Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 12


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Mage aliteremka kwenye gari na kumuaga shoga yake huku akifuta machozi yaliyokosa kizuizi kisha alielekea ndani mwao. Brenda aliingia ndani ya gari na kushangaa kumkuta Hans akifuta machozi wakati Mage naye alitoka akifuta machozi.
SASA ENDELEA...
“Vipi kuna usalama?”
“Kiasi.”
“Umeelewana?”
“Ndiyo.”
“Kwa hiyo tunaweza kwenda.”
“Ndiyo.”
Brenda aliwasha gari na kuliondoka kuelekea walipokuwa wameliacha gari la Hans, njiani alijaribu kudodosa kwani kila mmoja alionekana kulia.
“Hans, Mage anasemaje?”
“Hana la kusema bali nilitaka tu kumfikishia ujumbe, nashukuru amenisikiliza.”
“Kwa hiyo roho yako umetulia?”
“Nashukuru, tukifika kwenye gari nitakupa zawadi yako niliyokuahidi.”
“Nitashukuru.”
***
Muda ulizidi kukatika bila Mage kuonesha dalili zozote za kutoka kwenda kwa Colin, kitu kiliochomshtua mama yake ambaye aliwahi kurudi kwa ajili ya mwanaye kwenda kwa mchumba wake. Aliangalia saa ya ukutani ilimuonesha inakaribia saa nne usiku, alijiuliza labda mwanaye ametoka bila yeye kujua.
Ilibidi amuulize msichana wa kazi kama Mage ametoka yeye akiwa chumbani.
“Sofi Mage ametoka saa ngapi bila kuniaga?”
“Mmh! Mama sijamuona kutoka.”
“Una maanisha yupo chumbani kwake?”
“Sijajua ila sijamuona.”
Mama Mage alinyanyuka na kwenda chumbani kwa mwanaye, alikuta mlango umerudishwa alisukuma na kuingia bila hodi na kumkuta Mage amejilaza akiwa amekumbatia mtu huku machozi yakimwagika kama maji. Mama yake alishtuka na kutaka kujua kuliko mwanaye kuwa katika hali ile.
“Mage! Nini mwanangu?”
“Mamaa..maamaa,” Mage alishindwa kuzungumza aliangua kilio.
“Mage una nini?” mama yake alizidi kumshangaa.
“M..m..maa..ma,” Mage kila alipotaka kusema maneno yaligoma kutoka mdomoni.
“Mage mwanangu umepatwa na nini, hebu nieleze mimi ndiye mama yako nipo tayari kukusikiliza na kukusaidia.”
“Mama nipo kwenye wakati mgumu sana maishani mwangu.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Najua nitakuudhi wewe mama yangu lakini nina imani ndiyo tiba sahihi ya moyo wangu ambao umekuwa matesoni kwa muda mrefu.”
“Una maanisha nini?” mama yake alishtuka mpaka mapigo ya moyo yalianza kumwenda kasi.
“Mama nitakacho kisema najua kitakuwa sawa na kumng’oa mtu jino bila ganzi.”
“Una maanisha nini?”
“Mama sitaki kuolewa tena.”
“Niniii?” mama alishtuka.
“Mama sitaki kuolewa na Colin.”
“Kwa nini?”
“Si chaguo la moyo wangu.”
“Mwanangu unasema ukweli au unatania?”
“Nasema kweli kabisa.”
“Mmh! Na mipango ya ndoa?”
“Tunasitisha kwa vile muda bado.”
“Na watu tuliowachangisha fedha za send of.”
“Tutawarudishia fedha zao.”
“Wee mwana tutazupata wapi?”
“Mi najua pa kuzipata.”
“Hebu mwanangu nieleza tatizo nini, kama Colin amekukosea bado tuna nafasi ya kuzungumza tukalimaliza.”
“Mama, Colin hajawahi kunikosea toka tujuane, ila mimi ndiye nimekuwa nikimkosea muda wote. Najua ananipenda sana na uamuzi wangu utamchanganya, lakini ukweli utabakia palepale si chaguo la moyo wangu. Nimejilazimisha kumpenda lakini moyo umekataa hivyo sina budi kuusikiliza moyo wangu unachotaka.
“Siku zote moyo wa mtu huwa ndiyo muamuzi kwa jambo lolote kwa vile wenyewe ndiyo unaopokea furaha kwa jambo zuri au huzuri kwa jambo baya.”
“Kwa hiyo unasema hujakosana na Colin?”
“Walaa, najua Colin ananipenda sana na ataumizwa na uamuzi wangu lakini sina jinsi kila ndege hutua mtu aupendao.”
“Mage upo sawa mwanangu?”
“Nipo sawa mama.”
Kauli ile ilimfanya mama yake akae kwenye kitanda baada ya miguu kukosa nguvu.
