga kuzaa watoto wachache ambao angewamudu kuwahudumia kimalazi na elimu. Hakupenda kuwa na familia kubwa japokuwa wao walizaliwa sita, lakini yeye alitaka watoto wawili wakizidi basi wanne.
Alitaka ndoa yake ifanyike haraka ili kujipanga kwa maisha mapya. Wazo lake la kuanzisha kampuni aliliona litakwenda zuri kama Mage mwanamke mwenye Shahada ya uhusiano akiwa mkewe ambaye ingesaidia kampuni yao kukua na kutanuka.
Moyoni alimshukuru mama yake kuwa na jicho la tatu kumtafutia mwanamke ambaye hakuwa tofauti na samaki anayekaa kwenye maji marefu bila kuwa na chombo madhubuti huwezi kumpata.
Alijikuta akiyakumbuka maneno mawili ya Mage ambayo yaliuumiza moyo wake na kuamini ana deni kubwa kwa msichana yule:
“Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako,” Mage alisema huku machozi yakimtoka na kuweka michirizi kwenye mashavu.
Baada ya kumuhakikishia anampenda mapenzi ya dhati alimpa mtihani ambao Colin aliamini anauweza kwa vile hakuwa mwanaume kigeugeu.
“ Colin umeweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung’olewa jino bila ganzi.”
Baada ya kuyakumbuka maneno ya Mage, Colin alijiapiza kuwa tiba ya maumivu aliyoyapata siku za nyuma. Aliamini maumivu yale yalikuwa na sababu ya kuwakutanisha ili wajenge familia bora. Usingizi mororo ulimpitia Colin huku akitabasamu.
***
Asubuhi Cecy aliamka kama kawaida na kwenda kwenye gulio kununua ndizi za kuuza. Mama yake aliposhtuka alikuta ameishatoka muda. Baada ya kupata alirudi nyumbani na kuzipanga kwenye beseni kisha alikwenda kuoga na kutafuta nguo nzuri ambayo aliiteua kwa ajili ya kanisani tu.
Hakutoka kama siku nyingine anazokwenda kwenye biashara, alitumia muda mwingi kujipamba zaidi ya siku ya jumapili akienda kanisani. Baada ya kuhakikisha amependeza sana alitoka kwa ajili ya kwenda kuuza ndizi. Mama yake alishtuka kumuona mwanaye kwenye hali ile aliingiwa wasiwasi labda mwanaye ana safari nyingine si kwenda kufanya biashara.
“Cecy safari ya wapi?”
“Kwenye biashara mama.”
“Kwenye biashara! Ndiyo uvae vizuri hivi?”
“Basi tu leo nimeamua.”
“Si kweli toka jana sikuelewi kabisa, sasa nimeanza kupata mwanga.”
“Mwanga gani mama?” Cecy alishtuka.
“Si bure lazima utakuwa umepata mwanaume, Cecy angalia mwanangu, we bado mdogo usijishughulishe na wanaume mwisho wake mbaya.”
“Mamaaa!” Cecy alimshangaa mama yake.
“Unashangaa nini, ndiyo maana eti unatamani kuolewa kumbe una mwanaume,” mama Cecy alizungumza ameshika pua.
“Maama...mama kwa nini unanihukumu bila kosa?” Cecy alimlalamikia mama yake.
“Huna kosa, haya endelea ukiniletea tumbo hapa utatafuta mbereko ya kunibebea.”
“Mama yangu sijawaza kufanya hivyo, japokuwa nami napenda siku moja niolewe na mwanaume mwenye mapenzi ya dhati si kuanza mapenzi kihuni.”
“Haya kipi kilichokufanya nguo ya kanisani kwenda kuuzia ndizi na kujipamba kupita kiasi?”
“Mama nikueleze mara ngapi siku hazilingani.”
“Mmh! Haya biashara njema.”
“Asante mama.”
Cecy alibeba ndizi zake na kuelekea kwenye bishara zake, hakutaka kupita popote mpaka kwa mama Colin ndipo alipopanga kuanzia biashara yake kwa siku ile. Alipofika kama kawaida alibofya kengele na mlinzi alimfungulia.
