Header Ads

WAKILI WA MOYO - 07


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Mama tukiwaacha watatuzoea, nimeacha kwenda kwao bado tu hawajaridhika mama niache akanithibitishie alichokisema. Ni kweli nampenda Colin lakini hatujatamkiana mambo ya mapenzi yeye kayatoa wapi?” Cecy alisema kwa jazba.
“Mwanangu jasho la mnyonge haliendi joshi.”
“Sawa, lakini Mungu yupo.”
Cecy aliweka beseni lake na kwenda chumbani kwake akiwa amefura kwa hasira. Moyoni alijiapia siku akikutana na mama Colin siku hiyo atamkosea adabu kwa dharau aliyoifanya nyumbani kwao.
SASA ENDELEA...
****
Familia mbili zilikutana kupanga tarehe ya harusi ya watoto wao. Kila mmoja alitaka kufanyika harusi ya kifahari kutokana na watoto wao kuwa wa kwanza kuoa na kuolewa katika familia zao.
Baada ya makubaliano ya tarehe ya ndoa, waliwataarifu watoto wao kilichokuwa kikiendelea juu ya ndoa yao. Mara moja zilisambazwa taarifa kwa ndugu na jamaa kwa kupewa kadi na wengine kuhudhulia vikao vya maandalizi ya harusi vilivyoanza mara moja.
Mage alipanga picha zake za harusi kuzisambaza katika mitandao yote ili kumuonesha Hans naye ana watu wanaompenda kwa dhati kuliko yeye aliye upasua moyo wake kwa kisu butu bila ganzi.
Wakiwa katika Mgahawa wa Samakisaki Mlimani City walipokutana Mage na shoga yake kipenzi Brenda kwa ajili ya kula raha. Wakiwa wanakula piza na juisi, baada ya kutafuna kipande cha piza na kusukumia na juisi ya embe, alisema:
“Brenda yaani sijui siku ya harusi yangu itakuwaje?”
“Mage, litakuwa bonge la harusi ambalo halijawahi kutokea jijini. Mama yako alivyopania, sijui!”
“Yaani, baada ya ndoa wakati tupo honey moon nitazisambaza picha za harusi mitandao yote ili kuwakonga wavimba macho walionicheka baada ya Hans kuoa.”
“Najua Hans ataumia sana,”Brenda alisema huku akikata kipande cha piza.
“Aumie nini wakati amefurahia, lakini Mungu yupo, kisasi changu kwake hakijaisha ningekuwa na uwezo ningemmwagia tindi kali,” Mage alisema huku akikunja uso kwa hasira.
“Magee! Tindi kali ya nini ikiwa tayari umepata mtu mwenye mapezi ya kweli?”
“Brenda hujui tu jinsi nilivyoumia kwa kitendo cha Hans kunihalibia ndoto zangu za maisha.”
“Mage bado unampenda Hans!”
“Aah, wapi!”Mage aliruka kimanga.
“Muongo unampenda na akitokea leo haki ya nani ndoa hakuna,” Brenda alimwambia shoga yake akiwa amemkazia macho.
“Haitatokea hata siku moja, labda jua litoke Magharibi kwenda Mashariki.”
“Unajikomba tu, lakini upo na Colin kama bodi lakini injini ni Hans.”
“Mawazo yako, kwanza tuachane na mambo ya Hans tuzungumzia harusi yangu.”
“Kama kweli umedhamilia kuolewa na Colin basi litakuwa bonge la harusi.”
Wakiwa katika ya mazungumzo simu Brenda iliita, alipoangalia alikuta namba ngeni alipokea.
“Haloo.”
“Haloo Brenda.”
“Abee, nani mwenzangu?”
“Yaani nawe umenichukia kama shoga yako, Brenda nimekukosea nini?”
Sauti ile ilimshtua na kugundua anazungumza na Hans.
“Jamani shemu mambo mengi si unajua mitihani ilitukamata.”
“Pamoja na mitihani, lakini umenitenga shemeji yangu!”
“Siwezi kukutenga.”
“Naomba msaada wa kunikutanisha na Mage, kuna tetesi zimeniumiza moyo wangu. Usishangae wakati wowote ukisikia kifo changu.”
“Brenda unazungumza na nani?” Mage aliingilia kati mazungumzo kwa kusimama na kusogea kwa Brenda.
“Mage hebu subiri,”Brenda alimtuliza Mage na kuendelea kuzungumza.
“ Kipi tena kitasababisha kifo chako, unaumwa?”
“Heri ningeumwa kuliko ukatili anaonifanyia shoga yako. Anajua mimi na yeye tumetoka wapi na tuliahidiana nini. Kweli Mage unakubali kuolewa na mwanaume mwingine tofauti na mimi?” Hans alisema kwa sauti ya huzuni.
