Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 05


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

ILIPOISHIA:
Alijipenyeza katikati alipokuwa mdogo wake na baba yake mdogo waliokuwa wamepigwa na butwaa kwa kile alichokionyesha Malaika Mweusi, alimshika mabega na kumwita:
“Malaika wangu kulikoni mbona hivyo?”
Baada ya kusikia sauti ya Anderson alinyanyua kichwa ili kuhakikisha kuwa ni yeye. Alipitisha mikono yake nyuma ya shingo ya Anderson na kumkumbatia na kilio cha kuvuta makamasi kwa ndani.
SASA ENDELEA...
“Malaika wangu hebu nitoe kizani nini kilichokusibu muda mfupi ulikuwa na furaha lakini ghafla umebadilika baada ya kuiona familia yangu?”
“Hapana mpenzi sivyo ufikiliavyo,” Malaika alisema kwa sauti ya kilio.
“Kama si hivyo ni nini kimekusibu?”
Alijitoa mikono ya Anderson, kwanza alimfuta machozi na kupangusa kamasi nyembamba kwa kitambaa cha mkononi. Kisha alikohoa ili kutengeneza sauti yake na kuzungumza kwa sauti ya chini kidogo inayomuwezesha mtu yeyote aliyekuwepo sebuleni kumsikia.
“Kwanza niombe radhi kwa hali niliyoionyesha kila mmoja ana shauku ya kutaka kujua kilichonisibu. Haikuwa nia yangu bali hali hii imejitokeza ghafla bila ya mimi kutarajia, Naweza kusema kweli dunia ni watu wawiliwawili.
“Yaani marehemu mama yangu anafanana sana na mama mkwe, si kwa umbile bali hata sauti utafikiri walizaliwa mapacha. Wakati nanyanyua macho nionane na mama mkwe wangu nilipigwa na mshituko wa ajabu na kuona kama mama yangu mzazi amefufuka na siyo siri katika vitu nilivyovipenda ni mama yangu mzazi. Nilimpenda zaidi ya kitu chochote hasa kwa malezi na mapenzi mazito aliyonileana.
“Alipofariki ilikuwa ni pigo ambalo liliniumiza siku hadi siku kila nimkumbukapo marehemu mama yangu majonzi hunianza upya huwa kama nachubua kidonda ambacho kilianza kupona. Kwa kweli nilipomuona mama mkwe ilikuwa ni jeraha jingine la moyo wangu kwa hilo naomba baba, mama na shemeji yangu na wote mliokusanyika mnisamehe sana haikuwa nia yangu.”
Malaika mweusi baada ya kusema sababu iliyomfanya atokewe na hali ile huku akilia. Alikwenda moja kwa moja hadi kwa mama mkwe wake na kumkumbatia. Mama mkwe naye alimpokea na kumkumbatia na kumpa pole.
“Pole sana mwanangu kazi ya Mungu haina makosa….je, baba yupo?”
“Hapana sina, kwani mpaka mama anafariki nilikuwa simjui baba yangu.”
“Ooh! Pole sana, nani aliyekulea mpaka ukafikia hatua hii?”
“Ni walimwengu tu.” Malaika Mweusi aliondoka kwa mama na kwenda kwa baba mkwe wake na kumtaka kumshika miguu.
“Baba naomba unisamehe.” lakini alimuwahi kabla ajainama na kumnyanyua.
“Hapana mama huna kosa lolote jisikie huru kwa lolote lile hapa ni kwenu.”
“Asante kwa hilo wazazi wangu”.
Aliwageukia wageni walikwa na kuwaomba msamaha ambao nao hawakuliona kosa lake na walimpa pole kwa mkasa wake mzito. Baada ya muda Malaika Mweusi alijitajidi kurudi katika hali yake ya kawaida na shughuli zote zilikwenda kama walivyopangwa.
Alitambulishwa kwa ndugu na jamaa na wazazi wake wa Anderson na kuhitimisha kwa sherehe fupi lakini iliyofana vilivyo ya kuvishana pete ya uchumba. Baada ya sherehe Anderson na mchumba wake, mkewe mtarajiwa walikaa kikao kabla ya kuondoka kuzungumzia masuala ya harusi.
Japokuwa Anderson alitaka harusi ifanyike ndani ya mwezi mmoja, lakini Malaika Mweusi alitaka iwe baada ya miezi mitatu ili naye apate muda wa maandalizi kwa kuwaalika marafiki wake walio nje ya nchi. Wazo la Malaika lilipitishwa na baada ya kikao waliondoka pamoja siku hiyo alilala kwa Anderson. Ilipofika saa kumi na nusu usiku aliondoka.
