Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 13


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Alichukua kitambaa pembeni yake alifuta machozi na kuendelea na safari. Alisimamisha gari mbele ya geti la nyumba ya kina Colin, geti lilifunguliwa na kuingia ndani. Aliliweka kwenye maegesho kabla ya kuteremka alivaa miwani ya jua ili kuficha macho yake na kuteremka.
SASA ENDELEA...
Wa kwanza kuonana naye alikuwa mama Colin ambaye alimkimbilia na kumpokea Mage.
“Wawaooo mkwe wangu.”
“Waawoo mama, Shikamoo.”
“Marahaba.”
“ Colin yupo wapi?”
“Yupo chumbani kwake, aliniambia utakuja.”
“Ndiyo mama.”
“Vipi unaendeleaje?”
“Namshukuru Mungu nipo sawa.”
“Haya mwanangu kamuone mwenzio maana alikuwa na kimuhemuhe hasa baada ya kusikia unaumwa.”
“Sawa mama.”
Mage alielekea chumbani kwa Colin, mlango ulikuwa umerudishwa aliusukuma bila hodi na kuingia ndani alimkuta Colin akibadika picha kubwa ya rangi ukutani wakiwa ufukweni wamelaliana chini ya picha ule kulikuwa na maneno ya rangi nyekundu yaliyokuwa yanasomeka, kwa juu yaliandikwa: ASANTE MUNGU KWA KUNIPA MKE MWEMA na chini kuliandikwa MAGRETH NAKUPENDA ZAIDI YA KUPENDA .
Mage aliposoma yale maneno na kuiona ile picha moyo ulimuuma na kuangua kilio cha sauti, Colin alishtuka kusikia sauti ya mchumba wake, alipogeuka alimuona Mage amesimama akiwa ameshika kifua chake. Aliteremka haraka kitandani alipokuwa amepanda kubandika picha ile kubwa na kumfuata alipokuwa amesimama na kumkumbatia kwa kumlazia kifuani.
“Vipi mpenzi kipi kinakuliza?”
“Najua nina mtihani mzito moyoni mwangu lakini Mungu atanipa nguvu na nitashinda.”
“Kuna nini mbona unanitisha?”
“Kawaida tu, Colin naomba ujiandae tuna safari.”
“Ya wapi?”
“Surprise.”
“Waawoo!” Colin alisema huku akimkumbatia Mage.
Kwa vile alikuwa ametoka kuoga alibadili nguo na kumweleza Mage.
“Nipo kamili mpenzi.”
“Chukua na nguo nyepesi za kupumzikia.”
“Tunaenda wapi?”
“Utajua tu.”
Walichukua begi dogo na kuongozana hadi sebuleni, walimkuta mama Colin akimuelekeza jambo msichana wa kazi alipowaona aliacha na kuwageukia.
“Jamani wapendanao safari ya wapi?”
“Tunatoka kidogo,” alijibu Mage.
“Haya mwende salama.”
“Asante mama, ila hatutakuwa hewani kwa siku mbili.”
“Kwa nini?”
“Utajua tu,” Mage alijibu
“Kwa hiyo leo hamrudi?”
“Ndiyo mama tutarudi kesho kutwa.”
“Mmh! Haya wanangu nawatakieni safari njema,” mama Colin aliwakumbatia wote na kuwabusu kisha aliwasindikiza nje hakuondoka mpaka walipotoka nje ya geti ndipo aliporudi ndani.
***
Baada ya gari kuingia barabarani Mage alimgeukia Colin aliyekuwa ametulia na kumwambia.
“Colin zima simu yako.”
“Kwa nini?”
“Sitaki uwasiliane na mtu yeyote zaidi yangu.”
“Sawa mpenzi,” Colin alizima simu yake.
“Zima na yangu.”
Colin alichukua simu ya Mage ni kuizima, safari iliendelea, gari lilielekea barabara ya Kawawa mpaka Mwenge na kukata mtaa wa viwanda mpaka njia panda ya Kawe. Mage hakukunja alinyoosha na kutokea Afrikana alikata kulia kuelekea Tegeta. Colin hakuhoji gari lilivuka Tegeta likaingia Boko likavuka Bunju na kuitafuta Bagamoyo
Ndani ya gari muziki laini uliendelea kuunguruma kila mtu akiwa kimya kutokana na mwendo wa kasi aliokuwa akienda nao Mage.
Alisimamisha gari mbele ya hoteli ya Oceanic Bay, baada ya kusimamisha gari alimgeukia Colin aliyekuwa ametulia akiuangalia umahiri wake kuendesha gari.
