Header Ads

WAKILI WA MOYO - 03


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Cecy aliagana na mama yake na kurudi chumbani kwake kulala, alipofika chumbani alizima taa na kujilaza kitandani. Hakukubaliana na mama yake, akili yake kubwa ilikuwa kwenye zawadi aliyoahidiwa na Colin.
Alijiuliza ni zawadi gani anayotaka kumpa ambayo hakuweza kumpa siku ile mpaka asubiri siku ya pili. Alijikuta akiuona usiku ukienda taratibu sana, hamu yake kukuche upesi ili akaione zawadi aliyoahidiwa na Colin.
SASA ENDELEA...
***
Mage pamoja na kukubali kuolewa na Colin bado alikuwa na kovu moyoni mwake la kutendwa na mtu aliyempenda kuliko kitu chochote chini ya jua Hans, mwanaume aliyemuingia kwenye ulimwengu wa mapenzi.
Wasiwasi wake mkubwa kwa Colin kuwa na mpenzi mwingine ambaye ametoka naye mbali na mwisho kuwa kama Hans na kuumizwa kwa mara ya pili kitu ambacho hakutaka kijirudie. Japokuwa hakuwa tayari kuliona lile na alikuwa tayari kulipigania penzi lake kwa nguvu zake zote.
Wazo la peke yake liliisumbua akili yake alihitaji msaada wa mtu
wa karibu. Mtu muhimu katika maisha yake alikuwa shoga yake Brenda ambaye aliamini anaweza kumsaidia juu ya uamuzi wake wa ghafla wa kumkabidhi moyo wake Colin bila kumchunguza.
Akiwa amejilaza kitandani alichukua simu yake na kumpigia Brenda, baada ya kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.
“Vipi shoga kulikoni mpaka leo kupiga simu, badala ya kutumia njia ya whats up au twiter?”
“Shoga si la kulizungumzia kwenye mtandao, hili ni la uso kwa macho.”
“Mmh! Una nini tena shoga?” Brenda alishtuka.
“Kwanza upo wapi?”
“Nimerudi muda si mrefu natoka kufuatilia ile ishu.”
“Sasa naomba basi nikupitie tukakae ufukweni tuzungumze vizuri.”
“Hakuna tatizo.”
“Basi nakuja sasa hivi.”
“Poa.”
Mage alikata simu na kwenda kubadili nguo, kwa vile alikuwa ametoka kuoga muda si mrefu hakuwa na haja ya kwenda kuoga tena. Baada ya kuchagua nguo nzuri iliyompendeza alitoka kuelekea nje. Mama yake aliyekuwa sebuleni alishangazwa na mwanaye kutoka bila taarifa.
“Mage safari ya wapi?”
“Ufukweni mama.”
“Kufanya nini?”
“Mama akili yangu bado haipo vizuri ngoja nikaipoze kwa kuangalia maji.”
“Brenda mwanangu kumbuka sasa hivi wewe ni mchumba wa mtu, japokuwa hujavalishwa pete. Hiki huwa kipindi kibaya sana kwa msichana kwani anatakiwa kutulia. Unaweza kuharibu kila kitu na matokeo yake useme umerogwa.”
“Mama hujui kiasi gani nilivyo na msogo wa mawazo juu ya uamuzi wangu wa haraka wa kumkubali Colin. Katika mapenzi yangu na Hans sikuwaza kama kuna siku tutakuwa mbalimbali. Hivyo nimekuwa muoga sana mama naona kama nimefanya uamuzi wa ghafla sana.”
“Katika penzi lenu na Hans kuna kosa mlifanya ambalo nina imani kwa Colin limekuwa wazi sana.”
“Kosa gani mama?”
“Penzi lenu lilitawaliwa na usiri na mambo mengi mlifanya kwa siri bila wazazi wa mwenzako kujua.”
“Mamaa! Wadogo zake wote wananitambua.”
“Wazazi wake?”
“Ndiyo tulikuwa katika harakati za kutambulishana likatokea la kupatiwa mchumba,” Mage alisema kwa sauti ya masikitiko.
