Header Ads

WAKILI WA MOYO - 06

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Aliamini ingemtesa mwanaye kwa kipindi kirefu na kumfanya akose amani ya moyo wake. Lakini aliamini atampatia ushauri nasaha utakaomrudisha katika hali ya kawaida. Aliachana na mawazo yale na kwenda chumbani kwake kulala.
SASA ENDELEA...
Cecy siku ile ilikuwa mbaya katika siku alizowahi kuishi, aliyakumbuka maneno ya mama yake kuhusu Colin kumtamkia mpenzi wake zaidi ya utani wa uchumba.
Kwa vile kichwa kilikuwa kikimuuma, alimeza dawa za usingizi na kupanda kitandani kuitafuta siku ya pili.
***
Wakati hayo yakiendelea, Colin na Mage walikuwa kwenye furaha ya ajabu. Mage hakuamini tukio lililotokea usiku ule la kuvalishwa pete ya uchumba mbele ya watu.
Kilikuwa kitu kikubwa sana katika maisha yake, pamoja na kupendana sana na Hans kwa muda mrefu lakini hakikufanyika kitu kama kile.
Aliamini Colin alikuwa mwamaume aliyeletwa kwake na Mungu kwa kuonesha ana mapenzi ya dhati na yeye.
“Colin asante sana mpenzi wangu,” Mage alisema huku akiitazama pete yake ya kito cha Tanzanite kidoleni kwake.
“Kawaida tu, nina vitu vingi vya kukufanyia mpenzi wangu,” Colin alijibu huku akichezea vidole vya mikono ya Mage.
“Colin nakuahidi kuwa mke mwema.”
“Nashukuru, nataka harusi yetu isichukue muda mrefu.”
“Hujui tu, ukitaka sasa hivi nipo tayari hata unioe bure kwa vile upendo wa kweli ni ghari kuliko kuitafuta fedha. Nakuhitaji kuliko kitu chochote chini ya jua.”
Mage alisema huku machozi yakimtoka akikumbuka alichofanyiwa na mpenzi wake Hans, mwanaume aliyeamini ndiye wake wa kufa na kuzikana.
Lakini kilichotokea kilikuwa kinyume na matarajio yake, kiliufanya moyo wake kuingia wasiwasi wa kumkosa hata yule.
“Mage usilie nataka ulie kwa furaha ukiwa nami si kwa huzuni,” Colin alimwambia Mage huku akichezea vidole vyake na macho yake kutazama usoni kwake.
“Nina wasiwasi naweza kutendwa tena, Colin ukinitenda nitakufa mwenzio nakuona wewe ndiye uliyeshika uhai wangu,” Mage alisema kwa sauti iliyohitaji huruma.
“Nakuhakikishia furaha yako itapitia mikononi mwangu.”
“Kweli Colin?” Mage aliuliza huku ametoa macho.
“Amini nakupenda sana Mage, wewe ni ua la moyo wangu sitachoka kulitunza na kulimwagilizia ili liendelee kustawi na kuchanua.”
“Asante Colin, nami nitahakikisha chaguo la mama yako hutajutia maishani mwako. Hazina yote ya mapenzi nahamishia kwako.”
“Asante mpenzi wangu nami nitakuwa benki yenye usalama kwa ulichokiweka kila sekunde kinaongezeka faida ya upendo.”
“Nimefurahi kusikia hivyo, nina imani kovu la kutendwa litaondoka.”
“Niamini nikisemacho, kwa vile nami nahitaji furaha yangu itoke kwako.”
“Asante mume wangu mtarajiwa,” Mage alisema huku akimkumbatia Colin kwa mahaba mazito.
Baada ya sherehe, Mage alikataa kuondoka na mama yake na kulazimisha kubaki na Colin.
“Mage mwanangu muda wa kuwa karibu na Colin bado.”
“Hapana mama, alichokifanya leo ni zaidi ya ndoa. Naomba uniache nina mengi ya kuzungumza naye usiku wa leo.”
