Header Ads

WAKILI WA MOYO - 08


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Brenda mwenye uamuzi wa kumpenda nani ninao mimi.”
“Kwa hiyo Colin si chaguo lako?”
“Brenda huu si wakati wa kuzungumzia Colin zaidi ya kujua hali ya Hans ndiye aliyetuleta hapa.”
“Mmh! Sawa.”
SASA ENDELEA...
***
Colin baada ya kushtuka usingizini alijua mpenzi wake yupo msalani au bafuni, lakini muda ulikatika bila kuonekana. Alikwenda msalani kumtafuta huku akimwita bila kupata jibu. Alitoka hadi nje na kumuuliza mlinzi.
“John umemuona shemeji yako?”
“Ametoka asubuhi sana, hakukuaga?”
“Ameniacha nimelala.”
“Tena alionekana kama analia nilijua mmegombana.”
“Hata sielewi kitu.”
Colin alimpigia simu mchumba wake, lakini iliita bila kupokelewa. Alirudia zaidi ya mara tatu vilevile haikupokelewa. Alijiuliza Mage amepatwa na nini, wasiwasi wake labda kwao kumetokea tatizo. Aliingia ndani na kuvaa pensi na fulana chini alivaa ndala na kuingia kwenye gari kuelekea Kigamboni kwa kina Mage ili ajue amepatwa na nini.
Alikimbiliza gari, kutokana na foleni aliamua gari lake kulipaki Posta ya zamani na kuchukua bodaboda ili awahi kuifika. Baada ya kuvuka alichukua nyingine iliyo mpeleka nyumbani kwao Mage.
Alimlipa dereva na kuingia ndani ya geti, alipofika sebuleni alimkuta msichana wa kazi akifanya usafi.
“Habari Sofi?”
“Nzuri shemu, shikamoo.”
“Marahaba, vipi Mage yupo?”
“Sijamuona toka asubuhi.”
“Mama.”
“Yupo chumbani kwake.”
“Kaniitie.”
Colin alibakia sebuleni kumsubiri mama Mage, baada ya muda alitokea na kushangaa kumuona Colin katika hali ile.
“Vipi baba, kwema?”
“Kwema, sijui hapa.”
“Hapa hatujambo, mwenzio yupo wapi?”mama Mage alimuulizia mwanaye baada ya kumuona Colin peke yake.
“Nimeshtuka kitandani sikumkuta, nimempigia simu haipokelewi, nikawa na wasiwasi na kuamua kuja huku.”
“Hapa sijamuona, atakuwa amekwenda wapi? Mmh! Basi atakuwa kwa Brenda tu.”
Colin alipiga simu kwa mara nyingine lakini haikupokelewa, alirudia mara mbili vilevile haikupokelewa baadaye ikazimwa kabisa.
“Mama simu haipokelewi niliporudia imezimwa kabisa.”
“Mmh! Atakuwa wapi mtoto huyu la..”
Mama yake alinyamaza baada ya kumuona mwanaye akiingia, wote walipeleka macho kwake. Walishtuka kumuona macho yake yamevimba kuonesha alikuwa akilia.
Aliwapita bila kuwasemesha na kuelekea chumbani kwake kitu kilichomshtua mama Mage na kumuuliza Colin.
“Colin umemfanya nini mwanangu?”
“Mama sijamfanya kitu, si umuulize mbele yangu.”
Mama Mage alimfuata mwanaye chumbani na kumkuta amejilaza kwa kulilia tumbo.
“Mage.”
“Abee.”
“Kuna nini?”
“Hans ana hali mbaya asishangae kusikia amefariki.”
“Amefanya nini?”
“Amevamiwa na majambazi, mke wake na mwanaye wameuawa.”
“Mungu wangu! Ndipo unapotoka?”
“Ndiyo, mama.”
“Mbona hukumuaga mwenzio?”
“Ningemuaga nakwenda wapi?”
“Na mbona umempita bila kumsalimia.”
“Nitamweleza nini?”
“Kwa hiyo itakuwaje?”
“Mwambie aondoke siwezi kuzungumza naye chochote kwa sasa.”
“Magee, unajua Colin ni nani yako?”
“Mchumba wangu na mume wangu mtalajiwa, lakini kwa leo naomba aniache nitamtafuta mwenyewe.”
“Mage, unajua unanitafutia lawama, Colin atatuelewa kweli?”
“Mama tumia kila uwezavyo ili Colin aondoke nitamtafuta.”
“Unanitia kwenye ubaya, Mage unaibomoa ndoa yako kwa mikono yako, unapoteza uaminifu kabla ya ndoa.”
