Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 03


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
ILIPOISHIA:

Malaika Mweusi baada ya kumsikiliza kwa kina alimsogelea Anderson aliyekuwa ameweka mikono shavuni akionesha wazi kuwa amekosa ufumbuzi wa matatizo yaliyokuwa mbele yake.
Malaika Mweusi aliuweka mkono wake mgongoni kwa Anderson na kuongea kwa sauti yake tamu mithili ya kinubi cha mfalme Daudi, aliongea kwa sauti ya chini:
“Pole sana Anderson kweli mzigo uliokuwa mbele yako ni mzito sana unahitaji msaada mkubwa... sasa ni hivi….”
SASA ENDELEA...

Malaika Mweusi alizungumza huku akimpapasa Mr Anderson shingoni na kumfanya asisimke huku aliendelea kuzungumza:
“Ni hivi suala moja nitajaribu kulitatua lakini jingine liko nje ya uwezo wangu.”
“Lipi hilo?”
“La mkeo.”
“Utanisaidiaje?” Anderson aliuliza huku akigeuka kumtazama Malaika aliyeonesha hana wasiwasi.
“Unajua siku zote kila kitu kina nafasi yake, kazi ina nafasi yake na mkeo ana nafasi yake vilevile, kwa hiyo unaweza kupanga muda wako vizuri tu. Utashangaa kazi inakwenda na huku ukifurahia maisha yako ya nyumbani kama kawaida.
“Lazima uelewe kutokana na ugumu wa kazi yako lazima mwezi wako awe pozeo la yote yanayokuchanganya siku nzima,” Malaika alisema kwa sauti ya upole.
“Ungekuwa wewe ungefanyaje?” Anderson aliuliza akitegemea msaada wa Malaika.
“Swali zuri, ningekuwa mimi tena una nafasi ya juu wewe ndio top kuanzia asubuhi unadili na kazi za serikali lakini jioni unakuwa na mamaa ili kupoteza akili kwa ajili ya kupanga mikakati kwa kazi inayofuata.
“Ni wazi inaichosha sana akili yako huna muda kuiacha akili yako ipumzike kwa kufurahi na mkeo na mwanao, kitu kitakacho kufanya usahau matatizo ya mbele.”
“Sawa kuna matatizo yanatokea usiku unafikiri nitaacha kwenda?”
“Matukio ya usiku ni siku moja moja lakini imekithiri na kuwa kero kwenye ndoa hata mimi nisingekubali miezi miwili na nusu unanusa nyumbani na kuondoka mkeo ana haki, ni kweli kabisa unaweza kuzipunguza kazi zisizo na umuhimu.
“Haya tangu tuanze kumtafuta muuaji hata fununu yake hujaipata zaidi ya kujigeuza walinzi wa sungusungu.’’ Malaika alisema kwa utulivu tofauti na umbile na umri wake.
“Nimesikia nitajaribu.’’
“Si kujaribu anza kutekeleza sasa, mfuate mkeo ikiwezekana ukitoka hapa mweleze kama nilivyokueleza nakutakia muafaka mwema. Ila suala la kumpata muuaji hilo lipo nje ya uwezo wangu, nina imani umenielewa?”
“Nimekuelewa Malaika wangu nitatekeleza yote uliyonieleza.”
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda, Anderson na Malaika Mweusi waliongozana na kutoka nje ya Hotel ili kurudi mjini.
“Naomba nikupeleke kwako.”
“Hapana we nenda tu, mimi nina usafiri wangu nitafika sasa hivi ila mwisho wa wiki tukutane nijue umeutumiaje ushauri wangu.”
Anderson na Malaika Mweusi waliagana ilikuwa ni majira ya saa mbili usiku. Aliamua apitilize moja kwa moja hadi Sinza kwa mkewe mama Gift ili warudi nyumbani.
Alipofika alimweleza mkewe jinsi atakavyoutenga muda wake wa kazi na muda wa kukaa na familia yake kama alivyoelezwa na Malaika Mweusi. Mkewe alimjibu:
“Kama itakuwa hivyo mimi sina kipingamizi ila ukienda kinyume na haya unayonieleza basi nikiondoka tena usinifuate, sawa umenielewa?”
“Ndiyo mke wangu.”
Alimchukua mke wake na kurudi naye nyumbani Mikocheni walipokuwa wakiishi na familia yake.
