Header Ads

WAKILI WA MOYO SEHEMU: 22


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Gari alilokuwa akiendesha Colin liliendelea kuteketea na hatimaye lilishika moto lote kutokana na kukosa msaada wa kuzimwa kutokana na miundo mbinu mibovu na kuteketeza kila kilichokuwepo pamoja na simu zote za Colin na Cecy.
SASA ENDELEA...
Msichana mmoja shoga wa Brenda rafiki wa Mage ambaye alikuwa akimfahamu Colin kutokana na kuwepo siku Colin alipomvisha pete Mage. Alikuwepo kwenye ajali ile kutokana na kutemka kwenye daladala na kukuta watu wakitolewa kwenye gari lililokuwa likiwaka moto.
Kwa vile hakuijua namba ya simu ya mama Colin aliamua kumpigia simu Brenda amweleze Mage ili ampigie mama Colin kumjulisha ajali ile. Baada ya kupigiwa simu Brenda alipokea upande wa pili:
“Haloo Loveness, niambie shoga!”
“Aisee kuna tatizo,” alisema kwa sauti iliyojaa wasiwasi.
“Mbona unanitisha kuna nini?” Brenda alishtuka.
“Colin kapata ajali mbaya sana.”
“Colin! Yupi?”
“Aliyekuwa mchumba wa Mage.”
“Wewe! Ajali ya nini tena Mungu wangu?”
“Gari alililokuwa akiendesha nimepata ajali mbaya barabara ya Sam Nujoma jirani na Mlimani City kwa kugonga nguzo ya umeme.”
“Mungu wangu, vipi hali yake?”
“Mmh! Kwa kweli kuna taarifa nyingi japo si rasmi.”
“Mungu wangu nisaidie mja wako, taarifa gani tena Love?”
“Wapo wanaosema wamekufa papohapo.”
“Jamaniii! Kwani alikuwa na nani?”
“Na msichana mmoja ambaye anaonekana alikuwa na nguo za mazoezi.”
“He! Yaani nimechoka, siamini kama Colin amekufa kirahisi namna hiyo.”
“Sasa shoga nina imani Mage ana namba ya mama yake, mpigie ili awajulishe nina imani hawana taarifa.”
“Poa, lakini siamini mpaka niuone mwili wa Colin kwenye jeneza.”
Brenda akiwa amechanganyikiwa alimpigia simu Mage aliyekuwa amekaa kwao huku akichezea simu yake. Baada ya kumtumia ujumbe Colin alipiga simu ambayo iliita bila kupokelewa na mwisho ilizimwa kabisa.
Baada ya kuzimwa alijikuta akijiapiza:
“Lazima nimpate Colin kwa hiyari kwa nguvu, nitahakikisha nampoteza kinyago wake ili niipate nafasi yangu bila hiyo sina maisha heri ninywe sumu.”
Akiwa katikati ya mawazo simu yake iliita, wazo lake alijua Colin alikuwa akitafuta sehemu nzuri ili ampigie. Alipoangalia alikuta inatoka kwa shoga yake Brenda, aliipokea.
“Niambie shoga.”
“Mage kuna taarifa siyo nzuri.”
“Taarifa gani?”
“Zinamhusu zilipendwa wako.”
“Nani, Hans?”
“Hapana, Colin.”
“He! Colin kakupigia simu?”
“Siyo kunipigia simu bali kapata ajali mbaya.”
“Acha utani, acha kunirusha roho unione kama nampenda, sio siri Colin ndiye aliyebeba uhai wangu.”
“Mage hebu tuliza akili unisilize.”
“Haya niambie mpenzi.”
“Colin amepata ajali mbaya barabara ya Sam Nujoma jirani na Mlimani City na haijulikani kama mzima au amekufa.”
“Brenda sipendi utani wa kujinga, nimetoka kuzungumza na Colin hata robo saa haijapita.”
“Sasa wewe fanya utani naomba umpigie simu mama yake sasa hivi, mweleze Colin amepata ajali na amekimbizwa Muhimbili. Naomba usiongeze lingine usije muua mama wa watu kwa mshtuko. Najua anampenda sana mwanaye ndiye kama mboni ya macho yake.”
“Japo siamini nitampigia tu.”
