Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 21


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Ulikuwa mtihani mzito kwa Colin kutokana na msimamno wa mpenzi na kuliona kama dili lile litapeperuka kwani walikuwa wapo wapo nchini wakisubiri kauli yao ataanza lini kufanya kazi. Lakini kwa Cecy alikuwa haelewi kitu bado ya kutetea ndoa yake pia kuwa karibu na mpenzi wake kwa kuogopa vibaka vya wapenzi wa watu.
SASA ENDELEA...
Jioni ya siku ile Colin alikutana na mama Cecy na kumuelezea hatua waliyofikia na uamuzi wa Cecy.
“Mama nilikuwa naomba umweleze mwenzangu akubali kwanza kwenda kufanya kazi ndoa itafuata baadaye.”
“Mmh! Nitajaribu kumweleza, nina imani atanielewa.”
“Yaani nitashukuru sana, sijawahi kuona mwanamke mwenye msimamo kama Cecy.”
Kwa vile Cecy alikuwa amekwenda kuoga aliporudi alikaa pembeni ya mama yake na kumuacha Colin aliyekuwa amekaa kochi la peke yake. Baada ya ukimya mfupi mama Cecy aliuvunja ukimya ule.
“Cecy mama.”
“Abee mama.”
“Nina imani leo Mungu atuangazia maisha yetu?”
“Ni kweli mama, lakini maisha hayatakuwa na furaha bila kutimiza ndoto yangu.”
“Najua una hamu ya kutimiza ndoto yako, lakini kilichotokea ni muhimu kwa wakati huu ndoa yako ipo palepale.”
“Hilo nalijua, siku zote fimbo ya mbali haiuwi nyoka, kama nitaanza kazi naweza kukaa hata miezi mitatu bila kumuona Colin na wakati penzi langu limenitoa jasho la damu. Naweza kupata fedha lakini nikapata jeraha lisilopona mpaka nakufa na pengine likawa ndio sababu ya kifo changu.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Mama kama unavyojua mchumba wa Mage yupo ndani na kesi yake ni nzito, kwa habari za juujuu kweli anahusika katika vifo vya mkewe na mwanaye ili arudiane na Mage. Kwa hiyo uwezekano wa kutoka ni mdogo huoni muda huo nikiwa mbali na Colin penzi linaweza kuzaliwa upya na nafasi yangu kupotea.
“Kama nilijitoa kwa ajili ya Colin ifike wakati nimkose hizo fedha zitakuwa na faida gani kwangu. Nipo tayari kupoteza hata fedha zilizojaa bahari lakini si kumpoteza Colin, moyo wangu ndiyo unaojua thamani yake si yeyote. Mama hujui kiasi gani niliumia niliposikia Colin akioa lakini machozi yangu hayakwenda bure, Mungu alisikia kilio changu na kunirudishia mpenzi wangu mikononi mwangu na kuamini haki ya mtu huwa haipotei bali hucheleweshwa.”
“Sasa kama unafahamu hivyo kwa nini una wasiwasi na Mage?”
“Mama, Golden chance never came twise.”
“Hapo umeniacha feri una maanisha nini?”
“Kwangu hii ni nafasi ya dhahabu kamwe haijirudii mara mbili.”
“Cecy nakuahidi wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu, nilivyofahamu thamani yako ndani ya moyo wangu upengo wangu uliongezeka mara dufu. Cecy wewe ndiye wakili wa moyo wangu uliyenitetea wakati wa matatizo hakuahidi sitamfungulia mwanamke mwingine moyo wangu nilipokufungia moyoni mwangu ufunguo niliutupa baharini,” Colin alimuhakikishia mapenzi yake ya dhati kwake.
“Colin ufunguo kuutupa baharini ni usemi tu lakini mnasahau ufunguo unaweza kumezwa na samaki na kuurudisha watu wakauokota na kuufunguo moyo wako na mimi ukanitoa moyoni mwako. Colin unanipenda?” Cecy alimuuliza Colin huku amemkazia macho.
