Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 04


 
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

ILIPOISHIA:
Alijikuta akijiuliza muuaji ni nani na kwanini ameamua kuua familia yake au ni kwa sababu ameanza uzijua nyendo zake. Amefanya vile ili umtisha. Lakini alijiapiza kwa hali yoyote ile atahakikisha anamtia mikononi, iwe isiwe. Aliweka nadhiri kumsaka muuaji hadi tone la mwisho la damu yake.
SASA ENDELEA...
****
Mazishi ya mkewe na mtoto wa mkuu wa upelelezi Anderson yalifanyika kwa heshima zote. Kabla ya maziko wakati wa kuaga miili ya marehemu Anderson alimuahidi mkewe kwa sauti kubwa mbele ya kadamnasi:
“Ewe mke wangu na mwanangu mpenzi nendeni mkiwa mmeniachia jeraha kubwa moyoni mwangu nakuahidi damu yenu aitapotea bure. Nakuhakikishia muuaji nitamtia mkononi na kulipiza mara dufu kwa hili alilowafanyia. Eeh! Mungu wapokee na uwape makazi mazuri ili siku moja tukutane
“Ooh! Maskini ni nini nilichomkosea huyu muuaji mpaka afanye unyama wa kikatili namna hii. Eeeh! Mke wangu….Ooh! Mwanangu kipenzi Gifti, zawadi nilizopewa na Mungu baba leo inapotea kama kibatari kilichozimika kwenye upepo mkali.”
Anderson nguvu zilimwisha na kujitupa juu ya majeneza na mke wake na mtoto wake. Alilia kama mtoto mdogo kila alipofikilia kifo cha mkewe alikuwa anajiuliza kama muuaji ameona ameanza kugundua mbinu zake. Kwa nini awaue mkewe na mtoto wake ni bora angemuua yeye mwenyewe kuliko unyama alioufanya.
Kuua familia yake anakuwa hajafanya kitu chochote kwani ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto si kuuzima bali ni kuzidisha moto uwake kwa nguvu.
***

Wiki moja baada ya kifo cha mkewe na mtoto wake akiwa ofisini alikuwa ni mwingi wa mawazo kuhusu mbinu za muuaji. Alifikiria ujumbe ambao hupenda kuwaachia wauaji. Maneno ambayo hupenda kuyatumia ni ‘Mtetezi wa Haki za Binaadamu, Mshahara wa Dhambi ni Mauti, Hukumu baada ya Hukumu, na alioachiwa kwa mkewe kuwa ALINIMULIKA MIMI NIMEMCHOMA.
Alijuliza haya maneno yana maana gani ni wazi inaonyesha si muda mrefu muuaji atamtia mikononi kitendo cha muuaji cha kuteketeza familia yake ni dalili za mfa maji ambaye ameanza kutapatapa.
Akiwa bado kwenye lindi la mawazo simu yake ililia, alichukua juu ya meza aliziangalia zile namba kwa makini kwani zilikuwa ni ngeni kwake namba zile zilimfanya aingiwe na hofu ilikuwa ni sawa na kutonesha kidonda kilichoanza kupona.
Simu kama ile wiki iliyopita ilipoteza familia yake, alipandisha pumzi juu na kuzishusha ili kujipa ujasiri na baadaye alibonyeza kitufe cha kupokea na kuongea kwa ukali:
“Haloo nani mwenzangu?”
“Aah! Anderson mbona kila wakati unakuwa mkali hivi hata wifi anapata nafasi ya kucheka na wewe?” Ilikuwa ni sauti tamu ya kinubi cha mtume Daudi ya rafiki wake wa karibu Malaika Mweusi ambaye walipotezana kwa takribani wiki mbili kwa kuwa alikuwa safari nje ya nchi.
“Aaah! Samahani Malaika wangu umerudi lini?”
“Leo hii nina hamu kubwa ya kukuona rafiki yangu mpenzi nina imani wifi hajambo na mtoto wenu kipenzi Gift pia, nina matumaini ndoa yenu inashamiri na kuleta furaha isiyo na kifani.”
Kauli ile iliuchoma moyo wa Anderson ilikuwa ni kama kutonesha donda lililokwishaanza kupona. Jibu lilikuwa zito sana kutoka mdomoni kwake, kitu kilichomshtua Malaika Mweusi upande wa pili.
“Vipi mbona kimya nasikia ukivuta pumzi na kuzishusha au hupendi kuonana na mimi, basi samahani,” Malaika Mweusi alikata simu Anderson alikurupuka kama anatoka usingizini.