****
Tokea siku ile ikawa ni mazoea kwa Malaika Mweusi kulala na saa kumi na nusu huondoka. Kila alipotaka kusindikizwa alikataa kitu ambacho kilichoanza kumtilia wasiwasi Anderson.
“Malaika.”
“Unasemaje my sweet?”
“Unajua tabia yako ya kuondoka alfajiri kila unapokuja kulala hapa inanitia wasiwasi.”
“Wasiwasi wa nini?”
“Labda kuna mume mwenzangu.”
“Hilo ni wazo potofu, lakini siwezi kukukataza kuwaza hivyo lazima unionee wivu, kama ningekuwa na bwana kwako ningekuja kufanya nini. Nilitaka kuja kwako baada ya kunioa lakini nimekubali kwa sababu ya upendo wa dhati kwako. Umeniomba nije nilale kwako nimekubali tena kwa muda wa siku uipendayo kwa vile bado hatujaoana huu ni utaratibu wangu wa kuondoka alfajiri ili asubuhi unikute nipo nyumbani kwangu najua huwezi kuamini lakini huo ndio ukweli sina mwanaume yeyote zaidi yako ili ukweli utaupata utakapo nioa.”
“Mmh sawa,” alijibu Anderson kwa unyonge.
“Usihudhunike mpenzi hizi ni zako dhabibu utazila taratibu hakuna wa kukuibia.” Malaika Mweusi alimpiga busu Anderson na kuondoka na kumuacha akimkodolea macho.
*****
Mahusianao kati ya Malaika Mweusi na familia ya Anderson yalikuwa makubwa kitu kilichojenga mapenzi mazito kutoka ndani ya familia na kumsifu mtoto wao kwa kuchagu msichana mwenye upendo na huruma.
Kwa muda mfupi alitoa msaada mkubwa ikiwa ni pamoja kumaliza nyumba ya wakwe zake na kuwanunulia gari dogo la kutembelea kila mmoja aliomba siku ifike ili ndoa halali ifungwe.
Anderson alitaka kujua utajiri wa mchumba wake ameupata wapi wakati ni msichana mdogo tena yatima aliyelelewa na wasamalia wema. Hatua hiyo ilikuja baada ya kuonyeshwa mikataba.
“Najua utashangaa mpenzi baada ya kuona utajiri wangu wa kutisha nikiwa jijana mdogo na kuongoza vitu vyote hivi hili ni jambo linalotaka nafasi..si unakumbuka siku nilikueleza nilikupendea nini?”
“Ndio nakumbuka.”
“Basi vitu vyote navitafutia siku ili nikueleze kwa kituo, si haya tu kuna mengi yaliyo chini ya moyo wangu ambayo siku hadi siku yananiumiza akili yangu.
“Ni siku gani isiyokuwa na jina?”
“Ni baada ya ndoa yetu.. unajua bado ni muda gani tufunge pingu za maisha?”
“Mwezi mmoja na siku kama ishirini hivi.”
“Vizuri siku ya kesho nitakuwa na safari yangu ya mwisho ya kibiashara kabla ya harusi yetu vilevile nitatumia safari hiyo kufanya mambo makubwa wawili. Moja kumtambulisha mtu ambaye atakuwa anafuata bidhaa kwani baada ya ndoa sitatoka mbali nawe ili tuweze kuonja raha ya ndoa au sio dear?”
“Mimi sina cha kuongea.”
“Pili kufanya shoping kwa kwa ajili ya harusi yetu nataka nikakununulie bonge la suti ya gharama ilingane na harusi yetu itakayoacha kumbukumbu kwenye ubongo wa watu.”
“Sawa lakini usikae sana kuondoka kwako ni sawa na kunyang’anywa blanketi kwenye baridi kali.”
“Si wewe tu bali imebidi ndio maana baada ya harusi nitahakikisha sibanduki kwako nina imani wivu wangu ni maradufu zaidi ya marehemu mke wako mama Gift.”
Malaika Mweusi aliondoka kuelekea Uingereza, Marekani, Asia na Falme za Kiarabu, katika uwanja wa ndege aliagwa na mumewe mtarajiwa na familia nzima ya Anderson baba, mama na ndugu na jamaa zake.
Kabla ya kupanda ndege aliagana na kila mmoja wao kwa kukumbatiana naye na wa mwisho aliagana na mumewe mtarajiwa kwa kukumbatiana kwa muda huku kila mmoja machozi yakimtoka kwa sauti iliyojaa majonzi alisema:
“Japo moyo unaniuma kutengana kwa muda lakini imebidi kutokana na sababu maalum lakini cha muhimu ni kuniombea dua niende salama na nirudi salama ili tusheherekee harusi yetu na nanyi bakini salama mkiendelea na mipango ya harusi nina imani baada ya wiki mbili au tatu nitakuwa nimerudi kabla ya harusi au itanilazimu nikatize ziara yangu.”