****
Anderson alijitahidi kupanga muda wake wa kazi na wa kukaa na familia yake, kitu kilichorudisha upendo katika nyumba yake kama zamani. Alizidi kumuona Malaika Mweusi kiumbe cha ajabu kutokana na uwezo mkubwa wa kutatua tatizo lililokosa ufumbuzi kwa watu aliowaamini wenye busara.
Hakuamini msichana mdogo kama yeye kuwa na moyo wa busara na huruma uliojaa upendo, alipanga siku atakayokutana naye tena lazima ampe zawadi kubwa.
Alipanga zawadi gani itakayolingana na wema wake ambayo amgeiona nzuri kwake. Kumpa pesa ingekuwa utani kutokana na yule mwanamke kuonesha ana uwezo mkubwa kuliko yeye pengine mara kumi yake, aliamua kumuuliza mwenyewe anahitaji zawadi gani toka kwake.
Ilikuwa siku ya jumapili walikutana pale Puzzo Hoteli na kuongozana wote hadi Biski Hoteli. Wakiwa njiani kuna kitu kilikuwa kinagonga kwenye gari kila lilivyokuwa likienda kitu ambacho kilimkera Malaika Mweusi akabidi aulize:
“Anderson nini kinachogonga chini ya gari?”
“Aah! kuna matatizo kwenye Propela shafti.”
“Kwa nini usipeleke gereji?”
“Ugonjwa wake ni pesa nyingi kidogo na sasa sina pesa nasubiri mwisho wa mwezi.”
“Kwani kiasi gani?”
“Ni pesa nyingi kwani kuna spea mpya inatakiwa kununuliwa na matengenezo yake ni kama laki nne kasoro.”
“Sawa,” Malaika Mweusi alimjibu na kukaa kimya hadi walipofika Biski Hoteli.
Anderson kwa kuwa aliona hakukuwa na kitu kingine zaidi ya mazungumzo tu ya kawaida hakutaka kupoteza pesa kwa kuchukua chumba alionelea bora waongelee palepale kwenye gari au waende kwenye mchanga na kuzungumza.
“Kwani tatizo ni nini kama ningekuwa sina uwezo wa kulipia chumba nisingekueleza tuje huku,” Malaika alipingana naye.
“Hapana pamoja na hayo mimi naona maongezi yetu hayana haja sana ya kuongelea chumbani bora kama tungekuwa wape..,” Anderson hakumalizia.
“Nimekuelewa vizuri sana pengine labda kukushinda wewe mwenyewe lazima uwe mwelewa siku zote, ila samahani kama kauli yangu itauudhi. Wewe ni mume wa mtu sipendi kutia dosari ndoa yako ndio maana nachukua chumba ili tuongee kwa mapana zaidi.”
“Huoni kuwa ni pesa nyingi unazitumia bila sababu?”
“Pesa kazi yake ni matumizi ndio maana zinatafutwa ili zitumiwe, pesa kwangu si tatizo au ushanichoka sema tu usipindishe pindishe maneno kama safari ya nyoka?” Malaika alimuuliza akiwa amemkazia macho.
“Malaika wangu sina maana hiyo bali lazima nami nionyeshe ni jinsi gani ninavyokujali hata katika matumizi yako au hupendi ushauri wangu?” Anderson alimuuliza kwa sauti ya upole.
“Hapana, nauhitaji sana kwani umenizidi vitu vingi sikupati hata kimoja moja lakini hili halina tatizo na suala kuwa wapenzi mbona sisi ni wapenzi, siku zote hakuna urafiki bila kupendana sisi ni marafiki na pia wapenzi au mmeshazoea wapendanao wote lazima wafanye ngono?” Malaika aliuliza kwa sauti ya upole.
Anderson alikubali na kufanya waongozane wote hadi Hotelini kama kawaida Malaika Mweusi alilipia chumba.
Walipofika chumbani Malaika alitaka kujua wamefikia wapi na mkewe.
“Eeh! Lete stori, mmefikia wapi na mkeo? Ulinieleza kuwa anaitwa mama Gift eeh?”
“Ndio mama Gift.”
Anderson alimshukuru kwa ushauri wake na nasaha alizompa zilizorudisha furaha katika nyumba yake.
“Ooh, siamini kumbe nami naweza kuokoa nyumba za watu basi muda si mrefu nitafungua kituo cha ushauri nasaha,” Malaika alisema huku akionesha aibu na kumfanya achanue kama tausi bustanini na kuuongeza uzuri wake mara dufu.