“Nina imani tuna siku mbili ya kila mmoja kumaliza hamu zake kwa mwenzie.”
“Mage mpenzi siku zote kitamu hakiishi hamu, penzi lako kwangu siwezi kulikinai.”
Mage hakuongeza neno alimshika mkono na kuongozana naye mpaka mapokezi na kukodi chumba kizuri kwa siku tatu.
“Mage si umesema tunarudi kesho kutwa.”
“Tatizo nini hata tukikaa mwaka kuna mtu anatudai?”
“Hakuna.”
Baada ya kupata chumba walikwenda chumbani kwao, chumba kilikuwa kizuri sana.
“Colin unakionaje chumba hiki?”
“Kizuri sana, unaonaje fungate yetu tuje tuifanye huku.”
“Tutaangalia muda ukifika.”
Baada ya kuoga kwa vile muda ulikuwa umekwenda walivaa nguo nyepesi na kwenda hotelini kupata chakula cha mchana. Kisha walihamia ufukweni kupata upepo wa bahari, muda mwingi Colin alikuwa mtu mwenye furaha kuwa karibu na mpenzi wake mchumba wake mkewe mtalajiwa.
Lakini Mage alionekana kulazimisha furaha kutokana na siri nzito iliyokuwemo moyoni mwake. Baada ya kutosheka na upepo wa bahari walirudi ndani na kujilaza kitandani mkao wa mahaba huku wakiangalia video. Colin muda mwingi alijiuliza kwa nini wamezima simu ilibidi amuulize Mage.
“Mpenzi kwa nini tusiwashe simu hata kwa muda?”
“Colin hizi ni siku zetu ambazo ni muhimu kwetu sitaki kusikia chochote masikioni kwangu zaidi ya sauti yako.”
“Nimekuelewa mpenzi wangu.”
“Colin,” Mage alimwita.
“Naam mpenzi.”
“Hivi mfano uwe nyumbani kwenu mara mama yangu anakupigia siku kukueleza nimefariki utafanyaje?”
“Mage hayo ni maneno gani, umesema tupo kwenye furaha sasa maneno ya kifo yanafuata nini?”
“Najua hapa siyo sehemu yake lakini naomba unijibu.”
“Kwa kweli nitachanganyikiwa naweza hata kufa.”
“Hivi umpendaye akifa kuna sababu ya kuchanganyikiwa ikiwa baada ya mazishi yake kuna wengine wapo pengine zaidi ya yule aliyeondoka?”
“Ni kweli, lakini kinachomtesa mtu ni mazoea si uzuri wa sura wala umbile la mtu.”
“Kwa mfano mi nikisema sikupendi utafanyaje?”
“Nitafanyaje nawe umeamua.”
“Hutaumia?”
“Nitaumia lakini nitafanya nini, lakini naamini mimi na wewe tunapendana hakiwezi kutokea kitu kama hicho.”
Mage alibadili mazungumzo kwa kumshika mkono Colin na kuelekea naye bafu kuoga, waliingia kwenye jakuzi na kuoshana kisha walirudi kitandani kuburudisha mioyo yao. Mage alimpa penzi Colin penzi shatashata ambalo lilimrusha akili naye alijibu mashambulizi kitu kilichomfanya Mage aangue kilio na kumshtua mpenzi wake.
“Vipi mpenzi mbona unalia?”
“Colin sina jinsi lazima iwe.”
“Iwe nini?”
“Utajua tu.”
Mage alimvamia Colin na kuendelea kustarehe bila kuliweka wazi lililikuwa likimliza, alijitahidi kurudi katika hali yake ya kawaida ya uchangamfu na kumfanya Colin asahau kitendawili chake.
Walikaa kwenye hoteli ile kwa siku mbili huku wakiongozana kama kumbikumbi huku kila mmoja alijua watu wale wanapenda mapenzi ya dhati. Siku iliyofuata majira ya mchana baada ya kupata chakula walipumzika kwa muda kabla ya kurudi mjini. Mage akiwa amejilaza pembeni ya Colin alijinyanyua na kumgeukia mpenzi wake na kumwita.
“Colin.”
“Naam mpenzi.”
“Hivi unajua kwa nini toka juzi sijakuita mpenzi?”
“Sijajua.”
Mage alitulia kwa muda akimtazama Colin usoni mara machozi yalianza kumtoka, Colin alizidi kumshangaa mpenzi wake kwani toka wamefika Bagamoyo ameshindwa kumwelewa.
“Colin, “ alimwita tena.”
“Naam.”
“Najua unanipenda.”
“Sana.”
