Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 08


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

ILIPOISHIA:
“Si shemeji yenu.”
“Nani? Malaika wako?”
“Kuna nani zaidi yake?”
“Kafanya nini?”
“Amekufa…..
Hakumalizia kusema mzee mzima alianza kulia mbele ya vijana wake.
SASA ENDELEA...

“Utani huo bosi muda si mrefu uliniambia kuwa upo na mamaa kabla ya lile sheshe la maeneo ya kanisani, vipi amevamiwa akiwa nyumbani?”
“Ni historia ya ajabu ngoja niende mochwari nikaishuhudie hiyo maiti kama ni ya Malaika Mweusi.”
Kutokana na kuishiwa nguvu vijana wake walimsaidia kuingia chumba cha maiti ili ashuhudie. Walikwenda hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti, mhudumu baada ya kufika alipoulizwa kuhusu kupokea maiti ya mwanamke alisema:
“Kwa kweli nimepokea maiti nyingi sana leo za wanawake sasa sijui mnamhitaji nani labda tumtafute kwa pamoja.”
“Hamna tabu.”
Anderson alijibu huku wakiingia katika chumba cha maiti na kuanza kufungua dro moja hadi nyingine za kuhifadhi maiti zilizoigizwa siku hiyo. Maiti zote walizoziona zilizokuwa ndani ya chumba ajabu hawakuiona ya Malaika Mweusi.
Ilibidi wamuulize vizuri yule mhudumu wa mochwari.
“Mbona bado maiti moja?”
“Maiti gani hiyo?”
“Kati ya zilizoingia usiku huu.”
“Ni hizi tu hakuna nyingine.”
“Hapana bado moja.”
“Labda kama iliingia kabla yangu hebu tuangalie kwenye kitabu.”
Waliongozana moja kwa moja hadi kwenye kitabu cha maiti waliingia usiku ule lakini pia maiti ya Malaika Mweusi haikuwepo ili kumridhisha roho yake waliangalia maiti zote zilizokuwepo bila ya kujali maiti nyingine ambazo zilikuwa zinatisha sana kutokana na majeraha.
Lakini maiti ya Malaika Mweusi haikuwepo, ilibidi kijana wake amulize.
“Kwani bosi, taarifa za kifo ulizipata wapi na kutoka kwa nani?”
“Kuna mtu alinipigia simu akinijulisha kuwa mwili wa Malaika Mweusi umeokotwa ukiwa umelowa damu nyingi kifuani.”
“Alikueleza amepelekwa wapi?”
“Amesema hapahapa Muhimbili.”
“Sasa mbona haupo au yupo wodini?” alitoa wazo.
“Tangu lini maiti akawekwa wodini?” Anderson aliuliza.
“Una uhakika gani kama amekufa labda wingi wa damu tu inawezekana yupo hai au atakuwa amepoteza fahamu wakajua amefariki.”
“Kwa hiyo unaniambia twende wodini tukaulize?” Anderson aliuza swali kama mtoto mdogo.
“Ndio maana yake.”
Waliongozana pamoja hadi wodini na kuliza kama kuna majeruhi yeyote aliyeingizwa usku ule.
“Ni wengi waliovamiwa na majambazi, wapo waliopatwa na ajali pia kuna mwanamke mmoja aliyeokotwa inaonekana alijeruhiwa vibaya na risasi.”
“Eeh, ndiye huyo yupo wapi?” Anderson alirukia.
“Taratibu mzee yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi huwezi kuonanana naye kwa sasa.”
“Lakini yupo katika hali gani?”
“Sikudanganyi yupo katika hali mbaya sana kupona kwake ni majaliwa ya Mungu.”
“Mungu wangu sijui itakuwaje!”
“Kwani mzee ni nani yako?”
“Mke wangu.”
“Ina maana haya yote yanatokea alikuwa anatoka wapi?”
“Si wakati wake sasa cha msingi ni kujua hali ya mgonjwa kwanza.”
“Kwa leo hatuna jibu njoo kesho utapata habari kamili za mgonjwa.”
“Jamani hata kumuona kidogo?”
