Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 20


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Siamini maumivu ninayosikia juu ya mpenzi wangu kuwekwa ndani na kubambikiwa kesi nzito halafu familia yake inasema eti nimefurahi! Mimi Mage nifurahi kufungwa kwa mpenzi wangu?” Mage alimuuliza mama yake huku akibubujikwa na machozi ya uchungu.
SASA ENDELEA...
“Nani amekuambia hivyo?”
“Mama Hans.”
“Unaona mwanangu ile siyo familia badala ya kukuonea huruma ndiyo kwanza wanakulaumu, ufanye vile ili iweje ungeweza kuvuruga ndio yako kama mtu humpendi.”
“Mama nakuapia Hans akinioa sitaki kuwaona ndugu wa mume.”
“Mage mwanangu hayo siyo maneno, bado tunataka kuonesha upendo kwa wenzetu kipindi hiki kigumu.”
“Mama wakati Hans yupo ndani nataka kuzungumza na Colin naamini ananipenda sana.”
“Ukiisha zungumza naye?”
“Ili nikamate huku na huku kama Hans atafungwa basi niwe na Colin.”
“Na Hans akitoka gerezani na kukuta umeolewa?”
“Nitajua, nina imani Colin nammudu, nitamweleza ukweli kuwa kwake nilikuwa najiegesha na nimpendaye karudi. Mbona anajua kuwa kwa Hans nimekufa nimeoza.”
“Mage kumbuka ukianzisha uhusiano na Colin mpaka kufikia kufunga ndoa lazima watu watasema umehusika kumfunga mpenzi wako hapo ndipo utaongeza uhasama na familia ya kina Hans.”
“Nitafanya kwa siri.”
“Colin akitaka kukuoa?”
“Nitamvuta kwa muda ili kumsubiri Hans, kama anafungwa maisha sina jinsi kama miaka saba nitajishikiza kwa Colin.”
“Ulivyomuacha atakukubali kweli, ha..ha..lafu leo kaingia na msichana mrembo ni nani yake?”
“Mpenzi wa rafiki yake,” Mage aliongopa.
“Mmh! Ili kutengeneza mazingira mazuri unatakiwa kujipendekeza kwa mama Colin.”
“Nitafanya hivyo, najua yule mama ananipenda sana nikimfuata na kumweleza nimerudi kwa mwanaye nina imani atapiga vigelegele.”
“Mmh! Haya.”
Mage aliachana na mama yake na kwenda chumbani huku mawazo yake yote yakiwa kwa Colin kutokana na kuujua ukweli wa kesi ya Hans kwa kuamini kutoka kutakuwa muujiza. Alipanga kuanza kujipendekeza kwa familia ya kina Colin wakati akisubiri hukumu ya mpenzi wake.
****
Colin alimpeleka Cecy chuo cha urembo ambako alisoma kwa miezi mitatu, muda wote walikuwa kama kumbikumbi kila mmoja alionesha mahaba mazito. Taarifa ya kukamatwa mchumba wa Mage iliwafikia na kushagaa taarifa ya kukamatwa kwake kuwa alihusika na kifo cha mkewe na mwanaye ili tu amuoe Mage.
“Colin yaani naomba kama mama yako atasababisha tutengane usifanye kama mpenzi wa Mage alivyofanya. Heshimu uhai wa mtu, kama ipoipo tu, Mungu ana maajabu yake ameweza kutukutanisha pamoja bila sisi wenyewe kujua. Kwa hivyo ni makosa kulazimisha kitu.”
“Cecy kila dakika nakuwa mwanafunzi wako, wewe ni zaidi ya mwanamke pamoja na umri mdogo lakini Mungu amekupa busara na hekima.”
“Kama ni kweli mpenzi wa Mage anahusika kutenda unyama ule kwa ajili ya Mage atakuwa ametenda dhambi kubwa sana.”
“Mi’ siamini mtu anaweza kumuua mke na mwanaye kwa ajili ya mpenzi wake.”
“Kwa hiyo ungemuoa Mage, mimi ningekuwa na nafasi gani moyoni mwako?” Cecy alimuuliza swali la kizushi.
“Cecy tuachane na hayo, unakumbuka wiki ijayo ndiyo onesho lako la kwanza la mavazi, mazoezi yako yamenipa matumaini ya kuishtua dunia.”