“Ha! Cecy mbona umependeza hivyo?” mlinzi alimshangaa Cecy.
“Mbona kawaida yangu,” Cecy alisema huku akiingia ndani ya geti, aliweka ndizi chini na kumwita mama Colin kwa sauti ya juu.
“Mamkweee nimeisha fika.”
Colin ndiye aliyetoka kufuata ndizi kutokana na wasichana wa kazi kuwa na majukumu mengine. Macho yake yalishtuka kumuona Cecy.
“Ha! Mchumba ni wewe?”
“Ndiyo mpe...,” Cecy hakumalizia aliingia kigugumizi.
“Karibu sana.”
“Asante.”
Colin alinunua ndizi na kumlipa fedha yake.
“Mama mkwe yupo wapi?”
“Anatoka sasa hivi.”
Mara alitoka mama Colin, Cecy baada ya kumuona alimsalimia kwa kuchuchumaa chini kuonesha heshima.
“Shikamoo mkwe.”
“Marahaba mkwe wangu hujambo?”
“Sijambo.”
“Nyumbani?”
“Wanakusalimia.”
“Mkwe una safari nyingine?” mama Colin aliuliza Cecy.
“Kwa nini mama mkwe?”
“Umependeza sana.”
“Hapana nipo kwenye biashara, mwanamke kujipenda bwana,” Cecy alisema kwa pozi.
“Hongera, nina wasiwasi mwanangu anaweza kuibiwa.”
“Walaa,Colin mpenzi nipo kwa ajili yako na wewe ndiye itakuwa mwanaume wangu wa kwanza.”
“Muongo! Usimdanganye mwanangu,” mama Colin alisema.
“Kweli mamkwe.”
“Mchumba umenifuhisha sana, kesho ukija nitakupa zawadi,”Colin alisema.
“Zawadi gani?”
“Utaiona hiyo kesho.”
“Mmh! Asante.”
“Unakubali tu, hujui zawadi gani?” mama Colin alitania.
“Yoyote atakayonipa, zawadi haipangwi.”
Baada ya manunuzi Cecy aliondoka kuendelea na biashara zake. Colin na mama yake walirudi ndani, baada ya kuweka ndizi jikoni alirudi sebuleni alipokuwa amekaa mama yake.
Alipofika alikaa pembeni ya mama yake aliyekuwa yupo bize na simu. Baada ya kuachana na simu Colin alimuuliza mama yake.
“Mama unajua Cecy ni mzuri?”
“Ni kweli mwanangu, Cecy ni binti yule mzuri sana,” mama yake alimuunga mkono.
“Tena anajipenda, ana tofauti na wasichana wengi wanaofanya biashara kama yake. Hali hii anauza ndizi yupo vile akifanya kazi za ofisini itakuwaje?” Colin alisema huku akitazama mama yake aliyejenga tabasamu kutokana na maneno ya mwanaye.
“Ni kweli, ndicho kitu kilichonifanya nipende kununua biashara yake. Toka nimfahamu sijawahi kumuona mchafu.”
“Sasa kipi kilicho kufanya umwite mkwe?” Colin alimuuliza mama yake akiwa amemkazia macho.
“Nilitokea kumpenda sana binti yule na kutamani awe mkwe wangu lakini alikosa sifa muhimu.”
“Zipi mama?”
“Kwanza elimu yake darasa la saba tena la kuferi, pia anatoka katika familia ya kimaskini.”
“Tabia yake?”
“Kwa kweli binti yule ana tabia nzuri sana, ila tatizo ni hilo. Kama angekuwa na sifa angalau ya elimu ya kidato cha sita au chuo kama Mage basi yeye ndiye alikuwa chaguo langu la kwanza.”
“Kweli mama Cecy ni mzuri, lazima nikusifie unajua kuchagua wasichana wazuri.”
“Nataka mwanangu mwanamke utakaye muoa basi moyo utabasamu kila ukimuona.”
“Nashukuru kwa hilo mzazi wangu.”
***
Kama kawaida Cecy baada ya biashara zake, usiku aliwahi kuoga na kula kisha kuwahi kitandani. Alitaka kupata muda wa kuyatafari yote aliyokutanana nayo mchana. Mama yake hakutaka kupoteza wakati alimfuata na kumwita ili ajibiwe maswali yanayomsumbua mwanaye.