“Mama Mage mwache mtoto abakie na mwenziye, bado wana mengi ya kuongea wakiwa karibu,” mama Colin aliingilia kati na kufanya mama Mage kukubaliana na mzazi mwenzie kumuacha Mage alale na Colin siku ile.
****
Cecy alishindwa kutoka kwao kwa siku mbili, muda mwingi aliitumia kuwaza na kujiona ni kiumbe kwenye mkosi ambaye hakufaa kuishi katika dunia ile. Alijiona hana thamani yoyote kutokana na kukosa kila kitu ambacho mwanadamu alitakiwa kuwa nacho.
Maisha yao yalitawaliwa na umaskini wa kutupa, elimu nayo ilikuwa duni ya shule za kata, kwake alichombulia ni kujua kusoma na kuhesabu zaidi ya hapo hakuna alichokijua.
Kingine kibaya ambacho ndicho kilichomuuliza sana kukosa haki ya kupenda kwa vile tu hana elimu pia anatoka katika familia duni. Japokuwa hakuwa msomaji wa vitabu lakini alikuwa akipenda kusikiliza vipindi vya usiku hasa vinavyohusu mapenzi na uhusiano.
Alikuwa muumini mzuri wa vipindi hivyo kwa kujifunza vitu vingi, aliweza kujua thamani ya kuwa mwanamke pia mapenzi hayahitaji mtaji wa fedha wala elimu bali hisia za mtu ambazo hupokelewa na mtu mwingine na kuwa kama ncha mbili zinasababisha umeme zikiungana ndipo umeme hupatikana.
Siku zote mada zile zilimfanya ajiamini na kuamini anaweza kuwa na mpenzi wa aina yoyote mwenye hadhi yoyote kwa hali yake duni na elimu yake ileile. Alichojifunza kingine msichana kuwa msafi wakati wote hata kama anauza karanga hakutakiwa kijifuja na kutembea na nguo chafu au kutojijali.
Cecy aliamini kupendwa na watu wengi huku biashara yake ukiuzika sana ilikuwa ni kutokana na kujipenda kwa kununua nguo nzuri na muda wote kuwa msafi. Lakini kitendo alichofanyiwa na Colin kilimvunja nguvu na kuona hakuwa na sababu ya kupoteza fedha zake kununua nguo na vipodozi, kwa vile hakuona umuhimu wake zaidi kurudia maisha ya zamani ya kuvaa nguo nzuri siku jumapili atakapokwenda kanisani tu lakini siku nyingine alivaa hovyo.
Kitendo cha kutokwenda kwenye biashara kilimshtua sana mama yake na kutaka kujua kulikoni.
“Mwanangu kwa nini huendi kwenye biashara?”
“Mama yaani sijui nitatembeaje najisikia aibu naona kama kila mtu anajua kilichonitokea siku ile.”
“Mwanangu, kilichotokea ni siri yako kwa vile hakuna aliyejua moyoni unawaza nini.”
“Ni kweli, lakini moyo unaniuma sana mama.”
“Kuumwa moyo ni kujitakia kwa vile Colin hakukutamkia wala wewe hukumtamkia kipi kikuumize.”
“Kwa nini aliniita kwenye sherehe yake?”
“Kama walivyoitwa wengine.”
“Mmh! Sawa, lakini nimeapa sitapeleka tena ndizi kwa mama Colin.”
“Hiyo ni juu yako, lakini kumbuka katika sehemu uliyokuwa na uhakika wa fedha ni katika nyumba ile. Siku zote usiingize mapenzi kwenye biashara.”
“Siwezi..siwezi mama watanionaje?”
“Wakuoneje, kwani wao wanajua nini juu ya kuanguka kwako?”
“Hata kama hawajui siendi,” Cecy alishikilia msimamo wake.
“Siwezi kukulazimisha kwa vile wateja wale sikukutafutia uliwatafuta mwenyewe.”
Cecy alipanga kuendelea na biashara yake mwisho wa wiki huku akisimamia msimamo wake wa kutopeleka ndizi kwa mama Colin.
***
Upande wa Colin alishtushwa na ukimya wa Cecy kutoonekana kwa siku tatu nyumbani kwao kupeleka ndizi. Akiwa chumbani kwake alichukua picha alizopigwa Cecy na kuzitazama.