“Sasa itasaidia nini?”
“Angalau nimuone kwa macho roho yangu iamini.”
Anderson aliongozwa na daktari hadi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kushuhudia Malaika Mweusi akiwa amelala kitandani akipumua kwa msaada wa mashine maalum pia alikuwa ameongezewa damu.
Malaika alikuwa sawa na maiti kwani alikuwa hajui kinachoendelea, Anderson hakuwa na jinsi ilibidi aende nyumbani ili arejee kesho yake kufuatilia hali ya kipenzi chake.
****
Siku ya pili kabla ya kwenda hospitali ili kujua hali ya Malaika Mweusi hata hivyo jibu alilopewa halikuwa na tofauti na la jana kwani hali yake bado ilikuwa ni mbaya sana alikuwa bado anatumia mashine ya kupumulia.
Anderson alirudi ofisini alikuwa mnyonnge kutokana na hali ya kipenzi chake kuwa bado mbaya. Akiwa ofisini alijawa na mawazo mengi juu ya mkasa mzima na mazingira yaliyompata Malaika hadi kufikia kukumbwa na dhahama ile alijiuliza kwa nini aliondoka bila kuaga na gari lake lipo wapi. Baada ya muda mfupi simu yake iliita alinyanyua na kuongea.
“Habari za asubuhi bosi.”
“Nzuri tu.”
“Si kweli, pole sana.”
“Bado sijapoa, ulikuwa unasemaje?”
“Vijana wapo tayari kuonana na wewe.”
“Ooh, wambie waingie.”
Mara mlango uligongwa, vijana saba wa kazi waliingia ambao idadi yao walikuwa kumi lakini wenzao watatu walikufa kwenye mshikemshike wa usiku kuamkia jana yake.
“Habari za asubuhi,” aliwasabahi baada ya kuwaruhusu kukaa chini.
“Nzuri bosi sijui wewe?”
“Zangu ni mbaya kama mlivyosikia.”
“Pole sana inavyoonekana muuaji amepania.”
“Mimi wasiwasi wangu bado kidogo kumtia mikononi hivyo anajiamini ili kukutisha lakini nakuahidi sitaacha kumtafuta hadi damu ya mwisho”.
“Bosi usemayo ninakuunga mkono ni wasiwasi wake tu ndio maana anafanya vitu vya kukutisha,” kijana wake mmoja aliunga mkono.
“Sasa ni hivi, wanne nendeni mkafanye mipango ya mazishi, wawili mtakaa mmoja ndani ya hospitali na wengine nje ili kulinda Malaika wangu asipate shambulio jingine. Mimi na Lyasi tutaongozana hadi kanisani tukapate maelezo ya mchungaji Father Marco Gin labda tutapata picha yeyote.. haya tutawanyikeni tutaonana msibani.”
Anderson baada ya kugawa kazi kwa vijana wake alielekea kanisa kuu la WALIJITOA KWA AJILI YA MUNGU. Moja ya makanisa makubwa sana nchini japokuwa ni geni lilikuwa na tofauti na yanayotangulia kwa muda mfupi ilikusanya waumini wengi kutokana na mfumo mzima wa usambazaji wa neno la Mungu.
Ndiyo kanisa lililokuwa linaongoza kwa msaada na promotion kwa vijana wengi kwenda nje ya nchi kufanya kazi. Pia lilitoa misaada kwa vijana wengi wanawake wajane bila usahau waathirika wa ugonjwa wa ukimwi.
Kanisa lililoongozwa na mchungaji Marco Cin raia wa Marekani lakini aliishi sana nchini Italia ni mtu aliyekuwa na umaarufu mkubwa. Kwa muda wa miaka saba aliweza kufungua matawi mengi nchini mjini na vijijini makanisa ya WALIOJITOA KWA AJILI YA MUNGU yalisambaa nchi nzima.
Jina la Marco Cin lilikuwa kubwa ndani na nje ya nchi kwani alikuwa ni mtu mwenye huruma na mwenye kujali utu wa watu. Alikuwa ni mtu anayeheshimika serikalini.
