Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 14MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Pamoja na yote yaliyomtokea alishangazwa na ujasiri wa Cecy msichana aliyeonesha kuumizwa na kitendo cha kudhalilishwa na Mage. Kingine na uwezo wa kuzungumza kingereza kwa ufasaha mkubwa pia kuonekana binti mwenye mvuto kutokana na mavazi na muonekano.
“Cecy,” alimwita kwa sauti ya upole.
“Abee.”
“Kwanza samahani.”
“Ya nini Colin?”
SASA ENDELEA...
“Najua nimekudhalilisha kwa kitendo changu cha kumlilia Mage.”
“Colin siwezi kukulaumu kwa vile ile ni haki yako japo sijui sababu ya yeye kukudhalilisha kiasi kile ikiwa kila kitu kipo katika hatua za mwisho kilichobaki ni ndoa.”
“Mage amerudiana na bwana yake wa zamani na kuamua kuvunja uchumba wetu.”
“Kama amekueleza ukweli sasa unamng’anganiza wa nini?”
“Cecy ni ghafla sana heri kungekuwa na tatizo, kanifuata nyumbani juzi na kunipeleka Bagamoyo, niliamini ana mapenzi yake ya dhati kwangu lakini baada ya kukaa siku mbili za furaha siku ya tatu alinieleza kitu ambacho kimenichanganya sana.”
“Colin ulikuwa unampenda Mage mapenzi ya dhati au tamaa ya macho?” Cecy alimuuliza akiwa amemkazia macho.
“Mapenzi ya dhati.”
“Muongo! Umempenda kwa shinikizo la mama yako, kama amejitoa kwa hiyari yake huoni hii ni nafasi ya kuipanda mbegu yako sehemu sahihi ambayo utaotesha mti mwenye kivuli na matunda matamu?”
“Cecy kwanza unatoka wapi muda huu?”
“Shule.”
“Hongera.”
“Siwezi kusema asante.”
“Kwa nini?”
“Mpaka ufute machozi yangu.”
Colin alitoa kitambaa mfukoni ili amfute Cecy machozi, lakini alishikwa mkono na kumfanya aulize:
“Vipi Cecy mbona unanishika mkono?”
“Si machozi haya Colin.”
“Machozi gani Cecy?” Colin alishtuka.
“Ya moyoni, nimeumizwa sana pia nimedhalilishwa sana juu ya penzi lako, lakini Mungu si mnafiki leo amekudhihilishia mbele ya macho yangu kuwa mke uliyechaguliwa mara ya pili hakuwa mke sahihi bali lilikuwa penzi la kuingiza. Colin mimi ndiye mkeo uliyechaguliwa na Mungu. Nifute machozi yangu kwa kufunga ndoa na mimi si kwa kitambaa cha mkononi bali cha moyoni,” Cecy alisema kwa sauti iliyojaa hisia kali za mapenzi.
“Cecy nimekuelewa naomba unipe muda.”
“Muda wa nini wakati nafasi yangu imerudi tena nikiishuhudia si kwa kuhadithiwa na mtu.”
“Nimekuelewa, niache kwanza nifike nyumbani kwanza kumbuka toka juzi sipo nyumbani na ninarudi na taarifa hizo sijajua mama atazipokeaje?”
“Mmh! Sawa, ila pole kwa yote yaliyokukuta.”
“Nashukuru.”
“Colin naomba nikusindikize mpaka kwenu,” Cecy aimwambia Colin huku akiuchezea mkono wake.
“Hapana si unamjua mama atapata la kusema.”
”Nimekuelewa mpenzi.”
Colin alitoa hela mfukoni bila kuzihesabu na kumpatia Cecy, alizipokea na kushukuru kwa kupiga magoti kitu kilichomshtua Colin na kuona tofauti yake na Mage. Siku zote Cecy alikuwa msichana mtiifu ambaye mwanzo alikuwa chaguo la mama yake baadaye alimgeuka baada ya kumuona Mage. Waliagana kila mmoja kukodi gari mpaka kwao.
