Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 19


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Katika watu walikuwa na furaha siku ile alikuwa mama Colin baada ya kumwona mwanaye alivyopendeza akiwa na Cecy msichana aliyekuwa kama dhahabu iliyokuwa imechafuliwa na tope lakini mwanaye aliisafisha na thamani yake kuonekana mbele ya macho ya watu.
SASA ENDELEA...
Katika kitu kilichomvutia siku ile ni jinsi Cecy alivyojiamini sana, kwake lilikuwa kama jibu ambalo alitamani siku moja Mage alipate baada ya kumuacha mwanaye. Kitendo cha kuonesha mapenzi mazito kwa mwanaye kilimpa faraja kubwa moyoni mwake na kujiapiza kumpa zawadi kubwa japokuwa alionesha Cecy haitaji zawadi ambayo aliitafsiri kama hongo.
Alipanga siku ya harusi ya mwanaye ampe Cecy zawadi ya nyumba ambayo ataanza kuijenga wakati wowote na zawadi ya gari la kifahari ili kurudisha shukurani kwake kumwokoa mwanaye aliyeachwa ghafla kama chuma cha moto kilichozimwa kwa kumwagiwa maji ya baridi lazima kipinde.
Aliamini kitendo Mage kumuacha ghafla lazima angekuwa kwenye hali mbaya lakini yeye alikuwa wokozi wake na kulipigania penzi la mwanaye mpaka mwisho kuibuka mshindi. Kila alipoyafikiria yale na kuangali mwanaye na Cecy walivyopendeza alimshukuru Mungu kutenda muujiza.
Sherehe iliendelea ilifika wakati wa Mage kwenda kumnyanyua mumewe matarajiwa alipokaa. Alinyanyuka alipokuwa na kuanza kumtafuta Hans aliyekuwa amekaa nyuma, alizunguka taratibu kwenye meza akimtafuta. Kwa vile toka Colin aingie na msichana mrembo alikuwa na hamu ya kutaka kuthibitisha uzuri aliouona kwa mbali ni kweli au cosmetic na vazi ndivyo vililompandisha chati.
Alitembea taratibu kwa kumtafuta kila meza iliyokuwa na mwanaume, alikwenda hadi kwenye meza aliyokuwa amekaa Colin na Cecy. Akitembea kwa mwendo wa taratibu alisogelea karibu macho yake yakiwa kwenye uso wa Cecy. Pamoja na kupata jibu lililokuwa akiusumbua moyo wake tangu Colin alipoingia akiwa ameongozana na msichana mrembo ambaye aliamini yule msichana ndiye mrembo kuliko wote waliokuwepo pale ukumbini.
Alishtuka kuiona sura ya Cecy, moyo ulimshtuka baada ya kumkumbuka ndiye aliyemshushia kipigo siku alipomteremsha Colin kwenye gari lake. Moyo ulimuuma kuona pamoja na kumpenda Colin kumbe alikuwa na msichana wa pembeni. Japokuwa sura ilikuwa yenyewe alitaka kujua jina lake kwa vile jina aliloitwa na Colin siku ile alikuwa akilikumbuka ili kupata uhakika asilimia mia.
“Mambo Colin?” Mage alisimama kidogo meza ya Colin na kumsemesha.
“Poa, hongera.”
“Asante, huyu ndiye wifi?”
“Si wifi ni mke mwenzio,” Cecy alijibu.
“Mmh! Anaitwa nani?”
“Cecy.”
“Si..si ndiye aliye ni…ni..”
“Shoga ndiye mimi, wee kamtafute mumeo mengine achana nayo,” Cecy alimpa makavu huku akibinua midomo ya dharau na kumpiga busu Colin.
Mage hakuwa na jibu aliondoka bila kuongeza neno akitamani kuomba Cecy aondolewe kwenye sherehe yake na kujilaumu kumwalika Colin kwani aliharibu furaha yake yote ya siku ile.