“Mama ndoa ni zawadi toka kwa Mungu, kama si riziki yangu siwezi kuilazimisha.”
“Mmh! Sawa wacha nikajaribu,” mama Mage alitoka chumbani na kumwacha mwanaye amejilaza huku akiwa na mtihani wa kumweleza Colin ili aondoke bila kuhoji kitu.
Colin alibakia sebuleni akiwaza kipi kimempata mchumba, alijiuliza alikwenda wapi asubuhi ile mchumba wake kama hakurudi nyumbani na kwa nini ameonekana analia kipi kimemsibu. Alibakia kusubiri kwa hamu kujua kipi kimemsibu mchumba wake, ambaye aliamini ndiye moyo wake yeye alibakia na mwili tu.
Mama Mage alirudi hadi sebuleni, Colin aliyekuwa ametazama juu akiwa mwingi wa mawazo kutokana na kilichotokea asubuhi ile. Aliposikia sauti ya miguu ikisogea alipokuwa amekaa aliyahamisha macho yake na kumuona mama Mage, alijikuta akinyanyuka kama anampokea mheshimiwa.
“ Vipi mama?”
“Mmh! Safi tu,” Mama Mage alijibu huku akijitahidi kutengeneza uso wa mbuzi ili aweze kutengeneza mambo hasa kutokana kuwa mzazi.
“Vipi Mage alikuwa wapi na amepatwa na nini?” Colin aliuliza akiwa amemkazia macho.
“Mmh! Si..si..au fanya hivi, baba wewe nenda nyumbani mpenzi wako kuna mambo yao ya kitoto si unajua baba mwenzio bado mdogo?”
“Ndiyo najua, lakini amepatwa na nini na alikwenda wapi bila kuniaga ikiwa hawa wewe hujui?”
“Mwanangu, wala hakuna jambo la kutisha, u..u..najua mwenzio, baba eeh, hebu kwanza hili tuliache jioni mwenyewe atakueleza kila kitu,” mama Mage alijitahidi kubadili mazungumzo.
“Sawa mama, lakini Mage ni mchumba wangu ninatakiwa kujua kila kitu chake, sasa hivi ni mke wangu, tumetenganishwa na ndoa tu ambayo haipo mbali. Hivi nirudi nyumbani namweleza mama nilichokikuta hapa kisha naulizwa kimetokana na nini nitajibu nini?” Colin alitetea hoja yake.
“Mwanangu ngoja nikutoe wasiwasi, mwenzio alikwenda kwa shoga yake sijui nini anamdai, basi wametibuana ndiyo maana yupo vile,” mama alitengeneza uongo.
“Sasa mama kama ni hivyo kwa nini hataki kuzungumza na mimi?”
“Colin mwanangu, mi mkubwa naomba uondoke ili jioni uzungumze vizuri na mwenzako. Atakachokuambia hata wewe utacheka.”
“Mmh! Sawa, basi mi’ naondoka.”
Colin alisema huku akinyanyuka kuelekea nje, alipofika nje alikodi bodaboda hadi Kivukoni ambako alivuka upande wa pili na kukodi bodaboda nyingine hadi kwenye gari lake na kuingia ndani.
Kabla ya kuondoka alitulia mikono aliweka juu usukani na macho aliangalia mbele, alikuwa kama anaona lakini alizama kwenye mawazo na kujiuliza Mage alikwenda wapi bila kuaga na kwa nini amerudi akilia kipi kimempata alipokwenda na mwisho alijiuliza kwa nini amekataa kuzungumza naye.
Baada ya kukosa majibu ya maswali yake aliondoa gari kuelekea nyumbani, alitembea mwendo wa kawaida huku akili yake ikiwa haijakaa sawa. Alipofika katika makutano ya barabara ya Kawawa na Morogoro macho yake yalishtuka kumuona msichana mmoja akiuza ndizi.
Sura yake haikuwa ngeni machoni mwake lakini mavazi yalifanya macho yapingane na akili yake. Sura ilikuwa ya Cecy lakini mavazi yake yalikuwa machakavu na mwili ulimvaa vumbi kwa ajili ya kutembea barabarani kwa miguu kuuza ndizi. Kwa vile alikuwa kwenye foleni alituliza macho yake kwa binti yule ambayo yalimwambia ni Cecy.
Wakati anataka kuondoa gari alisikia mtu akimwita.
“Cecy leta ndizi mbili.”
Kwa vile taa ziliruhusu aliliondoa gari na kwenda kulipaki kituo cha mafuta cha Magomeni, alilizima na kutoka nje, kwa vile Cecy alikuwa amevuka barabara kwenda kuuza ndizi maeneo ya Hospitali. Alimtuma kijana mmoja aliyekuwa akiuza miwa.