Machozi yalimtoka Malaika Mweusi wakati akiagana na ndugu wa familia ya mumewe mtarajiwa, baada ya muda aliingia kwenye Gulf Air na kuondoka nchini alimuacha Anderson kama kinda la ndege lililoachwa kwenye kiota na mama yeke.
Wiki mbili baada ya Malaika Mweusi kuondoka kwenda kwenye ziara yake ya kibiashara Anderson aliendelea na mipango ya harusi yao wakati huo mauaji jijini yalikuwa yamepoa japokuwa uchunguzi haukufanikiwa kumtia mikononi muuaji.
Muda wote alikuwa akiwasiliana na kipenzi chake kipya Malaika Mweusi lakini wiki moja baada ya Malaika Mweusi kuondoka alimjulisha Anderson namba yake mpya kuwa amepoteza simu yake hivyo atamjulisha kwa namba mpya ili waendelee kuwasiliana.
Malaika kupoteza simu yake alikuwa akiwasiliana na mchumba wake kwa yeye kumpigia kila siku usiku. Siku zilikatika kama tatu bila ya mawasiliano kitu kilichomtia hofu Anderson na kujiuliza kulikoni mbona kimya cha ghafla ni kitu gani kimemsibu mchumba wake.
Alipokuwa ofisini kama kawaida yake alipokea simu ya baba yake mzee Chuma.
“Ndiyo baba, shikamoo.”
“Marahaba aisee njoo nyumbani haraka sana.”
“Kuna nini?”
Anderson habari zile zilimchanganya sana, aliingia kwenye gari akiwa na mawazo mengi juu ya simu ile ya baba yake. Aliendesha gari kwa mwendo wa kasi hadi Mbezi mwisho kwa wazazi wake alipofika alifungua geti na kuingia ndani moja kwa moja hadi ndani.
Ndani alilakiwa na vilio vilivyoonyesha kuna tukio lisilokuwa la kawaida wote walipomuona walimvamia kwa kilio.
“Jamani kulikoni?!”
“Ooh! Mama yako hatunaye,” aliambiwa na baba yake ambaye macho yake yalikuwa yamembadilikana kuwa mekundu kwa kulia na mkononi alishikilia kitambaa kwa ajili ya kujifutia machozi na kamasi.
“Eti unasema mama kafanyaje?” Anderson aliuliza kama hakusikia.
“Mama yako amefariki.”
“Amefanya nini, ameuawa?”
“Hapana amepata ajali amegonga mti wakati anakwenda shambani.”
“Una uhakika hajauawa?”
“Ni kweli taarifa zilitufikia na askari wa usalama barabarani.”
“Mwili wake upo wapi?”
“Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.”
“Kuna umuhimu wa kwenda sasa hivi.”
Aliongozana na baba yake hadi hospitali muhimbili kuchukua majibu ya kifo cha mama yake. Majibu yalionyesha kuwa amekufa kwa ajili ya kupata presha wakati anaendesha gari iliyosababisha ashindwe kuliongoza gari vizuri na kwenda kugonga mti.
Wakati anatoka hospitali na baba yake mara simu yake iliita. Ilikuwa ni simu ya kiofisi ambayo alipokea huku roho ikimdunda.
“Ndiyo lete habari.”
“Mkuu kuna maiti moja imekutwa imekufa maji kwenye bwawa la maji machafu chuo kikuu. Marehemu kandika ujumbe kwenye kikaratasi kuwa amejiua kwa sababu amejigungua kuwa ameathirika, maelezo yake tumeyakuta kwenye mfuko wake yaliyozungushiwa na karatasi ya nailoni ili usilowane.
“Kwa sasa hivi mpo wapi?”
“Tunakaribia hospitali ya Muhimbili.”
“Vizuri hata mimi nipo hapahapa mama yangu amefariki kwa ajali ya gari.”
Vijana wa Anderson waliwasili katika hospitali ya muhimbili harakaharaka walichukua machela kwa ajili ya marehemu tayari kumpeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Wakati wanateremsha mwili wa marehemu na kuuweka kwenye machela Anderson alikuwa amefika eneo lile alikisogelea kitanda alipokifikia wakati huo vijana wake walikuwa tayari kukisukuma, aliamua kuifunua shuka ili aione sura ya marehemu.
Anderson alishtuka na kupiga ukulele:
“Aaah!” nguvu zilimuishia baada ya kuiona sura ya marehemu alianguka chini na kupoteza fahamu.
Itaendelea

No comments