Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 27


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Walipofika walikwenda hadi ndani, Colin alionekana mwenye kimuhemuhe cha kumwona mpenzi wake. Kwa vile alikuwa akikijua chumba cha Cecy aliingia moja kwa moja. Lakini chumbani kwake hakuwemo alitoka na kukutana na mama Cecy.
“Mama mpenzi wangu yupo wapi?” Colin aliuliza macho yamemtoka pima na presha juu.
SASA ENDELEA...
“Colin taratibu umefika utamuona, subiri,” mama Colin alisema huku akielekea chumba alicholazwa Cecy.
Alipakaribia alipogusa mlango alishtuka kusikia Cecy akimwita sauti ambayo ilipotea toka alipopata ajali iliyokuwa ikimwita.
“Ma..a..ma...ma..a..ma.”
Alisogea haraka kitandani na kuitikia.
“Abee mwanangu.”
“Nigeuze nimechoka kulala hivi?”
Mama Cecy aliona ule ni muujiza mkubwa kwake kwa vile siku zote mgonjwa alikuwa wa kulala bila kujitikisa wala kusema neno zaidi ya kutumbua macho tu bila kuyapepesa. Alimgeuza na kumlaza vizuri.
“Niwekee mto chini.”
Mama yake haraka alichukua mtu na kumwekea mwanaye.
“Mama ulikuwa wapi?”
“Nilikuwepo nje.”
“Mbona dada alisema ulitoka?”
“Nilifika dukani.”
“Mume wangu Colin yupo wapi?”
“Yupo sebuleni.”
“Ana fanya nini?”
“Ndiyo amefika sasa hivi.”
“Alikuwa wapi?”
“Kwao.”
Cecy kusikia Colin yupo sebuleni alitaka kunyanyuka na kuishia kukaa kitako na kurudi tena chini. Kitendo cha kujinyanyua peke yake yalikuwa maajabu mengine kwa mama Cecy ambaye alipiga ishara ya msalaba na kumsukuru Mungu kwa kile alichokionesha muda ule mbele yake.
“Asante Mungu... Asante baba... Asante kwa kila akifanyacho mbele ya macho yangu.”
“Mama,” Cecy alimwita mama yake.
“Abee.”
“Naomba niende kwa Colin.”
“Subiri.”
Mama Colin alitoka hadi sebuleni ambapo Colin alikuwa akizungumza na dada wa kazi juu ya hali ya Cecy. Alimdodosa na kuelezwa yote toka akipofika na hali aliyokuwa nayo na maajabu ya siku ile alipokuwa akimtengeneza kitandani na kushtuka kumsikilia akiiita jina la Colini na baadaye aliita mama yake.
Dada wa kazi alimweleza ametoka, ndipo alipoanza kumuuliza maswali ambayo alimjibu kwa vile mambo mengi alikuwa akiyaelewa. Baada ya mazungumzo na dakika ishirini Cecy aliomba kugeuzwa tofauti na siku za nyuma alikuwa wa kulala tu na kugeuzwa kwa kipindi.
“Kwa hiyo toka apate ajali ndiyo kazungumza leo?”
“Ndiyo najua hata mama ataona muujiza.”
“Mmh!” Colin aliguna na kujiuliza nini hatima ya mpenzi wake ikiwa sehemu inayotegemewa na watu wote imeshindwa. Ile kwake ilikuwa picha mbaya sana kwake na kukiona kifo cha Cecy kipo mbele. Aliamini yote aliyasababisha yeye alijikuta akitokwa na machozi ya uchungu.
“Colin baba,” Colin alishtuliwa na mama Cecy.
“Naam mama,” Colin aliitikia huku akinyanyua kichwa.
“Ha! Unalia nini tena?” mama Cecy alishtushwa na machozi ya Colin.
“Inauma.”
“Cecy anakuita.”
Colin bila kujibu alinyanyuka na kuelekea chumbani ambako alimkuta Cecy amelala kitandani mwili ukiwa umepururuka kwa ugonjwa.
“Cecy,” aliita kwa sauti huku akisogea kitandani na kumkumbatia mpenzi wake.
“Colin mume wangu,” Cecy alisema huku akijitahidi kumkumbatia mpenzi wake.
Ilikuwa ajabu nyingine Cecy kuweza kumkumbatia Colin kwa mwili uliobakia mifupa mitupu.
“Ni mimi Cecy mke wa maisha yangu.”
“Colin nifurahi kukuona mpenzi wangu japokuwa nina muda mrefu nilikuwa siwezi kuzungumza wala kujigeuza. Lakini kuja kwako kumekuwa dawa ya kupona kwangu. Hata nikifa sasa hivi moyo wangu utakuwa na furaha kwa vile nimekuona chakula cha nafsi yangu,” Cecy alisema kwa sauti ya chini.
“Ni kweli naamini Mungu alituumba kwa ajili yetu, siamini niliyoyasikia na niliyo kutana nayo leo,” Colin bado alikuwa kama yupo ndotoni.
“Ni Mungu tu mpenzi wangu.”
Siku ile Colin alishinda pale mpaka jioni pembeni ya Cecy, pamoja na yeye hali yake kuwa katika uangalizi lakini hali aliyomkuta nayo mpenzi wake aliamini amepona kabisa. Jioni daktari aliyempeleka India alipopitia kuangalia hali mgonjwa wake alishikwa na mshangao baada ya kukuta hali ya Cecy ina mabadiko makubwa.