“Umeona! Pengine kama mngekuwa wawazi yote yasingetokea, sasa hivi ungekuwa mke wa Hans.”
“Mamaa! Usinikumbushe, kutaja ndoa yangu na Hans moyo unaniuma. Nampenda Colin lakini hawezi kumfikia Hans, kwake nilikuwa kama kipofu niliyebahatika kufumbua macho mara moja na kitu cha kwanza na mwisho kukiona kilikuwa ni yeye.”
“Ndiyo hivyo ukificha moto kwa kuufunika na shuka moshi utakuumbueni. Penzi mlilifanya la siri ndoa ya mwanamke mwingine imekuumiza.”
“Basi mama inatosha, niache nikapunguze mawazo ufukweni.”
“Kwa nini usimfuate mwenzio ili mwende pamoja, kufanya hivyo unaonesha jinsi gani unavyo muhitaji kama mumeo.”
“Mama siku za kutoka na Colin zipo, leo nina mazungumzo na Brenda.”
“Haya ila punguza mawazo, Mungu kasikia kilio chako umempata mwanaume wa haja anamzidi kila kitu Hans.”
“Kwa macho ni rahisi kusema hivyo, macho huwa yanaona lakini moyo ndiyo wenye jukumu la kuchagua ulichokipenda. Colin anaweza kuwa na umbile na sura nzuri lakini hakawa hana mapenzi kama Hans.”
“Mmh! Huyu Hans kakuchanganya sana mwanangu, ina maana akiachana na mkewe upo tayari kuolewa?”
“Mkewe angekuwa hajazaa ningekubali, lakini alichonifanyia Mungu anajua. Sasa hivi namchukia Hans kuliko kifo.”
“Basi mwanangu muwahi Brenda.”
“Sawa mama.”
Mage alitoka hadi nje na kuchukua gari aina ya Harrier Lexus na kuelekea Osterbay kwa shoga yake Brenda. Alimkuta akiwa tayari amejiandaa, hakuwa na haja ya kuingiza gari ndani kwani alikuta tayari ameishatoka nje ya geti.
Baada ya Brenda kuingia ndani ya gari Mage aliliondoa bila kusema kitu. Shogaye aligundua mabadiliko kwenye uso wa rafiki yake.
“Shoga kuna usalama?”
“Kiasi.”
Mage alijibu kwa mkato bila kumtazama shoga yake huku akifunga bleki katika foleni ndogo kwenye taa za daraja la Salenda. Baada ya taa kuruhusu aliondoa gari, Brenda hakubandua uso wake kwenye uso wa Mage na kugundua michirizi ya machozi kitu kilichomshtua sana.
“Shoga kulikoni?”
Mage alijikuta akipaki gari pembeni na kuanza kulia kilio cha chinichini. Brenda alishtuka sana na kumsogelea shoga yake aliyekuwa amelalia usukani huku akilia.
“Mage nini tena shoga si umesema tukazungumzie ufukweni?”
“Ni kweli, lakini inauma sana.”
“Sawa, hebu twende huko tutayaongea yote.”
“Papara ya mapenzi itaendelea kunitesa, hata sijui kwa nini nimeshindwa kujikontroo,” Cecy alisema akiwa bado ameinama kwenye usukani.
“Jamani Cecy, nani kakutenda tena?”
“Shoga hebu njoo uendeshe gari naweza kugonga maana kichwa changu hakipo sawa.”
Brenda alizunguka upande wa pili na kuingia kwenye gari na kuliondoa kuelekea Kigamboni. Baada ya kusubiri pantoni Kivukoni kwa robo saa, walivuka upande wa pili.
“Twende ufukwe gani?” Brenda alimuuliza baada ya kutoka nje ya geti.
“Yoyote ile,” Cecy alijibu akiwa amejilaza kwenye kiti ilichokilaza kwa nyuma.
“Mikadi panafaa?” Brenda alimuuliza huku akimtazama.
“Popote utapopaona panafaa.”
