Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 11


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Wazo lile alimwambia mama yake ambaye naye aliliafiki, jioni ilipofika alikwenda sehemu moja iliyokuwa ikifundisha twisheni na kuomba kusoma kingereza ambacho aliahidiwa kukijua baada ya miezi mitatu. Alilipa ada na kuanza kusoma siku ileile huku akiwa na ndoto za siku moja naye kuzungumza kingereza.
SASA ENDELEA...
***
Mipango ya harusi ya Colin na Mage ilizidi kupamba moto huku kila familia ikijipanga kufanya sherehe ya kufuru. Nayo Hali ya Hans iliendelea vizuri iliyofanya atolewe hospitali na kurudishwa nyumbani. Baada ya kutulia kwa wiki moja aliitwa polisi kutoa maelezo kutokana na tukio lililomtokea lililopeleka kupoteza mke na mtoto.
“Pole sana,” Inspekta Koleta alianza kwa kumpa pole.
“Asante.”
“Unajisikiaje kwa sasa?”
“Namshukuru Mungu sijambo kabisa.”
“Unakumbuka tukio lilivyotokea?”
“Ndiyo, nilikuwa chumbani mke na mwanangu wakiwa sebuleni ghafla nikasikia sauti kama ya amri, mwanzo nilifikiri labda sauti inatoka kwenye tivii kwa vile alikuwa akiangalia tamthilia. Lakini sauti ya maumivu ya mke wangu ilinishtua na kunifanya nitoke chumbani. Nilishtuka kuona mke na mwanangu wamelala chini.
“Nilipotaka kwenda kuwasaidia nilipigwa na kitu kizito kichwani kilichonifanya nipoteze fahamu. Nilipozinduka nilijikuta nipo hospitali na kupewa taarifa za kushtusha za kifo cha mke wangu na mwanangu,” Hans alipofika hapo alianza kulia na kumfanya Inspekta Koleta kumbembeleza.
“Pole sana.”
“Asante, lakini inauma sana heri wangeniua mimi kuliko mke na mwanangu!”
“Najua inauma, unawafahamu waliofanya unyama ule?”
“Kwa kweli siwafahamu kutokana na kuziba nyuso zao na kofia za kuziba kichwa.”
“Unamjua Mage?”
“Mage yupi?”
“Wewe unamjua Mage yupi?”
“Mmh! Mmoja.”
“Yupi?”
“Aliyewahi kuwa mpenzi wangu.”
“Unamfahamu vipi?”
“Alikuwa mpenzi wangu, lakini bahati mbaya nilioa mwanamke mwingine badala yake.”
”Kwa sasabu gani ulioa mwingine na kumuacha mpenzi wako wa muda mrefu?”
“Wazazi wangu walikuwa hawamtaki.”
“Unafikiri kitendo cha wazazi wako kumkataa Mage na kumchukua mwanamke mwingine kilimpandisha Mage hasira na kuamua kukukomoa?”
“Walaa, yule msichana hausiki kabisa.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Sasa hivi yupo katika mipango ya harusi anategemewa kuwa mke wa mtu afanye vile ili iweje?”
“Kwa hiyo huna mtu yeyote unayemshuku?”
“Mmh! Hakuna,” Hans alikataa.
“Basi tukikuhitahi tutakuita.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya mahojiano yale Hans aliruhusiwa kuondoka, alirudi kupumzika nyumbani. Kila alipokaa peke yake moyo aliendelea kuumia bila kuonana na Mage na kumweleza neno lililo moyoni mwake kabla ya kuolewa.
Aliamini kwa vile ulikuwa umebakia mwezi mmoja na nusu harusi ifungwe ingekuwa vigumu kuonana ana kwa ana. Wasiwasi wake ulikuwa kutopata nafasi baada ya kupata taarifa kwenda kumuona hospitali na kufukuzwa kisha kufunguliwa shtaki la kuishambulia familia yake. Aliamini Mage hatakuwa tayari kumsikiliza.