****
Mage baada ya kuachana Colin alijiendesha gari kwa kasi huku moyo ukimuuma kwa kitendo chake cha kikatili alichomfanyia mtu aliyeonesha mapenzi mazito kwake na aliyemkabidhi moyo wake mzimamzima kutokana na kumuamini. Aliyakumbuka maneno yaliyokuwa kwenye picha kubwa chumbani kwa Colin yaliyosema, moja lilisema: ASANTE MUNGU KWA KUNIPA MKE MWEMA na lingine MAGE NAKUPENZA ZAIDI YA KUPENDA.
Mage alijikuta akilia na kufanya machozi kuziba macho, alisimamisha gari pembeni ya kuendelea kulia kilio cha kwikwi. Aliisikia sauti ya Colin ikisema:
““Mage uamuzi uliochukua ni kuupasua moyo wangu bila ganzi, naomba urudishe moyo nyuma, mpenzi wangu bora ungeninyang'anya kila kitu katika mwili wangu na kuniachia moyo wako ni muhimu kuliko chochote duniani japo nipo nawe kwa muda mfupi lakini nimekuzoea sana.”
Sauti ile ilimfanya apaze sauti na kusema:
“Colin nisamehe sana, najua jinsi gani nilivyokuumiza najuayajua mapenzi yanavyo jeruhi moyo wa mtu. Colin nisamehe sina jinsi nilikupenda lakini Hans ni pumzi zangu siwezi kuiacha nafasi adimu aliyonirudishia.”
Mage aliongea kwa sauti kama anazungumza na Colin, alinamia usukani na kuendelea kulia. Uchungu ulimjaa moyoni kila alivyomfikilia Colin jinsi alivyokuwa akimbembeleza na kutokata tamaa ya kukubaliana na ukweli kwamba penzi limekwisha.
Aliamini asingeweza kuendesha gari kwa hali aliyokuwa nayo kwani hata nguvu zilikuwa zimemuisha kwa ajili ya uchungu uliomjaa moyoni. Aliwaza kumpigia Brenda ili aje amchukue. Wazo lile hakukubaliana nalo kwa vile siku ile alitaka kwanza kuonana na Hans ili amweleze kilichojili ndipo aende nyumbani.
Aliamua kumpigia Hans, alichukua simu ili ampigie ilibidi afute machozi kwanza kuziona ‘kiipadi’ .
Alitafuta jina la Hans na kupiga, hakuita mara mbili ilipokewa upande wa pili.
“Haloo.”
“Hans,” Mage aliita.
“Naam Mage vipi mpenzi?”
“Upo wapi?”
“Nipo Masaki.”
“Naomba uje haraka.”
“Nyumbani kwenu?”
“Hapana nipo njiani karibia na njia panda ya Masaki.”
“Mbona kama unalia?”
“Hans njoo kwanza.”
“Haya nakuja.”
“Kodi bodaboda.”
“Sawa.”
Baada ya kukata simu aliitupia kwenye kiti cha pili na kujilaza kwenye kiti baada ya kukiteremsha kwa nyuma ili kumsubiri Hans.
****
Cecy baada ya kuachana na alikwenda hadi nyumbani kwao, baada ya kusalimiana na mama yake aliingia chumbani kwake na kujifungia chumbani kwake. Baada ya kuvua nguo zote alijifunga upande wa kanga na kujilaza chali kitandani na kuweka mikono nyuma ya kichwa na kutazama kwenye dali. Alitulia kwa muda na kuanza kuyakumbuka matukio yalitokea muda mfupi.
Alijikuta akijilaumu kuingilia mambo yasiyo muhusu, kwani ule ulikuwa ugomvi wa wapendao, lakini kwa upande mwingine aliona kufanya vile ni kulipigania penzi lake. Aliamini ndoa ya Mage na Colin haitakupo na ile ndiyo ilikuwa nafasi yake kukipata alichokipoteza.