“Samahani mkubwa, naomba kwamwambia yule msichana alete ndizi kumi.”
Yule kijana alimfuata Cecy aliyekuwa ametua beseni lake chini akiuza ndizi, alipofika alimwambia.
“Dada peleka ndizi kumi kwenye lile gari.”
“Kumi hazitafika zitabaki sita.”
“Mpelekee zote.”
“Sawa, ngoja nichukue hela.”
Baada ya kuuza alibeba beseni lake na kuvuka barabara mpaka kwenye gari, kioo cha gari kilikuwa kimepandishwa kidogo hivyo hakumuona aliyekuwa kwenye gari. Aligonga kioo kidogo ili auze ndizi.
“Kaka.”
Colin aliteremsha kioo na kufanya Cecy amuone vizuri kitu kilichomfanya ashtuke.
“Ha! Colin?” mshtuko alioupata ulifanya adondoshe beseni la ndizi.
Hakuliokota alibakia amesimama mpaka Colin alipoteremka kwenye gari na kuokota ndizi zote kisha alimshika mkono Cecy.
“Cecy.”
“Abee,” Cecy aliitikia huku machozi yakimtoka na mwili kumtetemeka.
“Unalia nini mchumba?”
“Colin mimi si mchumba wako, mchumba wako Mage,” Cecy alijibu kwa ukali kidogo.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Mama yako amechotufanya kwa ajili yako, Colin lini nilikutamkia nakupenda?”
“Hujawahi hata siku moja.”
“Kwa nini mama yako amefunga safari ya kuja kunituka kuwa naingilia ndoa yako na kutudhalilisha kwa ajili ya umaskini wetu. Colin maskini hapendi?”
“Anapenda.”
“Ni kweli Colin nakupenda zaidi ya kukupenda, nailaumu nafsi yangu kuchelewa kukueleza ukweli kuwa nakupenda. Najua haikuwa bahati yangu unayetaka kumuoa ndiye chaguo la moyo wako. Kipi kilichomtuma mama yako kuja kunitukana na kutudhalilisha bahati yake sikumkuta najua ningemfanya nini!” Cecy alisema kwa sauti ya hasira.
“Lini?”
Cecy alimtajia siku na kukumbuka siku ambayo Colin alikumbuka ndiyo siku aliyokamata picha kumbe alikwenda kumtukana Cecy bila kutaka kuujua ukweli.
“Cecy samahani sana, pia pole kwa kushindwa kuujua upendo wako.”
Alimweleza ukweli juu ya uchumba wake na Mage alivyotengenezwa na mama yake.
“Kwa hiyo Mage si chaguo lako ni la mama yako?”
“Hapana, mwanzo lilikuwa chaguo la mama baada ya kumuona nilikubaliana naye na ndiyo tulipanga kuoana.”
“Kwa hiyo siku ile uliniita kuja kunidhalilisha na kuumiza moyo wangu?”
“Hapana nilikualika kama wageni wengine, pia nina mpango mkubwa sana kwako ambao utakusaidia kimaisha.”
“Colin mpango ambao naukubali kwako labda niwe mkeo lakini zaidi ya hapo usijisumbue,” Cecy alisema kwa sauti ya kike kwa kujiamini.
Colin alijitahidi kumwelewesha sababu ya picha zake na kipi alichokipanga juu yake.
“Hivi leo hii nifanye kazi kwenye kampuni yetu mama yako atakubali anajua sisi ni wapenzi, kuna kazi?”
“Kwanza hebu nieleze sababu ya wewe kuwa kwenye hali hii?” Colin alimuuliza huku akiangalia mavazi na hali aliyokuwa nayo Cecy.
“Sina thamani haya ndiyo maisha niliyoyachagua ili mama yako akiniona asiwe na wasiwasi na ndoa yako.”
“Cecy nitakutafuta tuzungumze akili yako ikitulia.”
“Usijisumbue.”
“Lazima nijisumbue kwako kwa vile kuna kitu ndani yako nilichokiona.”
“Colin niache nirudi nyumbani.”
“Unakaa wapi nikupeleke.”
“Colin unataka mama yako aje kuchoka pagala letu, aliona picha ikawa vile vipi anione kwenye gari lako?”
“Hawezi, na ungeniambia alichokifanya ningempa ukweli, tabu ya kina mama wa kiswahili wazungu hawajali vitu vya kijingakijinga.”
“We nenda tu.”
Itaendelea siku ya keshooooooooooooo

No comments