“Mmh! Nitafunikaje maana nguo zote nilizojipima hadi mwenyewe najione wivu, si vibaya kujisifia mi’ mzuri bwana.”
”Siyo mzuri bali mrembo,” Colin alimrekebisha.
“Bwana eeh, urembo unatengenezwa lakini uzuri ni wa asili.”
“Sawa mama umeshinda.”
Wiki moja baadaye liliandaliwa onesho la kwanza la mavazi la kampuni ya Colin litakalo ongozwa na Cecy. Matangazo yalirushwa mwezi mzima katika vyombo vyote vya habari na kufanya watu wengi wavutike na kuapa kutolikosa. Miongoni mwa watu walipanga kwenda kwenye onesho hilo la kwanza la kimataifa alikuwa ni Mage na shoga yake Brenda.
Washiriki walikuwa wengi kutoka ndani na nje ya nchi na kufanya onesho lile lizidi kuvutia watu wengi. Siku ya onesho ilipowadia Mage na shoga yake Brenda walikuwa miongoni ma watu waliohudhulia onesho hilo lililojaza watu wengi. Muda ulipofika maonesho yalianza kwa kuanza kupita wageni ambao walionesha mavazi ya kigeni na kuwafanya watu walipuke mayowe.
Baada ya kumaliza wageni lilianza vazi la Kitanzania kuanzia vazi la vitenge, khanga na vikoi.Walianza kutangulia mabinti ambao nao walikuwa katika kampuni hiyo. Baada ya kupita wote ikafika kipindi akatokea Cecy katika vazi la kitenge chenye kilemba kirefu na kufanya ukumbi ulipuke mayowe.
Alipita na mavai zaidi ya kumi ya ubunifu na kuacha historia kwenye onesho lile.
“Mage huyu si yule msichana aliyeingia na Colin siku ya Send of yako?” Brenda aliuliza baada ya kumfananisha Cecy.
“Ndiye yeye.”
“Mage tuache utani msichana huyu mzuri tena ana uzuri wa asili,” Brenda alimsifia Cecy.
“Hana lolote uzuri upo wapi?” Mage aliponda.
”Wivu huo, kwenye ukweli uongo hujitenga, yule msichana mzuri.”
“Brenda tutakorofishana tumekuja kuangalia mavazi au kuja kumsifia mtu, kwanza mavazi aliyovaa ya kishamba nani sasa hivi anavaa mavazi ya khanga na kitenge. Angejua wala hakupendeza lolote,’ Mage alimbeza Cecy.
“Mageee! Siamini kama una nafasi katika moyo wa Colin, kitu kama hiki hata mimi nikimuona yupo na mpenzi wangu lazima nipate presha,” Brenda alizidi kumuumiza roho shoga yake.
“Brenda naona umetumwa kuja kuniumiza roho, kosa langu kuja na wewe pamoja?” Mage alikuja juu.
“Lakini Mage kwani nikimsifia yule mwanamke kuna ubaya gani ikiwa wewe ni mchumba wa mtu na Colin si mtu wako?”
“Unajuaje kama nitarudiana na Colin.”
“Mrudiane kivipi ikiwa wewe utaolewa na Hans na Colin anaweza kumuoa huyo msichana.”
Wakiwa katikati ya onesho Colin ambaye alifahamika kama mkurugenzi wa kampuni ile ya urembo na mavazi alifuatwa na watu wenye majarida ya urembo kumtaka Cecy kwa ajili ya kuyapamba majarida yao kwa sura yake kwa mkataba mnono. Pia makampuni mengine ya Afrika ya kusini na Ufaransa ambao walikuwa wageni waalikwa walivutiwa Cecy na kuomba kufanya naye kazi kwa mkataba mnono.
Nyota ya Cecy ilizidi kung’aa, Colin aliwakubalia lakini walitakiwa waonane kesho kwa ajili ya mazungumzo zaidi, walikubaliana. Siku ile pia ilikuwa maalumu kwa Colin. Wakati burudani ikiendelea Mc alisimamisha kwa ili mkurugenzi aseme neno.