“No..no..hapana Malaika wangu sikuwa na maana hiyo wakati huo simu ilikuwa imekatwa. Kwa haraka alimpigia simu Malaika Mweusi aliipokea upande wa pili.
“Eeh! Unasemaje?”
“Samahani Malaika wangu sina maana uifikiriayo.”
“Kufikiria nini Anderson?”
”Kuwa labda sipendi kuonana na wewe Malaika, ni mambo mazito yamenipata sina msaada wowote nina imani wewe ndiye tegemeo langu la pekee. Kwanza nina shukuru kukutana nawe nipo chini ya miguu yako Malaika wangu, ni mtu wa pekee duniani unayeweza angalau kwa asilimia tano kunipa faraja maana najiona nipo katikati ya dunia na mbingu,” Andarson alibembeleza.
“Anderson mbona unanitisha una nini?” Malaika alishtuka.
“Ni mengi ya kuzungumza na wewe tukikutana, nahitaji msaada wako mkubwa kwa muda huu.”
“Sawa basi tukutane palepale pa siku zote muda uleule tafadhali jali wakati, usijali kila kitu nitalipia mimi.”
“Sawa Malaika wangu usiache kuja nakutegemea kuliko kitu chochote duniani kwa sasa.”
“Sawa Anderson lazima nifike usihofu nipo kwa ajili yako,” Malaika alimtoa hofu.
“Nitafurahi kama utafika.”’
“Usihofu nisubiri au nitawahi ili kukuonyesha jinsi ninavyokujali.”
Kwa vile muda ulikuwa umeisha Anderson alitoka ofisini na kurudi nyumbani tayari kwa kujiandaa kukutana na Malaika Mweusi. Baada ya kujiandaa aliingia garini na kuelekea Biski hoteli, aliwasili robo saa kabla ya muda waliopangaa kukutana, alitafuta eneo zuri na kuegesha gari lake aliteremka na kuhakikisha gari lake lipo kwenye usalama alielekea hotelini.
Akiwa anaelekea mapokezi alishtukia anashikwa bega alipogeuka alikutana na harufu kali ya manukato apendayo ujipulizia Malaika Mweusi alipogeuza shingo alilakiwa na tabasamu lililonakshiwa na meno madogo meupe yenye mwanya mwembamba.
“Ooh! Vizuri, kumbe tumewahi pamoja karibu sana,” ilikuwa ni sauti tamu ya Malaika Mweusi.
“Jambo nililonalo ni zito hivyo linatakiwa umakini na kujali muda,” Aderson alisema akielekea mapokezi.
“Asante, twende zetu moja kwa moja nimeshalipia mapema na ufunguo ninao.”
Waliongozana moja kwa moja hadi kwenye chumba ambacho Malaika alikuwa amelipia.
Sura ya Anderson ilikuwa imezongwa na lindi la mawazo yaliyokosa ufumbuzi. Kama kawaida Malaika Mweusi alifikia kitandani na Anderson alikaa kwenye kochi.
Kabla hawajaanza chochote kilichowapelekea pale chumbani, mara mlango ulipogongwa, alikuwa ni mhudumu alileta vinywaji na Malaika alivipokea na kufunga mlango kwa ndani.
Aliruhdi hadi kochini akiwa na glasi mbili za vinywaji na kukaa pembeni ya Anderson.
“Karibu,” alimkabidhi glasi moja.
“Asante,” alijibu huku akiipokea na kugongesha glasi kutakiana afya njema.
Baada ya kimya kifupi Malaika kwa sauti ya upole aliuvunja ukimya ule.
“Ndiyo Mr. Anderson nipo hapa kwa ajili yako, nipo tayari kukusaidia kwa kadri ya uwezo wangu,” maneno ya Malaika yalimpa faraja Anderson.
Kwa ujasili mkubwa alianza kumhadithia kuanzia mwanzo hadi mwisho yaliyomsibu wiki moja iliyopita. Simulizi lile lilimshtua sana Malaika Mweusi na kuangua kilio kilichomshtua hata Anderson.
“Malaika mbona unanivunja nguvu? Wakati wewe ndiye niliyekutegemea unaonyesha udhaifu sasa unafikiri nani atanisaidia?”
“Anderson inauma ni unyama wa aina gani huo, mkeo amekosa nini mpaka apewe adhabu kubwa namna hiyo, inauma…inauma….mtoto Gift amekosa nini? Mtu kama huyu si wa kuhurumiwa hata kidogo,” wakati huo Malaika Mweusi alikuwa analia akiwa kajitupa chini.