Kila sehemu walipofungua kanisa sehemu hiyo ilipata maendelea kama huduma za maji, shule, hospitali na huduma za umeme wa jua la solar power.
Sehemu zote hizo vijana wote walipata nafasi za kufanya kazi nje ya nchi hata waliokuwa hawana elimu jambo lililowafanya vijana wengi kwenda katika kanisa hilo.
Mchungaji Marco Cin alifungua miradi mingi ya vijana ili kuwapunguzia ukali wa maisha. Akiwa njiani na kijana wake Anderson alibadilishana naye juu ya wimbi la mauaji yaliyogubika jiji.
“Hivi Lyasi unaweza kujua haya mauaji yanafanywa na mtu mmoja au kikundi cha watu?”
“Yoye mawili yanawezekana.”
“Sasa inamaana haya mauaji ni ya kisasi au?”
“Sidhani kama kuna kisasi cha aina gani hiyo.”
“Sasa unadhani ni nini?”
“Nina wasiwasi mauaji haya yanafanywa na watu tofauti na si mtu mmoja.”
“Unadhani ni kwa nini?”
“Hilo ni swali gumu mkuu ndio maana tunaangaika kutafuta tatizo ili tujue kiini cha matatizo yote.”
Mara simu ya Anderson ililia alipoangalia ilikuwa ya kiofisi aliipokea na kuongea.
“Haloo.. en’hee..lete habari.”
“Bosi gari la Malaika Mweusi limekutwa Kibaha likiwa na alama za risasi na michirizi ya damu maeneo ya mlango wa dereva.”
“Inawezekana wezi walimpora?”
“Ni kweli kabisa mkuu wazo lako halitofautiani na langu kwani inawezekana waliamua kuliacha baada ya upasukiwa na gurudumu moja.”
“Kwa sasa gari hilo lipo wapi?”
“Lipo Kibaha katika kituo cha polisi.”
“Sawa nitalifuata baadae baada ya kupata maelezo kwa mchungaji.”
“Sawa mkuu tunaendelea na uchunguzi zaidi.”
Anderon alikata simu na kumgeukia kijana wake.
“Hivi Lyasi suala la kutaka kuuawa kwa mtu kama Father Gin mtu aliyejitoa kwa ajili ya watu leo hii anataka kuuawa bila ya sababu mbona kama sielewi.”
“Mkuu hii ishu lazima kuna watu hawapendezwi na huduma anazozitoa kwa jamii, siku zote si watu wote wanaopenda maendeleo ya watu.”
“Ni kweli Lyasi lakini ukweli tutaupata kwa mchungaji.”
Wakati huo gari lao lilikuwa limesimama mbele ya lango la kuingilia katika kanisa la WAUMINI WALIOJITOA KWA MUNGU. Baada ya mahojiano na walinzi wa getini waliruhusiwa kuingia ndani. Walipaki gari lao kuelekea kwenye ofisi za kanisa, walipokewa na sister wa kizungu aliyekuwa mapokezi.
“Ooh, karibuni sana,” aliwakaribisha kwa unyenyekevu.
“Asante.”
“Niwasaidie nini?” Anderson alijitambulisha na yule sister alimueleza.
“Mr Anderson subirini kidogo kaeni hapo kwenye kochi..sijui mnatumia kinywaji gani cha moto au baridi?” Walikaribishwa kwenye makochi.
“Asante hatuhitaji kwa sasa.”
“Hapana hii ni kwa ajili yenu hiki ni kinywaji kwa ajili wageni wanaomsubiri Father.”
“Sawa sista tuletee chochote”.
Waliletewa kinywaji baridi, baada ya robo saa walielezwa na yule sister:
“Mchungaji yupo tayari nendeni kwenye chumba cha wageni.”
Alitokea sister mwingine na kuwaongoza hadi kwenye chumba cha maongezi.
Walipoingia ndani walimkuta Father akiwa kwenye kibaiskeli cha matairi manne.
“Ooh! Mr Anderson, karibuni sana.”
Kabla hajajibu simu yake iliita.
