Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 28


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500
ILIPOISHIA:
Walikwenda kwa mama Cecy ambako kulikuwa na nyumba ya kisasa iliyojengwa na Colin kwa ajili ya mpenzi wake. Walipofika Mage hakushuka kwenye gari na mama Colin aliingia ndani, sebuleni kulikuwa na mama Cecy aliyekuwa ametulia macho yake yakiwa kwenye runinga.
SASA ENDELEA...
Alipomuona anaingia alihamisha macho kwenye runinga na kumtazama mlangoni alikuta ni mama Colin. Alinyanyuka alipokuwa amekaa na kwenda kumpokea.
“Karibu dada.”
“Asante,” mama Colin alijibu kwa sauti ya chini huku akificha hasira zake juu ya kitendo cha mzazi mwenzie kwenda kwake na kufanya mwanaye amchukie kwa kumficha kuwemo kwa mpenzi wake nchini.
“Karibu, Vipi hujafika nyumbani?” Mama Cecy alimshangaa usiku ule wakati alisema siku ile hawataonana.
“Colin yupo wapi?” mama Colin aliuliza kwa sauti kali kidogo.
“Dada hata salamu unakimbilia kumuulizia Colin?”
“Salamu si muhimu kama kujua hali ya mwanangu.”
“Mwanao hajambo.”
“Sitaki kusikia hajambo bali kumwona yupo au ameondoka?”
“Yupo chumbani na mchumba wake.”
“Chumbani? Anafanya nini?”
“Mama Colin ni swali gani hilo, ina maana chumbani kwangu kuna mzoga?” mama Cecy alijibu kwa hasira.
“Siyo hivyo dada, si unajua Colin bado mgonjwa mpaka sasa sijui yupo wapi.”
“Colin na Cecy nani mgonjwa na ugonjwa mwanangu kautoa wapi, mbona tumekwenda vizuri tunataka kuharibu mwisho?”
“Basi samahani dada najua Cecy anaumwa, lakini sijui Colin yupo wapi maana nilimwacha nyumbani amesikia amekuja kumwona mchumba wake.”
“Nimekujibu nini?”
“Sawa ngoja nikamwone.”
Mama Colin alielekea chumbani kwa mgonjwa akiamini atamkuta mwanaye pembeni ya kitanda huku akiumizwa na hali ya mpenzi wake aliye katika hali unusu mfu. Alipofika alipigwa na butwaa kumkuta Colin akimlisha Cecy matunda.
“Ha!” mama Colin alijikuta akipiga ukelele wa mshtuko.
“Aah! Mama karibu, Mungu mkubwa kuja leo mpenzi wangu kanyanyuka kama ningekuja mapema sasa hivi angekuwa hajambo kabisa,” japo yalionekana maneno ya kawaida lakini yalikuwa kama mkuki moyoni mwa mama Colin.
“Ha! Kweli Mungu mkubwa Cecy umenyanyuka mama!” mama Colin hakuamini alichokiona mbele yake.
“Karibu mama mkwe, sina cha kukulipa ina namuomba Mungu anipe afya niweze kukulea mama yangu katika maisha yangu yote. Umeweza kupigania maisha yangu kwa hali na mali. Naamini kabisa kwa Mungu hakuna kinachoshindikana, karibu mkwe,” Cecy alisema huku akijiweka vizuri.
“Asante mkwe wangu, Mungu ni muujiza ninachokiona mbele yangu ni kazi ya Bwana aliyotenda.”
Mama Colin alikwenda kumkumbatia Cecy ambaye alikuwa amepururuka na kubaki mifupa mitupu. Mama Cecy naye alikuwa amefika hakutia neno zaidi ya kukaa kimya akimwangalia mzazi mwenzie.
“Jamani leo ni katika siku ambazo nimepata furaha ya ajabu, nakuahidi kuipigania afya ya Cecy kwa gharama yoyote ili kuhakikisha anarudi katika hali yake ya zamani,” alisema mama Colin.
“Asante mkwe sina cha kukulipa bali kukuonesha mapenzi ya dhati yasiyo na chembe ya unafiki.”
“Asante mkwe wangu,” mama Colin alijikuta akitokwa na machozi kwa maneno mazito ya Cecy ambaye alipoteza kauli na viungo vya mwili kufanya kazi kwa zaidi ya miezi sita.
“Jamani nina imani Mungu ni mkubwa ameweza kutusimamia kwa hiyo tumshukuru kwa pamoja kwa kuweza kutenda juu yangu,” Cecy alisema huku akitaka kuteremka kitandani.
“Baki kitandani tutaomba ukiwa hapahapa kitandani,” Colin alimzuia mpenzi wake.
“Naomba niteremke ili nipige magoti pia kwa kauli yangu kufunguka naomba niongoze maombi kumshukuru Mungu.”
Baada ya wote kupiga magoti na kufumba macho Cecy alianza kuomba:
“Asante baba Mungu kwa wema na utukufu wako, umekuwa nami muda wote wa maradhi na mateso yangu mazito ambayo kila mwanadamu alikata tamaa lakini baba ulikuwa nami muda wote.