Alijiuliza kama ndoa ile itavunjika nani atakuwa mke wa Colin, kwake aliona ana nafasi ndogo hasa baada ya mama Colin kumdharau kutokana na umaskini wake lazima angemtafuta mwanamke mwingine kutoka familia yenye uwezo. Bado alitaka kujua sababu ya Mage kuuvunja uchumba ambao ulibakia siku chache kufunga ndoa kanisani
Moyoni alijiapiza kama ndoa ya Colin na Mage itavunjika basi ataipigania nafasi yake kwa nguvu zake zote. Mama yake alishangaa kumuona mwanaye yumo ndani muda mrefu, alipomfuata alikuta umefungwa. Aligonga mlango huku akiita.
“Cecy mbona umeingia ndani mwaka mzima kuna usalama?”
“Ndiyo mama.”
“Hebu toka basi.”
Cecy alitoka nje, mama yake macho yake hakucheza mbali na uso wa mwanaye na kugundua mabadiliko.
“Cecy upo sawa?”
“Ndiyo.”
“Hapana kuna kitu kimekutokea, si kawaida yako kuingia ndani moja kwa moja bila kunitania na kizungu chako cha kuombea maji.”
“Ni kweli mama kuna kitu kimenitoka kumenichanganya sana.”
“Kitu gani?”
Cecy alimweleza mama yake yote yaliyotokea wakati akitoka twisheni, mama yake alishtuka kusikia kampiga mchumba wa Colin.
“Cecy kwa nini unatafuta balaa, unakumbuka mama Colin alituambia nini?”
“Mama mimi sijavunja ndoa yao bali wenyewe mimi kiichoniudhi ni kashfa aliyokuwa akiitoa yule mwanamke.”
“Colin kasemaje?”
“Amesema amechanganyikiwa kwani maamuzi yalikuwa ya ghafla ila alisema atanitafuta.”
“Mmh! Sawa, basi kaoge ule.”
“Sawa mama.”
Cecy alipitia ndoo ya maji na kuelekea bafuni kuoga na kumuacha mama yake akimtazama mwanaye na kutikisa kichwa aliamini vita ya mapenzi ni nzito kuliko ya kumsaka gaidi mapangoni.
***
Colin baada ya kuachana na Cecy na kukodi gari lililompeleka hadi kwao, aliteremkia nje ya geti na kuingia ndani kwa miguu. Mama yake alikuwa wa kwanza kumuona akiingia sebuleni, lakini uso wa mwanaye haukuonesha furaha kitu kilichomshtua na kuhoji.
“Colin, baba vipi kwema utokapo?”
“Kwema si kwema.”
“Una maanisha nini?”
“Nitakwambia naomba kwa sasa niache nikapumzike kwanza.”
“Kuna nini? Mbona unanitisha?”
“Mama naomba uniache kwanza.”
“Mage yupo wapi?”
“Sijui.”
“Colin ni majibu gani hayo?” mama alishtuka majibu ya mwanaye.
“Mama yangu nipo chini ya miguu yako naomba uniache kwanza.”
“Mmh! Sawa.”
Mama Colin aliachana na mwanaye aliyeelekea chumbani kwake, moyo wake ulimsukasuka alichukua simu kumpigia mama Mage kutaka kujua kuna nini kimetokea. Baadaya simu kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo dada.”
“Za saa hizi?”
“Nzuri, lete habari.”
“Mage yupo hapo?”
“Mmh! Toka atoke juzi sijamuona kwani vipi?”
“Nimemuona Colin akirudi peke yake huku uso wake ukionesha kuna kitu si cha kawaida, nimemuuliza kuhusu Mage amesema hajui.”
“Mmh! Lazima watakuwa wametibuana, sasa Mage yupo wapi?”
“Hapo ndipo pananichanganya, nilipotaka kumchimba sana Colin ameniomba nimuache kwanza apumzike.”
“Mmh! Lazima watakuwa wametibuana tu.”
“Kwa hiyo hajafika?”
“Bado, akifika atanieleza tatizo, nitakujuza kila kitu.”
“Sawa dada.”