Aliusifia uwezo wa mpiga picha kwa kumpiga picha nzuri za tofauti, alituza macho na kuangalia uzuri wa asili wa Cecy.
“Hakika binti huyu ni mrembo,” alisema kwa sauti ya chini na kurudia tena picha moja baada ya nyingine.
Alitabasamu na kuamini wazo lake la kuanzisha kampuni ya mitindo litafanikiwa kwa kukusanya mabinti wenye uzuri wa asili wasiotumia madawa ya ngozi kama Cecy ambao angewatumia katika maonesho ya mitindo mbalimbali huku akiuza nguo.
Japokuwa elimu ya Cecy ilikuwa darasa la saba, kwa umri wake aliamini akisoma twisheni ya Kingereza kwa kipindi anajiandaa kufungua kampuni angekuwa amepiga hatua katika kuzungumza na kusoma Kingereza vizuri.
Alijikuta akitoka sebuleni na picha ya Cecy mkononi hadi alipokuwa amekaa mama yake.
“Mama mbona mchumba haonekani siku hizi?”
“Colin, wa nini kwani siku ambazo hakuja tumekosa ndizi?” mama yake alimuuliza huku akiondoa macho kwenye gazeti na kumtazama mwanaye.
“Hapana mama kumbuka alipata matatizo siku ya sherehe yangu huenda amezidiwa.”
“Daktari alisema hakuwa na ugonjwa wowote alichopata ni mshtuko tu.”
“Lakini kumbuka toka apate tatizo lile hatujamuona kuleta ndizi.”
“Hata tukimuona atatusaidia nini?”
“Mamaaa! Mbona majibu yako kama yanaonesha chuki.”
“Colin, mimi na wewe nani anamjua sana Cecy?”
“Wewe.”
“Sasa kipi kinakufanya kutaka kuyajua mambo yake?”
“Kwa kawaida mtu ambaye alikuwa akituletea biashara atoweke ghafla lazima nihoji.”
“Hiyo picha ya nani?”
“Ya Cecy.”
“Ya Cecy! Imefikaje kwako..hebu.”
Mama Colin alisema huku akinyanyuka na kumfuata alipokuwa amesimama mwanaye na kuichukua picha ya Cecy aliyokuwa amekaa pozi tata. Aliitazama kwa muda kisha alimuangalia mwanaye na kumuuliza.
“Hii picha umeitoa wapi?”
“Kwa nini unaniuliza hivyo?”
“Colin mwanangu sasa nimejua sababu ya Cecy kuja kwenye sherehe yako, yaani unajifanya unampenda Mage kumbe upo na Cecy.”
“Mamaa!” Colin alimshangaa mama yake kusema kauli ile.
“Nasema hivi sitaki kukuona na uchafu huu na tena nitakwenda kumkomesha.”
“Mama mbona unanihukumu bila kuniuliza?” Colin alizidi kumshangaa mama yake.
“Nikuulize nini, yaani uchafu huu sitaki kuuona,” alisema huku akiichana picha ya Cecy na kuvitupa vipande chini na kumwita msichana wa kazi kuja kuvizoa.
“Mama unafanya nini, nilikueleza nini kuhusu production yangu?”
“Production na mapenzi yako na msichana mchafu maskini tena mbumbumbu hainiingia akilini,” mama yake alisema huku akibinua midomo.
“Mama Cecy si mpenzi wangu bali niliamini kwa muonekano wake pamoja na wasichana wengine wa muonekano kama wake angenisaidia katika kampuni yangu kufanya vizuri.”
“Sitaki mazungumzo mengi nataka uvunje uhusiano wako na Cecy au nitamfanyia kitu kibaya ili nikanyogwe hawezi kuharibu mipango ya maisha yangu.”
“Mama sina mpango wowote na Cecy ulipoelekea sipo,” Colin alimshangaa mama yake.
“Naomba uondoke mbele yangu.”