“Zaidi ya sana na kama kuna kauli nyingine zaidi ya hiyo ungeijua ningeisema mbele yako.”
“Naomba unioe.”
“Nitakuoa kwa vile wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu.”
“Si kwa wakati mnaotaka ninyi bali kabla ya kuanza kazi yangu nataka nikisimama sehemu nijulikane kama mrs Colin na si miss Cecy.”
“Muda tuliopewa ni mdogo sana wa maandalizi ya harusi, hivyo ungekwenda kufanya kwanza kazi kisha ukirudi tutafunga ndoa utakuta maandalizi tayari ukifika tunafunga ndoa na kuondoka.”
“Kwani kazi si naanza mwezi unaokuja huu muda hatuwezi kufunga ndoa?”
“Cecy wewe sasa si Cecy muuza ndizi bali wa kimataifa kwani wiki ijayo sura yako inaruka dunia nzima kwenye Jariba la Ebony harusi yako haitakiwi ya kulipua bali iendane na wewe mwenyewe.”
“Mimi Cecy hata niwe vipi bado nitabakia Cecy muuza ndizi, kwa hiyo kama mna nia nifanye kazi tufunge ndoa ya kawaida ila sherehe nikirudi zaidi ya hapo kazi yenyewe siitaki na msiambie kitu kinachohusu hiyo kazi. Fedha inatafutwa kwa njia yoyote lakini upendo kwa kweli ni adimu kama maji jangwani.
“Naweza kumsifu Mage kwa kuvunja uchumba wetu si kwanza nimepata nafasi bali amezieleza hisia zake za kweli toka moyoni kwake kuwa kuna mtu aliyekuwa akipenda kwa dhati. Kosa walilofanya kuua viumbe wasio na hatia lakini walikuwa wapo sahihi kabisa. Kama mliona Mage yupo radhi kulaaniwa na dunia kwa ajili ya mapenzi basi na mimi nipo tayari kufa maskini kwa ajili ya mapenzi,” Cecy alisema kwa sauti kavu isiyo na mzaha hata kidogo.
“Mmh! Mwanangu Colin mpaka hapo mimi sina neno siku zote mwenye kujua maumivu ya moyo ni mhusika, wengine ni washauri na mwisho wa siku ana uamuzi wa kukubali au kukataa anabakia nao mwenyewe na mwenzio amekataa,” mama Cecy hakuwa na kuongeza baada ya kauli ya mwanaye.
“Mama nimesikia yote nitayafanyia kazi, najua kabisa Cecy ananipenda na ameteseka juu yangu. Nimemuhakikishia yeye ndiye chaguo la moyo wangu na mwanamke wa maisha yangu kwa vile moyo wake imeingia wasiwasi basi nitafanya anavyotaka mpenzi wangu ili aamini mbegu yake ya upendo imemea kwangu na kuzaa matunda.”
“Hilo ndilo neno nililokuwa nikilisubiri usiku na mchana, najua hukupenda maamuzi yangu lakini utaamini siku moja kwa nini nimeharakisha harusi.”
Baada ya makubaliano ya kufunga ndoa kabla ya kwenda kuanza kazi, Colin alikwenda kwa mama yake kumweleza taarifa ya Cecy kupata mkataba mnono na kutakiwa kwenda kufanya kazi nje na alivyong’ang’ania kuolewa kuliko kufanya kazi. Alipofika nyumbani alimkuta mama yake amekaa sebuleni, alimsalimia na kukaa pembeni yake.
“Vipi baba, una jambo?” mama yake alimuuliza kwa vile alifahamu vizuri mwanaye.
“Ndiyo mama.”
“Ehe,” mama yake aliweka vitu vyake chini na kugeuka amsikilize vizuri mwanaye kwa vile kila kukicha alikuwa na jakamoyo. Hasa baada ya ndoa ya mwanaye na Mage kuvunjika katika hatua za mwisho.
Colin alimweleza mkataba alioingia Cecy na makampuni yote ambayo yalimuacha mama yake kinywa wazi kufikia hatua ya kusema.
