Header Ads

HADITHI: MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 09


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Lakini alijipa moyo kuwa anamtafuta muuaji wake hadi tone la mwisho la damu yake. Hakuona hasara kwani mama yake mdogo wake mkewe, mwanaye na kipenzi chake Malaika mweusi hawapo, akuona ubaya naye kuwafuata.
SASA ENDELEA...
***
Siku ya pili alikwenda kanisa la WALIOJITOLEA KWA AJILI YA MUNGU ili apate mawili matatu kwa Father Gin.
Kama kawaida alikaribishwa na sister wa Kiswahili na kuletewa kinywaji baridi, wakiwa katikati ya vinywaji alikuja sister mwingine na kuwaomba waongozane hadi chumba cha maongezi na baada ya salamu zilipita kama dakika ishirini hivi ndiyo Father Gin alitokea akiwa kwenye kiti chake cha magurudumu(wheel chair) alipowaona tu aliwakaribisha kwa furaha.
“Ooh! Wapendwa karibuni sana.”
“Asante Father.”
“Za tokea jana, safari yenu ilikuwa yenye amani?”
“Ndiyo Father Gin.”
“Ooh, karibu sana.”
“Asante samahani Father.”
“Bila ya samahani.”
“Tulikuwa tunaomba kupata maelezo yako kutokana na sakata la juzi.”
“Kwa kweli siwezi ulieleza kwa undani zaidi kwa kuwa mengine siyajui ninachokumbuka nilitoka kwenye gari ili niwaangalie vijana waliokuwa wamelewa lakini baadaye niligundua hawajalewa bali dhamira yao ilikuwa ni kufanya mauaji.”
“Unafikiri nani mlengwa wa mauaji hayo?”
“Sijui labda ni mimi.”
“Unakumbuka sura zao?”
“Ni vigumu kwani ilikuwa ni usiku wa giza.”
“Pole sana Father Mungu atakusaidia upone haraka.”
”Amen, nanyi pia ila nitawaombea wote waliofanya unyama huu Mungu awarudishe kwani awana tofauti na kipofu anayehitaji msaada wa kuongozwa hata bwana yetu Yesu Kristo amefundisha kusamehe kwani wengi wetu hatujui tutendalo.”
“Ni kweli lakini watu hawa wakikamatwa ni lazima wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.”
“Hiyo ndiyo hukumu ya sheria.”
“Unasema baada ya kukugundua watu hao si walevi ulifanya nini?”
“Kwa kweli nilichelewa nilihisi maumivu upande wa bega la kulia na kilichoendelea sikujua mpaka nilipojikuta nipo Hospitali.”
“Pole sana Father Gin ila tutakapokuwa na shida na wewe tutarudi tena.”
“Hakuna tatizo karibuni sana Bwana atawaongoza mfike salama.”
Anderson aliagana na Father Gin na kuelekea ofisini kwake akiwa hajapata mwanga wowote wa kumsaidia katika uchunguzi wake.
Njiani alijawa na mambo mengi na moja ni kifo cha Malaika Mweusi ilikuwa ni vigumu kukubaliana adui yake kuwa ndiye mhusika mkubwa wa mauaji yote. Lakini mauaji yalianza kabla ya kuanza upelelezi pia alijua kurudi nyuma ni sawasawa na kusaliti jeshi.
Mwezi ulikatika bila ya matukio yoyote ya mauaji, mji ulikuwa shwari lakini Anderson muda wote roho ilikuwa juu safari hii kuwa ni nani atakayefuata kufa. Vijana nao waliangaika huku na huko kutafuta taarifa zozote zitakazo wasaidia jeshi kuwatia mikononi watuhumiwa.
Kilichomshangaza juu ya taarifa za vitisho toka kwa mtu anayejiita mtetezi wa haki za binaadamu siri zote za vijana wake zilikuwa hadharani japo kila mmoja alirudi kwa wakati wake.
Alijiuliza ina maana muuaji amekuwa na uwezo gani wa kujua siri yao. Kidogo alianza kuuona ugumu wa kumtia mikononi muuaji, lakini hiyo haikumkatisha tamaa ya kuendelea na uchunguzi wake kwani hakuwa tayari kusalimu amri.