“Nami nitakitangaza kila kona,” Anderson aliongezea.
Mara simu ya Anderson ikaita, naye alipokea na kuongea mara akasema:
”Hebu subiri,” Anderson alitoa pochi yake na kuchambua baadhi ya vitu fulani na kutoa business card na kuanza kumsomea mtu wa upande wa pili.
Wakati anaitoa ile business card, picha yake ya kipande ilidondoka chini ambayo Malaika Mweusi aliokota na kuangalia wakati huo Anderson alimaliza kuzungumza na simu.
Malaika mweusi alitazama ile picha na kupiga kelele ya mshituko.
“Haa! Huyu ndio mkeo?”
“Eeh, mbona umestuka baada ya kumuona una mfahamu?”
“Hapana ni mzuri sana unajua kuchagua.”
“Hakushindi wewe.”
“Ananishinda tena kwa mbali ndio maana yeye ameolewa na mimi bado nazurula.”
“Naamini ulikuwa umejificha kama ningekuona wewe nisingethubutu kuoa mwanamke mwenye kiburi kama huyu.”
“Na huyu ndiye mtoto wenu?”
“Eeh, ndio Gifti mwenyewe huyo.”
Ilikuwa ni picha ndogo ya pamoja ya familia ya Mr. Anderson yeye na familia yake.
“Sasa lini nitamuona wifi?”
“ Kwa kuwa tupo pamoja tutapanga siku ya kumuona.”
“Sawa nitafurahi kumfahamu wifi pamoja na mtoto wetu.”
Baada ya mazungumzo, kabla ya kutoka Malaika Mweusi alimuliza Anderson kuwa anahitaji kiasi gani cha pesa kwa ajili ya matengenezo ya gari lake.
“Laki nne kasoro,” Malaika Mweusi alifungua mkoba na kutoa laki nne taslimu.
“Nina imani tutakapokutana gari likuwa zima?”
“Asante sana, sijui nikushukuru vipi, sina cha kukupaa,” Teddy alizidi kumchanganya Anderson.
“Vipo vingi,” Teddy alijibu huku akitabasamu.
“Kimojawapo?”
“Ipo siku nitakwambia ni kipi.”
“Kipi mpenzi?” Anderson alitaka kujua.
“Ooh! Mbona umefika mbali, wewe ni mume wa mtu, naheshimu ndoa yako sitaki ndoa yako ivunjike, tutaendelea kuwa marafiki tu na usidhani kutaka msaada kwako ni kutaka penzi kwako la hasha bali moyo wangu umekutunuku hilo wazo litoe mawazoni,” Teddy alimkatisha tamaa Anderson.
“Sasa ni lini utaniambia kitu hicho?”
“Nilishakwambia nitakujulisha lini tena kitu hicho hakina gharama.”
“Sawa ngoja nisubiri ingawa umeniachia fumbo zito.”
“Tena imekuwa vizuri nimekumbuka kuanzia kesho nitakuwa na safari ambayo itaniweka mbali kwa wiki mbili nitakaporudi nitakujulisha.”
“Sawa japo sipendi kujua unaenda wapi.”
“Nami natarajia kukuta ndoa yako inashamiri, sitaki kusikia mkeo amerudi nyumbani kwao.”
“Sidhani, wewe nenda salama Mungu akijali tutaonana sio siri umeshaniambukiza ugonjwa wa mazoea moyo wangu huwa taabani nisipokuona hata sijui kwa nini?”
“Umenishiba, hata mimi mgonjwa juu yako ungekuwa ujaoa sijui….” Hakumaliza na kujikuta walicheka kwa pamoja huku wakigonganishiana mikono. Waliagana na kama ilivyokuwa kawaida kwa kutangulia Anderson na kumuacha Malaika Mweusi.
******
Siku ya pili tangu walipoagana na rafiki yake wa karibu aliyemteka mawazo yake Malaika Mweusi, msichana mwenye fumbo la ajabu kwake. Anderson baada ya shughuli zake za kawaida za wiki nzima aliamua kutoka na familia yake kwenye ufukwe mwanana wa Biski Beach ili kupumzisha misukosuko ya wiki nzima ya kumtafuta muuajia ambaye kwa wiki mbili alikuwa ametulia na kuacha swali kwake safari ile angefanya mauaji wapi au kamaliza kampeni yake.