Baada ya kuzunguka meza kadhaa alifika alipokuwa Hans, alimshika mkono na kufanya ukumbi ulipuke kwa furaha. Aliongozana hadi meza iliyoandaliwa maalumu kwa ajili ya kukaa pamoja. Sherehe iliendelea huku zoezi la chakula likianza kwa kutangulia Mage na mumewe mtarajiwa.
Baada ya maharusi watarajiwa kuchukua chakula, wengine walifuata na kurudi kwenye nafasi zao. Wakiwa katika ya chakula aliingia mwanaume mmoja mtanashati lakini mwenye mwili mkakamavu hadi kwa MC na kuzungumza naye kitu na kuonesha meza aliyokaa bibi na bwana harusi watarajiwa.
Yule bwana alikwenda kwenye meza ya chakula alipokuwa amekaa bwana harusi na kumwomba wazungumze nje ya ukumbi. Hans alikitaka wazungumze pale ilibidi yule bwana amnong’oneze kitu. Ghafla Hans alikuwa mpole na kumwambia Mage.
“Samahani mpenzi nakuja.”
“Kuna nini?” Mage alishtuka.
“Nakuja sasa hivi.”
“Fanya haraka bwana.”
“Poa.”
Hans alijibu kwa mkato na kuongozana na yule mtu hadi nje ya ukumbi, alipofika nje alielekezwa gari la kuingia lilikuwa limesimama pembeni ya ukumbi. Alipofungua mlango na kukaa alikutana na pingu huku akiambiwa.
“Tuna imani kosa lako unalijua?”
Hans hakujibu alikaa kimya, baada ya kutojibu askari alimuuliza swali lingine.
“Unamjua huyu?”
Alioneshwa kijana mmoja aliyekuwa amemekaa pembeni yake ameinamisha kichwa. Alipomwangalia vizuri alimkumbuka na alishtuka na kujisema moyoni. “Nimekwisha.”
Hans alichukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi. Alipofika aliingizwa chumba maalumu kwa ajili ya mahojiano. Kila aliloulizwa kuhusiana na kuhusika na njama za kuuawa mkewe na mwanaye alibakia bubu, baada ya kubana sana alikubali kuhusika kwa namna moja japo yeye hakuua.
Nyuma sherehe iliendelea huku Mage akiamini mchumba wake atarudi wakati wowote, baada ya muda bila kuonekana ilibidi aulize kuhusu mchumba wake.
Mara moja walianza kufuatilia, kwa kumuuliza rafiki kipenzi cha Hans, Ndubikile ambaye alikuwa amekaa bila kujua nini kinaendelea.
Hata yeye alishtuka sana na kuamua kupiga simu yake ambayo ilipokelewa na mtu mwingine.
“Haloo una shida gani?”
“Samahani nina imani napiga namba ya Hans?”
“Ndiyo.”
“Mwenye simu yupo wapi?”
“Yupo kituo cha polisi cha kati.”
“Ha! Amefanya nini?”
“Ukifika kituoni utajua kila kitu.”
“Sawa.”
Baada ya kukata simu aliwageukia waliokuwa wakitaka kujua kutoweka ghafla kwa Hans.
“Jamani waliomchukua hapa ni askari ambao wamempeleka kituoni cha kati.“
“He! Kwa kosa gani?” waliuliza wote kwa mshangao.
“Wamesema tufike kituoni tutajua kila kitu.”
Ilibidi watu watumie busara na kuficha kilichokuwa kikiendelea na kumdanganya Mage ili shughuli isivurugike kwa kumwambia Hans amekimbilia hospitali mdogo wake kapata ajali. Wakati sherehe ikiendelea familia ya Hans ilipewa taarifa zile nayo iliondoka kufuatilia kituoni.
Walipofika walielezwa kuwa Hans anashikiliwa na polisi kwa kosa la kupanga mauaji ya mkewe na mwanaye. Wote walishtuka na kutaka isibitisho wa habari zile, walielezwa jinsi walivyofuatilia mauaji yale taratibu mpaka kuwakamata wauaji ambao walijitetea kutumwa na Hans ili aweze kumuona mpenzi wake wa zamani.
Waliomba kukutana na Hans, walikutana naye na kutaka kujua habari zile zina ukweli wowote.