Brenda alipaki kwenye maduka na kununua vitu vya kutafuna wakiwa ufukweni kisha aliendesha gari hadi ufukwe wa Mikadi. Waliteremka na kuelekea upande wa bahari.
Hali ya hewa ilikuwa ya kawaida jua lilikuwa limefichwa kwenye mawingu huku upepo wa bahari ukipepea bila kuwa kero kwa mtu aliyekuwa ufukweni.
Kwa vile ilikuwa katikati ya wiki watu walikuwa wa kuhesabu ufukweni. Walitafuta sehemu nzuri na kutandika khanga na kukaa juu yake, kila mmoja kulinyoosha miguu kuelekea baharini.
Baada ya utulivu wa muda huku kimya kikitawala, Brenda alikuwa wa kwanza kuuvunja ukimya ule kwa kumsemesha shoga yake aliyekuwa ametuliza macho akitazama baharini.
“Mage.”
“Abee.”
“Hebu nitoe tongotongo, najiona kama nipo kizani na sauti ya upande wa pili ikiomba msaada bila kumuona mwenye tatizo. Siku zote tumekuwa watu tunaotegemeana kwenye matatizo yetu. Najua umeniita ili tusaidiane mawazo.
“Naomba unieleze tatizo lako, siku zote tunajua machozi si ufumbuzi wa tatizo zaidi ya kupambana nalo na kulitatua. Basi naomba unieleze kinachokusibu,” Brenda alisema kwa sauti ya kubembeleza.
“Brenda, nimekuwa nikikurupuka mara nyingi katika suala la mapenzi kitu ambacho kimekuwa kikinihukumu,” Mage alisema huku akimtazama Brenda.
“Mage mara ngapi umekurupuka? Suala la Hans pale ulikurupuka nini, ikiwa wote mlikuwa mkipendana tatizo wazazi wake.”
“Alichonitenda Hans hukijui?” Mage alimuuliza Brenda huku akimkazia macho.
“Mage nilikueleza toka siku ya kwanza, kitu kama kile hakiwezekanani. Hawawezi kulala pamoja kufanya mapenzi bila kinga ujauzito usipatikane.”
“Hans alinihakikishia hawezi kuzaa na yule mwanamke, kitu ambacho tungekifanya tukioana ili tuanze kutafuta mtoto pamoja.”
“Inawezekana alipanga vile, lakini imetokea bahati mbaya. Lakini nilikueleza mapema kuhusu mategemeo yako kwa Hans baada ya kuoa kuwa usimtegemee kabisa, lakini ulinibishia.”
“Brenda, unajua kiasi gani nilivyokuwa nampenda Hans?”
“Hilo lipo wazi, lakini ndiyo hivyo tena, kitu gani kingine kilichokufanya mpaka ukawa kwenye hali hii tofauti na la Hans?” Brenda alimuuliza Mage huku akimkazia macho.
Mage alimweleza kila kitu toka walipokutana kwa mara ya kwanza na mama Colin na kumwita mkwe kwa kujua anamtania mpaka siku alipomfanyia surprise ya kuletewa mwanaume nyumbani kwao.
“He! Makubwa, mbona kama umegeuzwa mbuzi hata bila ridhaa yako?” Brenda alihoji huku akigeuka kumtazama Mage usoni.
“Si kwamba sikutaarifiwa bali niliona kama utani, lakini kumbe yule mama alikuwa hatanii.”
“Ehe, baada ya kuletwa ikawaje?”
“Yaani hata sijielewi, baada ya kumuona nikawa nimevurugwa mtoto wa kike.”
“Mtume!” Brenda alisema huku akimtazama shoga yake kwa jicho la huruma.
Mage alimweleza chote kilichoendelea baada ya kumuona Colin.
“Mmh! Basi inaonekana Colin ni kitu cha haja?”
“Kwa kitu? Kitu hasa! Colin Mungu kajua kumtengeneza mwanaume yule. Yaani mpole na mstaarabu hadi raha,” Mage alisema huku akijishika kifuani na kufumba macho.
“Sasa tatizo nini?”