“Hans utakuwa unakosea kusema hivyo, wewe ndiye uliyesababisha yote. Ulikuwa ukifahamu Mage alikuwa akikupenda kiasi gani na unajua nini kilimpata baada ya wewe kufunga ndoa.”
“Najua, lakini nilimweleza kila kitu.”
“Mbona ulikwenda kinyume?”
“Nilikuwa na sababu yangu ambayo Mage alitakiwa kunisikiliza na kuelewa sababu ya mimi kufanya vile wala asingefikia huko.”
“Hans usimlaumu Mage kwa vile naye kafanya kama wewe.”
“Kivipi?”
“Mume katafutiwa na mama yake.”
“Duh! Haijawahi kutokea.”
“Basi imetokea.”
“Basi naomba anipe nafasi ya kuzungumza naye kwa dakika chache.”
“Sidhani kama anaweza kupata nafasi kwa muda huu wa maandalizi ya harusi.”
“Najua, ila nilikuwa nataka kuzungumza naye hata dakika kumi kabla ya ndoa yake.”
“Hans, hiki si kipindi cha kuzungumza chochote na Mage, unaweza kuivuruga ndoa yake.”
“Siwezi, nataka tu nizungumze naye ili akiolewa ajue mimi si adui yake.”
“Mmh! Nitafikisha ujumbe.”
“Naomba shemeji yangu unikutanishe na Mage nitakupa zawadi yoyote unayotaka.”
“Sawa shemu.”
“Nashukuru kwa kunisikiliza pia wewe ni daraja muhimu kati yangu na Mage.”
“Nimekuelewa.”
Brenda alikata simu na kumgeukia shoga yake aliyekuwa na kumuhemuhe cha kutaka kujua Hans alikuwa akisemaje.
“Vipi mzushi alikuwa akisemaje?”
Brenda alimweleza mazungumzo yote waliyozungumza na Hans.
“Mmh! Anataka kuniambia nini?”
“Sijui, ninyi ndiyo unajua mlizungumza nini katika ahadi ya penzi lenu.”
“Uhuu!” Mage alishusha pumzi na kusema:
“Brenda unanishauri nini?”Mage alionekana kama ametahayari kusikia taarifa za Hans.
“Kwa vile upo katika hatua nzuri ya harusi, huu si muda wa kuzungumza na Hans unaweza kuharibu kila kitu ukakosa bara na pwani,” Brenda alimtaadhalisha rafiki yake.
“Eti eeh, sijui Hans anataka kuniambia nini?”
“Achana naye.”
“Mmh! Sawa.”
Kwa vile muda uliokuwa umekwenda sana, kila mmoja aliingia kwenye gari lake kurudi nyumbani.
***
Brenda alipofika nyumbani kwao alikwenda kuoga na kupata chakula kisha alijifungia chumbani kwake na kuwasha Ipad yake na kuanza kuchati na marafiki zake kwenye Twiter na Skype.
Akiwa anaendelea kuchati simu yake iliita, namba ilikuwa ngeni aliipokea.
“Haloo.”
“Haloo Brenda.”
“Abee, nani?”
“Brenda unaniuliza nani wakati tumetoka kuzungumza muda si mrefu.”
“Hans?” Brenda aliuliza.
“Ndiyo.”
“Unasemaje?”
“Brenda samahani sana.”
“Bila samahani.”
“Naomba unikutanishe leo na Mage.”
“Hans, si tumeisha ongea?”
“Hapana Brenda, kuna kitu cha muhimu sana nataka nizungumza naye kabla siku ya kesho.”
“Samahani Hans, nipo Bagamoyo sitarudi leo.”
“Naomba hata umpigie simu ili anisikilize hata kwa sekunde tano tu.”
“Hans kwanza samahani, hapa nipo na boy friend yangu, ana wivu sana naomba tuzungumze kesho,” Brenda alidanganya.
“Samahani, ila utakacho kisikia kesho usishangae najua Mage atafurahi.”
“Unataka kufanya nini Hans?”
“Nilitakiwa kumweleza Mage mwenyewe, kwa heri.”
Hans alikata simu na kumfanya Brenda abakie na simu mkononi kama anatazama kitu cha kumshangaza, alijikuta akijuliza.
“Hans anataka kufanya nini? Au anataka kujiua? Mmh! Ngoja nimweleze Mage maana sasa imekuwa kazi. Lakini kipi cha ajabu Mage akiolewa? Kwani alitaka akae vile mpaka lini? Hivi Hans anashida na Mage au anataka kumvuruga maisha tu?”