Mama Colin alikata simu, alipogeuka alimuona mwanaye amebeba vitu akitoka navyo nje, hakujua amebeba nini. Alisubiri muda ili akaone mwanaye amechukua nini na anapeleka wapi. Colin baada ya kuachana na mama yake alikwenda chumbani kwake, baada ya kufungua mlango wa chumba chake macho yake yalikutana na picha kubwa aliyoibandika muda mfupi kabla ya kuelekea Bagamoyo akiwa na Mage katika pozi zito la mahaba.
Picha kubwa aliyoibandika ukutani ambayo mwanzo aliiona ni sehemu ya kuongeza furaha ya moyo wake. Lakini siku ile ilikuwa chukizo la moyo wake, alipanda kitandani bila kuvua viatu na kuibandua na kuitupa chini huku akiitemea mate. Alifungua kabati na kutoka picha zote alizopiga na baadhi ya nguo za Mage alizikusanya na kutoka nazo nje kwenda kujichoma moto.
Alipofika nje alizikusanya sehemu moja na kuzimwagia mafuta ya taa na kuzitia moto, mama yake alitokea kwa nyuma yake. Alipotupa jicho aliona moja ya picha ya Mage ikiteketea na moto pia nguo za mkwewe mtarajiwa.
“Colin! Unafanya nini?” alimuuliza kwa sauti mwanaye.
Colin hakujibu kitu aligeuka kumtazama mama yake aliyekuwa ameshangaa mkono kiunoni.
“Colin mwanangu una nini mbona unachoma picha na nguo za mchumba wako?”
“Mama uliponichagulia mchumba ulifanya uchunguzi kwanza.”
“Wa nini?”
“Kama ana mpenzi anayempenda kuliko mimi.”
“Mage hakuna na mpenzi, kwani nini unaniuliza hivyo?”
“Ndiyo maana nikakuuliza ulifanya uchunguzi kabla ya kumchagua kuwa mkweo?”
“Ndiyo, kwani vipi?”
“Tulitaka kujenga nyumba kwenye kiwanja cha watu.”
“Una maana gani?”
“Mage ni mchumba wa mtu.”
“Una maanisha nini kusema hivyo?” mama Colin alishtuka kusikia habari ile.
Colin alimweleza yote yaliyojili Bagamoyo walipokaa siku tatu mpaka kumteremsha njiani na kumtupia mfuko wake. Lakini hakumweleza jinsi Cecy alivyo ingilia ugomvi ule na kipondo alichompa Mage.
Mama yake alibakia macho yamemtoka kama kaona meli ikitembea barabarani. Alishusha pumzi nzito na kubakia akimuangalia mwanaye asipate la kusema.
***
Hans alifika na bodaboda sehemu aliloelekezwa na Mage, aliliona gari limepaki pembeni. Alimuomba dereva wa bodaboda amshushe, aliteremka na kumlipa hela yake na kuchepua mwendo hadi kwenye gari alilolikuta limefungwa vioo vyote. Aligonga kwenye kioo na kumfanya Mage anyanyue kichwa kuangalia, alimuona Hans alifungua mlango.
Hans alishangaa kumkuta Mage macho yamemuiva kwa kulia.
“Vipi mpenzi?” alishtuka kuiona hali ile.
“Hans mpenzi umekuja?”
“Ndiyo mpenzi wangu mbona unalia?”
“Hans nimekaza moyo ili niumeze mfupa nisikupoteze mpenzi wangu.”
“Una maanisha nini?”
“Hii si sehemu sahihi ya mazungumzo, endesha gari tuondoke,” Mage alisema huku akihama kwenye usukani kumpisha Hans.
“Mmh! Safari ya wapi, nyumbani?” alimuuliza huku akimtazama usoni.
“Nyumbani siendi sasa hivi mpaka tumalizane na wewe.”
“Sasa twende wapi?”
“Sea Cliff hoteli.”
“Hakuna tatizo.”
Hans aligeuza gari na kuelekea Masaki, muda wote Mage alikuwa amejilaza kwenye siti baada ya kuilaza kwa nyuma. Hans alisimamisha gari kwenye maegesho ya Sea Cliff hoteli.
ITAENDELEA

No comments