“Najua kabisa nitakachokueleza kitakushtua na kukumiza moyo wako sawa na kuupasua bila ganzi kwa kisu butu. Lakini ukweli utabakia palepale sina jinsi, nina imani penzi la kweli huwa alitengenezwi na mtu bali mhusika mwenyewe.”
“Ni kweli kabisa.”
“Unajua penzi letu halikuwa la sisi kupendana bali kutengenezwa na wazazi wetu?”
“Najua lakini tulipoonana kila mtu alimpenda mwenzake.”
“Unajua hiyari yashinda utumwa?”
“Najua.”
“Nina imani nilikueleza jinsi mapenzi yalivyoniumiza.”
“Ndiyo.”
“Na aliyesababisha nilikueleza.”
“Ndiyo.”
“Basi napenda kukueleza hili ambalo moyo wangu unavuja damu kwa maumivu kwa vile sikupenda liwe kwa vile hiyari yashindwa utumwa, lazima niseme ukweli wa moyo wangu kuwa Colin nilikupenda lakini Hans nilimpenda zaidi. Hans baada ya kufiwa na mkewe amerudi kwangu na yupo tayari kutimiza ndoto yetu tuliiweka muda mrefu,” Mage alimeza mate huku akiendelea kutokwa machozi kisha aliendelea kuzungumza kwa sauti ya chini yenye mchanganyiko na kilio.
“Najua kauli yangu itakumiza lakini ndiyo ukweli wenyewe, Colin nimeamua kwa hiyari na mapenzi yangu nikiwa na akili timamu kuuvunja uchumba wetu kwa hiyo harusi yetu haitakuwepo tena, Penzi tamu tulilopeana ndilo la mwisho tukitoka hapa kila mtu ashike hamsini zake.”
“Mage,” Colin alimwita kwa sauti ya chini.
“Abee.”
“Unasema kweli au unatania?”
“Nasema kweli,” Mage alijibu huku akikaza macho.
“Hapana acha utani Mage unaweza kuniua kwa presha.”
“Huwezi Colin, wewe ni mwanaume umeubwa kukabiliana na matatizo, kumbuka amenikuta tayari nimeishaanza uhusiano na mtu ambaye ndiye aliyenionjesha dunia ya mapenzi na aliniahidi kunioa. Toka niachane naye sikuwahi kuwa na mwanaume mwingine zaidi yako kilichotokea ni kutoelewana lakini sasa hivi tumeelewana na mipango yetu lazima itimie.”
“Mage japo Hans ndiye alikuonjesha dunia ya mahaba lakini alikutenda, Mage nimekukosea nini mpaka uchukue uamuzi mzito na wa kikatili kama huo?” Colin aliuliza huku machozi yakimtoka.
“Hujanikosea kitu, hata mimi nilikupenda sana, lakini siwezi kuishi na wewe kwa kujilazimisha au kukufanya kama bodi lakini injini awe Hans. Colin, Hans nampenda sana aliniudhi na kuumiza moyo wangu lakini siku aliponiomba msamaha moyo wangu aliyeyuka kama bonge la mafuta kwenye kikaango cha moto. Siwezi kuwa nawe kimwili wakati mawazo yangu yote yapo kwa mwanaume mwingine.
“Narudia naomba ukubaliane na uamuzi wangu wa kuvunja uchumba tukiwa na mioyo safi, kuachana kwetu kusijenge uadui tuendelee kuwa marafiki kwenye harusi yangu uje ya kwako nije.”
“Mage uamuzi uliochukua ni kuupasua moyo wangu bila ganzi, naomba urudishe moyo nyuma mpenzi wangu, bora ungeninyang'anya kila kitu katika mwili wangu na kuniachia moyo wako ni muhimu kuliko chochote duniani japo nipo nawe kwa muda mfupi lakini nimekuzoea sana.”
“Siwezi kuishi mapenzi ya kuigiza niache nimpende aliyechaguliwa na moyo wangu.”
"Mage siwezi kukubali kirahisi namna hiyo nasema sikubali, lolote na liwe nasema huondoki kama sio nitamwaga damu ya mtu," Colin alisema huku akisimama.
"Colin mapenzi si lazima usisababishe nikakasilika na kutoa maamuzi yatakayokuumiza mara mbili."
"Nasema sikubali...toa uamuzi wowote kumbuka nimekutoa kwenye mateso ya kutendwa , leo nikuache uondoke hivihivi sikubali," Colin alikuwa mkali.
"Colin nasema hivi kila usemalo ni kweli tupu na una haki yoyote ya kufanya lakini kumbuka penzi alilazimishwi nina imani umenielewa kuwa mstaarabu tuachane kwa usalama."
