Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 17


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Yule nani?” aliuliza huku akinyoosha kidole sebuleni.
“Mke wangu mtarajiwa chaguo sahihi la moyo wangu.”
“Colin… Colin una tatizo gani wanawake wote wameisha mpaka umfuate huyu maskini mbumbumbu asiyejua kitu. Mwanangu tuna fedha tunaweza kumuona msichana yeyote mzuri mwenye elimu yake kwa fedha yoyote na popote duniani.”
SASA ENDELEA...
“Mama naomba kwa hili usizungumze chochote uniache kabisa, umetafuta mwanamke ambaye leo katuvua nguo kwa vile ulimfuata msomi mwenye uwezo.”
“Lakini suala la Mage bado tulikuwa tunalishughulikia bado lilikuwa halijafika mwisho. Hivi leo Mage aje na mama yake wakikute kinyago hiki kuna ndoa kweli?”
“Penzi langu na Mage liliishia Bagamoyo, lilikufa tukalizika halitafufuka tena.”
“Lakini bado wazazi hatajabariki uamuzi wenu.”
“Mama si uamuzi wetu bali wa Mage, kasema ukweli ana mtu anayempenda tatizo lipo wapi?”
“Basi Cecy si chaguo langu.”
“Mama, mimi ni mwanao umenizaa na kunilea na kunifundisha kila kitu, lakini suala la nimpende nani ni matakwa ya moyo wangu. Nilikukubalia kwa Mage kwa vile ni mzazi wangu zoezi lako limefeli sasa huu ni muda wangu.”
“Lakini siyo kwa Cecy.”
“Mama Cecy ni zaidi ya mwanamke ndiye mwenye nafasi moyoni mwangu zaidi ya hapo sitakuwa na mwanamke mwingine.”
“Colin, Cecy umemjulia wapi kama siyo mimi?”
“Basi hili ndilo chaguo lako lililokuwa sahihi hujui tu.”
“Nilikuwa namtania tu lakini si kwa ajili ya kuwa mkeo.”
“Basi imekuwa hivyo bila kutegemea.”
“ Basi mimi simtaki.”
“Kwa hiyo unatafuta aibu nyingine?” Colin alisema huku akifungua simu upande wa picha na kumuonesha mama yake.
“Umeona unayempenda?”
Aliangalia picha za Mage na kuuliza:
“Hizi picha za nani?”
“Mage na mpenzi wake,” Colin alimjibu huku akimtazama usoni.
“Picha hii imepigwa lini?”
“Leo.”
“Wapi?”
“Wapo Afrika ya kusini wanakula raha katika hoteli ya Hilton jijini Durban, sasa naomba uniache na Cecy wangu.”
“Colin bado hujanieleza kitu, tafuta msichana mwingine lakini kwa Cecy sipo radhi kuingiza uchafu katika familia yangu.”
“Mama nakupenda na kukuheshimu sana naomba kuhusu Cecy usiniingilie kabisa zaidi ya hapo nitaondoka na kukuacha na fedha zako.”
“Colin mwanangu mbona umefika mbali,” mama alishtuka.
“Kwa sababu umeingilia haki ya moyo wangu, wewe ni mzazi gani usiye na huruma nimeumizwa badala ya kunihurumia bado unataka kuniongezea maumivu,” Colin alisema kwa uchungu.
“Lakini kumbuka wewe ni msomi unawezaje kuoa mwanamke mbumbumbu?”
“Mama mapenzi si cheo, elimu wala fedha, Cecy ni zaidi ya vyote hivyo kwangu.”
“Sawa, lakini utakuja kunikumbuka na uamuzi wako hata nikifa.”
“Ni kweli mama nitakukumbuka kwa kunitafutia mchumba aliye bora kuliko Mage. Cecy ni lulu iliyokuwa imejificha kwenye matope.”
“Nimekuelewa mwanangu, naomba unisamehe kwa kukukwaza.”
“Nilikusamehe kabla hujatenda.”
“Basi naomba ya huku yaache hukuhuku.”
“Sawa mama.”