“Yaani Cecy muuza ndizi alipwe mamilio ya fedha kwa kazi ya kupamba jarida na kuonesha mavazi huoni atakutana na watu wengi wenye fedha na wewe kumkuacha. Kwa nini umemtafutia kazi kama hiyo wakati shida yako ilikuwa awe mkeo kwa vile hatuna shida katika maisha yetu.”
“Mama, yote hayo tisa kuna kitu Cecy kanichanganya sana yaani mpaka kichwa kinaniuma,” Colin alisema kwa sauti ya unyonge.
“Kitu gani? Nilijua lazima uhusiano wenu utaingia dosari pesa atakazolipwa ni nyingi sana hasa akizingatiwa alikuwa hohehahe,” mama Colin alichangia bila kujua anataka kuambiwa nini.
“Sivyo unavyofikiria, mama Cecy anataka ndoa kabla ya kwenda kuanza kazi.”
“He! Si umesema mwezi ujao anatakiwa kuondoka?”
“Ndiyo, lakini yeye amesema bila ndoa na kazi hataki.”
“Mbona sikuelewi hataki kazi kwa ajili ya ndoa?”
“Ndiyo mama, anataka akiondoka hapa awe tayari mke wangu.”
“Kwa nini anafanya haraka hivyo, kwa nini asiende kwanza kisha arudi kufunga ndoa wakati huo maandalizi yatakuwa yamekamiliksa anaolewa na kuondoka.”
“Amekataa, amesema nikimlazimisha kwenda na kazi yenyewe hataki.”
“Kweli elimu ni muhimu. Yaani anataka kuyakataa mamilioni kwa ajili ya ndoa tu?” mama Colin alishangaa.
“Mama Cecy ni tofauti na wanawake wengi, mimi kwake ni kila kitu hasikii wala haoni anasema anaweza kuondoka huku nyuma Hans akafungwa hivyo naweza kurudiana na Mage na yeye kupoteza alichokitafuta muda mrefu. Yupo radhi kuendelea kuuza ndizi lakini si kunikosa mimi.”
“Mmh! Kazi ipo, sasa utafanyaje?”
“Nilikuwa naomba ushauri wako japo nilimkubalia kufunga naye ndoa kabla ya kuanza kazi.”
“Ninafikiri wazo lako zuri, japokuwa sikupenda harusi ya aina hiyo, lakini kwa vile naujua msimamo wa yule msichana sina budi kukubaliana nawe. Sijawahi kuona mwanamke msimamo mkali kama yule binti. Anajiamini katika kitu anachokitafuta hasa akiwa na haki nacho.”
Walikubaliana kufanya maandalizi ya harusi kwa kuandaa vikao vya wiki tatu, wiki ya nne inakuwa harusi.
***
Baada ya upelelezi wa kesi ya Hans kupanga njama za kifo cha mkewe na mwanaye kukamilika ilisomwa hukumu katika mahakama kuu. Siku hiyo walijaa watu pomoni kutaka kusikiliza nini kitakacho amuliwa juu ya tuhuma za Hans kumuua mkewe. Baada ya jaji kukaa kwenye kiti chake na watu wote kukaa chini alitulia kupanga kalatasi zake vizuri kisha alikohoa kidogo kuwafanya watu wote wakae tayari kumsikiliza wakiwemo Mage, mama yake shoga yake Brenda, familia nzima ya Hans pia alikuwepo mama Colin, Colin na mchumba wake Cecy.
Watu wote walitulia kumsikiliza jaji huku mioyo ikiwadunda wakiomba utokee muujiza utakao badili damu kuwa maji meupe. Kwa sauti yenye kusikika alisema:
Nina imani wote uliopo hapa mnajua tupo hapa kwa sababu gani, leo ndiyo siku tunayo hitimisha kesi inayomkabiri Hans Simgao ambaye anakabiriwa na kesi ya mauaji iliyochukua takribani mwezi mzima na leo ndiyo siku ya hukumu yake.