Alijaribu kumpigia shoga yake Brenda ili amsaidie aweze kuzungumza naye hata kwa dakika mbili kisha moyo wake uwe radhi Mage kuolewa. Alichukua simu yake na kumpigia Brenda ambaye aliipokea upande wa pili.
“Haloo.”
“Haloo Brenda.”
“Abee, nani mwenzangu?”
“Hans.”
“Hans yupi?”
“Shemu kweli umenichoka yaani leo unaniuliza hivyo?”
“Ha! Kumbe wewe? Vipi unaendeleaje?”
“Nipo fiti kama chuma.”
“Wewee! Utani huo upo wapi?”
“Nyumbani, kwanza niwapeni pole kwa kitendo cha familia yangu kuwazuia kuniona kimeniuma sana kwa hiyo nakuombeni radhi sana.”
“Hans wewe siku zote huna kosa, familia yako ndiyo kikwazo katika maisha yako.”
“Hilo nalijua.”
“Hans mtoto bado ana mapenzi na wewe baada ya taarifa zile kachanganyikiwa mbio hospitali lakini walichomfanya familia yako hawezi kusahau kibaya zaidi wamempakazia tatizo lako.”
“Yaani wamenichanganya ile mbaya, Brenda naomba unikutanishe na Mage ili nimuombe msamaha.”
“Mmh! Sijui kama utampa kwa vile sasa hivi yupo katika maandalizi ya ndoa yake.”
“Sikiliza Brenda naomba nikupitie kwenu twende hadi nje ya nyumba yao Mage kisha uje naye nizungumze naye kwa dakika tano kisha nikurudishe nyumbani kwenu. Nakuahidi zawadi nzuri ukiniwezesha kumuona Mage kwa dakika hata mbili tu.”
“Mmh! Kwani sasa hivi upo wapi?”
“We nieleze nikufuate wapi?”
“Njoo home basi.”
“Fanya hivi chukua gari la kwenu tukutane Kivukoni.”
“Haina tatizo.”
Hans baada ya kuelezwa vile alitoka na kuingia kwenye gari aina ya Toyota Verosa na kuelekea Kigamboni kwa kina Mage. Alipofika Kivukoni hakukaa sana simu yake iliita ilikuwa ya Brenda, aliipokea.
“Haloo Brenda.”
“Hans nimefika, upo wapi?”
“Nami nimefika umekuja na gari gani?”
“Nissan Patrol nyeupe.”
“Basi tuvuke.”
Walikubaliana kuvuka upande wa pili, baada ya watu na baadhi ya magari kujaa ndani ya kivuko safari ya kuelekea Kigamboni ilianza. Kivuko kiliposimama upande wa Magogoni, watu waliteremka na kuelekea maeneo ya Kigamboni, Mji mwema mpaka Geza ulole na kwingineko.
Brenda alitangulia baadaye aliliona gari la Hans likija nyuma, hakusimama aliendelea na safari mpaka karibia na kwa kina Mage alisimamisha gari pembeni Hans naye alisimamisha pembeni yake na kuteremka.
Hans na Brenda walikumbatiana na kupeana pole upya huku Brenda akiwa haamini kama Hans amepona.
“Dah! Pole sana.”
“Asante.”
“Sasa inakuwaje?”
“Fanya hivi hili gari langu tuliache sehemu salama ili twende na lako tukifika utaingia ndani kwenda kumuita akija utamuingia kwenye gari lako najua atashangaa kuniona lakini nitatumia muda huo kuzungumza naye kisha atarudi ndani mwao na sisi tuondoke.”
“Hakuna tatizo.”
Hans alilipaki gari lake sehemu ya usalama na kuingia kwenye gari la Brenda hadi nyumbani kwao na Mage. Alipofika alilisimamisha gari pembeni ya geti hakutaka kuliingiza ndani na kuteremka. Mlinzi alishangaa kuliacha gari nje na kumuuliza.