“Mage mwanangu mbona sikuelewi, kipi kimekusibu mama?”
“Mama najua itakuwa vigumu kunielewa lakini utanielewa tu.”
Mara simu ya Mage iliita, aliichukua na kuitazama na kuirudisha bila kuipokea kitu kilichomfanya mama yake kuuliza.
“Mbona upokei kwani inatoka wapi?”
“Kwa Colin.”
“Sasa kwa nini hupokei?”
“Sasa nitazungumza naye nini?”
“Pokea mwambie leo huwezi kwenda hujisikii vizuri.”
“Siwezi kuzungumza naye kwa leo, nitajisikia vibaya.”
Simu iliita tena lakini haikupokelewa mpaka inakatika, baada ya muda msichana wa kazi alimwita mama Mage kuwa kuna simu yake inaita. Alitoka na kuichukua ilikuwa inatoka kwa mama Colin, aliipokea mara moja.
“Haloo dada.”
“Eeh! Kuna usalama huko?”
“Kiasi.”
“Kulikoni?”
“Mage kichwa kilimshika ghafla.”
“Jamani mkwe wangu! Vipi hali yake?”
“Kidogo hajambo amelala kwa sasa.”
“Basi tunakuja kumuona.”
“Usisumbuke, alitaka kuja nikamzuia hayupo serious sana.”
“Basi augue pole maana mwenzake alikuwa na wasiwasi baada ya kupiga simu isipokelewe.”
“Mwambie asiwe na wasiwasi ni kichwa tu lakini anaendelea vizuri kesho atakuwa hajambo.”
“Basi niwatakie usiku mwema.”
“Na ninyi pia.”
Mama Colin baada ya kumaliza kuzungumza alimgekia mwanaye aliyekuwa pembeni ya mama yake akifuatilia mazungumzo yale.
“Vipi mama?”
“Kumbe kichwa kilimshika ghafla amekunywa dawa kimetulia, alitaka kuja lakini mama yake kamwambia alale kwa leo atakuja kesho.”
“Duh! Afadhali, nilikuwa na wasiwasi sana.”
“Kapumzike, kesho mchumba wako atakuja.”
“Sawa mama.”
Colin alikwenda chumbani kwake, kabla ya kulala alichukua simu yake na kuangalia picha zote alizopiga na Mage na nyingine iliyopigwa siku ile mchana aliyotumiwa na Mage alipokuwa na shoga yake Brenda Mlimani City Samakisamaki. Aliibusu picha picha kubwa ya mpenzi wake aliyokuwa katika tabasamu la kufa mtu na kusema kwa sauti ya chini.
“Mage wewe ndiye mke wa maisha yangu,” aliikumbatia na kujilaza.
***
Mama Mage usingizi uligoma kabisa na kukiona kichwa kikitaka kupasuka kutokana na kuchanganywa na kauli ya mwanaye, alijiuliza kama mwanaye atasimamia uamuzi ule angeuweka wapi uso wake. Wasiwasi wake huenda amemfumania Colin na mwanamke mwingine na kuamua kuvunja uchumba.
Bado aliona kama ni hivyo linazungumzika kwa vile wote wamejuana wakiwa tayari wanayajua mapenzi. Alinyanyuka kitandani na kutoka kwenda kwa mwananaye kupata ukweli kwani alikuwa amechanganyikiwa sana. Alitoka taratibu taa ya sebuleni zilikuwa zimezimwa kulikuwa na hali ya ukimya kutokana na watu wote kuwa wamelala.
Hakutaka kuwasha taa ya sebuleni alitembea taratibu hadi chumba cha Mage alipotaka kuushika mlango alimsikia mwanaye akizungumza na simu alitulia ili asikilize anazungumza nini na nani. Alimsikia mwanaye akisema:
“Kama hivyo nimeisha litibua yote kwa ajili ya mapenzi yangu mazito kwako, kama umemejitoa muhanga kwa ajili yangu nami sina budi kujitoa kwa ajili yako. Najua uamuzi wangu utamchanganya mama na yule mchovu lakini wewe ni zaidi yao wote nakupenda sana zaidi ya kukupenda.
“ Nipo radhi vyote duniani viondoke ubakie peke yako, please mpenzi usinitende kosa lako ni mauti yangu, nashukuru kwa kujali mapenzi yangu kwako. Asante mpenzi wangu naomba ulale usingizi mororo huku ukiniota. I love you and i need you in all my life, mmmmwa.”
Mama Mage alijiuliza mwanaye anazungumza na nani, wazo lake lilipelekea labda ni Hans, lakini hakukubaliana nalo kutokana na maumivu aliyoyapata mwanaye kutoka kwa Hans na familia yake. Wazo lilielekea huenda kapata mpenzi mwingine ambaye kamzidi kete Colin.