“En’heee ndiyo mimi….eti… acha utani Malaika amefanya nini?... ameibiwa hospitalini? Hii kali nakuja sasa hivi. Anderson ilibidi amuage mwenyeji wake Father Gin.
“Vipi ofisa kuna habari gani, naona kama zimekushitua sana?”
“Aaa..a. samahani Father ni habari za kikazi tu nitarudi baadaye.”
“Ooh! Bwana awafikishie salama ili tuonane tena.”
“Asante Father.”
Anderson aliondoka na kijana wake Lyasi kuwahi Muhimbili kupata taarifa rasmi za kutoweka kwa Malaika Mweusi katika mazingira tata.
“Lyasi sasa huu ni mchezo, ina waana watu wote walikuwa wapi mpaka aibiwe?”
“Ndiyo suala la kushangaza mkuu.”
“Unajua Lyasi naona kama utani vile yaani atoweke katika hali kama ile ina maana wale wauaji hawakuridhika baada ya kusikia hakufa?”
“Mkuu mbona kama kitendawili, inavyoonekana hawakutaka kumuibia gari bali nikumuua.”
“Unajua Lyasi kama Malaika Mweusi akiuawa mimi ndiye nitakuwa nimechangia kifo chake,” alisema Anderson.
“Kwa nini mkuu?”
“Baada ya kifo cha mke wangu na mwanangu nilipotaka kumuoa Malaika Mweusi alikataa kwa kuhofia naye anaweza kuuawa.”
“Sasa wewe unahusika kivipi?”
“Nimeshindwa kumlinda vijana wangu safari hii mmeniangusha,” Anderson alisema kwa masikitiko.
“Si hivyo tulijaribu kumlinda kwa karibu sana lakini kwa Malaika Mweusi ilikuwa vigumu kumlinda.”
“Kwa nini?”
“Kwani anaweza kuwapotoea katika mazingira ya ajabu mnabaki mnaulizana amepita wapi!”
“Kuwapotea kivipi?”
“Siku moja baada ya kutoka hapa kwako tulimfuatilia hadi kwenye maegesho ya magari Kinondoni lakini cha kushangaza ndani ya gari alitoka bibi kizee kikongwe ambaye aliingia kwenye gari lingine na kuondoka.”
“En’he ikawaje?”
“Basi mkuu tuliilinda lile gari ili kujua Malaika Mweusi ataenda wapi lakini cha kushangaza hakuonekana kutoka hadi kunakucha na tulipokwenda kwenye lile gari hatukumkuta!!”
“Mmh! Ipo shughuli.”
“Acha hiyo bosi kuna siku moja alituacha hoi watu wote.”
“Ilikuwaje?”
“Kama kawaida alipotoka kwako siku hiyo ilikuwa ni mchana kwa bahati mbaya gari lake liligongana na gari kwa nyuma tena eneo lenyewe lilikuwa na trafic ilibidi amtoe kwenye gari na kumpeleka kituoni.
“Mmh?”
“Tuliona si vyema mama mtarajiwa afikishwe kituoni ni lazima angetuuliza tunafanya kazi gani.”
“Mkamfanyaje sasa?”
“Tulilipita lile gari lilikuwa limembeba Malaika, tulisimamisha trafiki alituelewa na kumuachia, lakiini kilichotokea kilikuwa kama mazingaombwe.”
“Nini kilitokea?”
“Mkuu hakuwa Malaika Mweusi lakini wanafanana sana kwa umbo na sura kopi raiti. Hakuna kutofautisha.”
“Kwa nini msihoji yupo wapi?”
“Tulimhoji mkuu.”
“Akasemaje?”
“Akasema kuwa tumemuacha kwenye gari na tulipokwenda tulimkuta.”
“Hamuoni hapo mlifanya uzembe?”
“Najua utasema uzembe kumlinda Malika Mweusi ni kazi ngumu kwa kweli hatumuelewi vizuri.”
“Kivipi?”
“Anabadilika kama kinyonga.”
“Habadiliki chochote pupa yenu tu kutokuwa makini kwa yale mnayotumwa.”