“Mungu mkubwa siamini ninachokiona leo,” mama Cecy alisema huku akifuta machozi kwa kiganja cha mkono.
“Ni kweli Mungu katenda muujiza wake,”Colin alisema huku naye akifuta machozi.
“Jamani msinililie tena, kama nilikuwa nusu mfu kwa muda mrefu na leo nipo hivi, basi aminini nimepona,” Cecy alisema kwa kujiamini.
Siku ile kazi ya masaji aliifanya Colin huku akimpa moyo mpenzi wake kuwa atapona.
“Kweli nitaweza kutembea? Maana kwa hali ya kulala kitandani kama nyoka nimechoka.”
“Utapona tena na kusimama, nakuahidi baada ya kupona nakufanyia bonge la surprise.”
“Colin nawe kwa kunipa moyo, je nisipopona?”
“Ugonjwa utakuwa wetu sote.”
“Hutafuti mwanamke mwingine?”
“Cecy baada ya kukufungia moyoini mwangu ufunguo niliutupia baharini, mimi ni kipofu mbele yako. Wewe ndiye uliyekuwa mwanamke wa mwisho kuonwa na macho yangu. Siamini kama nitapenda tena katika maisha yangu kama tutatengana. “Nakupenda Cecy zaidi ya kupenda. Amini usiamini muda si mrefu utasimama na kutimiza ndoto yetu ya kuwa mke na mume.”
“Colin sikuwahi kumwamini mtu katika maisha yangu lakini wewe kwangu sina la kuongeza nakuamini mpenzi wangu. Mungu ana maajabu yake amani kila litendekalo lina makusudio yake.”
“Cecy Mungu waajabu wewe ni yule wa jana leo na kesho, Mungu alikupa azina ya busara na hekima ni mtaji mkubwa katika maisha yetu.”
“Asante kwa kulitambua hilo.”
Pamoja na Cecy kuwa mgonjwa aliweza kuzungumza mengi mpenzi wake mpaka ulipofika muda wa kumwacha apumzike. Colin hakutoka alilala pembeni ya mpenzi wake. Daktari Mariam alishangazwa na hali aliyomkuta nayo Cecy ulikuwa muujiza mkubwa maishani mwake.
“Kweli Mungu mkubwa hutenda pasipo mtu kutegemea, siamini... siamini kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu wetu,” dokta Mariam Shaka alichanganyiwa na hali aliyomkuta nayo Cecy.
Dokta Mariam alisema baada ya kumwona Cecy akijigeuza kitandani na kumwita mpenzi wake.
“Colin.”
“Naam mpenzi.”
“Nataka kwenda msalani.”
Colin alimnyanyua na kumkalisha kisha aliomba chombo cha kujisaidia na kupewa, kazi yote ya kumhudumia mpenzi wake alifanya mwenyewe. Baada ya kumwogesha alimrudisha kitandani. Baada ya huduma zote dokta Mariam alimchunguza ilionesha kila kiungo kimepata ufahamu.
Kila alipomminywa kwa nguvu alipiga kelele, ile ilikuwa dalili nzuri kuonesha mwili mzima umeisharudisha mawasiliano. Baada ya kufanyiwa uchunguzi alikalishwa kitako na kuelezwa aliyekuwepo mbele yake ni dokta Mariam Shaka dokta aliyekwenda naye India kwa siku zote alizokuwa naye huko katika kukuchua mwili.
“Asante dada yangu Mungu atakulipa,” Cecy alisema huku machozi yakimtoka.
“Usijali, Mungu mkubwa naamini muda si mrefu utasimama tena, hatua ya leo ni kubwa kweli kila lililo zito kwa mwanadamu kwa Mungu ni jepesi.”
“Hakika,” alisema mama Cecy.
Colin alikuwa karibu muda wote kuonesha jinsi gani anavyomjali mpenzi wake ambaye aliamini ni mwanamke wa maisha yake. Siku hiyo kila kitu Colin aliomba amfanyie mpenzi wake. Ilikuwa faraja kubwa kwa Cecy ambaye pamoja na kuwa bado mgonjwa lakini ukaribu wa kipenzi chake uliongeza faraja moyoni mwake.
***
Upande wa pili baada ya Colin kuondoka na mama Cecy, Mage hakuondoka alibakia kumsubiri Colin kwa kuamini kutokana na maelezo ya mama yake Cecy alikuwa nusu mfu mtu wa kulala tu. Hivyo asingekaa muda mrefu angerudi mapema na kumkuta, alitumia muda mwingi kuangalia mikanda ya video.
Mama Colin alirudi saa mbili kasoro usiku na kumkuta Mage peke yake amejaa tele sebuleni. Mage alipomwona mama mkwe zilipendwa alinyanyuka na kumpokea.
“Wawooo, karibu mama.”
“Asante mwangu, za kushinda?”
“Mmh! Nzuri.”
“Mbona kwanza umeguna kabla ya kujibu.”
“Hamna mama.”
“Mwenzio yupo wapi?”
“Ametoka.”
“Ametoka! Kaenda wapi?”
“Kumwona mgonjwa.”
“Mgonjwa! Mgongwa gani?”
“Cecy.”
“Cecy! Nani kamwambia kama Cecy yupo?” mama Colin alishtuka kusikia habari zile.
Itaendelea

No comments