Ilibidi Anderson afanye kazi ya ziada kumbembeleza:
“Malaika wangu wewe ndiye niliyekuwa nakutegemea, unalia hivyo nani atakaye nisaidia?”
“Inauma sana wacha nilie nikamue uchungu uliopo moyoni mwangu ili niweze kujua nini nitakachokusudia,” baada ya kimya ndipo Malaika Mweusi alipoanza kusema:
“Ni kweli inaniuma sana lakini cha kufanya kwanza kabisa kabla ya yote nakuahidi nitashirikiana na wewe katika kipindi chote cha majonzi nitakuliwaza na kukufariji,” Malaika alisema huku akinyanyuka alipokuwa amekaa.
“Hilo nashukuru sana, je, la huyu muuaji utanisaidia vipi?”
“Sipendi kukudanganya suala la polisi mimi sijui chochote lakini kuna umuhimu wa kuwatumia hata Interpool (polisi wa kimataifa) nina imani ninyi kazi iliyopo mbele yenu naona imewazidi na siku zinakatika na mauaji yanaongezeka kila kukicha. Ni vizuri kusema umeshindwa ili upate msaada.”
Malaika alitumia muda mwingi kuongea na Anderson baada ya kikao chao kilichowarudisha katika fikira nyingine ambazo ndizo zingekuwa suluhu ya matatizo ya Anderson.
Hata hivyo kila mmoja alikuwa na fikra tofauti ndani ya moyo wake kutokana na ukaribu wao waliokuwanao. Anderson hisia zake zilikuwa katika mapenzi yaani wako bibi na bwana.
Alijikuta akiongeza mapenzi kwa Malaika Mweusi na kumwona ndiye mwanamke anayefaa kuziba pengo la mkewe, kwani alionekana kuwa msichana aliyesimama kidete kumliwaza muda wote wa matatizo.
Kilichomshangaza ni tofauti ya mawazo yake, alihisi labda pamoja na kupenda lakini Malaika Mweusi alishindwa kumweleza kwa sababu alikuwa akijua kwamba yeye ni mume wa mtu.
Lakini alijua huo ndio ulikuwa muda mzuri wa Malaika Mweusi kulionyesha penzi kwake. Hata hivyo aliishia kuona penzi la kirafiki kama la dada na kaka.
***
Siku zote Anderson alipokuwa na Malaika Mweusi hasa sehemu za faghara, mikao na nguo alizovaa zilimfanya awe na matumaini kuwa Malaika Mweusi anamwonyesha alivyojirahisi kwake. Siku zilikatika bila mabadiliko yoyote katika uhusiano wao.

MIEZI 6 BAADA YA VIFO VYA FAMILIA YA ANDERSON.
Siku moja wakiwa faragha Mr Anderson hakuamini masikio katika mazungumzo yake na Malaika Mweusi.
“ Anderson,” Malaika Mweusi alimwita akiwa amemchanulia tabasamu pana.
“Unasemaje Malaika wangu?”
“Utakaa hivi hadi lini?”
“Una maana gani?”
“Lazima uoe ili kuondoa mawazo ya matatizo yaliyonikuta, lazima uwe na mwenza ambaye atafungua ukurasa mpya.”
Anderson alijua sasa wazo lake la kumpenda Malaika Mweusi limepata jibu.
“Ni kweli kabisa Malaika wangu, sijui utanisaidiaje?”
“Tafuta mwanamke ili ufungue ukurasa mpya yaliyopita yamepita , imebaki historia.” Malaika alisema huku akimuangalia kwa jicho la huruma.
“Ni kweli Malaika wangu, na nina imani wewe unajua nani ni chaguo langu.”
“Ni vigumu, mimi si mnajimu wala hujawahi kunidokeza nani anaweza kuwa chaguo lako baada ya kifo cha kipenzi chako mama Gift.”
“Wamjua wazi ila hutaki kumweka bayana na…”
“Ni kweli simjui, hebu nifumbue macho nami nimjue wifi yangu atakayeziba pengo la wifi yangu mama Gift.”
“Ni kweli humjui?” Anderson alimuuliza akiwa amemkazia macho.
“Simjui, kwa nini nikukatalie?”
Anderson mdomo ulikuwa mzito kumtamka huyo mwenza mtarajiwa, Malaika Mweusi alipoona amepata kigiugumizi alimuliza.
“Vipi Anderson mbona umekuwa bubu ghafla?”
