Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 07


 
 MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

ILIPOISHIA:
Anderson alikaa kimya chini ya uvungu huku akijiuliza maswali mengi kuhusu vile vitu vina maana gani, aliona wazi kabisa Malaika anajihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Hofu ilimuingia endapo Malaika atagundua yupo uvunguni? Tena na mkoba wake atamuelewaje.
SASA ENDELEA...

Malaika baada ya kushtuka usingizini alijiuliza mpenzi wake yupo wapi alimwita tena.
“Sweetie uko wapi?”
Hakuwa na jibu, aliangalia saa yake ndogo ya mkononi ilimuonyesha ni saa tisa na nusu usiku. Alijinyanyua na kujipekecha macho kutokana na usingizi alijua lazima Anderson atakuwa msalani alipitia taulo lake na kwenda msalani.
Anderson aliutumia muda ule kutoka uvunguni mwa kitanda na kurudisha mkoba ulipokuwa na kujilaza kitandani na kujifanya kukoroma.
Malaika alipotoka kuoga alishtuka kumuona Anderson kitandani akiwa katika usingizi mzito. Alijiuliza alipoamka alikuwa na usingizi mzito kichwani uliomfanya ashindwe kumuona. Alijikuta akishindana na mawazo yake kwani alikuwa na uhakika aliamka usingizini Anderson hakuwa kitandani.
Alijua yupo msalani vilevile alishangaa kutomkuta kama alivyotarajia na cha kushangaza zaidi alipotoka kuoga alimkuta kitandani tena kwa usingizi mzito.
Aliyapuuza mawazo yake kwani aliona yanampotezea wakati, hakuwa na haja ya uendelea kulala pale. Alikwenda hadi kitandani wakati huo Anderson alijifanya yupo kwenye usingizi mzito na kumshika mgongoni huku akimtingisha taratibu akimuita.
“Sweet….sweet,” Anderson hakushtuka mapema mpaka alipomuita zaidi ya mara sita na kujifanya anashtuka.
“Eeeh.” Aliitikia huku akijifanya kujigeuza kitandani.
“Sweet” Malaika Mweusi alirudi tena.
“Naam,” aliitika bila kufumbua macho.
“Mi’ ndio naondoka.”
“Kwani saa hizi ni saa ngapi?”
“Kumi kasoro.”
“Kumi kasoro mbona ni usiku sana?” aliuliza huku akifumbua macho na kujifanya kupiga miayo.
“Aah, nimeamua kuondoka tu.”
“Nikusindikize?”
“Hapana we endelea kulala tu.”
Malaika Mweusi alipitia mkoba wake bila kuchunguza alimbusu Anderson na kutoka nje. Nje alisikia sauti ya gari likiondoka. Anderson alikaa kitandani baada ya Malaika kuondoka akiwa na mawazo mengi juu ya vitu alivyovikuta kwenye mkoba. Chupa ya manukato, chupa ya dawa ya sindano yenye maji meupe, bomba la sindano na glovu.
“Hapana kuna haja ya kufuatilia nyendo zake lazima kesho niwape kazi vijana wangu kufuatilia miradi yote iliyo chini ya msichana mdogo lakini mwenye utajiri wa kutisha,” alijisemea kwa sauti ya chini.
Swali lingine lilikuwa ni kuhusu Malaika Mweusi kuondoka ghafla usiku huku akionyesha kitu kama hasira. Alijiuliza inawezekana amepekua mkoba wake na kugundua jambo? Alijua kama itakuwa hivyo basi uhusiano kati yao utaingia ufa au kufa kabisa kwani ni msichana aliyeonyesha msimamo wa hali ya juu.
Alfajiri ilimkuta akiwa macho alioga na kwenda ofisini kwake mapema, kitu kilichomshtua Secretari wake hata vijana wake pia. Hakupoteza muda aliwaita vijana wake na kuwapa jukumu la kufuatilia miradi yote iliyopo chini ya leseni ya TEMA na kuchunguza pia inashughulika na nini ikiwa ni pamoja na kuwahoji kwa siri baadhi ya wafanyakazi na majibu aliyataka jioni ile.
Vijana walitawanyika na kuanza kazi ile mara moja, wengine walianza kwenye miradi wote inayofahamika wengine kwenye ofisi ya kodi ya mapato huku wengine wakiingia kwenye mtandao ili kujua TEMA inashughulika na nini katika mtandao wa www.mate.com.tz.
***
Majira ya saa moja jioni Mr Anderson alikutana na vijana wake ili kumpa majibu ya kazi alizowatuma.
“Vipi jamani za kutwa?”
“Nzuri tu bosi.”
“Eeh mambo yamekwendaje?”
“Si mabaya sana tumepata baadhi ya dondoo nina imani unaweza kupata mwanga wa kitu unachokitaka.”
“Sawa mmefikia wapi?”
