Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 18


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Cecy alizipokea na kumfanya mama Colin kutabasamu kwa kuamini fedha ni sabuni ya roho. Alizitazama zile fedha kwa uchungu huku machozi yakimtoka na kuona jinsi gani umaskini wao ulivyotumiwa kama kisu butu cha kuupasua moyo wake bila ganzi. Alitulia akilia huku machozi yakidondokea kwenye zile fedha.
SASA ENDELEA...
Kwa hasira alizinyanyua na kumpiga nazo usoni mama Colin na kutoka ndani ya gari, kitu kilichomuacha mdomo wazi mama Colin. Mama yake alishangaa kumuona mwanaye akitoka ndani ya gari akilia.
“Cecy kuna nini?”
“Mama niache kwanza, huyu mama ni mchawi.”
“Mchawi! Kafanya nini?” mama yake alishtuka.
Wakati huo mama Colin kwa aibu aliwasha gari lake na kuondoka bila kuaga. Aliushangaa ujasiri wa Cecy msichana maskini lakini mwenye kujiamini kupita kiasi kwa kukataa fedha zile na ofa ya kuyabadili maisha yao. Hakuamini binti muuza ndizi kukataa fedha zile wakati maisha yao ya kubahatisha. Lakini alijiapiza kwa nguvu kwa hiyari kwa fedha kwa damu lazima Cecy ataachana na Colin.
Mama Cecy alimfuata mwanaye aliyeingia chumbani huku akilia na kushindwa kuelewa mazungumzo ya ndani ya gari yalikuwa ya nini. Alikumta akiendelea kulia kitu kilichomfanya ajiulize kipi kikubwa walichokizungumza ndani ya gari.
Alimkuta amelala kifudifudi akilia kwa sauti ya kwikwi, wasiwasi wake labda Colin amepata tatizo.
“Cecy mwanangu kuna tatizo gani tena?”
“Mama inaumiza sana.”
“Kuna nini mpenzi wako kapata tatizo?”
“Mama mtu anaweza kuununua moyo wangu hata kuuchukua bure nikiwa nimekufa, lakini nikiwa hai siuuzi kwa gharama yoyote kwa vile furaha ya mtu hainunuliwi dukani.”
“Una maana gani?” mama yake alikuwa bado njia panda.
Cecy alimweleza mama yote aliyozungumza na mama Colin, mama yake macho yalimtoka pima kusikia taarifa ile baada ya kuamini kila kitu kilikuwa vizuri kilichobakia ni ndoa ya mwanaye na Colin.
“Mmh! Mbona makubwa madogo yana nafuu,” mama Cecy alisema akiwa amechoka na maneno yale.
“Mama mimi na Colin basi,” Cecy alisema kwa hasira.
“Huo ni uamuzi wa hasira lazima umsikilize mwenzako si amesema atakupitia jioni basi msubiri umsikilize naye anasemaje kama lao moja na mama yake una haki ya uamuzi wako.”
“Mama kosa langu nini? Yaani anatumia fedha zake kuinunua furaha yangu?” Cecy alisema kwa uchungu.
“Mwanangu kama Colin si chaguo la Mungu basi hamtaoana lakini kama ni chaguo la Mungu hakuna kitakachozuia.”
“Yule mwanamke ni mnafikia akiwa na mwanaye ananichekea kicheko cha mamba lakini kumbe ananitamani kunimeza.”
“Wee yaache tusubiri jioni.”
“Sawa, lakini nina amini hakuna ndoa yangu na Colin labda mapenzi ya sisi wenyewe lakini mama yake hanipendi na yupo radhi kutumia njia yoyote kukwamisha mapenzi yetu.”
”Ngoja tumsubiri Colin anasemaje.”
“Namsubiri kwa ajili yako lakini ningekuwa peke yangu asingekanyaga hapa.”
****
Majira ya jioni Colin alimpitia Cecy kama alivyomweleza, aliposimamisha gari alishangaa kutomuona mpenzi wake kama kawaida, kwani aliisha mzoesha vibaya kumpokea kwa kumrukia kwa mahaba motomoto. Baada ya kusimamisha gari aliteremka na kwenda ndani huku akiita jina la Cecy mkononi alikuwa amebeba zawadi za mpenzi wake.