Kama kawaida kesi hii ilianza kusikiliza mahakama ya mwanzo ambayo haikuwa na uwezo wa kuhukumu na kuamuliwa kuletwa huku mahakama mkuu yenye uwezo wa kutoa hukumu kwa kesi yoyote nzito.
Baada ya hukumu kama mtuhumiwa hata ridhika na hukumu hii bado ana nafasi ya kwenda mbele zaidi kwenye mahakama ya rufaa.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote za mashtaka na utetezi na mahakama kuridhika utetezi wa pande zote. Kutokana na maelezo upande mashtaka unaosema kuwa mtuhumiwa aliwatuma watu kumuua mkewe ili arudiane na mpenzi wake wa zamani ambaye wakati huo alikuwa kwenye maandalizi ya kuolewa na mwanaume mwingine.
Baada ya mashahidi wote waliopanda kizimbani akiwemo mchumba wa marehemu kutoa ushahidi wao ambao ulifanyiwa kazi na hatimaye kujiridhisha na ushahidi upande wa mashtaka ambao unatia hatiani moja kwa moja mtuhumiwa kwa hiyo mahakana inamuhukumu Hans Simgao kifungo cha maisha gerezani na kazi ngumu. Narudia tena kusema kuwa kama hamjalidhika na hukumu hii mna nafasi ya kukata rufaa mahakama ya rufaa,” hakimu alimaliza hukumu yake.
Hakimu baada ya kutoa hukumu ile iliamsha vilio mahakamani huku mama mzazi na Mage kuanguka chini na kupoteza fahamu. Ilibidi huduma ya kwanza ifanye kazi yake ya ziada kutoa huduma ya kwanza kutokana na watu wengi walipoteza fahamu baada ya hukumu nzito iliyompoteza Hans uraiani.
Baba yake hakukubaliana na huku ile na kuapa kukata rufaa kuhakikisha mwanaye anachiwa huku kwa vile makosa yalionekana ya kutengeneza lakini aliamini mwanaye hawezi kumuua mkewe kwa ajili ya mwanamke. Wakili aliyewekwa kutetea kesi ile aliomba nakala ya hukumu ili waweze kukata rufaa.
***
Mage alizinduka na kujikuta amelala kwenye kitanda cha hospitali akiongezwa maji, pembeni alikuwa mama yake na shoga yake Brenda. Alipowaona aliangua kilio upya huku akisema:
“Mama mkosi gani nimekosa Bara na Pwani, hivi nitaweka wapi uso wangu mbele ya jamii wakijua mimi ndiye niliyesababisha kifo cha mke wa Hans huku wengine wakiniona mimi ndiye sababu ya Hans kufungwa maisha.”
“Mage aliyoyafanya Hans hukumtuma kafanya kwa matakwa yake siamini kama angekushirikisha ungemkubalie afanye unyama kama ule. Ni heri angempa talaka kuliko alichokifanya,” alisema Brenda.
“Brenda naamini nuksi ndiyo nyota yangu haiwezekani Hans afungwe maisha Colin naye awe na mpenzi. Nina imani sina faida ya kuendelea kuishi.”
“Mage unataka kufanya nini?” Brenda alishtuka.
“Mwanangu hayo ni mawazo gani, Hans kufungwa si mwisho wa maisha bado una nafasi ya kuitafuta furaha,” mama yake alimtia moyo.
“Sasa mama hiyo furaha nitaipata wapi ikiwa hata aliyemweka kama spare tyre ana mwanamke mwingine ambaye ni mzuri kuliko mimi.”
“Brenda yote umeyataka mwenyewe ungenisikiliza sasa hivi ungekuwa kwa mumeo.”
“Mama sikubali nitalipiganie penzi la Colin kwa gharama yoyote.”
“Sasa Mage unataka kuchanganyikiwa, juzi tu Colin kamtangaza mchumba wake mbele za watu tena mtu maarufu utaanzia wapi?” Brenda alimuuliza.
“Kama mnataka niendelee kuishi naomba hili ninalotaka kuamua mniachie mimi mwenyewe zaidi ya hapo mtaokota mzoga wangu,” Mage alitoa vitisho.