MWAKA MMOJA BAADAYE
Anderson akiwa amekwisha kata tama ya kumkamata muuaji wake, kipindi chote cha mwaka mzima kilikuwa shwari amani ilijirudia hapakuwa na taarifa za mauaji kitu kilichomfanya Anderson na vijana wake kulala usingizi. Siku zote alijipa matumaini adui yake amesitisha mauaji baada ya kuona yupo mbioni kutiwa nguvuni na askari wa upelelezi.
Taarifa zilizomfikia zilimtibua akili yake kuwa nyumba zote na vituo vya mafuta vinavyomilikiwa na tajiri mmoja wa kiarabu vimelipuliwa na mabomu na kusabaabisha hasara kubwa pamoja na kupoteza maisha ya watu zaidi ya mia moja akiwemo tajiri na familia yake.
Kazi aliiona ni nzito mbele yake kweli kimya kingi kilikuwa na mshindo mkubwa.
Kama kawaida vijana wake waliendelea na upelelezi wao naye alichukua maelezo muhimu ambayo aliyafanyia kazi.
Aliamua kurudi nyumbani kwani tukio lile lilimshtua sana hakutegemea, aliendesha gari lake hadi kwenye baa na kuagiza kinywaji baridi ili kutuliza akili yake ambayo nusura ipasue kichwa kutokana na mawazo.
Baada ya kuridhika na kinywaji chake aliingia ndani ya gari lake na kuondoka kuelekea nyumbani kujipumzisha akijua wazi kuwa hana ujanja wowote wa kumkwepa muuaji anayemfahamu kama kiganja cha mkono.
Alifika kwake majira ya saa tatu na nusu usiku alishangaa kukuta taa ndani inawaka huku kukiwa na sauti ya muziki ukilia. Alijiuliza ina maana wakati anaondoka asubuhi alisahau kuzima taa na bila kuzima redio.
Lakini hata hivyo akili yake ilishindana na mawazo yake kwani alikuwa na uhakika kuwa alipoondoka asubuhi alizima taa na kuzima redio. Baada ya kupaki gari lake alikwenda hadi mlangoni alitoa ufunguo na kufungua. Alipoingia sebuleni alishangaa hali aliyoikuta, ilikuwa na usafi wa hali ya juu alijiuliza ni nani aliyefanya usafi ule.
Kilichomshangaza zaidi ni kuwa funguo za nyumba alikuwa nazo yeye na marehemu Malaika Mweusi. Alijiuliza maswali mengi atakuwa nani, muziki wa taratibu uliendelea kulia chumbani mlango ulikuwa umeegeshwa tu aliusukuma na kuingia ndani.
Alishtuka kumkuta mwanamke amelala kitandani akiwa amevaa night dress alikuwa amempa mgongo amelala kifudifudi huku akiwa ameukumbatia mto alijiuliza kuwa huyu mwanamke atakuwa nani, tangu afariki Malaika Mweusi hakuwa na uhusiano na kiumbe chochote cha kike.
“Mmh!… atakuwa nani….mbona kama a..a..ana..fa..fanana…. hapana….. haiwezekani kuwa yeye sasa ni nani au jini nipige kelele…mmh! Ngoja,” alijikuta akiwaza vitu vingi.
Kwa ujasiri mkubwa alisogea kitandani kwa mwendo wa kunyata, alisimama pembeni ya kitanda huku akitetemeka na kumshika bega aliyelala ili amuulize. Pombe zote zilimtoka.
Anderson alipotaka kumgusa yule mwanamke aliyekuwa amelala kitandani roho ilisita. Alimwangalia kwanza usoni ili ajue ni nani hasa, huku akihema kwa hofu ya kutaka kujua ni nani, alizunguka upande wa pili wa kitanda yule mwanamke alipokuwa ameelekeza uso wake, baada ya kumuona alijikuta akipingana na mawazo yake.
''Mmmh haiwezekani...haiwezekani hawezi kuwa ni yeye huu lazima utakuwa ni mzimu wake...sijui nifanyaje.''
Akiwa katikati ya mawazo mara yule mwanamke alijigeuza na kufumbua macho yake yalikutana sawia na ya Anderson.
"Ooh! My sweet! Umerudi?! Karibu sana mpenzi wangu my husband to be'',alisema yule mwanamke ambaye hakuwa mwingine bali ni Malaika Mweusi.