“Fanya haraka, unaambiwa hata gari alilokuwa akiendesha limeteketea lote.”
“Mungu wangu ! Brenda unasema kweli?” Mage aliuliza kwa sauti ya kilio.
“Kweli, siwezi kukutania kwa jambo zito kama hili.”
“Mungu wangu hii nuksi gani? Kama Colin akifa nitakuwa na faida gani ya kuendelea kuishi,” Mage alizungumza peke yake huku macho yamejaa machozi na mikono kumtetemeka wakati wa kutafuta namba ya mama Colin.
Kila alivyokuwa akilitafuta machozi yalizidi kuyafunika macho yake hata alipoyafuta kwa mkono yalijaa tena. Alitoka chumbani na simu mkononi hadi sebuleni na kumkuta mama yake.
“Mage nini?” mama yake alishtuka na hali ya mwanaye.
“Colin, mama,” alisema huku akilia na kumpa simu mama yake.
“Colin! Kafanya nini?”
“Ajali.”
“He! Lini?”
“Sasa hivi.”
“Taarifa umezitoa wapi?”
“Kanipigia Brenda sasa hivi?”
“Dah! Vipi hali yake.”
“Na..na..sikia a..a..meku..”
“Wewe mtoto ushia hapohapo,” mama Mage alimkata kauli mwanaye hakutaka kulisikia neno la mwisho kwa vile aliamini litamuumiza moyo wake.
“Mama mpigie simu mama yake hana habari.”
“Mmh!”
Mama Mage alichukua simu yake kutafuta namba ya mama Colin huku naye mikono ikimtetemeka. Baada ya kuipata alipiga simu ambayo ilipokelewa upande upande wa pili.
“Haloo dada vipi?”
“Kwema, una habari gani?”
“Za nini?”
“Kuhusu Colin.”
“Mmh! Sina habari zozote.”
“Kuna taarifa kapata ajali.”
“Ajali!?” mama Colin alishtuka.
“Eeh, ndiyo, kuna mtu kampigia simu Mage na kutaka tukujulishe kwa vile hakuwa na namba yako ya simu.”
“Mungu wangu wee, yupo katika hali gani?”
“Hebu subiri,” alisema na kuziba sehemu ya kuzungumzia na kumgeukia Mage.
“Eti Mage mwili wa Colin umepelekwa hospitali gani?”
“Mama sijasema amekufa ila watu wanafikiria hivyo,” Mage alimgeuka mama yake.
“Sasa kapelekwa wapi?”
“Mama mwambie amekimbizwa muhimbili, ila usimwambie yupo kwenye hali gani mengine atayajua hukohuko mwenyewe. ” Baada ya kuzungumza na mwanaye aliachia sehemu ya kuzungumzia na kuzungumza na mama Colin.
“Anasema baada ya ajali wasamalia wema wamewapeleka Muhimbili.”
“Wanasema hali yake ipo vipi?”
“Hawajajua kwa vile amebebwa na kuingizwa kwenye gari na kuwahishwa hospitali.”
“Na..na.. Cecy?”
“Sijajua hebu subiri...Eti Cecy alikuwepo? Alimuuliza mwanaye.
“Ndiyo.”
‘Ndiyo walikuwa pamoja.”
“Na..nashukuru dada.”
“Nami nakuja huko.”
“Sawa tutakutana.”
Baada ya kukata mama Mage alinyanyuka kuelekea chumbani kuchukua funguo ya gari, baada ya kuchukua alitoka nje na Mage alitoka kumfuata mama yake waliingia kwenye gari na kutoka kuelekea Muhimbili. Muda wote Mage alikuwa akilia kitu kilichomfanya mama yake kuingilia kati.
“Unasema hajafa unalia nini mbona unamchulia mwenzio.”
“Mama inauma Colin ndiye lilikuwa tumaini langu mwisho.”
“Muombee basi apone.”
“Yaani Mungu asikie dua langu, Colin apone lakini mchumba wake afe.”
“Wee mtoto roho gani hiyo?”
“Mama wakipona wote sina changu.”
“Hebu achana na mawazo hayo,” mama Mage alisema huku kanyaga mafuta kuwahi hospitali.