“Da’ Brenda mbona huingizi gari ndani?”
“Hapana sikai sana,” Brenda alijibu huku akiingia ndani ya geti.
Alitembea kwa mwendo wa kukimbia hadi ndani, alimkuta msichana wa kazi akiondoa vyombo mezani na kumuuliza.
“Mage yupo wapi?”
“Chumbani kwake.”
Alikwenda hadi chumbani na kugonga.
“Ingia,” sauti ya Mage toka ndani ulisema.
Brenda alisukuma mlango na kuingia ndani Mage alishtuka kumuona shoga yake muda ule, kwa vile hawakuwa na miadi ya kukutana muda ule wakati mchana wa siku ile walikuwa pamoja na kuachana jioni.
“He! Vipi mbona huku muda huu?” Mage alimshangaa Brenda.
“Shoga hebu twende nje mara moja.”
“Kuna nini?”
“Utajua huko, we twende mara moja.”
Mage bila kuongeza neno alinyanyuka kitandani na kuongozana na Brenda hadi nje, alishangaa kuona wanatoka nje ya geti. Lakini hakuhoji alisubiri kuona Brenda kamuitia nini. Alipotoka nje ya geti aliliona gari la Brenda, kwa vile alikuwa akisubiri muda wa kwenda kwa Colin na alichelewa kwenda kutokana na mama yake kutoka alimwambia shoga yake.
“Brenda siwezi kufika mbali namsubiri mama ili niende kwa mume wangu.”
“Hata huendi popote twende ndani ya gari.”
“Kuna nini?”
“Hebu punguza maswali.”
Waliongozana wote hadi kwenye gari.
“Ingia mlango wa nyuma,” Brenda alimwambia Mage, naye hakubisha aliingia.
Ndani ya gari palikuwa giza, Brenda baada ya kuingia mbele aliwasha taa na kumfanya Mage ashtuke kumuona Hans.
“Ha! Hans?”
“Ndiyo mimi Mage samahani kwa kukushtukiza.”
“Bila samahani, kwanza unaendeleaje?”
“Namshukuru Mungu sijambo kabisa.”
“Pole na kufiwa mke na mtoto.”
“Asante, pole na wewe kutokana na ulichotendewa na familia yangu.”
“Hans achana na hayo yameisha pita, nina imani kuna kitu kimekuleta naomba tuzungumze kwa haraka nataka kwenda kwa mume wangu muda si mrefu.”
Hans alijikuta akitulia huku maneno yakigoma kutoka mdomoni, Mage alishangaa kuona mpenzi wa zamani akitokwa na machozi. Brenda alitoka nje ya gari na kuwaacha wapenzi ndani ya gari wazungumze yao.
“Jamani nipo nje.”
“Hakuna tatizo, usikae mbali natoka sasa hivi,” Mage alisema.
Baada ya kutoka Mage alimuuliza Hans aliyekuwa akitokwa machozi.
“Hans ameniita kuona machozi yako au kuna kitu kingine kama ni machozi nimeisha yaona, naomba niende zangu,” Mage alizungumza kwa sauti ya upole huku akimtazama usoni Hans.
“Ma..ma..ge,” Hans alisema kwa kigugumizi.
“Jina langu.”
“Kilichonileta si kuja kukuonesha machozi bali moyo wangu umejaa maumivu makali.”
“Najua inauma kupoteza mke na mtoto si kitu cha kawaida yataka moyo wa chuma kuyashinda maumivu yake lakini Mungu siku zote ni mfariji na kukufanya utayasahau yote kisha atakuletea mke mwingine.”
“Mage mimi na wewe tuliahidiana nini?”
“Kuoana kuwa mke na mume.”
“Baada ya matatizo ya familia yangu nilikueleza nini?”
