Header Ads

Wanaolipwa 40m/-kwa mwezi mwisho Juni 30


•Katika utawala wa serikali yangu, sikubali wachache waishi kama malaika na wengi waishi kishetani. Niwahakikishieni kuanzia bunge lijalo, tutaanza kufanya kazi hiyo (ya kupungua mishahara) ili nao waishi kama shetani," alisema Rais Magufuli.
 

SIKU chache baada ya Rais John Magufuli kusisitiza dhamira ya kupunguza mishahara mikubwa ya 'vigogo' wa mashirika na taasisi za umma kutoka Sh. milioni 40 hadi kufikia si zaidi ya Sh. milioni 15 kwa mwezi, vitita hivyo vitafyekwa kuanzia Julai mosi, imeelezwa.

RAIS MAGUFULI AKIHUTUBIA WAKATI WA SIKUKUU YA WAFANYAKZI MEI MOSI MJINI DODOMA
Akiwahutubia wafanyakazi katika maadhimisho siku yao duniani, Mei mosi, mjini Dodoma Jumapili, Rais Magufuli alisisitiza kuwa atapunguza mishahara ya wakuu wa mashirikac na taasisi za wauma wanaolipwa mpaka milioni 40 ili kiasi kitakachookolewa kitumike kuwaongeza mishahara wafanyakazi wenye kima kidogo.
 

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro alisema agizo hilo litaanza kutekelezwa rasmi Julai mosi, mwaka huu.
Msimamo wa Rais Magufuli ambao ni punguzo la asilimia 63 ya mishahara hiyo, ilikuwa ni marejeo ya kauli aliyoitoa Machi 29 wakati akizungumza na wananchi katika mutano wa hadhara kwenye uwanja wa Mazaina, wilayani Chato, Mkoani Geita.
 

Magufuli alikuwa Chato alipokwenda kwa mapumziko, ikiwa ni mara ya kwanza kufika nyumbani kwao tangu aapishwe kuwa Rais wa Tano Novemba 5, mwaka jana.
 

"Katika utawala wa serikali yangu, sikubali wachache waishi kama malaika na wengi waishi kishetani. Niwahakikishieni kuanzia bunge lijalo, tutaanza kufanya kazi hiyo (ya kupungua mishahara) ili nao waishi kama shetani," alisema Rais Magufuli.
“Bahati nzuri hivi sasa tuna wasomi wengi. Yule atakayeona hawezi kuishi kwa mshahara wa Sh. milioni 15, bora aachie ngazi ili waje wengine wanaofaa.”
 

Dk. Ndumbaro alisema tayari wameanza mchakato wa kutekeleza agizo hilo kwa utaratibu maalumu.
Hata hivyo, Dk. Ndumbaro hakuwa tayari kueleza kwa kina kuhusu utaratibu waliopanga kuutumia kwa madai kuwa "muda ukifika, umma utafahamu."
“Wewe fahamu kwa sasa kuna utaratibu unafanyika wa kutekeleza agizo hilo, na kila kitu kitafahamika muda ukifika," alisema Dk. Ndumbaro. "Ila agizo hilo tumeanza kulifanyika kazi.
"Upangaji wa mishahara mipya umeshaanza na itaanza rasmi Julai Mosi mwaka huu, utaratibu wa kurekebisha mishahara hiyo unaendelea."
 

Baadhi ya taasisi na mashirika ambayo yamekuwa yakidaiwa kulipa vigogo wake mishahara ya kati ya Sh. milioni 20-40 kwa mwezi ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
 

Akizugumza katika mkutano huo wa Chato, Rais Magufuli aliahidi pia serikali yake imejiandaa kuboresha maslai ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo.
 

Wakati ahadi ya kufyeka mishahara itaanza kutekelezwa rasmi Julai mosi, Rais Magufuli alitangaza kupunguza kodi ya mishahara ya wafanyakazi (PAYE) kutoka asilimia 11 mpaka 9, katika mktano wa Jumapili.
Akiwa Chato, Rais alisema "Kiwango tunachopunguza kutoka mishahara minono ya wakubwa tutawaongezea watumishi wa chini ambao baadhi wanalipwa mishahara midogo inayoanzia Sh. 300,000."


CHANZO: NIPASHE

No comments