“Najiona nimejirahisi mapema sana bila kuijua historia yake.”
“Lakini si amekuhakikishia kuwa yupo tayari kukuoa?”
“Ndiyo, lakini mvulana mzuri kama yule lazima atakuwa na mpenzi tu. Mimi kumkubali nitakuwa naingilia penzi la mtu. Huoni kumkubali Colin ni sawa na kuyatafuta maumivu mengine?”
“Lakini bado hamjavishana pete ya uchumba una nafasi ya kumchunguza, kwani mmeisha du?”
“Bado.”
“Kumbe! Sasa tatizo nini?”
“Hata kama bado, najua nimechelewa kwa vile Colin, maisha ya Tanzania hajaishi sana. Kuna vitu aliniambia vimenichanganya sana.”
“Vitu gani?”
“Nilimweleza jinsi nilivyoumizwa na mapenzi na kumweleza najitupa tena ndani ya dimwi la huba bila kujua kina chake. Kuwa yeye ni boya la kuniokoa bila hivyo nitakufa maji.”
“Ukasemaje?”
“Alinieleza ananipenda zaidi ya kupenda huku akinithibitishia kuwa yeye ndiye tiba sahihi ya maumivu ya moyo wangu. Nilimweleza huenda hanipendi bali ananitamani na baada ya kuufaidi mwili wangu akinimbie.”
“Akajibu nini?”
“Brenda, Colin alizungumza kwa taratibu na kunihakikishia ananipenda sana nakumbuka baadhi ya mazungumzo yetu baada ya kumbana na maswali, nilimwambia:
“Najua ndiyo siku yako ya kwanza kuniona, siamini kama Colin unanipenda kama ninavyokupenda?”
Colin alinijibu: Mage toka nilipoelezwa nimepatiwa mchumba moyo wangu ulikuwa taabuni kutaka kukuona. Nilikuumba akilini kwa kila umbile na kukupamba kwa rangi nyingi.
“Amini Mage kila nilichokiwaza moyoni mwangu kilikuwa uongo. Nilichokiona ni zaidi ya vyote nilivyoviwaza,” Colin alisema huku amemshika mabegani na kunitazama usoni kwa jicho la huruma.
Nilimuuliza: Vitu gani hivyo Colin?” niliuliza huku nikijitahidi kuyatoa macho nje kama naweza kuyaona maneno atakayo niambia kwa macho.
Colin alinijibu: Kila mtu anapenda kuwa na mwenza mwenye sura anayoiwaza ambayo huamini huenda moja wapo, nami niliitengeneza yako niwezavyo. Lakini imekuwa kinyume kabisa,” Colin aliniambia huku akiachia tabasamu ambalo lilivunja nguzo za moyo wangu.
Nilijitahidi kumuuliza: Mmh! Colin, kwa nini?” nilimuuliza nami niliilazimisha tabasamu.
Alinijibu: Mage we ni mzuri wa wazuri mrembo wa warembo. Najiona kiumbe mwenye bahati kama nitakuwa mume wako,” Colin alisema huku akiwa ameyakaza macho kuonesha anachokizungumza hatanii.
Huku moyo wangu akiwa umetawaliwa na tabasamu nilimwambia: Siamini, Colin siamini,” nilisema mikono yangu nikishika kifuani huku machozi yakinitoka.
“Mage huamini nini?” Colin aliniuliza kwa uso wa huruma.
“Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako,” nilisema huku machozi yakinitoka na kuweka michirizi kwenye mashavu yangu.
“Mage amini nakupenda kama ugonjwa wa shinikizo la damu linavyochukuwa uhai wa mtu ghafla,” kila kauli ya Colin ilizidi kuusambalatisha moyo wangu.
“Colin sijui wewe ni mwanaume wa aina gani?” nilijisema huku akijitahidi kutengeneza tabasamu ndani ya machozi.
“Kwa nini mpenzi?” aliniuliza huku akinitazama kwa huruma kitu ambacho sikuwahi kukiona kwa Hans pamoja na kumpenda kote.