“Beeeebi.”
Hakuwa na jibu zaidi ya kusikia sauti ya kilio toka ndani kitu kilichomshtua na kufanya akimbilie ndani kwa kuamini mpenzi wake yupo kwenye matatizo. Alimkuta Cecy amelala kifudifudi akilia kilio cha sauti.
“Cecy mpenzi una nini?”
“Colin unaweza kununua kila kitu chini ya jua lakini si furaha ya mtu,” Cecy alisema bila kugeuka.
“Kuna nini mpenzi wangu?” Colin alishangaa.
“Umenikuta maskini hata siku moja sikuja kwenu kuomba pesa ya kula, nimeishi kwa kuuza ndizi nitaendelea kuuza ndizi lakini hamuwezi kuutumia umaskini wetu kama siraha ya kununua haki ya moyo wangu.”
“Cecy hebu geuka mpenzi wangu, kipi nimekukosea mpaka useme maneno makali hivyo?”
“Najua hunipenda lakini usitumie gharama kubwa kuniacha, tamko lako ni tosha kuliko gharama na nguvu mnayotaka kuitumia. Ni kweli nakupenda jambo ambalo lipo wazi mbele ya muumba. Lakini ni vigumu kulazimisha mapenzi ni sawa na kumvuta punda mtoni lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji.”
“Cecy mpenzi wangu mbona toka jana tumekuwa na siku nzuri ambayo nilitegemea kuimalizia leo. Kipi nilichokufanyia ikiwa nimekuaga nimekwenda kwenye mipango ya maisha yetu ya mbeleni. Nimekuja na furaha ili kukujulisha nimekupatia chuo cha mambo ya urembo ambacho utasoma miezi sita na ukitoka hapo utakuta nimeisha kukufungulia kampuni yako ya urembo.
“Kwa nini wanawake mnapenda kuumiza moyo wangu, Cecy kabla hatujaanza mapenzi ulionesha kunijali lakini kuanza kwa ukaribu wetu hata mwezi bado unataka kuupasua moyo wangu bila ganzi. Cecy niliamini wewe ndiye tiba ya moyo wangu, lakini unataka kuongeza msumali wa moto kwenye kidonda. Naomba basi mnihurumie nami binadamu ninayehitaji upendo. Mapenzi yangu yamekuwa kama mtu anayemwaga maji baharini yasiyoonekana.
“Kwa nini hukuniambia mapema Cecy umeacha nijirushe juu ya ghorofa ya mapenzi nikiamini utanidaka, lakini najiona naangukia pabaya nawe umekataa kunidaka nitakufa kifo kibaya. Cecy utajiri wetu hauingiliani na mapenzi yetu, fedha inaweza kununua kila kitu lakini si penzi la kweli bali upendo wa dhati toka chini ya uvungu wa moyo wa mtu mwenye mapenzi ya kweli asiyeangalia kitu bali mtu mwenyewe alivyo.
“Ni kosa gani nililokufanyia mpaka kufikia kusema maneno mazito yaliyoushtua moyo wangu, kama moyo ungekuwa ukitoka nje naamini ungekuwa unavuja damu kutokana na mshtuko na maumivu ya kuona unatolewa sehemu salama na kutupwa kwenye miba.”
Maneno ya Colin ambaye alionekana hajui kilichokuwa kikiendelea kilimfanya Cecy aongeze sauti ya kilio na kujinyanyua alipokuwa amejilaza na kwenda kujitupa kifuani kwa Colin kitu kilichomshangaza mpenzi wake.
“Cecy mpenzi wangu hebu kuwa mkweli tatizo nini mpaka kusema maneno makali? Nipo radhi kujitoa muhanga ili kuliokoa penzi letu.”
“Colin najua unanipenda lakini mama yako hanipendi,” Cecy alisema kwa sauti ya kilio.
“Bebi, maneno gani hayo ikiwa jana uliona alivyokufurahi, yasahau yote yaliyopita.”
“Colin, mama yako mnafiki, ana tabia ya unafiki wa mamba anakuchekea machoni lakini moyo anakuchukia.”
“Kwa nini unasema hivyo?” Colin alishtuka kusikia vile.