Baada ya makubaliano Colin alirudi kwa Cecy na mama yake kwenda chumbani, alipofika alimpigia simu mama Mage kutaka kupata ukweli wa kauli ya mwanaye.
Baada ya simu kuita ilipokelewa upande wa pili:
“Haloo, dada vipi?”
“Mmh! Yaani bado nachanganyikiwa ulisema Mage kaenda wapi?”
“Nilikuambia amekwenda kwa shoga yake.”
“Wapi?”
“Aliniaga anakwenda Kibaha,” mama Mage alidanganya.
“Mmh! Mbona Colin anasema katumiwa picha za Mage akiwa na mwanaume Afrika ya kusini wakila raha kwenye ufukwe wa Hilton Hotel?”
“Mmh! Labda maana ametoka toka jana, dada wee hebu tuachane na Mage tufanye mambo zingine.”
“Sawa dada nimekuelewa.”
Baada ya kukata simu alitulia kwa muda akiwaza, alijikuta akimchukia Cecy na kuuapia moyo wake hatakuwa tayari kuona mwanaye akioa mwanamke asiye na hadhi. Alipanga kuhakikisha anauvunja uhusiano ule kwa hali na mali ili Colin aoe mwanamke mwingine mwenye elimu na kutoka familia yenye uwezo.
Alitoka chumbani na kujifanya kujichekeza kwa Cecy huku akimtania.
“Jamaniii mmependezaje wapenzi!”
“Asante mkwe,” alijibu Cecy kwa furaha huku Colin aliuona unafiki wa mama yake uliojificha moyoni ambao mpenzi wake hakuujua.
Kwa vile mama Colin hakupenda Cecy kuwa pale aliondoka na kwenda chumbani kwake na siri yake nzito moyoni.
JIJINI DURBAN AFRIKA KUSINI
Katika ufukwe wa hoteli ya Hiltoni wapenzi wa wawili walikuwa wakila raha, Mage alikuwa amelala kifuani kwa Hans huku akichezea kidevu chenye ndevu chache.
“Hans nikuambie kitu?”
“Niambie mpenzi.”
“Ningebugi vibaya kuolewa na mrugaruga kama yule(Colin).”
“Si haraka zako, nilikueleza piga ua lazima mke wangu utakuwa wewe pamoja na wazazi kunilazimisha kumuoa yule mwanamke.”
“Nilichanganyikiwa baada ya kuona umepata mtoto.”
“Ilikuwa lazima iwe vile ili wasijue nimepanga nini mbeleni.”
“Asante Hans kwa kuponya majeraha ya moyo wangu.”
“Nami nashukuru kukubali kurudi mikononi mwangu.”
“Kwa hiyo ndoa lini?”
“Tukirudi tu nyumbani mipango inaanza mara moja.”
“Nitafurahije mpenzi wangu.”
“Usijali nipo kwa ajili yako.”
“Basi naomba turudi nyumbani ili tukalisema hili mbele ya wazazi wetu wote.”
“Hakuna tatizo nakusikiliza wewe.”
“Nataka kesho jioni tuwe mbele ya wazazi wako ukiwaeleza kwa mdomo wako kuwa mimi ndiye mkeo baada ya hapo twende kwetu nikamweleze mama kuwa wewe ndiye mume wangu.”
“Hakuna tatizo mpenzi wangu.”
Walikubaliana kuondoa Afrika ya kusini siku ya pili mchana warudi Tanzania ili kwenda mbele ya wazazi wao kuthibitisha mapenzi yao ya dhati.
***
Colin na Cecy baada ya kutoka nyumbani walikwenda Bagamoyo katika hoteli ya Malaika ambako alipanga kukaa kwa siku moja. Majira ya jioni wakiwa wamejilaza mchangani huku wakipepewa na upepo mwanana wa bahari Colin aliyaangalia mawimbi ya bahari na mitumbwi ya wavuvi aliokuwa wakivua samaki.