Brenda alijikuta akiwaza peke yake, wakati huo simu aliyopiga ilikuwa ikiita. Ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo shoga lete stori,” Mage alipokea.
“Mmh! Mtu wako ananisumbua sana.”
“Nani?”
“Hans.”
“Kakupigia tena?” Mage alishtuka.
“Ndiyo.”
“Brenda achana naye, kwa nini unamsikiliza?”
“Mage siwezi kumkatia simu kwa vile sina ugomvi naye.”
“Yaani hivi najiandaa kwenda kwa Colin, tulikuwa tunachati tukaona haitoshi, tukaongea vilevile tukaona haitoshi, nimeamua kwenda kabisa kuonana uso kwa macho.”
“Duh!”
“Brenda, nimeamini Colin ananipenda sana.”
“Sasa ndiyo utulie.”
“Brenda, lazima nitulie Colin kaniahidi vitu vingi sana baada ya ndoa nina imani ndoto zangu nilizoziota kwa Hans zitakuwa mara kumi.”
“Basi ndiyo hiyo mtu wako wa roho ya Mungu anatapatapa kama mfa maji.”
“Kwani alikuwa akisemaje?”
Brenda alimweleza yote aliyoelezwa na Hans na alivyomdanganya, Mage baada ya kumsikiliza alishusha pumzi na kusema:
“Kwani Hans anataka kuniambia nini?” Mage aliuliza.
“Akwambie nini! Yule muharibifu, huu si muda wa kumsikiliza, ukirogwa kumsikiliza tu ndoa huna.”
“Mmh! Nimekuelewa japo moyo unatamani kumsikiliza ili nijue anataka kusema nini?”
“La kusema hakosi, anaweza kukuvuruga akili na ndoa yako ukaiona chungu. Najua bado unampenda sana Hans, kama utampa nafasi narudia tena ndoa hakuna,” Brenda alimtaadhalisha Mage.
“Hata siku moja, labda siyo Mage mimi, siwezi kuumizwa mara ya tatu mbili zinatosha.”
“Basi ndiyo hivyo kuwa makini na Hans, kwa nini muda wote akae kimya, kusikia unataka kuolewa ndiyo ajifanye anakupenda sana.”
“Nimekuelewa basi wacha niwahi kwa mahabuba wangu.”
“Mambo si hayo.”
Brenda alikata simu na kuendelea kuchati na mashoga zake.
***
Sauti ya simu kuita ilimshtua Brenda aliyekuwa bado amelala, alipoangalia ilikuwa namba ngeni, aliipokea.
“Haloo.”
“Haloo, nazungumza na Brenda?”
“Ndiyo, nani mwenzangu?”
“Naitwa Ndubi rafiki mkubwa wa Hans.”
“Ndiyo Ndubi.”
“Kuna habari siyo nzuri.”
“Habari gani?”
“Hans amepata matatizo makubwa sana, nilijaribu kumpigia Mage simu yake haipatikani nikaona nikupigie wewe ili umjulishe.”
“Mmh! Matatizo gani?”
“Jana usiku wamevamiwa nyumbani kwake na majambazi, mkewe na mwanaye wameuawa na yeye hatujui kama yupo hai.”
“Mungu wangu! Yupo wapi kwa sasa?”
“Yupo hospitali ya muhimbili chumba cha wagonjwa mahututi.”
“Mungu wangu! Ngoja nimjulishe Mage.”
“Itakuwa vizuri.”
Baada ya simu kukatwa Brenda alimpigia simu Mage aliyekuwa bado yupo kwa mchumba wake Colin. Baada ya simu kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo Brenda mbona unaharibu pozi za watu,” Mage alisema kwa utani.
Brenda hakupoteza muda alimweleza taarifa aliyopokea asubuhi ile, taarifa ile ilimshtua sana Mage.
“Mungu wangu! Yupo wapi?”
“Mihimbili.”
“Nakuja sasa hivi twende.”
“Noo, tutakutana hospitali.”
Mage alinyanyuka kitandani na kupitia nguo zake na kuvaa bila kuoga, hakutaka kumwamsha Colin aliyekuwa bado amepitiwa usingizi. Alitoka hadi kwenye gari lake na kuondoka kuelekea muhimbili kumuona Hans. Njia nzima alijilaumu kukataa kusikiliza wito wa Hans kwa kuamini kuna kitu cha muhimu alitaka kumweleza.
Alijiuliza Hans alitaka kumweleza nini na kwa nini alilazimisha waonane usiku wa jana yake kisha asubuhi asikie habari kama zile za kushtusha.
“Mungu wangu kama Hans atakuwa amekufa atakufa na kinyongo, sikutakiwa kuwa katili kiasi kile. Japokuwa sikuwa tayari kurudiana naye lakini nilitakiwa kumsikiliza.”