“Bosi baada ya kutugawa tumefanya uchunguzi wetu wa kina na kila mmoja akiwa na jukumu lake nina imani kila mmoja wetu mambo yake yamekwenda vizuri,” Alisema Aziz.
“Baada ya kila mmoja kupata alichokidodosa tulikutana pamoja kabla ya kukuletea jibu moja litakalokuwa limejitosheleza,” Aliongezea Suzana aliyekuwa kiongozi.
“Sawa nawasikiliza.”
Taarifa ilionyesha kuwa miradi iliyopo chini ya leseni ya TEMA ni mingi ambayo yote ipo chini ya msichana mmoja mdogo jina lake Tereza Maria Magdalena, anamiliki shule za kimataifa sita, nne zipo jiji la Arusha na moja Mwanza, pia anamiliki viwanda vitano viwili za dawa za binadamu na mifugo kimoja cha plastiki kwa ajili ya kutengenezea bidhaa za maji, biskuti na juisi ambavyo amevitenga mahsusi kwa ajili ya wanawake wajane wenye maisha magumu.
Pia ana hospitali mbili kubwa hapa jijini inayotoa huduma kwa gharama pia alitenga sehemu maalum kwa ajili ya magonjwa ya ukimwi ili afanye kazi nyepesi ambazo hazitawachosha sana. Amejenga vituo ishirini kwa ajili ya kulelea watoto yatima ambavyo vina shule ndani, ni msichana anayeishi katika mazingira ya kawaida hajaolewa.
“Mmedodosa vyanzo vyake vya pesa?”
“Inaonyesha pesa nyingi anapata kwa wafadhili, kuna mashirika zaidi ya ishirini yanatoa pesa zaidi ya dola milioni elfu moja ili kuboresha shughuli zote za kujitolea kama watoto yatima, kuanzisha mfuko wa kuwahudumia wagonjwa wa ukimwi ikiwa ni pamoja na kugawa dawa bure ambazo hununua kwa pesa zake.
“Siku zote NGO’s za nje zinatafuta watu au vikundi vyenye kutoa msaada kwa jamii na kuiongezea nguvu.”
“Miradi mingi ameiongeza baada ya kupata fedha kutoka kwa wafadhili nje kabla ya pesa za wafadhili hizo za kuanzia ametoa wapi?”
“Ukweli hapo hatukupata habari za pesa zake za kuanishia hiyo miradi aliipata wapi.”
“Ok kazi si mbaya ila kesho nataka kupata jibu kuwa pesa za kuanzia alizipata vipi.” “Asante nashukuru kwa kazi nzuri tutaonana kesho.”
Aliagana na vijana wake na kujirudisha nyumbani huku akiwa na mawazo kuhusu utajiri wa kutisha wa Malaika Mweusi. Ni msichana wa ajabu anayeonyesha ni jinsi gani anajali binadamu wenzake ukweli usiopingika kuwa msichana Tereza ni Malaika mwenye umbile la kibinaadamu.
Ni msichana mwenye huruma na mapenzi ya kweli lakini je, chanzo cha utajiri wake kimetokana na nini? Mara nyingi watu wengi wenye roho nzuri walio mstari wa mbele kusaidia jamii misaada yao huwa kama kinga ya kulinda maovu yao lakini nyuma yao ni uozo unaotapisha na kutotamani kuuona wala kusikia.
Anderson alijua kesho yake ni lazima atajua ukweli juu ya chemchemi ya utajiri wa Malaika Mweusi unatokana na nini pia vitu alivyoviona kwenye mkoba vilikuwa na maana gani. Alijikuta akijilaumu ni kwa nini asimulize lakini angeanzia wapi na ni nani aliyempa ruksa ya kupekua mkoba wake bila ya idhini ya mhusika.
Akiwa sebuleni alijikuta kila achokiwaza hakupata jibu kamili, hata usingizi ulivyomchukua hakujua alishtushwa usingizini na sauti ya Malaika Mweusi.
“Sweetie.. vipi ulalaji gani huo kama si askari?”
“Aah! Hivi umekuja muda mrefu, kwani sasa hivi ni saa ngapi?”
“Ni saa tatu kasoro.”
“Mungu wangu kumbe nimelala bila ya kujijua!”
”Pole sana shughuli ya leo ilikuwa nzito nini?”
“Si sana.”
“Ushakula?”
“Bado nilikuwa nakusubiri wewe.”
“Muongo ulijiua nakuja saa ngapi?”
Muda wote hata kama ingekuwa ni alfajiri ningekusubiri tu.”
Walijikuta wakiangua kicheko pamoja na kwenda kuoga, waliporudi walikwenda kwenye mgahawa wa karibu kupata chakula na waliporudi walilala.
Kama kawaida Anderson alipanga kuwa Malaika Mweusi atakapolala atafanya uchunguzi wa kina pamoja na kuandika majina ya chupa zile mbili ili awapelekee wataalam wa maswala ya kemikali.
Kama kawaida alijifanya amelala Malaika Mweusi alipitiwa na usingizi, muda mrefu aliangalia saa ya ukutani akisubiri ifike saa saba ya nusu au nane aamke. Alijitahidi kuwa macho hadi saa sita na nusu aliamua kujinyoosha kidogo na usingizi ukampitia. Aliposhituka macho yake yalikuwa juu ya saa kubwa ya ukutani ikimuonyesha ni kuwa saa nane na nusu saa moja zaidi ya muda aliopanga.