“Mama yako hataki tuwe pamoja yupo radhi kutumia gharama yoyote kuhakikisha anatutenganisha.”
“Lakini mbona yaliisha.”
Cecy aliamua kumweleza ukweli, ujio wa mama yake na ahadi na fedha aliyotoa kwa ajili kulivunja penzi lao. Colin alibakia macho yamemtoka pima asiamini maneno ya Cecy.
“Cecy unayosema ni kweli?”
“Nimzulie uongo mama yako ambaye kama tungeoana angekuwa mama mkwe wangu.”
“Kama kafikia hatua hiyo naomba kwanza unisamehe sana, najua nitafanya nini. Ila nakuahidi kwa kuonesha msimamo umezisha upendo moyoni mwangu, pia hela aliyotaka kukupa nitakupa mara kumi yake na kutimiza ahadi yangu kwa kulijenga penzi letu.”
“Colin, narudi huwezi kuununua moyo wangu.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Sihitaji pesa zako kwa ajili yakuonesha kuwa unanipenda bali mapenzi ya dhati toka kwako. Pendo langu halina gharama japo ni ghali kwa vile nilikubali kukupenda kama ulivyo wala si kwa ajili ya gari, majumba au fedha zenu.”
“Asante kufahamu hivyo, basi naomba ukaoge ili twende nilipokueleza jana.”
“Sawa mpenzi wangu.”
“Pia, kesho mtahama ili kupisha ujenzi wa nyumba yenu kwa muda, nimewatafutie nyumba nzima ambayo nimelipia kwa mwaka mzima.”
“Kwani hiyo nyumba unachukua muda gani kujengwa?”
“Nitaka ijengwe vizuri hata miezi miwili au mitatu.”
“Basi si ungechukua miezi mitatu?”
“Msiwe na wasi, niliwaambia wakakataa wakataka mwaka mzima.”
“Ipo wapi?”
“Kimara Baruti.”
“Asante mpenzi wangu,” Cecy alimkumbatia Colin kwa furaha na kuyasahau maumivu yote.
Cecy alikwenda kuoga akimuacha Colin ambaye alihisi kichwa kinataka kupasuka kwa mawazo kutokana na alichokifanya mama yake aliyeamini ndiyo muongozo wake na kuitengeneza furaha lakini kwake ilikuwa kinyume. Alipanga akitoka pale kwenda na Cecy nyumbani kwao ili mama yake akayasema yale mbele yake.
Baada ya Cecy kumaliza kuoga na kubadili nguo ambazo zilizidi kumpandisha chati na kumfanya aonekane binti mrembo kuliko wanawake wote duniani mbele Colin. Walishikana mikono na kuelekea ndani ya gari na kuelekea moja kwa moja nyumbani kwao Colin.
“Colin unanipeleka wapi?” Cecy alishtuka.
“Usihofu naomba unifuate na mimi.”
“Mmh! Sawa.”
Gari lilipiga hodi na geti lilifunguliwa na Colin kuliingiza ndani, kama kawaida alizunguka na kumfungulia mlango kisha alimshika mkono na kuingia naye ndani. Sebuleni alikuwa mama Colin akizungumza na msichana wa kazi alipomuona Colin alinyanyua macho na kumuona ameongoza na hasimu wake.
Alijikuta akiponyokwa na glasi ya juisi aliyokuwa ameshikilia. Cecy alisogea hadi karibu na mama Colin na kumsalimia.
“Shikamoo ma mkwe,” kama kawaida alipiga goti la heshima mpaka chini.
Mama Colin alinyanyuka alipokuwa amekaa na kumfuata Cecy na kumnyanyua alipokuwa bado amepiga magoti na kumkumbatia kwa muda huku machozi yakimtoka.
Colin alishangazwa na mama yake kufanya vile aliamini alifanya vile kujitakasa mbele ya macho ya mwanaye lakini moyoni alikuwa na nia mbaya kuliko bomu la kutegwa. Alijiuliza mama yake atamwambia nini kwa kitendo cha kigaidi alichokifanya cha kusambalatisha penzi lake.
“Cecy,” alimwita huku akimshika mabegani na kumtazama usoni kwa macho yaliyojaa machozi.