“Ulisema huwezi kuzaa na yule mwanamke, baadaye utamuacha na kunioa mimi.”
“Kwa nini umekubali kuolewa na mwanaume mwingine?”
“Kwa sababu umevunja ahadi yetu.”
“Mage nina imani unajua jinsi gani ninavyokupenda?”
“Siyo unavyonipenda bali ulivyokuwa ukinipenda.”
“Mage moyo wangu hautachoka kukupenda, nilikueleza nini baada ya kulazimishwa kuoa mwanamke mwingine?”
“Ulisema wakikulazimisha kuoa utajiua.”
“Ulinishauri nini?”
“Nilikuwa radhi uoe lakini si kukupoteza maishani, ulichoniahidi ndicho kilinipa moyo na kuwa radhi kukusubiri hata miaka mia. Lakini wewe ndiye ulivunja mkataba na kuamini sina changu na kuamua nami kutafuta wangu japokuwa ilikuwa sawa na kunimezesha mfupa.”
“Ndiyo sababu ya mimi kuja kuzungumza na wewe, baada ya kunisikiliza uamuzi utakaoutoa hapa sitapingana nao hata kama utaniumiza.”
“Haya niambie hicho kilichokuleta.”
Hans alianza kuzungumza kwa sauti ya chini yenye kusikika huku machozi yakiweka michirizi kwenye mashavu. Mazungumzo yalikuwa (Of air) ambayo hayakutakiwa mtu yeyote kusikia zaidi ya watu wawili tu. Hans alimaliza kuzungumza huku machozi na kamasi zikimtoka chapachapa.
Muda wote Mage alijitahidi kumbembeleza Hans japokuwa naye alikuwa akilia.
“Hans nimekuelewa lakini hukutakiwa kufanya hivyo.”
“Sikuwa na jinsi, hukutaka kunisikiliza nilikuwa na wakati mgumu wa kuweza kunisikiliza. Kama ningekufa bila wewe kuujua ukweli wa moyo wangu ningekuwa nimekufa kibudu. Kama ningeshindwa kabisa ningekuja kujiua kwenye harusi yako ili ujue nilichokuahidi hakitabadilika moyoni mwangu kuwa kifo pekee ndicho kitanitenganisha na wewe.”
“Mmh! Mbona Hans unanipa mtihani mkubwa, japokuwa uamuzi ni wangu lakini dunia itanitenga.”
“Lakini Mage nilikueleza kila kitu juu yetu, wewe ndiye uliyeshikilia uhai wangu kwa mara nyingine wa kuniua au kuniacha hai ni wewe.”
“Hans hata siku moja kifo chako hakitatoka mikononi mwangu, naombani uniache kwa leo mengine tutazungumza kesho kichwa changu kimevurugika hata sielewi jifanye nini.”
“Ila kumbuka uhai wangu umeubeba wewe.”
“Naelewa Hans.”
“Kwa hiyo niondoke na jibu gani?’
“Niache kwa leo, nimekuelewa Hans.”
“Sawa lakini bado nipo njia panda.”
“Hans kuwa muelewa nimekueleza nimekuelewa unataka nini tena?”
“Basi nashukuru.”
“Nikutakie usiku mwema.”
“Na kwako pia.”
Mage aliteremka kwenye gari na kumuaga shoga yake huku akifuta machozi yaliyokosa kizuizi kisha alielekea ndani mwao. Brenda aliingia ndani ya gari na kushangaa kumkuta Hans akifuta machozi wakati Mage naye alitoka akifuta machozi.
“Vipi kuna usalama?”
“Kiasi.”
“Umeelewana?”
“Ndiyo.”
“Kwa hiyo tunaweza kwenda.”
“Ndiyo.”
Brenda aliwasha gari na kuliondoka kuelekea walipokuwa wameliacha gari la Hans, njiani alijaribu kudodosa kwani kila mmoja alionekana kulia.
Itaendelea

No comments