Wakati huo alikuwa anasimamisha gari mbele ya hospitali ya Muhimbili. Aliteremka harakaharaka na kukimbilia wodini. Alikutana na dokta Bon Mandi ambaye alionekana hajatulia vizuri.
“Vipi Dokta?”
“Hili mzee ni tukio la kigaidi.”
“Una maana gani?”
“Yaani madaktari wote wameleweshwa kwa kupuliziwa dawa.”
“Na mgonjwa?”
“Mzee nikueleze mara ngapi hili ni tukio la kijasusi baada ya kuwalewesha wote na kumuiba mgojwa”
“Wewe ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa nipo chumba cha upasuaji, dokta Mbilinyi aliponiletea taarifa kuwa mgonjwa ametoweka.”
“Yeye alijuaje?”
“Dokta Fanuel alikuwa anatoka alimtumia ujumbe kuwa akiingia aende kumjulia hali mgonjwa, alipokwenda wodini alishangaa kuwaona wauguzi wote wakiwa wamejilalia na mgonjwa hakuwepo ndipo aliponiita chumba cha upasuaji na kunieleza yaliyojitokeza.”
“Mpaka sasa mmechukua hatua gani?”
“Tumeitalifu polisi nao wamekuja kufanya uchunguzi wao na kuchukua maneno mawili matatu.”
“Hakuna aliyekufa?”
“Hakuna mheshimiwa.”
“Sawa nitarudi baadaye kupata taarifa zaidi.”
“ Anderson alirudi ofisini na kuanza kuwasema vijana wake.”
“Jamani naona wazi kazi imetushinda ni bora kila mtu akashike jembe akalime sioni umuhimu wa sisi kuwepo hapa zaidi ya kuitia hasara serikali.”
“Bosi hii ngoma ni nzito si ya kitoto kama tunavyofikiria adui tunayepambana naye ana utaalamu wa hali ya juu hivyo sasa hivi si muda wa kufanya kazi kwa kufuatana fuatana kila mtu ahangaike kivyake na kwa mbinu nyingine kabisa ni wazi adui yetu anatuelewa vizuri sana mpaka udhaifu wetu na ndio maana anatuzidi maarifa.
“Sasa kwa mawazo yangu kila mmoja atoweke kijijini na arudi baada ya mwezi mmoja ataleta taarifa kwa wakati wake atakaporudi …..sijui hapo mnasemaje?”
“Wazo lako ni zuri sana kesho baadhi ya watu nitawapa pesa ya kujikimu na kutoweka kijijini kila mtu aje kivyake na kuanza kazi mara moja.”
Anderson aliagana na vijana wake na kurudi nyumbani alipofika nyumbani alishangaa kukuta barua imebandikwa mlangoni kwake. Aliichukua na kuingia nayo ndani kabla hajaisoma ile barua aliyoingia nayo ndani ilikuwa imeandikwa:
Anderson ukaidi wako ndiyo umesababisha lkifo cha Malaikwa Mweusi sasa hili ni onyo usiingilie yasiyo kuhusu ukaidi wako utakufanya kila siku upoteze roho za watu na mwisho wake itakuwa roho yako. Bado tunaipenda hatupendi kuiona inapotea kwa jambo la kuacha kila yamkute basi yakazua mwenyewe siku zote akumulikae wewe mchome kabisa, wacha walinywe wamelikoroga wenyewe.
Ndimi apendaye maisha yako.
Anderson baada ya kuisoma ile barua alishusha pumzi na kujiona sawa na mtu aliye jangwani anayeonekana kwa uwazi. Aliona jinsi adui zake walivyo mzunguka kila kona kuliko yeye anavyowafuata usiku na mchana bila ya kuwaelewa wapo wapi.
Vita aliiona ni nzito aliifananisha na mpiganaji aliyefungwa kitambaa machoni na kupigana na mtu anayeona tena ana nguvu za ziada.
Lakini alijipa moyo kuwa anamtafuta muuaji wake hadi tone la mwisho la damu yake. Hakuona hasara kwani mama yake mdogo wake mkewe, mwanaye na kipenzi chake Malaika mweusi hawapo, akuona ubaya naye kuwafuata.

Itaendelea

No comments