''Hapana si wewe,'Anderson aling`aka.
''Kusema sio mimi una maana gani?''
''Wewe ni mzimu!''
''My sweet Ander mbona sikuelewi? Kwa nini unanifananisha na mzimu?''
''Wewe ni kivuli cha mzimu wa mpenzi wangu Malaika Mweusi!''
''Ni nani amekueleza kuwa nimekufa?''
''Hao waliokuua''
''Anderon mimi sijafa kama hao watu wanavyonizushia.”
''Kama hujafa ulikuwa wapi?!''
''Ni historia ndefu inahitaji nafasi zaidi ya kuzungumza, maadam tuko pamoja utanielewa vizuri na utajua baada ya kupigwa risasi na kutoroshwa hospitali nilikuwa wapi katika kipindi cha mwaka mzima.”
''Pamoja na maelezo yako yanalingana na ukweli lakini mimi bado sikuamini.”
''Naomba uniamini mimi si mzimu bali ni yule Malaika wako aliye hai na wala si kivuli cha mfu,” Malaika kwa sauti tamu.
Malaika Mweusi alinyanyuka kitandani alipokuwa amekaa na kumfuataAnderson amkumbatie lakini Anderson aliruka nyuma kwa hofu.
''Mpenzi usiniogope mimi ni yuleyule malaika wako.'' Alizungumza huku akimshika mabega Anderson na mkono mmoja akiuzungusha shingoni ili amkumbatie.
''Mpenzi hawakuwahi kuniua niliokolewa, onyesha furaha kuniona au ulipenda nife? Haya basi nitakunywa sumu mbele yako ili ushuhudie kifo changu na wala hutaona mzimu wangu.''
''Nina imani hutaona huo mzimu wangu unaoufikiria, nifanye nini ili unielewe? Mimi mzima,naona sina budi kuiaminisha akili yako kuwa mimi si mfu hadi utakapoiona maiti yangu mbele yako.”
Kauli ile ilimshitua Anderson, wakati huo Malaika Mweusi alikuwa akijitoa kifuani kwake. Kwa muda mfupi machozi yalilowesha shati la Anderson.
Hali ya Malaika Mweusi ilimchanganya ilibidi awe mpole kwani hali aliyoionyesha ilimtisha.
“Si hivyo Malaika wangu lilikuwa ni jambo la ajabu kwa mtu aliyejua umekufa kisha baada ya mwaka nikuone ukiwa hai.”
''Ni kweli kama ulielezwa hivyo lazima uwe na wasiwasi, ni kweli nilinusa mauti baada ya kupigwa risasi begani na watu walionipora gari yangu lakini Mungu mkubwa ameokoa maisha yangu.”
''Basi yameisha mpenzi wangu karibu sana jisikie kama uko kwako kwa mara nyingine tena,” Anderson aliyasema huku akimkumbatia Malaika Mweusi aliyejilaza kifuani.
***
Malaika Mweusi akiwa amerudi tena kwa mara nyingine baada ya mapumziko Anderson alitaka kujua ilikuwaje mpaka tukio lile likamkuta baada ya kuondoka bila ya kuaga tena katikati ya usiku mkubwa kama ule.
''Unajua mpenzi mapenzi yangu mazito kwako ndiyo yaliyosababisha yanikute yaliyonikuta.”
''Una maana gani kusema hivyo?”
''Nilikuwa nimelala nilipigiwa simu kuwa kama nitaendelea kulala humu ndani basi tutakufa wote nyumba ilikuwa imetegwa kwa bomu.”
''Ni nani aliyekupigia simu?''
“Kwa kweli simjui.”
“Wewe uliamini vipi na kwanini hukunieleza.”
''Alinitisha kuwa kama nitachelewa bomu lingelipuka muda uleule.”
“Uliamini vipi?”
''Kutokana na matukio yanayoendelea kutokea upande wako.”
''Kwa nini hukunieleza?”
“Lazima pangetokea ubishi kati ya mimi na wewe hivyo ingefanya tupoteze muda na kufanya nyumba yetu ilipuliwe na kupoteza maisha yetu hatuna ujanja zaidi ya mimi kuondoka.”