“Lakini Mage wanaume wameisha? Mbona kuna wavulana wazuri kuliko huyo Colin na Hans?” Brenda alimuuliza.
“Ni kweli wapo wanaume wazuri lakini si kila mbegu humea kwenye udongo wowote. Mapenzi yangu kwa Hans na Colin ni kama mtende kwenye jangwa si rahisi mti mwingine kumea sehemu ile basi ndivyo mapenzi ya Hans na Colin walikuwa kama mapacha ndani ya moyo wangu.”
“Basi ndivyo hivyo mtaka pupa hadiliki kula tamu.”
“Jamani nimewaeleza naomba mniache ni uwamuzi wangu mtu atakayeingilia uamuzi wangu ajue ndiye atakayehusika na kifo changu.”
“Mmh! Fanya mchezo utakwenda kufunga ndoa na Hans gerezani,” mama Mage alitoa taadhari kwa mwanaye aliyetaka kuingilia mapenzi ya watu.
***
Kufungwa kwa Hans kuliongeza umakini kwa Cecy kuhakikisha kila kona aliyokuwepo Colin na yeye yupo huku moyo wake ukimpa tahadhari ya yeye kuwa mbali na Colin lazima kuna kitu kitatendeka. Wazo lake lilikuwa kuachana na kazi ya kufanya maonesho ya mavazi ili kumlinda mumewe na Mage msichana aliyebakia kama genda heka ambalo linaweza kuvamia mume wa mtu bila aibu.
Baada ya kutoka gym wakati wa kurudi nyumbani Cecy alionekana mtu mwenye mawazo mengi kitu kilichomfanya apoteze mchangamfu wake wa kawaida.
“Bebi.”
“Abee, Cecy alitikia huku akichukua chupa ya juisi.
“Vipi mazoezi ya leo yamekuchosha?” alimuuliza huku akimtazama.
“Hapana kawaida tu,” Cecy alimjibu bila kumtazama.
“Mbona huna uchangamfu wako wa kawaida.”
“Kuna kitu kinaniumiza kichwa nafikiria kubadili uamuzi.”
“He! Uamuzi tena mpenzi wangu?” Colin alishtuka kidogo agongane uso kwa uso na gari lililokuwa likija kwa mbele yao lakini alijitahidi kulirudisha sehemu yake.
“Ndiyo mpenzi kuna jinamizi linataka kuivamia furaha ya moyo wangu.”
“Jinamizi gani tena mpenzi wangu?” Colin aliipaki gari pembeni ya barabara ili amsikilize vizuri mpenzi wake.
“Colin naomba unisikilize vizuri.”
“Sawa mpenzi.”
“Nimeamua kuvunja mkataba wa kwenda kufanya maonyesho nje ya nchi.”
“He! Kwa nini jamani? Si nimekubali kufunga nawe ndoa ndipo uondoke,” Colin alishtuka.
“Hukumu ya Hans imeondoa kabisa amani ya moyo wangu.”
“Kivipi mpenzi?”
“Najua nikiondoka utarudiana na Mage.”
“Siwezi...siwezi mpenzi, yule ni matapishi sitayarudisha mdomoni mwangu.”
“Hapana Colin, yule mwanamke nikiondoka lazima atatumia hila za kike kukurudisha mikononi mwako na mimi kutoka kapa. Kwa hiyo mimi siendi popote wapigie simu waeleze nimevunja mkataba yote.”
“Mpenzi utafungwa, una hela za kuwalipa ili kuvunja mkataba?”
“Kwani kazi nimeanza?”
“Hakuna kitu kama hicho, ukitaka fanya hata mwaka mmoja ndipo uvunje.”
“Basi kama hivyo tutaondoka wote kwenda huko nitakapokuwa.”
“Sawa hakuna tatizo lakini usiache kazi.”
“Hapo tutaelewana kidogo na sitaki kumuona Mage kwenu wala kukupigia simu.”
“Yote yanatekelezeka mpenzi wangu.”