Colin hakusema kitu aliondoka na kurudi chumbani kwake, alipofika alizichukua picha zote za Cecy na kuzificha kwa kuamini kwa jinsi alivyopendeza hata Mage angeziona angejua lazima ana uhusiano naye.
Kitendo cha Colin kuwa na picha ya Cecy pia kumkaribisha kwenye sherehe ya kuzaliwa kwake, kiliamsha hasira za mama yake na kujikuta akimchukia Cecy ambaye aliamini kabisa mwanaye anampenda kuliko Mage.
Alinyanyuka na kutoka nje akiwa mwenye hasira hadi kwenye gari. Aliingia na kuondoka nalo kuelekea nyumbani kwao na Cecy ili kwenda kumkomesha aachane na mwanaye.
Aliendesha gari kwa kasi mpaka nyumbani kwao na Cecy. Alipofika aliteremka bila kufunga mlango na kwenye anapoishi Cecy na mama yake. Alimkuta mama yake akitengeneza samaki wa biashara.
“Cecy yupo wapi?” aliuliza kwa hasira hata bila salamu.
“Dada yangu hata bila salamu?” mama Cecy alisema kwa sauti ya upole.
“Haikusaidii kitu, huyo kiinyago wako yupo wapi?”
“Tatizo nini mzazi mwenzangu?”
“Sina shida ya maswali namtaka Cecy.”
“Amekwenda kwenye biashara zake.”
“Ooh! Kumbe ndiyo janja yake mwambie nimeisha mbaini. Akija mwambie sitaki kuvuruga maisha ya mwanangu nasema amkome.”
“Kwani kafanya ni...” alikatwa kauli.
“Ee..ee, nimesema amkome kama ana tabia ya kenge basi damu itamtoka maskioni.”
“Mbo..mbona ..si..si.”
“Nimesema nikisikia tena usije kunilaumu, mwambie mwanao amkome mwanangu kama alivyokoma kunyonya ziwa lako.”
Baada ya kusema vile aligeuka na kuondoka na kumuacha mama Cecy ameganda kama sanamu asielewe chochote zaidi ya kashfa walizomiminiwa na mama Colin.
Alilitizama gari liliondoka kwa kutimua vumbi mpaka lilipopotea kwenye macho yake.
“Maama, ” alishtuliwa na kauli ya Cecy aliyetokea nyuma ya nyumba akiwa na beseni tupu baada ya kumaliza ndizi.
Mama yake aligeuka na kumtazama mwanaye aliyegundua kulegwa kwa machozi kwa mama yake ambaye uso wake ulipoteza furaha.
“Mamaa! Kuna nini?” Cecy alishtuka.
“Mwanangu umaskini mbaya,” mama yake alisema huku akielekea kukaa kwenye kizingiti cha nyumba.
“Kwa nini mama?”
“Umemfanya nini mama Colin?”
“Kivipi?”
Mama yake alimweleza yaliyotokea muda mfupi, Cecy alishtuka sana kusikia habari zile.
“Mama yaani ndiyo kasema hivyo! Hayo mapenzi na mwanaye yameanza lini?”
“Sijui.”
“Mama namfuata sasa hivi anieleze kuja kututukana bila sababu, kama umaskini wetu tumeridhika nao.”
“Hapana mwanangu mwenye nguvu mwache apite.”
“Si kwa hilo, wameniumiza bado wananifuatafuata,” Cecy alisema kwa sauti ya kilio.
“Wee waache.”
“Mama tukiwaacha watatuzoea, nimeacha kwenda kwao bado tu hawajaridhika mama niache akanithibitishie alichokisema. Ni kweli nampenda Colin lakini hatujatamkiana mambo ya mapenzi yeye kayatoa wapi?” Cecy alisema kwa jazba.
“Mwanangu jasho la mnyonge haliendi joshi.”
“Sawa, lakini Mungu yupo.”
Cecy aliweka beseni lake na kwenda chumbani kwake akiwa amefura kwa hasira. Moyoni alijiapia siku akikutana na mama Colin siku hiyo atamkosea adabu kwa dharau aliyoifanya nyumbani kwao.
ITAENDELEA

No comments