Baada ya kugandisha macho baharini alijikuta akitokwa na machozi baada ya kukumbuka sehemu kama ile ndiyo iliyotumika kuvunja uchumba wake na Mage japokuwa ilikuwa hoteli tofauti lakini ni Bagamoyo ileile.
Machozi yalimdondoka bila kujua na kuangukia kwenye paji la uso la Cecy aliyekuwa amejilaza mapajani kwa mpenzi wake na kumfanya anyanyue macho kumwangalia. Alishtuka kumuona akibubujikwa machozi kitu kilichomfanya amuulize.
“Vipi mpenzi wangu mbona unalia?”
“Nimekumbuka kitu ambacho kimesababisha nitokwe machozi.”
“Kitu gani mpenzi wangu?” Cecy alimuuliza huku akimfuta machozi kwa upande wa mtandio aliojifunga.
“Ni juzi tu maeneo hayahaya yaliujerudi moyo wangu lakini, leo hii maeneo yaleyale yameujenga upya na kujiona kama nimezaliwa upya.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Juzi tulikuja huku na Mage kuvunja uchumba wetu ambao ulinishtua sana na kuumiza moyo wangu japokuwa haikuwa hoteli hii, lakini ni hukuhuku Bagamoyo. Lakini leo nimezaliwa upya kwa kulipata penzi la kweli ambalo naamini nilitaka kulipoteza haya ni machozi ya uchungu na furaha.”
“Nifurahi kusikia hivyo, lakini moyo wangu bado haujaamini kama tayari wewe ni wangu.”
“Kwa nini Cecy?”
“Naogopa Mage anaweza kurudi na wewe kunitosa, nitaumia mara mbili kwa vile nimeonja utamu wa mapenzi naweza kufa kwa presha kama utafanya hivyo,” Cecy alisema kwa sauti ya kulalamika.
“Cecy unataka kuamini vipi wakati penzi langu lilikuwa wazi mbele ya mama yangu.”
“Mama yako alikuitia nini pembeni?”
“Tulikuwa na yetu wala haikuhusiana na sisi,” Colin alitengeneza uongo ili kuendeleza furaha ya siku ile.
“Mmh! Nilikuwa na wasi labda chokoraa nilimeingia kwenye nyumba ya malkia,” Cecy alitania utani wenye ukweli.
“Hapana wewe ndiye malkia wangu.”
“Nashukuru kusikia hivyo,” Cecy alimkumbatia mpenzi wake kwa furaha bila kujua palichimbika mpaka yeye kuwa pamoja muda ule.
***
Mage na Hans waliwasili katika aridhi ya Tanzania katika jiji la Dar na ndege ya shirika la Afrika ya Kusini. Nje ya uwanja wa ndege walisubiriwa na gari la kifahari Land Cruiser V8 nyeusi. Baada ya ndege kutua waliteremka na kwenda moja kwa moja ndani ya gari lililokuwa likiwasubiri na kuingia.
Gari liliondoka kuelekea Mikocheni anapoishi Hans, njiani Mage alikuwa na furaha ya ajabu kurudi mikononi kwa mpenzi wake mwanaume wa maisha yake. Baada gari kuingizwa ndani na kusimama Hans alizunguka upande wa pili na kumfungulia Mage mlango na kumkaribisha.”
“Karibu utamu wangu.”
“Asante raha zangu.”
Walishikana mikono na kuingia ndani, mapokezi ya familia ya Hans yalikuwa tofauti na siku za nyuma waliufurahia ugeni wa Mage huku wadogo zake wakimwita wifi na shemeji na wazazi wakimwita mkwe. Ilikuwa ni faraja kubwa moyoni kwa Mage aliona sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano kukubalika katika familia ile.
Moyoni alijilaumu kukubali kuolewa na Colin kumbe ahadi ya kuvumilia ili ndoto yao ya muda mrefu waliyoahidiana kutenganishwa na kifo ilikuwa njiani. Familia haikuwa na tatizo tena kuingilia uamuzi wa mtoto wao kwa vile chaguo lao Mungu alilichukua hawakuwa na jinsi.