Colin alichukua kipaza sauti na kuwasalimia wote kisha alisema:
“Ndugu zangu kwanza nashukuru kwa muitikio katika onesho la leo ambalo limekuwa na mafanikio makubwa tofauti na nilivyofikiria. Mpaka sasa tumepata naombi ya kumtaka Malkia Cecy kupamba majarida na pia kwenda kufanya maonesho Afrika ya kusini Marekani na Ufaransa,” kauli ile ilifanya ukumbi ulipuke kwa mayowe.
“Lakini hilo silo lililonifanya nimnyang’anye kipaza sauti Mc, nia yangu nilikuwa nimeweka ahadi moyoni mwangu siku ya leo nifanye kitu gani. Naomba nimwite malkia wa usiku wa leo Cecilia hapa mbele.”
Cecy alitoka chumba maalumu akiwa na gauni refu jekundu lililokuwa likiburuza kwa nyuma, lililokuwa limempendeza sana kama bi harusi.
“Ndugu zangu, wazazi wangu na wageni waalikwa katika onesho hili la kwanza la kimataifa. Leo ndiyo namtambulisha kwenu wakili wa moyo wangu binti mrembo Cecy kuwa ndiye mke wangu mtalajiwa,” ukumbi ulilipuka tena kwa mayowe.
Colin aliendelea kwa kujipapasa na kutoa mkebe mdogo na kusema:
“Cecy mpenzi fumba macho,” Cecy alifanya vile.
Colin alitoka pete ya tanzanite iliyochanganywa na almasi na kukishika kidole cha Cecy na kumvisha na kufanya ukumbi wote kulipuka kwa mayowe kila mtu akisema kuwa kila mmoja kampata mwenzake.
Lile lilikuwa pigo mujarabu kwa Mage aliyekuwa na ndoto za kurudi kwa Colin kama Hans atafungwa.
Mapigo ya moyo yalianza kumwenda mbio na jasho kumtoka kwa wingi, kizungumzungu kikali kilimshika na kiza kinene kilitanda mbele yake na kumfanya adondoke alipokuwa amekaa.
Alichukuliwa haraka kwenda kupewa huduma ya kwanza kwa vile pale ukumbuni kulikuwa na kila kitu.
Shughuli ilendelea kwa Mc kulitangaza vazi jipya la wachumba siku ya kuvishana pete lililompendeza vilivyo Cecy. Baada ya onesho yale Colin alijiandaa kuingia mkataba mnono wa Cecy na hayo makampuni.
***
Cecy aliingia mkataba wa mamilioni ya fedha ya miaka miwili kwa makampuni mawili ya majarida makubwa Marekani moja la Vibe na Ebony kwa ajili ya kupamba ukurasa wa mbele pia aliingia mkataba mnono wa kampuni ya maonesho ya mavazi ya Ufaransa ambayo yabadili maisha ya Cecy toka umaskini wa kutupa mpaka msichana bilionea.
Baada ya kuingia mkataba mnono uliomtaka aanze kazi hiyo mwezi mmoja baadaye kwa ajili ya mazoezi ya mwezi mmoja na kujifunza lugha vizuri kabla ya kuianza kazi hiyo mara moja. Cecy aliomba kuzungumza kwanza na familia yake pamoja na mpenzi wake Colin ili ajue ataanza lini kazi yake, walikubalia na kumpa siku mbili za kutoa jibu ili wakiondoka wajipange vipi.
Ilikuwa tofauti na mapokeo ya Cecy baada ya kulala maskini na kuamka tajiri mkubwa. Ndoto yake ilikuwa kuolewa na Colin na si kufanya kazi ya mabilioni, alijiuliza kukaa miaka mwili nje ya nchi lazima Colin atatafuta mwanamke mwingine na yeye kupoteza kitu muhimu maisha zaidi ya fedha atakazolipwa katika kazi yake.
Kwake alichokitafuta kilikuwa kuwa karibu na Colin na kufanikiwa kuwa naye karibu na kubakia kitu kimoja ndoa ambayo aliiota siku zote. Baada ya kuachana wa wenye makampuni toka nchini za nje. Cecy alionekana mtu mwenye mawazo tofauti na kitu alichokipata cha kugeuka bilionea kwa kufanya onesho lake moja na kuonekana.
Baada ya kufika nyumbani ilibidi amuulize:
“Vipi mpenzi wangu mbona kama hauna furaha wakati leo umeuaga umaskini?”
“Mi kwangu naona kama ndiyo unataka kuniongezea umaskini,” Cecy alijibu kinyonge.