Alishangaa mabadiliko yake ya ghafla kwani mpaka saa tatu kasoro usiku mwanaye alikuwa na kimuhemuhe cha kwenda kwa mchumba wake Colin na kumuhimiza kuwahi. Lakini aliporudi alikuwa mambo yamebadilika ghafla kama saa sita mchana ugeuke kiza totoro na watu wasionane.
Alipata wazo la kwenda chumbani kwa Sofia msichana wa kazi kumuuliza kuna kitu gani kilitokea kabla ya kurudi na kusababisha hali ile. Alikwenda kugonga chumba cha msichana wa kazi aliyeamka.
“Abee mama.”
Mama Mage aliingia chumbani bila kusema kitu kisha alirudisha mlango na kumuuliza kwa sauti ya chini.
“Sofi.”
“Abee mama.”
“Eti nilipotoka, Mage alitoka?”
“Hapana hajatoka,” Sofi alikataa huku akitikisa kichwa.
“Colin alikuja?”
“Hapana.”
“Nani alikuja.”
“Mmh! Da’ Brenda.”
“Brenda si alikuja mchana na kuondoka na Mage?”
“Hata usiku alikuja na kwenda chumbani kwa dada Mage kisha walitoka nje baadaye nilimuona dada Mage akirudi peke yake huku ameshikilia kitambaa mkononi kama anafuta machozi lakini sikumtilia maanani.”
“Mmh! Sasa nimeelewa,” mama Mage alisema huku akishika mikono kiunoni.
“Kuna nini mama?” Sofi alishtushwa na kauli ya mama Colin.
“Kawaida, ila nimeelewa,” alisema huku akitoka chumbani kwa Sofi na kurudi chumbani kwake.
Alipoingia chumbani alichukua simu na kumpigia Brenda ili amwambie alimpeleka wapi mwanaye mpaka kugeuka ghafla na kumtia gharama na fedheha kubwa. Baada ya kupiga simu ya Brenda ulipokelewa upande wa pili.
“Haloo mama.”
“Brenda za saizi?”
“Nzuri mama.”
“Eti Brenda kumetokea nini mama?”
“Kuhusu nini?”
“Ulimpekeka wapi Mage?”
“Sijampeleka popote nilitoka naye nje mara moja akarudi ndani kujiandaa kwenda kwa shemeji Colin.”
“Unajua wewe ndiye umevunja ndoa ya Mage?”
“Kivipi mama?” Brenda alishtuka.
“Umemwambia nini Mage mpaka akakataa kuolewa, gharama za harusi utazilipa wewe?”
“Mama kwa nini unasema hivyo?” Brenda alishtuka.
“Haiwezekani kuja wewe ghafla na Mage kubadili uamuzi wa kuolewa.”
“Mamaa! Hebu subiri,” Brenda alikata simu na kumpigia Mage.
Baada ya kuita kwa muda simu ilipokelewa.
“Haloo Brenda afadhali umenipigia.”
“Mage kuna nini?”
“Nimevunja uchumba na Colin.”
“Mungu wangu! Kwa nini tena?”
“Nimepata tiba ya moyo wangu.”
“Mage unajua lawama zote nabebeshwa mimi?”
“Brenda walaa hilo halikuhusu, kila kitu kitaeleweka, nitazungumza na mama muda si mrefu.”
“Mage ndugu yangu naomba usivunje ndoa yako utaniweka mahari pabaya,” Brenda alimbembeleza Mage.
“Nitaolewaje na mtu nisiyempenda?”
“Mage leo yamekuwa hayo? Si ni wewe ndiye ulinihakikishia Colin ndiye tiba ya moyo wako?”
“Hakuwa tiba bali dawa ya kupunguza maumivu lakini Hans ndiye tiba kamili, kama alijitoa kwa ajili yangu nami sina budi kujitoa kwa ajili yake.”
“Colin anajua?”
“Hajajua ila sitaki mtu yeyote amwambie nitamwambia mimi mwenyewe nina imani tutaelewana tu.”
“Mmh! Mbona najuta kiherehere cha kumleta Hans!” Brenda alijua yeye ndiye chanzo cha yote yaliyotokea.
Alijiuliza Hans alimweleza Mage kitu gani kilichomfanya abadili ghafla uamuzi wa kuolewa. Aliamua kumpigia simu Hans kutaka kujua aliwambia nini Mage mpaka kuamua kuvunja uchumba wakati kila kitu kilikuwa kipo katika hatia za mwisho. Lakini simu ya Hans haikuwa hewani, alijikuta akijiuliza atamwambia nini mama Mage mpaka amwelewe. Usiku ulikuwa mrefu kwa Brenda na kujuta kwa nini alimkubalia Hans kwenda kuonana na Mage.
***
Siku ya pili Mage aliamka asubuhi na kuoga na kujipamba kisha alitoka, alimkuta mama yake amekaa sebuleni ameshika tama.