Kitandani alikuwa peke yake alijiuliza Malaika Mweusi amekwenda wapi au msalani. Alisubiri kwa robo saa hakumuona na na alipomuangalia msalani pia hakuwepo. Alijikuta akijiuliza atakuwa amekwenda wapi alizunguka nyumba nzima lakini hakumuona ufunguo ulikuwepo mlangoni na mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani.
Anderson aliingiwa na wasiwasi inawezekanaje mtu atoke ndani bila ya kufungua mlango au Malaika Mweusi si binadamu wa kawaida ni jinni. Akiwa kati kati ya mawazo, mara simu yake ililia alipofuata kwenye kitanda na kwenda kuichukua namba zilizokuwa za ofisi. Moyo ulimlipuka usiku kama ule simu ya nini tena na aliinyanyua na kuanza kuongea.
“Enhe lete habari?”
“Bosi habari ni mbaya.”
“John Masu na Mustachi wameuawa.”
“Wameuawa na nani na vifo vyao vimetokana na nini?”
“Bosi usiombe, vita iliyotokea saa moja na nusu iliyopita sijawahi kuiona toka nijiunge na kazi ya jeshi.”
“Ilikuwaje?”
“Tulifanikiwa kuwazingira wauaji waliokuwa wamevamia kanisa shida yao ubwa ilikuwa kumuua Mchungaji Marco Gin.”
“Kwa kuwa tuliwazingira vizuri tulijitahidi kupambana nao na kufanikiwa kuwatia mikononi sita kati ya kumi, tulijua ndio mwisho wao.
“Huwezi kuamini ni vijana wadogo sana hata umri miaka kumi na tano bado tena ni watoto wa kike wazuri lakini wote wana ujuzi wa hali ya juu wa kutumia siraha za aina zote.
“Tukiwa tunasheherekea ushindi mara kuna gari mbili zilifunga breki mbele yetu bila ya kutarajia walianza kutumimia risasi wakiongozwa na wanawake mmoja hatari sana kwa kuwa tulikuwa tumejisahau aliua watu wetu wawili palepale Mustach na John….Masu alimuwahi yule mwanamke alionyesha amevaa nguo nyeusi tupu ya kitambaa cha mpira mwili mzima.
Alimuwahi risasi ya begani ambayo nina uhakika atakuwa amemuua lakini mfuasi wa yule mwanamke alimuwahi risasi iliyohitimisha idadi ya wenzetu watatu.”
“Shughuli bado pevu na kanisani hawakudhuru mtu?”
“Wamekufa walinzi wanane pia wamemjeruhi mchungaji Marco Gin.”
“Vipi hali yake?”
“Bado mbaya.”
“Ok nakuja.”
Wakati anajiandaa mara simu iliita iliingia namba ngeni machoni mwake alipokea na kuongea.
“Haloo… haloo...eeh ndiyo mimi…eti unasema Malaika Mweusi amefanya nini? Hapana…hapana haiwezekani…lazima nije nishuhudie mwenyewe kama ni kweli itakuwa pigo la tatu takatifu,” taarifa zile zilimchanganya Anderson alichanganyikiwa alijikuta anapanda gari na taulo tena kifua wazi.
Taarifa za Malaika Mweusi zilimchanganya kwa kiasi kikubwa na kujiona kiumbe mwenye mkosi mapigo ya moyo yalimtingisha lakini mke wangu na mwanangu na sasa wamemuua kipenzi changu Malaika Mweusi nani sasa atakuwa amebaki kama si mimi mwenyewe?” Anderson alizungumza mwenyewe huku akiendesha gari kuelekea kwenye tukio.
Aliwaza mengi baada ya kupata taarifa za Malaika Mweusi. Akiwa njiani alijigundua kuwa yupo kifua wazi na amevaa taulo tu, hilo hakujali alisimamisha gari mbele ya mapokezi ya Muhimbili na kwenda moja kwa moja mapokezi huku akihema utafikiri alikuwa anatembea kwa miguu na wala hakupanda gari.
“Samahani ndugu kuna taarifa zozote za kipolisi zilizofikishwa hapa?”
“Ndio..ndio.. mzee.”
“Ya kwanza kuna maiti zimeletwa kutoka kwenye eneo la kanisa.”
“Na nyingine?”
“Maiti ya msichana iliyookotwa barabarani.”
“Ooh Mungu wangu ipo wapi?.... ni bora nikaishuhudia mimi mwenyewe.”
“Mzee maiti itakaa wapi zaidi ya monchwari?”
Mr Anderson aliishiwa na nguvu alijikuta anakaa chini, vijana waliokuwepo hospitali walianza kumshangaakumuona bosi wao katika hali ile.
“Vipi bosi mbona upo katika hali hii?”
“Nyie acheni tu mbona mwaka huu wangu?”
“Nini tena bosi?”
“Si shemeji yenu.”
“Nani? Malaika wako?”
“Kuna nani zaidi yake?”
“Kafanya nini?”
“Amekufa…..
Hakumalizia kusema mzee mzima alianza kulia mbele ya vijana wake.

Itaendelea

No comments