“Abee ma’ mkwe,” Cecy aliitikia huku naye machozi yakimtoka.
“Najua siku ya leo huenda hutanielewa, unaweza kuwa msichana wa kwanza kunionesha kitu si cha kawaida. Lakini nilichokifanya leo ni mtihani wangu wa mwisho kwako, nakili kwa moyo wangu katika wasichana niliowapenda ulikuwa wewe namba moja.
“Lakini sikumaanisha kuwa utakuwa mke wa mwanangu kwa vile nilikuwa na Malengo makubwa kwa mwanangu baada ya kutumia kiasi kikubwa kumsomesha.
Niliamini mwanamke atakayemfaa ni mwenye elimu kama yake pia anayetoka katika familia yenye uwezo ambaye atakuwa na mapenzi ya kweli na hatafuata mali aliyonayo mwanaume.
“ Niliamini chaguo langu lilikuwa sahihi la kumchagua Mage kwa vile ni msomi tena anatoka katika familia yenye uwezo pia mama yake ni shoga yangu. Lakini kumbe siyo, nakiri toka moyoni mwangu mapenzi niliyokuwa nikimpenda Cecy yaligeuka na kumuona ni adui namba moja anayetaka kuvuruga ndoto zangu.
“Mwanzo nilidhani utani lakini siku ya birthday ya Colin nilivyokuona ulivyopendeza mpaka kukusahau na picha nilizomkuta nazo Colin niliona ndoa hakuna. Moyo wangu ulikosa amani mpaka mipango ya harusi kwenda vizuri huku nikiwa sisikii taarifa yako.
“Kwa kweli niliumia sana kwa kitendo cha Mage kuuvunja uchumba tukiwa katika hatua za mwisho. Siku zote nilikosa usingizi nimekuwa nikipungua siku hadi siku. Kitendo cha kuibuka wewe kwa kweli kilinichanganya sana, sikuamini kama una mapenzi ya kweli na mwanangu zaidi ya kufuata mali zetu.
“ Mtihani niliokupa leo umenipa sababu sahihi ya mwanangu kukuchagua wewe kuwa mkewe. Cecy kitendo cha leo kilifukua mapenzi yote ya nyuma na kukiri mapenzi si elimu wala mali bali upendo wa dhati toka moyoni mwa mtu. Umenionesha jinsi gani unavyo mpenda mwanangu mapenzi ya dhati si kwa ulichonacho.
“ Napenda kuwaomba radhi wote kwa kuwakwaza kwa namna moja ana nyingine.
Colin mwanangu nataka kukutamkia hili mbele ya mpenzi wako na Mungu shahidi yangu kama nitakwenda kinyume naomba anifanye kitu chochote kibaya. Kuanzia leo namtambua rasmi Cecy kama mkwe wangu na mipango ya harusi itaanza mara moja. “Cecy mkwe wangu kuna zawadi nitakupa kwa kuonesha msimamo na mapenzi ya dhati kwa mwanangu naamini wewe ndiye mke aliyechaguliwa na Mungu.”
Mama Colin alisema huku machozi yakimtoka, kila mmoja alitokwa na machozi, yalikuwa maneno yenye kuumiza moyo yaliyotaka moyo wa chuma kukufanya usidondoshe chozi.
Colin hakuwa na la kumuuliza mama yake baada ya kila kitu kuwekwa wazi. Mama yao aliwakusanya na kuwakumbatia wote kisha aliwaachia na kutaka kupiga magoti kuwaomba msamaha lakini walimuwahi mama yao kabla hajapiga.
“Hapana mama huna kosa, bali sisi ndiyo tulikwenda tofauti na mawazo yako, tunaomba utusamehe sana. Ombi letu utupe idhini toka moyoni mwako ili tufunge ndoa yenye baraka,” Colin alimwambia mama yake.
“Mungu ananisikia nimeibariki ndoa yenu duniani na mbinguni.”
“Ma’ mkwe, naomba usinipe zawadi yenye gharama kubwa bali kunipa mume wa ndoto yangu, inawezekana uliponiita mkwe na kunieleza nitaolewa na mwanao anayesoma Ulaya ulidhani utani. Na siku nilipomuona nilichanganyikiwa zaidi, moyoni niliamini nimeokota dhahabu katikati ya soko.