“Mama vipi mbona hivyo?” alimuuliza huku akijilazimisha kujenga tabasamu.
“He! Safari ya wapi?”
“Naenda kwa Colin mama.”
“Kweli?” mama yake alishtuka.
“Ndiyo mama.”
“Haya wasalimie.”
“Sawa mama, ila sitakuwa hewani kwa siku mbili.”
“Kwa nini?”
“Utajua nikirudi.”
“Kwani mnakwenda wapi?”
“Itajua tu mama.”
“Haya mwanangu safari njema.”
“Asante mama.”
Mage kabla ya kutoka alimbusu mama yake na kuelekea nje na kumfanya mama yake kumsindikize kwa macho kisha alinyanyua mikono juu kumshukuru Mungu kwa kuweza kumbadili msimamo wake. Alijiuliza kama angesimamia msimamo wake kwake ingekuwa aibu na fedhea ya kuvunjika harusi aliyoiandaa kwa nguvu kubwa.
Ilikuwa toka aamke alikuwa hajaoga zaidi ya kukaa sebuleni kutafuta njia ya kuinusuru ndoa ya mwanaye ambayo aliamini ni muujiza pekee ndiyo wenye kuiponya kwa kuamini nguvu za kibinaadamu zisikingeweza. Alinyanyuka na kwenda kuoga ili apate kifungua kinywa.
Mage alikwenda kuchukua gari aina ya Prado nyeupe na kutoka kuelekea nyumbani kwa kina Colin. Aliendesha gari taratibu tofauti na siku zote aliendesha kwa fujo. Alirudisha kukumbuka ya muda mfupi ya picha ya mama yake aliyokuwa amekaa ameshika tama kuonesha kabisa uamuzi aliochukua umemchanganya sana na kumnyima raha.
Alipeleka macho yake kwenye simu yake iliyokuwa pembeni yake na kuichukua alitafuta namba ya Hans na kumpigia. Iliita kidogo na kupokelewa.
“Haloo ma adorable.”
“Vipi umeamka salama?” alimuuliza kwa sauti iliyopooza.
“Mmh! Naweza kusema nimezaliwa upya nimelala usingizi mtamu nilioukosa muda mrefu.”
“Nashukuru kama ni hivyo.”
“Mmh! Niambie moyo wangu?”
“Hans nilitaka kukujulisha kuwa sitakuwa hewani kwa siku mbili ila ya tatu nitarudi kama kawaida.”
“Kuna nini?”
“Utajua baadaye.”
“Upo wapi?”
“Nimetoka mara moja.”
“Sawa nimekuelewa mpenzi.”
“Basi nikutakie siku njema yenye furaha.”
“Na kwako pia.”
Mage alikata simu na kumpigia shoga yake Brenda, haikuchukua muda ilipokelewa upande wa pili.
“Vipi shoga?”
“Poa, za asubuhi?”
“Nzuri tu.”
“Nilitaka kukujulisha sitakuwa hewani kwa siku mbili.”
“Kwa nini shoga halafu mbona leo kama hujachangamka?”
“Aah! Nipo katika kipindi kigumu lakini nitakivuka tu japokuwa najua jasho la damu lazima litoke.”
“Bado unamsimamo uleule?”
“Utajua baada ya siku mbili.”
“Sasa upo wapi?”
“Nakwenda kwa Colin.”
“Loh! Afadhali shoga maana mimi mwenyewe nilikuwa sina amani moyoni mwangu.”
“Basi ndiyo hivyo tutawasiliana kesho kutwa.”
“Na kesho?”
“Sitakuwa hewani kwa siku mbili.”
“Mmh! Umeamua, safari njema msalimie sana shemu Colin mwambie nimemmisi.”
“Salamu zimefika.”
Baada ya Mage kukata simu shoga yake Brenda alitipa simu kwenye kochi na kushika kifua na kusema:
“Ooh! Afadhali Mage kabadili uamuzi sijui kama mama yake angenielewa.”
Mage baada ya kumaliza kuzungumza na Brenda aliweka simu pembeni na kuiweka mikono yote juu ya usukani na kukanyaka mafuta kuelekea nyumbani kwao Colin. Macho yake yalitulia kutazama mbele huku machozi yakijaa taratibu katika macho yake. Alijikuta akisema kwa sauti kama anazungumza na mtu.
“Mapenzi haya! Kwa nini Mungu uliumba mapenzi kwa nini yakuwa kila siku yanachukua furaha yangu badala ya kunifariji?”
Alichukua kitambaa pembeni yake alifuta machozi na kuendelea na safari. Alisimamisha gari mbele ya geti la nyumba ya kina Colin, geti lilifunguliwa na kuingia ndani. Aliliweka kwenye maegesho kabla ya kuteremka alivaa miwani ya jua ili kuficha macho yake na kuteremka
ITAENDELEA

No comments