Akiwa na familia yake mkewe na mtoto wake Gift walijiandaa kutoka majira ya saa sita alasiri, wakati huo mkewe alikuwa akijipodoa kwenye meza ya kujipodoa. Mara simu yake iliita na alipoziangalia namba zilikuwa ngeni kwake alijiuliza kabla ya kupokea ni nani, wasiwasi wake huenda mambo yameharibika.
Kilichomshangaza namba zote zinazopigwa katika simu yake hutoa jina, namba ile wanaoijua ni wachache na majina yao yamo kwenye simu.
Alijiuliza sijui anatakuwa ni nani na anataka nini tena katika muda ambao anahitaji kupumzika na familia yake, aliamua kupokea kwa ukali kidogo akihoji:
“Haloo, nani? Na unataka nini?” aliuliza kwa ukali kidogo.
“Samahani wewe ni Mr Anderson?” sauti ya kike iliuliza.
“Wewe ni nani?” hakumjibu alimuuliza swali.
“Kabla ujajua mimi ni nani kwanza nijue wewe ni Mr, Anderson?”
“Hii namba kakupa nani?” Anderson hakujibu zaidi ya kuongeza swali lingine.
“Mzee huu muda si wakulizana maswali mengi kuchelewa kwako ni kuendelea kuharibu mambo,” kauli ilimtaadhalisha.
“Una maana gani kusema hivyo?” alishtuka kidogo.
“Mimi ni msamalia mwema si lazima ujue ni nani aliyenipa namba yako, ukija katika eneo la tukio tutaelewana vizuri,” kauli ya upande wa pili ilizungumza kwa taratibu na kujiamini.
“Tukio! Tukio gani tena hilo?” moyo ulimpasuka kwa kujua mambo yameiva.
“Mzee, kuna vijana watatu wameingia katika moja ya ofisi tumewatilia mashaka huenda ndio wauaji wenyewe wanaofanya mauaji jijini.”
“Ooh! Ni eneo gani hilo?”
“Ni maeneo ya Jengo la Ushirika, Mnazi Mmoja pembeni kuna jengo moja lenye ghorofa mbili. Wameingia humo ndani fanyeni haraka mkichelewa tu mtakuta watu wameuawa.”
“Ooh! Ishakuwa tabu, sasa hii ni kazi gani isiyokuwa na mapumziko?” Anderson alizungumza peke kwa sauti.
“Vipi tena mume wangu ?” mama Gift aliuliza.
“Kuna tukio limetokea mnazi mmoja karibu na jengo la ushirika. “
“Sasa ndio itakuwaje?”
“Hakuna kitakachoharibika nyie jiandaeni kama kawaida ngoja niwajulishe vijana wangu waende katika tukio ili tuedelee na safari yetu.”
Anderson aliwajulisha vijana wake kuwa wakutane katika eneo la Mnazi Mmoja kwenye jengo lililo pembeni na Ushirika tayari kulivamia. Alimwacha mkewe akiwa analalama hakusikiliza lawama za mkewe aliingia kwenye gari na safari ya kuelekea Mnazi mmoja ilianza.
Alikwenda kwa mwendo wa kasi ya kuruka alitumia dakika kumi na mbili kufika katika eneo la tukio na kuwakuta vijana wake wakiwa tayari wameshafika mara moja walilitafuta jengo lililoelezwa limevamiwa.
Hali katika eneo la Mnazi Mmoja ilikuwa shwali hakukuwa na dalili yoyote ya kuwepo tukio lolote la hatari. Ilibidi wawahoji baadhi ya watu waliokuwepo kwenye eneo lile lakini kila mmoja habari ile ilikuwa mpya kwake. Walijaribu kuzunguka katika eneo lote bila kuona dalili zozote za hatari.
“Bosi hebu mpigie basi huyo mtu atuelekeze vizuri.”
Alipojaribu kupiga namba ilikuwa haipatikani.
Anderson aliwachagua vijana wake zaidi ya watano waendelee kulinda katika eneo lile na yeye alirudi nyumbani kumwahi mkewe ambaye alijua lazima safari yenyewe ataisusa.
Ilikuwa imepita saa moja tangu aondoke nyumbani kwake kwenda kwenye tukio aliendesha gari kwa mwendo wa kasi ili kumuwahi mkewe alijua akifika tu hata ndani haiingii zaidi ya kumpigia honi na kuondoka.