“Wazazi wangu hakuna ukweli wowote, haiingii akilini nimuue mke wangu na mwanangu kwa ajili ya mwanamke.”
“Basi mwanangu haki itapatikana, nina imani mpaka kunakucha utakuwa umetoka nje,” baba Hans alimpa moyo mwanaye ambaye moyoni alijua kila kitu kinachoendelea.
Kuondoka ghafla kwa familia ya Hans ilizidi kumshtua Mage na kujikuta akikata kususa sherehe. Ilibidi achukuliwe na kupelekwa pembeni na kuelezwa ukweli kuwa mpenzi wake kachukuliwa na polisi. Aliomba kupelekwa kituo cha polisi ili akamwone mpenzi wake kwa kuamini kupitia kwa rafiki wa baba yake mkuu wa polisi atatoka.
Alifikishwa kituo cha polisi na kupelekwa chumba alichokuwemo mpenzi wake na kuonana naye. Mage akiwa amechanganyikiwa macho yakiwa yamemvimba kwa ajili ya kumlilia mpenzi wake ambaye hakujua yupo pale kwa kosa gani.
“Vipi mpenzi kuna nini?”
“Mmh! Mambo magumu.”
“Kivipi?”
“Ile ishu imebumburuka.”
“Ishu gani?”
“Off air”
“Mungu wangu! Sasa itakuwaje?”
“Sijui, lakini naamini imekaa vibaya kwa vile kuna ushahidi mkubwa wa kunimaliza naamini siwezi kutoka.”
“Kwa nini?”
“Kila kitu kipo wazi lazima nitaozea gerezani.”
“Sasa harusi yetu itakuwaje?”
“Mmh! Itategemea muujiza wa ngamia kupita katika tundu la sindano.”
“Yupo ba’ mkubwa naamini utatoka tu,” Mage alimtia moyo mpenzi wake.
“Nami ndicho ninachokiomba.”
“Hebu subiri.”
Mage alichukua simu na kumpigia baba yake mkubwa mkuu wa polisi mzee Clarence. Baada ya kuita ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo.”
“Haloo baba,” Mage alisema kwa sauti ya kulia.
“Vipi mama, mbona unalia?”
“Baba mchumba wangu amechukuliwa kwenye send of yangu na kuwekwa ndani.”
“Kwa kosa gani?”
“Hakuna kosa lolote zaidi ya uonevu.”
“Naomba kuzungumza na mkuu wa kituo.”
“Sawa baba.”
“Mpenzi nimeisha zungumza na baba utatoka sasa hivi ngoja nipeleke simu kwa mkuu wa kituo,” Mage alimueleza mpenzi wake huku akielekea kwa mkuu wa kituo.
“Hakuna tatizo.”
“Samahani kaka kuna simu kutoka kwa mkuu anataka kuzungumza na mkuu wa kituo,” alimwambia askari mmoja aliyekuwa kaunta.
“Mkuu gani?”
“Mkuu wa polisi wote.”
“Nenda chumba cha pili mkono wa kushoto.”
Mage alikwenda hadi mlangoni na kuingia bila hodi kitu kilicho mkasirisha mkuu wa kituo na kutaka kumfukuza.
“We binti toka nje unaingiaje kama msalani.”
“Kuna simu yako toka kwa mkuu wako unatakiwa kuzungumza naye.”
“Mkuu gani?”
“IGP.”
“He! Nipe,” mkuu wa kituo Aloyce Jacob alishtuka na kuichukua simu haraka aliweka sikioni na kusema kwa sauti ya juu.
“Samahani afande.”
“Bila samahani pole na majukumu.”
“Asante mkuu.”
“Kuna kijana mmemkamata usiku huu akiwa kwenye send of ya mchumba wake?”
“Ndiyo mkuu.”
“Kwa kosa gani?”
“Lile la mauaji tulilokuwa tukipeleleza.”
“Sasa yeye anahusika vipi?”
“Ndiye mtuhumiwa mkuu.”
“Una uhakika?”
“Kila kitu kipo wazi, kesho faili lake tunaifikisha mahakamani.”
“Nipe huyo binti.”