Mage alikuwa kwenye lindi la mawazo juu ya Hans kuwa katika hali ile. Alijikuta akitokwa na machozi kumlilia. Alijiuliza kama ndiye yeye angekuwa mke wa Hans na tukio lile likatokea ina maana angekufa yeye.
Kutokana na mawazo mengi alijikuta akiendesha gari pasipo umakini, alifunga breki mbele ya gari lililosimama baada taa nyekundu kuwaka za makutano ya barabara ya Oceon na Upanga. Alikanyaka breki kwa nguvu zote huku akifumba macho na kuuma meno. Gari lilisota na kwenda kujigonga kidogo kwenye Land Cruser la Mwarabu.
Kelele za breki zilifanya watu wote kugeuka kuangalia, askari wa barabarani alifika lakini Mwarabu hakutaka kesi kwa vile gari lake halikuharibika sehemu yoyote. Aliliruhusu na kumfuata Mage kumuuliza:
“Vipi mbona hivyo?”
Mage alishindwa kumjibu kwa vile presha ilikuwa juu na uso ulikuwa umejaa machozi. Askari hakutaka kumuhoji kitu alimruhusu kuondoka. Mage aliondoa gari kuingia barabara ya Upanga kuelekea Muhimbili kumuona Hans.
Njia nzima Mage alikuwa akilia, alikumbuka maisha aliyoishi na Hans, mwanaume akiyempenda kuliko kitu chochote chini ya jua. Waliishi maisha ya mapenzi kama njiwa, kila mmoja alimpenda mwenzake penzi la glasi halikuwa na kificho kila mmoja aliamini anapendwa na mwenzake.
Alikumbuka ahadi ya Hans alipomwambia kumuacha yeye ni sawa na roho kuachana na mwili. Alimuhakikisha yeye ndiye mwanamke wa maisha yake. Baada ya Hans kuozwa kwa shinikizo la wazazi, walikubaliana avumilie ili baadaye amuache mwanamke wa kulazimishwa ikiwa pamoja na kuitozaa naye.
Lakini Hans alionekana kugeuka pale alipopata mtoto ndani ya ndoa yake tofauti na walivyokubaliana kutozaa na yule mwanamke na kwenda kinyume na kumfanya naye akubali kuolewa na Colin.
Alijiuliza nani aliyefanya kitendo kile, alijikuta akitengeneza mawazo ya kijiunga kuwaza labda mpango ule kaufanya Colin kutokana na wasiwasi wa kurudiana na Hans.
“Nikigundua Colin kama ndiye aliyemuua mpenzi wangu, nitamchukia mpaka kufa na nitakuwa shahidi namba moja kuhakikisha na yeye ananyongwa,” Mage aliwaza.
Alipofika Muhumbili alisimamisha gari na kuelekea kwenye wadi ya wagonjwa mahututi. Nje ya wadi aliikuta familia ya Hans, hakuna aliyemjali japokuwa alionekana amevimba macho kutokana kumlilia Hans.
Alipojaribu kuingia wadini alikatazwa na kuamua kusimama pembeni peke yake, baada ya muda shoga yake Brenda alifika na kwenda aliposimama.
“Vipi shoga?”
“Yaani mama Hans kanifukuza kama mbwa!”
“Kwa nini?”
“Hata sijui wakati anafahamu mimi na mwanaye tulikuwa vipi.”
“Kwa hiyo hujui hali ya Hans?”
“Sijui chochote.”
Mara simu ya Mage iliita alipoangalia ilikuwa ikitoka kwa Colin, aliitazama na kukunja uso bila kuipokea. Brenda aliyekuwa akimtazama usoni alimuuliza.
“Simu ya nani?”
“Achana nayo,” alijibu kwa mkato.
“Mmh!”
Baada ya muda simu iliita tena, Brenda alishtuka kuona jina la Colin bila kupokelewa.
“Shoga mbona hupokei?”
“Achana naye.”
“Ha! Wewe si ulikuwa kwa Colin na umeondokaje?”
“Sijamuaga nimemuchana bado amelala.”
“Unajua unacho kifanya unaiweka ndoa yako njia panda.”
“Kwani asiponioa nitapungukiwa nini?” Mage alijibu huku akibinua midomo.
“Mage, usipoteze muda wa Colin, kuamini unampenda kumbe upo naye kivuli tu.”
“Brenda mwenye uamuzi wa kumpenda nani ninao mimi.”
“Kwa hiyo Colin si chaguo lako?”
“Brenda huu si wakati wa kuzungumzia Colin zaidi ya kujua hali ya Hans ndiye aliyetuleta hapa.”
“Mmh! Sawa.”
ITAENDELEA

No comments