Header Ads

A-Z MUHIMBILI KUCHANGANYA MAITI, TUKIO JIPYA LAIBUA MASWALIDAR ES SALAAM: Ikiwa imepita takriban miezi miwili tangu chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kufanya makosa ya kuruhusu miili ya marehemu kuchukuliwa na ndugu kimakosa na hivyo kuleta mtafaruku mkubwa, Risasi Mchanganyiko lina A-Z ya mkasa mpya kama huo uliotokea wiki iliyopita ambapo mwili wa mwanafunzi wa Dar es Salaam ulienda kuzikwa kama hausigeli mkoani Mtwara. Wiki iliyopita, mwanafunzi aliyekuwa kidato cha tatu Shule ya sekondari ya Ulongoni, Mamy Venancy alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, alishindwa kuzikwa, baada ya kubainika wakati wa kuuaga mwili kuwa hakuwa yeye. Maiti iliyokuwa ikiagwa nyumbani kwa marehemu Mamy huko Gongo la Mboto
jijini Dar es Salaam ilibainika kuwa ni ya msichana wa kazi aliyetajwa kwa jina moja la Teresia, mwenyeji wa Mtwara. Wakiwa wamekaa msibani kwa siku tatu kusubiri siku ya mazishi, Jumatano ya wiki iliyopita, jamaa ndugu na marafiki walikusanyika ili kumuaga mpendwa wao, tayari kwa ajili ya kumpumzisha katika nyumba yake ya milele katika Makaburi ya Pugu. Ulipofika wakati wa zoezi la kuaga, mama mzazi wa marehemu, Mwanamkuu Juma alipita na kuaga, lakini kutokana na uchungu wa msiba huo, hakuweza kukaza macho katika mwili uliokuwa ndani ya jeneza, badala yake, mdogo wa marehemu ndiye aliyegundua kuwa hakuwa ndugu yake kwa kuwa aliyelala mbele yao alikuwa ametoboa pua, wakati dada yake hakuwahi kufanya hivyo. Akisimulia mkasa mzima, mama mzazi Mwanamkuu Juma, alisema mwanaye alipatwa na ugonjwa wa kuishiwa damu ambapo alilazwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa wiki nzima lakini akafariki Jumapili na hivyo kwenda kuuhifadhi mwili mochwari. “Baada ya kufariki mimi niliondoka nyumbani nikiwa na mama yangu mdogo, ndugu wengine ndiyo walishughulikia mwili na kuupeleka
mochwari kilichojiri huko sikujua ni nini mpaka siku ya kuaga ilipofika ambayo ni Jumatano,” alisema mama huyo. “Aliyebaini kuwa yule si mwanangu Mamy ni mdogo wake ambaye alipopita alianza
kusema mama mbona huyu si dada, yeye ametoboa pua, ndiyo tukahamaki na kuuangalia mwili kweli tukabaini siyo yeye kwani hata rangi ya mwili uliokuwa kwenye jeneza ulikuwa mweusi, wakati Mamy alikuwa mweupe,” alisema. “Hatukupoteza muda, tuliurudisha Muhimbili, tulipowaeleza kuwa mwili tuliopewa si wetu, wafanyakazi wa Muhimbili wakatuambia kwa nini tusizike hivyo hivyo huku wakitaka uhakika kama kweli haukuwa mwili wa mtoto wetu. “Nikawaambia mwanangu ana kovu kubwa kwenye paja, wakafunua wakalitafuta wakalikosa, tulizungushwa hadi saa kumi jioni, wakituambia tumsubiri daktari mmoja anakuja lakini tulipoona wanataka kufunga ofisi zao tuliamua kwenda Kituo cha Polisi Msimbazi ambapo walituamuru kwenda Salenda. “Kule Salenda tukaambiwa turudi kwa wakurugenzi wa Mochwari na kama watazungushwa wapande ngazi kubwa zaidi ili
kusaidiwa. “Tulipofika Muhimbili tukakuta wanaume watatu, tukaitwa Mochwari na tukatambulishwa kuwa kumbe wale walikuwa ndugu wa Teresia, wakakiri kuwa mwili ulipelekwa Mtwara na tayari ulishazikwa Jumanne.” Mama huyo alidai wale watu walisema walimzika wakijua ni ndugu yao, kwa kuwa weupe wake walijua ni mambo ya vijana ya mkorogo. Hata hivyo, mwishowe walikubaliana kuapa mahakamani ili mwili huo urudishwe na Muhimbili ingegharamia kila kitu. Mwili ulifika Dar Alhamisi saa kumi jioni na Ijumaa ukazikwa saa nane mchana pasipo kupata msaada wowote kutoka Muhimbili. Hata hivyo, tayari uongozi wa hospitali hiyo kubwa nchini, umetangaza kuwasimamisha kazi vigogo wawili waliohusika na sakata hilo. Hii inatokea mara ya pili ndani ya miezi miwili, kwani Aprili 11, mwaka huu, hospitali hiyo iliruhusu mwili wa Janeth Bambalawe kusafirishwa kuelekea Usangi mkoani Kilimanjaro, wakiamini ni wa Amina Msangi jambo lililozua mtafaruku mkubwa baada ya ndugu halisi wa marehemu kufika na kugundua kuwa mwili waliopewa haukuwahusu.


CHANZO: GPL

No comments