Kauli ya Colin ilirudisha furaha ya Cecy na kujikuta akitabasamu na kumnywesha juisi mpenzi wake aliyekuwa amezima gari kwa mshtuko. Aliwasha gari na safari ya kurudi nyumbani iliendelea. Wakiwa njiani simuya Colin iliita Cecy aliichukua na kuangalia na kukuta haina jina alimpa Colin.
“Mpenzi pokea simu.”
“Kapiga nani?”
“Haina jina.”
“Achana naye.”
“Hapana pokea hujui nani anakupigia.”
Colin aliichukua siku na kupokea:
“Haloo.”
“Ooh! Mpenzi wa maisha yangu, za toka jana mahakamani nina imani unajua kabisa sasa ndiyo nafasi yetu ya kufunga ndoa na kuwa mke na mume.”
“We! Nani?” Colin pamoja na kujua aliyepiga simu ni Mage alijifanya hamjui aliyepiga ili Cecy asijue kitu.
“Colin mpenzi kipi kilichokufanya usahau sauti ya malkia wa moyo wako au sababu ya hicho kinyago?”
“Jitambulishe au siyo nakata simu,” Colin alijifanya kuja juu.
Cecy alishtuka majibu ya mpenzi wake lakini alitulia amalize kuzungumza ndipo amuulize.
“Ni mimi Mage mwanamke pekee uliyeshushiwa na Mungu, amini kufungwa kwa Hans Mungu ametenda ili ile ndoa yetu ya ahadi itimie.”
“Umekosea namba,” Colin alisema huku akikata simu.
“Nani?” Cecy alimuuliza.
“Kuna mtu anaonekana amekosea namba.”
“Basi unakuta mtu anapiga simu na kuanza kutoa maagizo mengi bila kujua anazungumza na nani,” Cecy alimuunga mkono mpenzi wake.
“Umeona eeh, mpenzi nawe yamekukuta?”
“Mara chache.”
“Mara nyingi watu huwa wanachanganya namba badala ya sita wanaandika tisa basi akipiga inakwenda kwa mwingine,” Colin alizidi kuficha kilichopita.
Wakiwa katika ya mazungumzo ujumbe uliingia kwenye simu ya Colin, aliichukua simu haraka kwa kuamini unatoka kwa Mage. Kabla hajafungua upande wa ujumbe Cecy alidaka na kusema:
“Nipo kwa ajili yako nitasoma na kukueleza kimeandikwa nini.”
Colin alipoangalia namba ya ujumbe ule ilikuwa iliyopigwa muda mfupi na Mage, alijikuta njia panda kumuachia simu Cecy asome ujumbe ule ambao aliamini si mzuri kusomwa naye. Lakini hakuwa na jinsi huku akiomba usiwe ujumbe mbaya ambao utamchanganya mpenzi wake na kulizua jipya pengine kukataa hata kazi yenyewe..
Cecy alichukua simu na kufungua upande wa ujumbe na kuanza kusoma, ghafla macho yalimtoka pima na mapigo ya moyo yalianza kumwenda mbio huku jasho likitanda kwenye maji la uso.
Ujumbe ulikuwa umeandikwa:
Colin wewe ndiye mpenzi wangu wa maisha, kumbuka ahadi yetu tuliyoahidiana kuwa mume na mke ipo palepale. Huu ndiyo wakati wangu hicho kinyago chako hakina nafasi mimi na wewe tunajulikana kwa wazazi wetu na mbele ya Mungu. Colin nakupenda zaidi ya kupenda, kufungwa kwa Hans Mungu ametenda ili ahadi yetu itimie. Mimi ndiye mkeo uliyechangulia na Mungu. I love you my husband to be Colin forever and ever mmmmwaaa.
Colin aliyekuwa akifuatilia uso wa Cecy alishtuka kuona macho ya Cecy yakikodolewa pima kisha kuanza kutoka machozi, alijua kimenuka, kwa mchecheto bila kujielewa kama yupo barabarani gari lilihama njia na kwenda kujingonga kwenye nguzo ya umeme na kufanya utokee mlipuko mkubwa baada ya waya za umeme kugusana.
Itaendelea

No comments