Mage alinyanyuka na kumsogelea Colin aliyekuwa ameinama akilia na kumpigapiga mgongoni.
"Sweet naomba usilie mwanaume kaumbwa kukabiliana na matatizo hili ni moja wapo.”
Colin alinyanyuka kama mbogo na kumsukuma Mage aliyeanguka chini huku akibwata.
"Muongo mkubwa mnafiki wewe unanipaka mafuta kwa mgongo wa chupa eti sweet!"
"Huwezi amini Colin nakupenda sana japo Hans nampenda zaidi, nipo yatari kulipa gharama zote za maandalizi ya harusi yetu, pia hata kulipa gharama zozote ili kuhakikisha nawe unakuwa na mke atakayeziba pengo langu."
Mage pamoja na kusukumwa hakukasirika akiamka pale chini alipoanguka Colin hakumjibu neno lolote zaidi ya kuinama huku akilia. Mage alimshika mkono na kunyanyua, alimtazama kwa macho yaliyojaa machozi na kusema kwa sauti ya chini.
“Colin nisamehe sana siwezi kuwa mnafiki mapenzi nayajua, nipe ruksa mpenzi wangu. Nilikuja huku ili tupate muda wa kulizumgumza hili, sikutaka tulizungumze juujuu. Nakupenda lakini sitaki nikutese kwa kukunyanyasa kimapenzi kwa vile mapenzi nayajua yanavyoumiza.”
Colin alitulia huku akimtazama Mage aliyekuwa akitia huruma, alijiona mjinga kulazimisha mapenzi. Alikohoa kidogo na kusema:
“Sawa nimekuelewa.”
“Nashukuru.”
“Kuna la zaidi?” Colin alimuuliza Mage.
“Hakuna.”
“Tunaweza kuondoka.”
Walichukua vitu vyao na kuelekea nje kwenye gari ili warudi mjini.
***
Cecy baada ya kutoka twisheni alisimama chini ya mti kuagana na shoga yake huku wakijikumbusha baadhi ya mada walizopewa wakasome nyumbani. Alikuwa amepiga hatua kubwa katika kusoma na kundika hata kuzungumza lugha ya kingereza baada ya kusoma kwa uchungu mkubwa.
Siku zote aliamini kumkosa Colin kulitokana na kukosa elimu, kwake umaskini hakuuona sababu kama ungekuwa na elimu yake ambayo hata mama Colin angeiheshimu. Toka aanze kusoma alionekana ndiye mwanafunzi aliyetaka kujua lugha kuisoma kuiandika na kuizungumza.
Japokuwa hakukijua sana lakini aliweza kumsikia mtu na kumwelewa hata kumjibu mawili matatu. Ile ilimpa kiburi cha kuzungumza muda wote hata alipokosea hakujisikia vibaya kwa vile alielekezwa. Baada ya kujadiliana na shoga yake alisogea mbele kuelekea njia ya kwao japo palikuwa mbali kidogo lakini hakujali umbali ule kutembea kwa miguu kwa vile alikuwa akitafuta kitu.
Siku zote aliingia darasa la mchana kwa vile asubuhi alikuwa akienda kwenye biashara zake. Ada ya mwanzo alitumia fedha aliyoachiwa na Colin siku aliyompeleka kwao na kuwaacha kwenye mataa kwa ahadi tamu ya kuyabadili maisha yao. Alikumbatia daftari lake na kutembea taratibu kukifuata kichochoro cha kuingilia njia ya mkato. Aliangalia saa yake ilimuonesha ni saa kumi na moja na nusu jioni.
Alishtushwa na sauti ya gari aina ya Prado jeupe new model lililosimama nyuma yake. Alipogeuka aliona msichana akiteremka kwenye gari huku akibwata kwa sauti kuonesha anazozana na mtu ndani ya gari. Alipomwangalia aligundua ni Mage mwanamke aliyezima ndoto zake za kuwa mke wa Colin. Alisimama nyuma ya mti kumwangalia, alimuona akisema kwa sauti:
“Wewe mtu gani unayelazimisha mapenzi nimekueleza ninaye ninayempenda hutaki kunielewa. Naomba uteremke kwenye gari langu, siwezi kutembea na mtu asiyeelewa. Sasa hiyo elimu uliyosoma inakusaidia nini ikiwa hutambui nini maana ya upendo?
Nasema teremka la sivyo nitakuachia gari niondoke zangu.”
Baada ya muda Cecy alishtuka umuona mwanaume aliyekuwa akiambiwa vile ni Colin, baada ya kuteremka kwenye gari kinyonge na alisogea pembeni na kusimama bila kujua nyuma yake yupo Cecy.