Alifika nyumbani kwake majira saa kumi na robo hakuwa na haja ya kuingia ndani alipofika tu alipiga honi ili mkewe atoke na kuondoka. Alipiga honi zaidi ya mara kumi lakini mkewe hakutoka alijua amesusa ilibidi ateremke garini amfuate ndani, sio siri tabia mkewe zilimchosha, jambo ndogo lazima asuse na kuwa kubwa hata kama lina umuhimu.
Aliteremka kwenda ndani, mlango wa sebuleni ulikuwa umeegeshwa aliusukuma kuingia moja kwa moja ndani huku akimuita mkewe.
“Sweet ... Ma Sweet heart, Mama Gifti upo wapi mpenzi au ndio umesusa? Njoo mpenzi nimerudi mumeo sijachelewa najua umeshajiandaa twende basi mpenzi au umerudi ndani kulala?”
Sebuleni hapakuwepo mtu alijua wapo chumbani alikwenda moja kwa moja hadi chumbani, mlango wa chumbani nao ulikuwa umesindikwa aliusukuma na kuingia ndani. Picha aliyoiona machoni mwake hakutarajia kuiona maishani mwake mpaka anakufa. Alijiuliza yupo ndotoni au wapi, alijikuta akisema kwa sauti ya juu:
“Hapana…hapana...haiwezekani,” alisema huku akishika mikono kichwani. Kilichokuwa mbele yake kilikuwa ni kweli, mwili wa mke wake ulikuwa umelazwa kitandani ukiwa mtupu kama alivyozaliwa akiwa ameuawa kifo cha kinyama.
Kilikuwa kifo cha kinyama na cha ukatili wa hali ya juu alikuwa amelazwa chali mwili wote ukiwa umechanwachanwa na matumbo yote yakiwa yapo nje, sehemu za siri zikiwa zimeharibiwa vibaya zilikuwa zimechanwachanwa na sehemu za siri zilikuwa zimewekwa kipande cha mti.
Kilikuwa ni kifo cha unyama wa hali ya juu na pembeni yake alikuwa mwanae Gifti akiwa amelalia kifuani kwa mama yake naye alikuwa ameuwawa pia. Ilionyesha kuwa Gifti alikufa kwa kunyongwa kwa kamba au mshipi kwani alikuwa hana jeraha lolote mwilini Anderson alijikuta nguvu zikimwishia na kujibweteka chini pwaaa! Huku nguvu zikimuishia kabisa.
Alilia kama mtoto mdogo akiwalilia mke na mtoto wake Gitfi, lakini alijikuta akijisemea ni upumbavu kulia kama mwanamke kwani adui anaweza kuwa yumo humo ndani na anaweza kunimaliza kirahisi.
Alijikaza kiume na alichukua bastola yake mkononi, alinyanyuka kutoka pale chini alipokuwa amejibweteka na kuanza kuanza kumsaka mbaya wake kwa taadhari kubwa. Alizunguka kila kona bila kumuona mtu yeyote aliamua kurudi ndani kuifadhi miili ya marehemu mkewe na mtoto wake Gifti zilizokuwa zimejitandaza katika kitanda kizima huku akiwa ametapakaa damu nyingi na kuchuruzika kwenye sakafu.
Aliunyanyua mwili wa mtoto wake Gifti na kuulaza pembeni ya mama yake huku mwili wake ukimtetemeka na jasho likimvuja kama maji mwili mzima. Aliuchunguza mwili wa mtoto wake na kugundua kuwa ulikuwa na jeraha shingoni likionesha kuwa amenyongwa na mshipi.
Aliuchukua mwili wa mkewe na kuufunika vizuri alinyanyua simu na kuwajulisha vijana wake yaliyomsibu. Vijana wake waliwasili haraka kumpa msaada bosi wao, miili ya marehemu wote ilipeleka Hospitali ya taifa ya Muhimbili na vijana wengine walifanya usafi sehemu zote zenye damu.
Anderson alionyesha kuwa mtu mwenye mawazo mengi juu ya tukio lile zito la kutisha. Alijawa na mawazo juu ya mbinu za hali ya juu wanazotumia wauaji, ikiwemo kumuondoa nyumbani na kupata nafasi ya kuitelekeza familia yake.
Alijikuta akijiuliza muuaji ni nani na kwanini ameamua kuua familia yake au ni kwa sababu ameanza uzijua nyendo zake. Amefanya vile ili umtisha. Lakini alijiapiza kwa hali yoyote ile atahakikisha anamtia mikononi, iwe isiwe. Aliweka nadhiri kumsaka muuaji hadi tone la mwisho la damu yake.

No comments