Mama Colin baada ya kuzipata taarifa zile alimpitia mama Cecy aliyekuwa hana taarifa zozote kwa kujua mwanaye alikwenda mazoezi asubuhi na mpenzi wake. Naye alishtuka lakini mama Colin alimpa moyo wafike hospitali ili wajue kipi kinaendelea japokuwa hakujua watoto wao wapo kwenye hali gani.
Walijikuta wakifika pamoja na Mage na mama yake, waliongozana wote mapokezi kuulizia taarifa za wagonjwa wao. Waliambiwa wote wamekimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi kwa vile hali zao si nzuri. Walikwenda kuonana na mganga mkuu, aliwakaribisha ofisini kwake.
“Ndiyo wazazi wangu kwanza poleni sana.”
“Mmh! Hatujapoa kwani hatujui hali za watoto wetu,” alijibu mama Colin.
Dokta Bukos kwanza alitulia kama anasoma taarifa kwenye kalatasi kutafuta neno la kuwaeleza ili wasipagawe kutokana na hali za wagonjwa wao. Baada ya kutulia kwa muda alinyanyua uso wake na kusema kwa sauti ya upole.
“Wazazi wangu hali za wagonjwa si mbaya wala nzuri sana lakini bado tunapigania maisha yao.”
“Lakini baba mtu mpaka kuletwa chumba cha wagonjwa mahututi lazima hali yake ni mbaya sana?” aliuliza mama Colin.
“Ni kweli, chumba hicho ni kwa ajili ya uangalizi wa karibu kwa mgojwa.”
“Kwani hali zao zikoje?” aliuliza mama Cecy.
“Bado kwa vile wameletwa hawajitambui hivyo kwanza tunashughulika na suala la kurudisha ufahamu kisha tutajua tufanye kitu gani.”
“Mbona nilisikia wamekufa?” Mage aliropoka.
“Si kweli, kama wangekuwa wamekufa wodini tumewapeleka kufanya nini?” daktari alijibu kwa ukali kidogo.
“Wee Mage acha kuropoka,” mama yake alimkanya.
“Jamani naomba kuzungumza na wahusika wa wagonjwa wengine msubiri nje,” daktari alisema.
Mage na mama yake walitoka nje na kubakia mama Colin na Cecy, baada ya kubakia wawili dokta alitaka kujua uhusiano ya waliobakia na wagonjwa. Wote walijitambulisha.
“Basi wazazi wangu ajali waliyopata ilikuwa mbaya sana, majeraha si makubwa sana lakini inaonesha wamejigonga kwenye kitu kigumu wakati gari likipata ajali hivyo kusababisha mtikisiko wa ubongo uliopelekea kupoteza fahamu. Lakini tunahangaika ili kurudisha fahamu zao.”
Itaendelea Jumatano
Baada ya kuwapa wapenzi wangu burudani ya kutosha kwa muda mrefu, sasa hivi nitakuja kivingine hadithi zangu zitatoka katika group la Whatsapp tu kuanzia tarehe moja mwezi wa sita. Litakuwa la kulipia kiasi kidogo cha pesa ambacho mtapendekeza wenyewe kwa mwezi.
Katika group kutakuwa na kila kitu MACHOMBEZO YA NGUVU, SIMULIZI ZA KUSISIMUA. RIWAYA ZA MAPENZI, KIPELELEZI NA ZA KIJASUSI. Zitapatikana huko, mtu atakayekuwa tayari nitamuunganisha kwenye group ili tarehe moja tuanze pamoja. Pia itakuwa mwisho wangu wa kutoa riwaya au simulizi kwenye Face Book. Kujiunga kila mtu atatuma namba yake ya simu ili aunganishwe.
Pia vitabu vyangu vyote vitapatikana kupitia Application muhimu ambayo itakuwezesha kununua vitabu vya kwa gharama nafuu...kupitia application hii ambayo itapatikana katika smartphone zote zenye uwezo wa kuwa na Google Play, utatakiwa kudownload hii application (SIM GAZETI) kisha utachagua kama kununua kitabu cha hadithi au gazeti kwa bei ya shilingi 300 kila kitabu. Pia kutakuwa na vitabu vya Watunzi wote hii ni nafasi adimu kupata kitabu katika simu yako

No comments