“Hapana, basi kesho tukikutana utamjua vizuri hata nikikueleza utashangaa.”
“Anderson… nikueleze mara ngapi kuwa mtu huyo simjui au kuna mtu ulimuonyesha ukafikiri kuwa ni mimi? Katu sijui.”
“Utamjua tu,” Mr Anderson alimtoa wasiwasi.
“Ni vizuri na mimi nimjue wifi yangu mtarajiwa ili nikupe maksi, lakini nakuamini mjuzi wa kuchagua wasichana warembo. Ina maana huna hata picha yake?” swali lile lilizidi kumchangaya sana Anderson roho ilimwambia kwani nini asimweleze ukweli kuliko kuyaficha maumivu yake.
Alipandisha pumzi na kuzishusha kitu kilichomfanya Malaika Mweusi amwangalie usoni na kupandisha macho yake kwenye uso wa Anderson ambaye alipopeleka macho yake kwenye uso wa Malaika yalikutana na kuona aibu. Ilibidi aangalie pembeni Malaika Mweusi alimsogelea karibu na umshika bega.
“Una nini, mbona umebadilika?”
“Aah! Wacha tu,” alipoteza ujasili wa kiume.
“Hapana nipo hapa kwa ajili yako kwa hiyo usihofu nieleze tu nipo tayari kukusaidia kwa vile wewe ni mtu muhimu sana maishani mwangu.”
“U…naaa…jua,” bado Mr Anderson alipata kigugumizi
“Simjui ndio maana nataka unieleze nimjue wifi yangu.”
“Kweli unanipenda?” aliuliza swali badala ya kujibu swali.
“Hilo si swali bali upendo wangu kwako upo wazi hauhitaji maswali,” Malaika alijibu kwa sauti tamu huku akimuangalia kwa jicho la huruma.
“Upo tayari kunisikiliza?”
“Nimekusikiliza mara ngapi hadi hili linishinde kusikiliza.”
“Malaika wangu,” Anderson alimwita kwa sauti ya upole.
“Unasemaje?”
“Nakupenda sana Malaika wangu.”
“Hata mimi naelewa ndio maana nipo pamoja nawe baada ya kuelewa ulivyo na umuhimu kwenye maisha yangu.”
“Sasa mbona unielewi?” aliongea kwa sauti nyonge sana.
“Kwa lipi?”
“Kuhusu upendo wa dhati juu yako, unafikiri ni nani atakayeziba pengo la mke wangu mama Gift kwa asilimia mia kama si wewe!”
Malaika Mweusi alivyosikia vile alishituka na kuuliza kama kwamba hajasikia.
“Eti unasemaje?”
“Ni kweli kabisa kuwa wewe ndiye chaguo langu sina mwingine zaidi ya hapo sitaoa tena mwingine maishani mwangu.”
“Mmh! Mbona unanipa mtihani mkubwa nisio uweza kujibu.”
“Mtihani gani huo, kwani umeolewa?”
“Hapana.”
“Una mchumba?”
“Hapana.”
“Rafiki wa kiume?”
“Sina.”
“Sasa Malaika wangu ugumu upo wapi?”
“Sikiliza Anderson chaguo lako lilikuwa zuri ambalo hata mimi ningeweza kulipokeakwa mikono miwili lakini…”
“Lakini nini tena Malaika wangu, elewa moyo wangu wote umeubeba wewe.”
“Anderson aliyoyasema ni sawa lakini kuna vitu vinanipa ugumu wa mimi kuwa mkeo.”
“Vitu gani?”
“Unaelewa vizuri kuwa uhusiano wetu umeanza muda mrefu kabla ya kifo cha mkeo.”
“Hilo naelewa sasa tatizo ni nini?”
“Kama ulivyonieleza kifo cha mkeo kilivyokuwa.”
“Naelewa lakini mbona unapindisha si useme kipingamizi kingine lakini nina imani hakuna kipingamizi ni wazi ulikuwa hunipendi bali unanidanganya tu, nafikiri hiki ndicho kipindi cha kudhihirisha mapenzi yetu bayana.”
“Unajua Anderson unaongea tu bila ya kufikiri unachokisema kimesimama upande gani.”
“Una maana gani?”
“Mimi kama nitaolewa na wewe watu watafikiri mambo mengi kuhusu kifo mkeo labda tumemuua ili tuishi pamoja.”
“Hivi nani duniani aliyewahi kuzuia mwanadamu asizunguze anayotaka kusema. Ukisikiliza maneno ya watu unachelewa maendeleo, kwanza nani anajua uhusiano wetu?”