Baada ya mapokezi mazuri katika familia ya mpenzi wake Mage na Hans walielekea Kigamboni nyumbani kwao Mage ili kujitambulisha rasmi kwa mzazi wake. Walipofika Kigamboni Mage alimkaribisha Hans nyumbani kwao.
“Karibu mume wangu.”
“Asante mke wangu.”
Walishikana mikono na kuingia ndani kwa mwendo wa mahaba, sebuleni walimkuta mama Mage. Mage alimuachia mkono Hans na kumkimbilia mama yake na kumkumbatia.
“Waaawoo mama.”
“Mage mwanangu karibu mama.”
“Asante mama.”
Mage alichukua nafasi ile kumtambulisha Hans.
“Mama leo nimemleta mume wangu chaguo la moyo wangu.”
“Nimemuona, karibu baba,” mama Mage alisema kwa sauti ya unyonge.
“Asante mama, shikamoo.”
“Marahaba.”
“Mama mbona mnyonge unaumwa?” Mage alimuuliza mama yake.
“Walaa, mwili umechoka tu.”
Mama Mage alinyanyuka na kuelekea chumbani kuwapisha alipoondoka eneo la sebule alimwita mwanaye.
“Mage mama njoo mara moja.”
“Nakuja mama,” kabla ya kuondoka alimuaga mpenzi wake.
“Mpenzi nakuja.”
“Hakuna tatizo msikilize mama.”
Mage alimbusu shavuni Hans na kuchepua mwendo kwenda kumsikiliza mama yake.
“Abee mama.”
“Njoo chumbani.”
Waliongozana hadi chumbani, walipofika mama yake alisimama na kumwambia Mage akae kwenye kochi, baada ya kukaa alimgeukia na kumwita.
“Mage.”
“Abee mama.”
“Hivi ndiyo umeamua kunivua nguo?”
“Kukuvua nguo! Kivipi mama.”
“Kwa hiyo hutaki kuolewa na Colin?”
“Mamaaa! Mbona hilo tuliisha limaliza, si nimekueleza ukweli wangu na Colin anajua kila kitu. Sasa swali kama hilo linatoka wapi?”
“Mage kwa nini unalamba matapishi yako?”
“Mama Hans si matapishi ni chakula kilichowekwa kwenye Hot port nimekipakuwa bado kina moto. Unajua jinsi gani nilivyoteseka baada ya Hans kulazimishwa kuona mwanamke mwingine. Ni wewe uliniambia niwe na subira sasa leo karudi mikononi mwangu unaniuliza hivyo?”
“Kama ungekuwa huna mchumba nisingekuuliza lakini wewe tayari umeishakuwa mchumba wa mtu tena upo kwenye hatua za mwisho za ndoa.”
“Mama wewe ndiye unayekuza mambo Colin tumeisha malizana na sasa hivi tunatoka nyumbani kwao Hans ambako sikuamini kama wangenipokea kama malkia. Yaani mama nimefurahi kukubalika katika familia ya mpenzi wangu.”
“Mwanangu siku zote mkataa pema pabaya panamwita.”
“Mamaa maombi gani hayo?”
“Nakuambia utamkumbuka Colin, ipo siku Hans atakukimbia na kurudi kwa Colin utambembeleza ukitembea kwa magoti, kibaya ukute ameoa mwanangu utakuja jutia uamuzi wako,” mama alitoa taadhali.
“Mama kuwa na Hans sitajuta katika maisha yangu ni chaguo sahihi la moyo wangu.”
“Mmh! Sawa.”
“Kuonesha Hans hataki kunichezea wiki ijayo barua inakuja na baada ya majibu maandalizi yanaanza mara moja. Kinachotakiwa vikao vya harusi visogezwe mbele ili michango ya harusi yangu na Colin iwe yangu na Hans. Hapo nina imani hakuna kitakacho haribika.”
“Sawa, siwezi kukuingilia kwa vile umeamua mwenyewe, ila kila aliyae ushika kichwa chake.”
“Mama hiyo misemo, ninacho shukuru nimepata tiba ya moyo wangu, kuna lingine?”
“Hakuna.”