Cecy roho ilimuuma kuona mtu ampendaye akidhalilishwa vile, Colin alionekana machozi yakimtoka kitu kilichozidi kuumiza moyo wake na kushangaa watu ambao muda si mrefu walitegemea kufunga ndoa lakini ajabu mwanamke kutoa maneno makali kama yale ya kumdhalilisha mumewe mtalajiwa.
Alitulia aione sinema ile inaishaje kwa kujificha nyuma ya mti ili wasimjue, baada ya muda alisikia sauti ya Colin.
“Mage pamoja na hayo lakini kumbuka tumepanga nini mimi na wewe katika maisha yetu?”
“Hainihusu! Nimekwambia mapenzi siyo lazima, ninaye nimpendaye wewe nikuweke wapi?”
“Mage...Mage.”
“Jina langu, kwa heri.”
Mage alisema huku akielekea kwenye gari ili aondoke na kumuacha Colin aliyekuwa bado amesimama akilia. Kitendo kile kilimuumiza sana Cecy bila kujitambua alitoka nyuma ya mti na kwenda kumvamia Mage kwa nyuma na kuzivuta nywele zake na kuanza kumshushia kipigo.
Colin alishtuka kumuona Cecy eneo lile na kujiuliza ametokea wapi, ilibidi amuwahi kumtoa juu ya Mage aliyekuwa akipiga kelele za maumivu.
“Cecy muache.”
“Hawezi kukudhalilisha kiasi hicho kama umalaya wake apeleke mbele,” Cecy alisema huku akitweta kwa hasira akitaka kujitoa mikononi mwa Colin ili akamfunze adabu Mage.
“Colin have you sent this bastard to come and attack me?“ (Colin umemtuma chokoraa huyu aje anipige?) Mage alibadili lugha na kusema huku akisikilizia maumivu.
“No, baby, I’m also suprised as to where she came from.” (Hapana mpenzi hata mimi nashangaa sijui katokea wapi.) Colin alijitetea.
“Colin, what type of a man who forces to be loved, what’s wrong with you? Let her go!” (Colin wewe ni mwanaume gani unang’ang’aniza mapenzi una kasoro gani mwacha aende) Cecy safari hii naye alivunja yai na kufanya Colin abakie mdomo wazi.
“Colin thank you, stay with that bastard whom you sent to beat me.” (Colin asante, baki na huyo chokoraa uliyemtuma kunipiga) Mage alisema huku akielekea kwenye gari.
Colin aliyekuwa amemshika Cecy ili asiendelee kumuadhibu Mage, alimuachia na kumfuata Mage kumuomba msamaha.
“Please Maggie excuse me, do not be so cruel to me.” (Tafadhali Mage rudisha moyo nyuma usinifanyie ukatiri huo.)
Alipopiga hatua ili amfuate Mage kwenye gari, Cecy alimfuata na kumzuia kwenda kuomba msamaha.
“Colin...Colin... why do you cling to her, how good is her; do you love her for her riches or behaviour? (Colin... Colin... unamng’ang’ania ana sifa gani, unampendea utajiri au tabia?)
Colin alijitahidi kujitoa mikononi mwa Cecy lakini alikamatwa madhubuti, wakati huo Mage alikuwa ameingia kwenye gari na kutupa nje begi la Colin na kuondoa gari kwa kasi na kumuacha Colin akilisindikiza kwa macho. Baada ya gari kupotea machoni alitulia huku machozi yakiziba macho.
Cecy roho ilimuuma kuona mtu ampendaye akitokwa machozi kwa ajili ya kulilia penzi lisilokuwepo.
“Colin, mbegu ya penzi humea kwenye moyo wenye rutuba ya mapenzi, kwa nini unalazimisha kupanda mbegu yako kwenye mawe? Kwani nini unakuwa kenge asiyetaka kuelewa. Mshukuru Mungu msichana wa watu amekuwa mkweli mapema,” Cecy alisema kwa sauti ya kilio iliyomshtua Colin na kurudisha macho kwake.
Pamoja na yote yaliyomtokea alishangazwa na ujasiri wa Cecy msichana aliyeonesha kuumizwa na kitendo cha kudhalilishwa na Mage. Kingine na uwezo wa kuzungumza kingereza kwa ufasaha mkubwa pia kuonekana binti mwenye mvuto kutokana na mavazi na muonekano.
“Cecy,” alimwita kwa sauti ya upole.
“Abee.”
“Kwanza samahani.”
“Ya nini Colin?”

No comments