“Baba sina cha kukulipa zaidi ya kukuabudu kwa kufuata yote unayotaka tuyafanye na kuyaacha yote uliotukataza. Baba rudisha furaha mioyoni mwa wote waliopoteza matumaini na kuwafanyia wasiyo yategemea rudisha furaha kati nyumba yetu iliyopotea kwa muda mrefu tupe afya njema.
“Baba kila aliyetokwa na machozi kwa mayeso yetu mfute na umpe furaha kama kuna aliyefurahia matatizo yetu baba msamehe kwa vile hajui atendalo. Umetuumba wanadamu kwa udongo ulio safi basi tupe mioyo yetu upendo tupendani tuoneane huruma na kuombeana mazuri.
“Asante Baba kwa kuninyanyua leo, asante kwa kurudisha furaha iliyitoweka kwa muda mrefu katika familia zetu.Walipe mara mia wote waliotoa kwa ajili ya matatizo yetu. Baba yaliyotokea ni majaribu tupe imani ya kusimama upande wako na usimpe nafasi adui shetani kutupotosha.
“Baba timiza ndoto yetu ya mimi kuwa mke halali wa Colin, Baba Mungu nashukuru kwa kunichagulia mume mwema mwenye mapenzi ya dhati, nami namwahidi kuwa mke mwema katika siku za pumzi zangu. Simamia ndoa yetu ondoa kila jicho la hasada roho chafu za chuki, uongo na uadui kwa jina la mwanao Yesu Kristo aliye hai, Ameni.”
“Ameni,” waliitikia pamoja huku kila mmoja akifuta machozi kutokana na maombi mazito aliyoporomoshwa na Cecy.
“Naombeni maji,” Cecy aliomba maji baada ya kuomba kwa muda mrefu na kuvunjwa jasho kama maji, kutokwa na jasho jingi ulikuwa muujiza mwingine kwa mama Cecy baada ya kutotoka jasho jingi kwa zaidi ya miezi sita.
Alipatiwa maji na kuomba kupumzika, Colin alimpandisha kitandani na kumfunika shuka.
“Colin mpenzi napumzika kidogo ila usiondoke wewe ndiyo furaha yangu.”
“Sawa mpenzi.”
Walimwacha Cecy amelala na kutoka nje kwa ajili ya mazungumzo.
“Jamani kuna nini kimefanyika ambacho mimi sikijui?” mama Colin aliuliza.
“Hakuna kilichofanyika na muujiza wa Mungu, wakati narudi nilisikia Cecy ananiita nilipoingia nilishtuka kumwona akiniita. Nilipomsogelea sikiamini kumwona mwanangu katika hali ile kwani niliisha kata tamaa.”
“Kweli nimeamini muujiza wa Mungu upo,” alisema mama Colin.
“Ni kweli.”
“Sasa kwa vile nilikuwa nimekuja ghafla wacha nikapumzike pia tumwache mgonjwa apumzike ili kesho tujue tutafanya nini.”
“Dokta Mariam amesema lazima tumpeleke hospitali akafanyiwe vipimo.”
“Hakuna tatizo, Colin baba,” alimgeukia mwanaye.
“Naam mama”
”Itaidi tuondoke ili ukapumzike kwa vile nawe hali yako haijatengemaa vizuri.”
“Mama mimi nimepona kabisa mgonjwa ni Cecy na nipo hapa kwa ajili ya kuhudumia kwa kila kitu.”
“Sawa, lakini twende nyumbani tutakuja kesho.”
“Mama naomba unisamehe, leo siondoki nitalala na mpenzi wangu.”
“Mmh! Sawa.”
“Nikutakie usiku mwema.”
Mama Colin alimkumbatia mwanaye kisha alimuaga kuelekea alipopaki gari. Alimkuta Mage amesinzia baada ya kumsibiri kwa muda mrefu, alipofika alimwamsha.
“Mage pole kwa kukuweka.”
“Isijali mama mkwe, vipi mbona umechelewa Colin ameisha ondoka?”
“Yupo.”
“Mbona umemwacha?”
Mama Colin alimweleza Mage yote aliyoyakuta na kumfanya asindwe kuamini na kujikuta akiuliza:
“Mama unayosema ni kweli?” Mage hakuamini.
“Kweli kabisa, yaani nilichokiona mbele yangu ni muujiza Cecy amenyanyuka tena anaonekana kama mtu aliyepata nafuu wiki nzima.”
“Mmh! Nimekwisha!” Mage alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
“Kwa nini unasema hivyo?” mama Colin alishtuka.
“Mama kweli Colin atanioa?”
“Sikudanganyi, Colin anampenda sana Cecy, hakuna kiumbe kitakacho mbadili mawazo, yaani nimemkuta kama mwenda wazimu sijui Cecy angekufa mwanangu angekuwaje.”
“Mmh! Sawa,” Mage alisema huku nguvu zikimwisha na kujikuta akijilaza kwenye usukani badala ya kuondoa gari.
“Vipi mbona hivyo?”
“Mama kupona kwa Cecy ni pigo zito moyoni mwangu, hapa nilipo sina hata nguvu za kuendesha gari. Naomba mama yangu uendeshe naweza kugonga.”
Itaendelea

No comments