Header Ads

Yanga bingwa? Hilo siyo swali


Musa Mateja, Shinyanga
YANGA Bingwa? Hilo siyo swali ndivyo zilizokuwa kelele za mashabiki wa Yanga waliokuwa wakishangilia ushindi wa timu yao wa mabao 3-1 dhidi Stand United, jana jioni kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini hapa.


Kwa ushindi huo ilioupata, Yanga imefikisha pointi 68 katika mechi 27 ilizocheza, imebakisha mechi tatu tu. Stand United imebaki katika nafasi ya saba na pointi 34. Simba ina pointi 58 katika nafasi ya tatu, moja nyuma ya Azam inayoshika nafasi ya pili.
Ushindi umeifanya njia ya Yanga kuelekea kutwaa ubingwa kuwa nyepesi kwani kama Azam ikipoteza mechi yake ya leo dhidi ya JKT Ruvu itajiweka katika nafasi ngumu ya kutwaa ubingwa.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema; “Stand ni timu nzuri kwani ilicheza vizuri ila sisi tulikuwa wazuri zaidi yao, nawapongeza wenzangu kwa kujituma na kupata ushindi huu.”
Kwa upande wake nahodha wa Stand United, Jacob Massawe alisema: “Umakini ndiyo umetuponza, hatukuwa makini na Yanga wametumia nafasi hiyo kutufunga, tunajipanga kwa mechi ijayo.”
Katika mchezo huo, Yanga ilianza kwa kasi kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupata bao dakika ya pili tu mfungaji akiwa Donald Ngoma akiuwahi mpira uliopigwa na Salum Telela.
Kabla ya kufunga bao hilo, Ngoma alimtoka beki wa Stand United, Athuman David. Baada ya kuingia kwa bao hilo, Stand United walikuja juu na kutaka kusawazisha wakiwatumia viungo wao, Amri Kiemba na Seleman Kasim Selembe na straika Elias Maguri lakini hawakuweza kupata bao.
Ngoma aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 45 ikiwa ni sekunde chache kabla ya kwenda mapumzikoni akipokea pasi ya Amissi Tambwe.
Tambwe aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 63 kwa kichwa akiunganisha kona iliyopigwa na Simon Msuva. Kabla ya bao hilo, Pluijm alimtoa Telela na kumuingiza Mbuyu Twite, halafu baadaye akawatoa Kelvin Yondani (dk 66) na Ngoma (dk 76) na nafasi zao waliingia Vincent Bossou na Simon Matteo.
Stand United ilipata penalti dakika ya 81 baada ya Thabani Kamusoko kumchezea vibaya Selembe ndani ya eneo la hatari. Maguri alipiga penalti hiyo dakika ya 82 na kuifungia timu yake bao la kufutia machozi.

TAMBWE AWEKA REKODI
Tambwe amempita Amissi Kiiza kwa bao moja katika orodha ya wafungaji katika ligi kuu akifikisha mabao 20, pia ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kufikisha idadi hiyo ya mabao katika Ligi Kuu Bara.
Tambwe raia wa Burundi amevunja rekodi yake mwenyewe aliyoweka wakatia kicheza Simba ambapo aliifungia mabao 19 msimu wa 2013/14. Rekodi nyingine aliyoweka ni kufunga mabao 53 tangu alipoanza kucheza soka nchini mwaka 2013 akitokea Vital’O ya Burundi.

CHANZO: CHAMPIONI

No comments