“Basi mama yangu naomba unipe baraka zako kinyongo chake kinaweza kuvuruga ndoto zangu.”
“Siwezi kuna na kinyongo kwa vile nipo kwa ajili ya kuyaona maisha yako yanakuwa mazuri na salama.”
“Asante mama,” Mage alimshukuru mama yake kwa kumkumbatia.
Mage baada ya kuachana na mama yake alikwenda sebuleni alipokuwa amemuacha mpenzi wake.
Alirudi sebuleni na kumvamia Hans kwa mahaba motomoto bila kujali yupo sehemu gani. Mama yake hakutoka ndani alijikuta moyo ukimuuma na kuanza kulia peke yake huku akilaumu mapenzi ya mumewe kumuharibu mtoto.
****
Siku ya pili Colin na Cecy alirudi nyumbani, alimpitisha nyumbani kwa kisha yeye alirudi nyumbani kwa vile kulikuwa na mambo ya kufuatilia kuhusiana na shughuli zake alizoanza ikiwemo kupata kibari cha kuanzisha kampuni ya mitindo na mavazi ambayo alipanga kumtumia Cecy kwa ajili ya maonesha ya mitindo ya nguo.
Walipofika kabla ya kuondoka Colin alimwambia Cecy:
“Mpenzi pumzika ila jioni nitakufuata tutakuwa na mazungumzo marefu ila utarudi kulala nyumbani najua bi mkubwa amekumisi.”
“Hakuna tatizo msalimie mkwe.”
“Kuanzia wiki ijayo nategemea kutimiza ile ahadi.”
“Ahadi gani?”
“Ya ujenzi wa nyumba yenu, leo nitamtuma mtu awatafutie nyumba ili kesho muhame ili kupisha ujenzi.”
“Kama ni kweli tutashukuru.”
Colin alimwita mama Cecy na kumpa laki mbili.
“Mama utakunywa soda.”
“Asante baba.”
“Hakuna tatizo.”
Colin aliaga na kuondoka kuwahi nyumbani ili awahi mjini kwenye mipango yake na kumuacha Cecy akikumbatiana na mama yake kwa furaha. Kwa vile alikuwa na haraka alifika nyumbani hakukaa alibadili nguo na kuvaa suti ili kwenda kwenye miadi yake. Wakati anatoka alikutana na mama yake sebuleni.
“He! Baba umerudi saa ngapi?”
”Sasa hivi mama, Leo namiadi ya jamaa wale wa kampuni ya matangazo.”
“Na mwenzio yupo wapi?”
“Nimemuacha kwao.”
“Sawa baba baadaye.”
“Sawa mama baadaye.’
Colini aliagana na mama yake na kutoka nje ambako alichukua gari kuwahi Posta mpya katika Jengo la Benjamini Mkapa ghorofa ya kimi na nne. Baada Colin kuondoka mama yake aliamini ile ndiyo nafasi ya kwenda nyumbani kwao Cecy ili kuhakikisha ndoa na mwanaye haifungwi.
Alioga harakaharaka na kutoka kwenda nyumbani kwao Cecy, aliendesha gari kwa kasi kidogo ili kuwahi kabla mwanaye hajarudi. Aliamini kutumia fedha zake ataweza kuisambaratisha ile ndoa. Alisimamisha gari mbele ya nyumba ya kina Cecy na kuteremka.
Alimkuta mama Cecy amekaa kwenye kibalaza cha nyumba, alipomuona alimkaribisha kwa furaha na bashasha.
“Ooh! Karibu dada.”
“Asante, za hapa?”
“Nzuri, karibu japo maisha yetu ya kuungaunga.”
“Aah! Kawaida tu wala msijali.”
Alipotaka kumkaribisha ndani alikataa alisimama mbele ya nyumba, aliyatazama mazingira wanayoishi Cecy na mama yake moyo wake ulichefuka kwa kuona jinsi gani mwanaye alivyopotea maboya kutaka kumuona mwanamke fukara kama yule ambaye halingani na sifa na hadhi ya familia yao.

No comments