''Ee’he baada ya kuondoka nini lilitokea?”
''Inavyoonesha muuaji hataki kukudhuru bali kuiteketeza familia yako na watu waliokuzunguka shida yake ni kunitoa pale na kuniua.”
“Ikawaje baada ya kutoka kwangu.”
“Nikiwa naelekea kwangu mara gari mbili zilinipita na kusimama mbele yangu kitu kilichonifanya na mimi nisimame kwani hapakuwa na njia ya kupita.”
" Mara nilisikia milio ya risasi ikipigwa kwenye gari langu kabla sijaamua nini cha kufanya nilipigwa risasi ya bega. Kutokana na kuvuja damu nyingi pamoja na jeraha walijua nimeua ndipo waliponitoa garini na kunitupa chini na kuondoka na gari langu zaidi ya hapo sikujua nini kilichoendelea mpaka miezi miwili ndipo nilipopata fahamu na kujua hapa ni wapi.
“Nilijua nipo hospitali lakini sikujua ni wapi wakati huo nilikuwa napata huduma ya hali ya juu. Nilirudishwa kwenye hospital ya dini inayomilikiwa na shirika moja la kidini. Nilielezwa kuwa pale ni nchini Kenya niliokotwa kwenye gari lililokuwa lipo kama gari la wagonjwa baada ya lile gari kupata ajali na wahusika kukimbia.
“Baada ya kupona nilirudishwa Tanzania nilipofika tu niliamua kwenda kuishi nchini Marekani nilikuwa na mawazo mengi juu yako nilijua kuwa nilikuacha kwenye hali mbaya na maswali mengi kichwani mwangu.
“Kwa kweli niliamua kurudi nchini nakuamua kama kufa bora tufa wote ndio maana nimeamua kurudi mikononi mwako sitaogopa vitisho vyovyote nakuahidi mpenzi kwanzia leo hii nitakuwa kifuani kwako sitaachana na wewe hadi kifo,” Malaika alisema kwa hisia kali.
''Mpenzi kwanza pole kwa yote yaliyokukuta nina imani Mugu yuko ndani yako hivyo hutapungukiwa na kitu na maisha yako bado ni marefu Mungu atuhepushe na mabaya yote.”
Penzi la Anderson na Malaika Mweusi lizaliwa upya, tabia ya Malaika Mweusi ilikuwa ile ile ya kuondoka usiku wa manane. Baada ya muda walikwenda kumtembelea baba mzaa chema akiwa na kipenzi chake Malaika Mweusi.
Siku hiyo aliongea mengi pamoja na mipango ya harusi yao ambayo walipanga kufanya miezi mitatu ijayo. Pia siku ile ilihitimmishwa usiku na Malaika kumpa penzi zito Anderson lililomrusha akili na kujiuliza alikuwa wapi siku zote kumpa penzi tamu kama lile.
Hata asubuhi Malaika alipoamka ili amuage sauti yake ilitoka kivivu kwani mwili wake ulikuwa umechoka kwa patashika ya usiku. Baada ya Malaika kuondoka aliendelea kujilaza kwa uchovu.
***
MlLIO wa simu ulimshtua mkuu wa upelelezi aliyekuwa katikati ya usingizi, alipotupa macho yake kwenye saa ndogo iliyokuwa juu ya droo ya kitanda ilimuonyesha kuwa ni saa tisa na robo usiku ikiwa ni nusu saa tangu amsindikize Malaika Mweusi.
Aliinyanyua simu yake iliyokuwa pembeni ya mto aliokuwa ameulalia, ilimuonesha ni simu maalumu kutoka ofisini, mara nyingi simu hiyo hutumika kwa ajili ya dharura hasa pale panapotokea matatizo yasiyokuwa ya kawaida.
Alibofya kitufe cha kupokelea simu na kuzungumza kwa sauti ya uchovu kwani shughuli ya usiku haikuwa ya kitoto iliyongonyesha mwili. Mwanaume yeyote asingeweza kujizuia kutangaza ndoa kwa binti anayetoka katika familia ya kitajiri. Akizungumza kwa sauti ya kivivu :
“Ndiyo nakupata leta habari.”
“Afande mambo yameharibika .“
“Wapi tena?”

Itaendelea

No comments