Simu alipewa Mage aliyekuwa akifuatilia mazungumzo ambayo yalimtisha na kuona tatizo la mpenzi wake lilivyo zito lakini aliamini kupitia wadhifa wa baba yake mkubwa lazima ataachiwa tu.
“Haloo baba.”
“Sasa mama suala la mpenzi wako lipo kisheria sana, hivyo nakuomba rudi nyumbani ili vyombo vya dola vifanye kazi yao.”
“Sasa baba harusi yangu itakuwaje?”
“Naomba urudi nyumbani kesho nitakuja.”
“Sawa baba.”
Mage alirudi kwa Hans kumweleza alipofikia, Hans aliamini hali ilivyo kulikuwa hakuna dhamana mpaka upelelezi ukamilike. Aliamini ukikamilika lazima utamtia hatiani na kufungwa.
Ilibidi Mage arudi nyumbani kwao akiwa amechanganyikiwa kutokana na tukio lile aliamini ndoa hakuna na atakuwa amepoteza mwana na maji ya moto. Kwa vile sherehe ilimalizwa alirudi nyumbani. Mama yake naye aliona sherehe ya mwanaye imeingia nuksi alitaka kujua kipi kilichompeleka mchumba wake polisi.
“Si lile tatizo lililoniweka ndani.”
“La kifo cha mke wa Hans?”
“Ndiyo.”
“Sasa yeye anahusika vipi?”
“Eti kahusika kumuua mkewe.”
“He! Ili iweje?” mama Mage alishtuka kusikia habari zile.
“Mimi sijui, eti mama mtu akishtakiwa kwa kosa la kupanga mauaji hukumu yake ipo vipi?”
“Kama hajatenda hawezi kufungwa lakini kama kweli amehusika hukumu yake ni miaka 30 au maisha.”
“Mungu wangu nimekwisha!” Mage alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
“Mbona unasema hivyo?”
“Mashtaka ya Hans ni ya kupanga njama za kifo cha mkewe.”
“Sasa wasiwasi wako nini ikiwa haimuhusu, nitampigia simu baba yako mkubwa yataisha.”
“Mama nilizungumza na baba na kutaka kuzungumza na mkuu wa kituo baada ya mazungumzo aliniambia mashtaka yapo kisheria hivyo tuache vyombo vya dola vifanye kazi yake.”
“Mmh! Kama baba yako kasema hivyo itabidi tuwe watulivu.”
“Mama nina wasiwasi huenda harusi yangu haipo.”
“Kwa nini?”
“Nina wasiwasi mpenzi wangu atafungwa.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Hata sijui, mama hivi nikimfuata Colin atakubali kweli kunirudia?”
“Mage umefikiria nini tena mama! Kwa nini umefikia huko, mchumba wako yupo ndani na hana kosa asilotenda atatoka tu.”
“Sasa tutafanyaje?”
Mara simu ya Mage iliita ilikuwa ikitoka kwa mama Hans, alichukua na kuiweka sikioni.
“Haloo mama.”
“Nina imani sasa imefurahi.”
“Nifurahi nini mama?”
“Haya sasa mwanangu anafungwa kwa ajili yako, haya fanya sherehe kwa vile dhamira yako imetimia, imekuwa kama jini wa kutumwa humuachi mtu mpaka uone amefukiwa. ”
“Mama utanionea bure.”
“Tunashukuru ila Mungu yupo,” baada ya kusema vile alikata simu na kumuacha Mage kasimama kama sanamu kitu kilichomshtua mama yake.
“Nini tena?”
“Mama huu mkosi gani?” Mage alisema huku akilia.
“Kwani kuna nini tena mwanangu mbona unatakaa kuniuguza presha?” mama yake alitaharuki.
“Siamini maumivu ninayosikia juu ya mpenzi wangu kuwekwa ndani na kubambikiwa kesi nzito halafu familia yake inasema eti nimefurahi! Mimi Mage nifurahi kufungwa kwa mpenzi wangu?” Mage alimuuliza mama yake huku akibubujikwa na machozi ya uchungu.
Itaendelea

No comments