“Kivipi?”
“Hivi nikiwa huko tutakuwa pamoja?”
“Hapana ila tutaonana mara chache kwa vile utakuwa bize na kazi yako ya kuizunguka dunia kufanya maonesho.”
“Uoni kama nitakuwa nimepata fedha zisizo na faida kwangu.”
“Kivipi?”
“Colin wewe ni kila kitu kwangu, niliapa kuwa mbali na wewe ni pale mmoja wetu akichukuliwa na umauti na si vinginevyo.”
“Hilo tu, nitakuwa naonana na wewe kila mara wala usihofu.”
“Colin nina wasiwasi nikiwa mbali kuna vipanga watu watakunyakuwa na mimi kuichukia dunia, kukupata nimetoka jasho la damu. Furaha yangu ni kuwa karibu yako na si kuingiza mamilio ya fedha.”
“Najua mpenzi unanipenda lakini hili dili ni zaidi ya mapenzi kwa vile litayabadilisha maisha yako sasa hivi una uwezo wa kujenga gharofa Masaki au Kunduchi.”
“Colin mimi huko siendi na hizo hela zao sizitaki.”
“Usifanye hivyo, ukilipoteza hutakuja kujuta maisha yako yote.”
“Moyo wangu naujua hauna shida ya mabilioni ya watu bali upendo toka kwako, pia naona umekwenda kinyume na makubaliano yetu.”
“Kivipi mpenzi?”
“Ulisema unataka kunifungulia kampuni ili niwe nafanya maonesho na si kwenda kufanya kazi nje ya nchi.”
“Mpenzi, yaani dili ulilopata fedha utakayoipata kwa miaka yote hiyo unaweza kukaa bila kufanya kazi na kuishi maisha ya juu.”
“Sina maana hiyo, uliniahidi baada ya kumaliza masomo unanioa sasa ahadi yetu ipo wapi? Au ndiyo unanitoa kijanja urudiane na Mage baada ya mpenzi wake kufungwa?” Cecy alilia wivu.
“Ahadi yetu ipo palepale, we fanya kazi mwaka mmoja kisha tunafunga ndoa ndipo nitajua nitafanya nini.”
“Cecy mpenzi hujui tu kiasi gani cha fedha utakacholipwa, ni wasichana wachache dunia wenye bahati hii. Tukitaka tufanye harusi itachukua muda wakati mwezi ujao unatakiwa Afrika ya Kusini kwa mazoezi ya wiki mbili kabla ya kwenda Ufaransa. Kutokana na makubaliano picha za jarida la Ebony watatumia za kwenye onesho na zile walizokupiga siku ile. Malipo yako ya kwanza yataingia mwezi ujao ya dola elfu mia mbili arobaini(408,000,000) kwa mwaka. Baada ya mwaka malipo yataongezeka na kuwa dola elfu mia tatu (510,000,000). Pia utapata bonas ya asilimia tano kutokana na mauzo huoni kwa miaka miwili utakuwa mbali mpenzi wangu kwa kutengeneza dola elfu mia tano arobaini (918,000,000).
Bado kampuni ya maonesho itakulipa dola elfu mia tatu (510,000,000) kwa mwaka na bonasi kila onesho la nchi kubwa barani Ulaya na Amerika. Unataka nini tena mpenzi wangu, kipindi hiki hebu ndoa iweke pembeni tupige pesa.”
“Colin nakuona kama unampigia mbuzi gitaa, nakueleza kwa mara ya mwisho pesa inaweza kununua kitu chochote chini ya jua lakini si furaha ya moyo wa mtu dawa ya mtu ni mtu si kitu.”
“Mmh! Sasa wewe ulikuiwa unatakaje?”
“Kwanza tuoane kisha tutajua kama kwenda au kufanyia kazi hapa lakini si kukaa mbali na wewe.”
Ulikuwa mtihani mzito kwa Colin kutokana na msimamno wa mpenzi na kuliona kama dili lile litapeperuka kwani walikuwa wapo wapo nchini wakisubiri kauli yao ataanza lini kufanya kazi. Lakini kwa Cecy alikuwa haelewi kitu bado ya kutetea ndoa yake pia kuwa karibu na mpenzi wake kwa kuogopa vibaka vya wapenzi wa watu.
Itaendelea

No comments