“Ina maana katika dunia hii tupo wawili tu?”
“Hapana ila sidhani kama watafikiri hivyo, huo ni wasiwasi wako tu japo waswahili wanasema jino la pembe si dawa ya pengo lakini kwangu wewe si jino la pembe ni jino jipya linaloota na kuziba pengo.”
“Usemavyo sikatai lakini tatizo jingine huoni kama utanioa utakuwa umeniingiza kwenye matatizo?”
“Matatizo gani tena?”
“Nina imani bado muuaji atataka kuiteketeza familia yako, huoni kuwa uhai wangu utakuwa umeuweka sokoni?”
“Nakuhakikishia kuwa kosa nililofanya awali sitarudi tena nitakulinda kama mboni ya jicho langu sidhani kama muuaji atanisogelea tena.”
“Mmh! Sawa.”
“Sawa nini, mbona uniweki sawa?”
“Nimekubali.”
“Aah! Siamini…Siamini Malaika wangu, nimeamini kuwa wewe si mtu wa kawaida bali Malaika uliyeubwa kwa ajili yangu ili kunipa faraja,” Anderson alimkumbatia Malaika Mweusi na kumbeba juu juu hadi kitandani.
Alimuomba Malaika Mweusi siku ileile wakalale nyumbani kwake.
“Hapana mpenzi sina budi kulitamka neno mpenzi kutoka uvunguni mwa moyo wangu,” Malaika alisema kwa sauti ya kinanda.
“Kwa nini honey tusiende nyumbani kwako ili ukapazoee kabla ya harusi?”
“Ni haraka sana, lakini nimeshakukabidhi moyo wangu hivyo siku zote mambo mazuri hayataki haraka.”
“Hapana lazima niwe na haraka mimi kwako kama msafiri aliye jangwani aliyedondosha chupa ya maji na kuteswa na kiu kwa kipindi kirefu bila matumaini ya kupata maji. Ghafla anakiona kisima chenye maji sidhani kama atasubiri.”
“Maneno yako yana ukweli wa asilimia mia, lakini siku zote subira waswahili wanasema ni dhahabu.”
“Sawa nimekubali, basi wiki endi hii nitakupeleka kwa wazazi wangu nina imani ndio siku itakayokuwa maalum wa sherehe fupi ya kuvishana pete ya uchumba na mipango ya ndoa ianze mara moja.”
“Nina furaha sana tena sana kufahamiana na familia yako.”
Ilikuwa ni siku ya furaha kwa watu wawili Anderson pale alipopata tulizo la moyo wake lililokuwa likimpa kimuhemuhe usiku na mchana. Naye Malaika Mweusi alikuwa na furaha kubwa kumpata yule aliyemuota usiku na mchana kuwa siku moja atakuwa mumewe wa ndoa.
***
Ilikuwa ni siku maalum iliyoandaliwa kwa vitu viwili muhimu kwa wakati mmoja, moja kutambulishwa kwa Malaika Mweusi kwa wazazi wa Anderson pili kuvishwa pete ya uchumba. Malaika Mweusi alimpitia Mr Anderson kwake akiwa kwenye gari lake la kifahari aina ya Range Rover Vogue sport ya rangi nyeusi.
Hakuwa yule Malaika Mweusi aliyependa kuvaa mavazi yanayomweka nusu uchi na mapambo ya gharama, la hasha huyu alikuwa mwingine kabisa.
Alikuwa amevalia vazi refu la kitenge cha rangi ya njano na nyeusi kilichoshonwa kwa ustadi mkubwa na kilemba chake na mkoba wa ngozi ya pundamilia, hakika alipendeza sana. Ukimwangalia harakaharaka ungesema ameteremka kutoka Lagos Nigeria au DR Congo.
Vazi alilolivaa hupendelewa kuvaliwa na wanawake matajiri nchini Nigeria au wafanya biashara wa Kikongomani. Chini alivaa viatu virefu vya ngozi ya pundamilia vilivyofanana na rangi ya mkoba wake. Shingoni alivaa mkufu mpana wa dhahabu. Hakuvaa mingi kama kawaida yake na mkononi hakuvaa bangili ya dhahabu aliivaa saa yake ndogo ya dhahabu.
Hakika Malaika Mweusi alipendeza sana machoni mwa mtu yeyote alionekana msichana mrembo mwenye heshima anayefaa kupelekwa kwa wakwe. Anderson alipomwona Malaika Mweusi alichanganyikiwa kwani kila siku alimuona mwanamke mpya.