“Cecy.”
“Abee mama.”
“Tabia gani uliyoanzisha akimaliza kula inawahi kitandani?”
“Mama kazi ya kuzurura na ndizi inachosha.”
“Umeanza leo?”
“Mama siku azilingani.”
“Hebu njoo.”
Cecy kwa mara ya kwanza alimuona mama yake anamsumbua kwa kumnyanyua kitandani wakati yeye alitaka kuzama kwenye dunia nyingine ya kufikilika yenye raha zisizo na kikomo.
Alitoka ndani akiwa amekunja uso kitu alichokigundua mama yake na kumuonya:
“ Tabia ya kukasirika nikikuita imeanza lini?”
“Mama nimechoka.”
“Hata ukichoka hujawahi kunikunjia uso, hebu njoo hapa.”
Cecy alikaa kwenye kigoda pembeni ya mama yake huku ajitahidi kuficha hasira alizokuwa nazo.
“Umepata mwanaume?” mama yake alimuuliza kwa sauti kavu.
“Hapana mama.”
“Cecy, mi mtu mzima nimeona jua kabla yako, wasichana wakipata wanaume hujenga kiburi na kujiona wapo sawa hata na wakubwa zao.”
“Haki ya Mungu mama sijapata mwanaume,” Cecy alijiapiza.
Mama yake alimweleza yote aliyoyaona kwa mwanaye usiku wa kuamkia siku ile.
“Haya bisha ninakusingizia?”
“Najua utasema hivyo, lakini mama sina mwanaume ila kuna mtihani moyoni mwangu wenye majibu tata.”
“Mtihani gani?”
Cecy alimwelezea ukaribu wake na mama Colin wa kuwa mteja mzuri wa ndizi zake na tabia ya kumwita mkwe mpaka siku aliporudi Colin kutoka Ulaya na kutambulishwa kama mchumba wake.
“Sasa hapo kipi kinakitatiza?” mama yake alimuuliza baada ya kumsikiliza.
“Mama sielewi kama kweli mama Colin amenichagua niwe mchumba wa mwanaye.”
“Mwanangu kumbe ndicho kinachokuchanganya?”
“Ndiyo mama yangu hakuna kingine, sijawahi kupenda wala simjui mwanaume. Lakini nimetokea kumpenda sana Colin na kutamani awe mume wangu.”
“Umesema ametoka Ulaya kusoma, sasa akuoe wewe mbumbumbu ambaye hata darasa la saba limekushinda?”
“Mama elimu haina mwisho, naweza kujiendeleza najua tatizo labda kuzungumza kingereza.”
“Sasa hicho kingereza utakijualia wapi?”
“Zipo shule nitajifunza nitajua.”
“Nataka nikuambie mwanangu, mama Colin kukuita mkwe ni kukutania tu, siku zote matajiri huwapeleka watoto wao kusoma Ulaya ili wawaoe watoto wa matajiri wenzao tena wasomi. Sasa wewe pangu pakavu wapi na wapi?”
“Sawa mama, lakini naamini ipo siku maji yatapanda mlima.”
“Hizo ni ndoto za mchana.”
“Sawa mama, ipo siku utakubali ndoto za mchana huwa zina ukweli.”
“Mwanangu naomba uachane na mawazo hayo muda ukifika Mungu atakupa mume mzuri mwenye mapezi na wewe.”
“Asante mama yangu.”
“Haya kalale mwanangu.”
“Haya mama usiku mwema.”
“Na kwako pia.”
Cecy aliagana na mama yake na kurudi chumbani kwake kulala, alipofika chumbani alizima taa na kujilaza kitandani. Hakukubaliana na mama yake, akili yake kubwa ilikuwa kwenye zawadi aliyoahidiwa na Colin.
Alijiuliza ni zawadi gani anayotaka kumpa ambayo hakuweza kumpa siku ile mpaka asubiri siku ya pili. Alijikuta akiuona usiku ukienda taratibu sana, hamu yake kukuche upesi ili akaione zawadi aliyoahidiwa na Colin.
Itaendelea

No comments