“Maneno yako yamekuwa na sumaku yenye nguvu ya ajabu kuweza kunasa chuma kilichomo moyoni mwangu,” nilimweleza nilivyo kuwa radhi kuwa mateka wa penzi lake.
“Sijakuelewa mpenzi?” Colin aliniuliza.
“Ameweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung’olewa jino bila ganzi,” nilimtaadhalisha Colin.
“Amini Mage nakuahidi kuwa mume mwema,” Colini aliniahidi japokuwa sikujua aliyosema yanatoka moyoni au mdomoni.
“Nami nakuahidi kuwa mke mwema,” nami nilimuahidi ahadi toka moyoni wangu.
Baada ya Brenda kumsikiliza kwa muda shogaye alisema:
“Mmh! Mbona kina kitu kipo wazi tatizo nini?”
“Wasiwasi wangu anaweza kuwa na mtu wake.”
“Anaweza kuwa naye lakini si wa malengo ya kuwa mke na mume, kwani picha yake unayo?”
“Ndiyo, tulipiga siku ile tena alilazimisha yeye.”
Mage alisema huku akifungua simu yake upande wa picha. Baada ya kuijaza kwenye kioo cha simu alimuonesha Brenda. Shoga yake alishtuka kumuona mwanaume mzuri akiwa na Mage katika pozi tofauti za mahaba.
“Mage! Colin ni mwanaume mzuri sana, mlivyokaa kama mke na mume sijui picha za ndoa yenu zitakuwaje?”
“Nina wasiwasi nimekurupuka sana katika kumkubali.”
“Walaa, mapenzi shoga yangu hayana fomula, mnaweza kukutana hivi na penzi lenu likadumu milele, lakini mnaweza kuandaana mwisho mkawa maadui wakubwa kama unavyomuona Hans.”
“Umeona! Yaani sasa hivi sitakiwa kumuona wala kusikia jina lake.”
“Nina imani hili litakwenda vizuri kwa vile hata mzazi wake amekupenda pia familia zenu zinafahamiana na zinapendana.”
Wakiwa katikati ya mazungumzo simu ya Mage iliita, namba ilikuwa mgeni. Aliiangalia kwa muda bila kuipokea.
“Mbona hupokei?” Brenda alihoji.
“Hata sijui nani, inawezekana ni Hans, niliapa sipokei simu yake.”
“Hebu pokea hujui anataka kukuambia nini?”
“Hana chakuniambia.”
Wakati huo simu ilikuwa imekatika, baada ya muda uliingia ujumbe mfupi wa maneno. Mage aliufungua na kuusoma:
Najue upo bize na mambo ya mchana, ushikapo simu naomba unipigie, Moyo wangu u taabuni mpaka sikie sauti yako.
It ‘s me Colin.
Mage baada ya kusoma ujumbe ule alipiga kelele huku akishika kifua.
“Mungu wangu!”
“Nini tena mbona unanitisha?” Brenda alishtuka.
“Mungu wangu! Kumbe alikuwa Colin,” Mage alisema huku akishika kifua.
“Mmh! Ina maana huna namba yake?”
“Sina.”
“Ina maana mlipokutana hamkupeana namba za simu?”
“Hatukupena, wote tulichanganyikiwa.”
“Basi mpigie.”
“Duh! Sijui anielewaje?” Mage aliingia wasiwasi.
“Mage akuelewe kivipi? Brenda alimshangaa rafiki yake.”
“Ataona kama ninalinga au siyo muaminifu!”
“Hawezi kwa vile leo ndiyo siku yake ya kwanza kukupigia.”
“Mmh! Ngoja nijaribu.”
Mage alichukua simu na kumpigia Colin, iliita kwa muda bila kupokelewa. Alirudia zaidi ya mara nne lakini haikupokelewa kitu kilichomnyima raha Mage.
“Brenda lazima Colin atakuwa amekasirika, siwezi kupiga mara nne bila kupokelewa.”
Itaendelea

BAADA YA KUSOMA SHARE HAPA CHINI

No comments