“Malaika Mweusi! Hakika mwenyezi Mungu lazima nimpe shukrani zangu kwa kumuumba mrembo asiye na mapungufu yeyote ya sura, umbo na hata tabia hongera sana umependeza,” Anderson alimsifia akiwa amechanganyikiwa na urembo wake.
“Asante kwa kunisifia lakini sikushindi wewe ulivyopendeza kwenye suti nzito, hali hii tunaenda kutambulishana je, itakuwaje siku ya harusi yetu, Anderson mpenzi na mimi sina budi kumshukuru mwenyezi Mungu kunichagulia mume bora, unajua nilichokupendea?”
“Sijui Malaika wangu hebu niondoe tongotongo zililotanda kwenye ubongo wangu.”
“Si tupo pamoja habari hizi zinataka kituo kwa vile tuna safari ambayo tunasubiriwa kwa hamu kubwa kama ulivyonieleza huu si wakati wake fanya twende tuwahi tusije onekana kama tuna ahadi za ubabaishaji na kuwafanya wazazi wako kupunguza maksi.”
“Sawa mpenzi wacha tuwahi japokuwa unaniweka roho juu kama kiuno cha mnazi juu sipo na chini pia sipo nipo katikati.”
“Ushaanza, tangu lini mnazi ukawa na kiuno? Ninyi ndio mnaosema eti nyoka ana kiuno.”
Walicheka kwa pamoja na kuingiaa ndani ya gari la Malaika Mweusi alikuwa anaendesha mwenyewe kuelekea nyumbani kwa wazazi wa Anderson. Walipofika walipokewa kwa shangwe na vifijo walifika sebuleni ambako palikuwa pamepambwa kwa maua ilionyesha kuwa ni siku maalum iliyoandaliwa kwa shughuli maalum.
Sebuleni kulikuwa na wageni wasiopungua kumi na mbili ila wazazi wa Anderson walikuwa ndani baada ya mgeni kufika na kutulia ndio walipokwenda kuitwa.
Baba na mama Anderson walitoka wakiwa wameongozana pamoja, wakati wanaingia Malaika mweusi alikuwa ameinama alinyanyua uso wake baada ya kusikia sauti ya mama mkwe wake mtarajiwa.
“Ooh! Karibu sana mwanangu!”
Macho ya Malaika Mweusi alikutana juu ya macho ya mama mkwe wake, wakati huo alikuwa ananyanyuka ili amlaki mama mkwe wake mtarajiwa. Alijikuta akipatwa na mshtuko wa ajabu na kupiga ukelele mdogo.
“Ooh! Mungu wangu!” alijikuta akirudi tena chini kwenye kochi wakati huo alikuwa ameshikilia kifua chake kuonyesha amepatwa na hofu, kitu kilichomfanya mama Anderson abaki amesimama kama sanamu.
Watu waliokuwepo pale walikuwa na mshangao Anderson naye alipigwa na butwaa asijue nini kilichotokea. Baba na mdogo wake ilibidi wamfuate Malaika Mweusi aliyekuwa akihema kwa shida. Walipofika pale alipokuwa amekaa na kumuuliza.
“Nini tatizo mama?”
Malaika kabla ya kujibu alinyanyua uso wake na na kukutana tena na sura za watu wawili baba na mkwe wake na shemeji yake mdogo wa Anderson. Alishtuka zaidi kitu kilichozidi kuwashangaza wote waliokuwa pale.
Ilionyesha kuna kitu kilimtisha pale ndani na kupatwa na mshtuko. Anderson ambaye alikuwa amesimama pembeni ya mlango walioingilia wazazi wake alishangazwa na hali aliyojitokeza kwa mchumba wake. Alitoka pale mlangoni na kwenda moja kwa moja kwa mchumba wake ambaye muda mchache angemvisha pete ya uchumba na kuwa mke wake mtarajiwa.
Alijipenyeza katikati alipokuwa mdogo wake na baba yake mdogo waliokuwa wamepigwa na butwaa kwa kile alichokionyesha Malaika Mweusi, alimshika mabega na kumwita:
“Malaika wangu kulikoni mbona hivyo?”
Baada ya kusikia sauti ya Anderson alinyanyua kichwa ili kuhakikisha kuwa ni yeye. Alipitisha mikono yake nyuma ya shingo ya Anderson na kumkumbatia na kilio cha kuvuta makamasi kwa ndani.

No comments