“Lakini niliumia siku nilipojua kumbe kuna chagua sahihi la Colin, kuanguka kwangu si ungonjwa bali presha ilipanda na kushindwa kujizua. Niliamua kujitoa na kukaa pembeni huku nikiwa nimejikatia tamaa. Niliumia zaidi siku Mage alipomshusha Colin kwenye gari na kumdhalilisha kwa kweli japo nilikuwa sipendwi niliingilia ugomvi kwa vile chenye thamani kwenye moyo wangu nikikiona kikidhalilishwa.
“Mpaka leo mama unasema maneno matamu kama haya si kwa urahisi bali nimetoka jasho la damu. Nashukuru mama mkwe, nakuahidi kuwa mke bora na kufurahia chaguo lako la awali.”
Ilikuwa furaha siku hiyo iliagizwa shampeni na kufurahi kutambulika rasmi kwa Cecy katika nyumba ya kina Colin.
****
Mipango ya harusi ya Hans na Mage ilikwenda vizuri, mama Mage hakuwa na haja ya kukusanya tena michango ya sherehe zaidi ya kugawa kadi za send of ya harusi ya mwanaye. Katika watu waliopelekewa kadi ya send of ya Mage ni familia ya mama Colin, tena Mage alisisitiza Colin ahudhulie send of yake.
Taarifa zilifika Colin alikubali kuhudhulia kwa kujua hataumia kwani Cecy alikuwepo.
Siku ya sherehe ya send of Colin na Cecy waliingia wakiwa watu wa mwisho, ilikuwa siku ambayo Cecy aliitafuta kwa udi na uvumba kuwaonesha walimwengu kuwa kila mguu hutulia kwenye kiatu saizi yake wala si kuvaa kikubwa kikakupwaya au kidogo kikakubana lakini kwake kilikuwa kimetulia.
Wakiwa wamependeza Colin katika vazi la shati refu la kitambaa cha maua laini na suruali nyeusi na viatu vyeusi vilivyo chongoka kidogo mbele. Cecy alivaa gauni refu jekundu la mikanda mabegani la kitambaa chepesi na viatu virefu vilivyoongeza mzuri wake.
Waliingia taratibu huku Cecy akiuweka mkono wa Colin kwapani kwake na kuushika kwa mbele. Waliingia taratibu na kufanya watu wote wageuze shingo kuwatazama wapenzi wawili walionekana kama ndiyo wamepata shahada ya mapenzi muda si mrefu.
Mage alishtuka kumwona Colin akiwa amependeza sana akiwa na msichana mrembo ambaye alimsahau kama ndiye aliyempa kipigo siku alipomdhalilisha Colin. Moyo ulimlipuka na kujikuta akiingia wivu, Colin alikuwa na tofauti kubwa na Hans kimuonekana alikuwa ana mvuto kwa mwanamke yoyote.
Lakini mapenzi yake Hans yakuwa makubwa kuliko kitu chochote chini ya jua. Colin pamoja na umbile na sura nzuri lakini kwake moyoni kwake alikuwa na nafasi ndogo.
Naye mke matarajiwa alipendeza katika gauni la kitenge alililoshonwa kwa ustadi mkubwa na kumwongezea urembo wake. Aliamini kabisa msichana aliyechukua nafasi yake alikuwa kama maji ya bahari na yeye, kuvunja uchumba na Colin ilikuwa sawa na kuchota maji kwa kikombe ndani yake na kufanya pengo lake lisionekane kabisa.
Sherehe ilienda vizuri kila mtu aliyekuwepo aliisifia jinsi ilivyofana kwa burudani iliyoandaliwa ilifanya wageni wasichoke kuwepo ukumbuni pale.Katika watu walikuwa na furaha siku ile alikuwa mama Colin baada ya kumwona mwanaye alivyopendeza akiwa na Cecy msichana aliyekuwa kama dhahabu iliyokuwa imechafuliwa na tope lakini mwanaye aliisafisha na thamani yake kuonekana mbele ya macho ya watu.
Itaendelea Jumatatu

No comments