Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: 30


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Nilichokiwaza mimi ni kuhusiana matukio yote hivyo naamini huku tutafunga ndoa isiyo na starehe ambayo itakuwa na baraka ya wazazi wa pande zote. Kwa hiyo wazazi wetu tunaomba mkubali ombi letu ili tukirudi Tanzani tuwe tayari mke na mume. Kuhusu sherehe tutaifanya tukijipanga.”
“Mmh! Colin we ulikuwa unasemaje?” mama Colin alimuuliza mwanaye.
“Mi namuunga mkono mpenzi wangu amekuwa na jicho la tatu ambalo wote tulikuwa hatuna.”
SASA ENDELEA...
“Mipango ya harusi mmeisha andikisha kanisani?”
“Tumeisha kamilisha kila kitu mlikuwa mkisubiliwa ninyi tu.”
“Basi hakuna tatizo kwa vile jambo ni la heri tutakuwa pamoja, sijui dada unasemaje?” mama Colin alimuuliza mama Cecy.
“Hata mimi naungana na wewe.”
Wazazi hawakuwa na pingamizi lolote walikubaliana kusimamia ndoa ya watoto wao ili wakirudi nyumbani Tanzania wajipange kwa sherehe.
***
Baada ya taratibu zote kufuatwa Colin na Cecy alifunga ndoa katika kanisa la Roman Cathotic la Mtakatifu Augustine jijini Port Elizabeth Afrika ya Kusini. Ndoa iliyokuwa na watu wachache lakini ilikuwa ni furaha isiyo kifani moyoni mwa Cecy pale alikupoulizwa kama anakubali kuwa mke halali wa Colin katika shida na raha pia Colin kukubali kuwa Cecy ni mkewe katika shida na raha na kifo ndicho kitakacho watenganisha.
Baada ya kufunga ndoa waliondoka na kurudi kwenye hoteli waliyofikia na jioni ya siku ile ilifanyika sherehe ndogo katika ufukwe wa hoteli ya The Beach na baadhi ya jamaa zao walikuwa katika mji wa Port Elizabeth.
Japo ilikuwa sherehe ndogo iliyoanzia ufukweni na kuishi kwenye ukumbi wa hoteli ile. Ilikuwa sherehe yenye kufana kila aliyekuwepo alifurahia sherehe ile ambayo watu walikunywa na kusaza. Baada ya shehere maharusi waliingia ndani ya chumba cha VIP ambacho walikichukua mahususi kwa ajili ya fungate.
Siku ya tatu mama Colin na Cecy walirudi Tanzania na kuwaacha watoto wao wakila fungate. Wakiwa ndani ya ndege kila mtu alimshukuru Mungu kwa kutenda ambalo lililoonekana kwa akili ya kibinadamu limeshindikana.
“Yaani unajua dada mpaka muda huu siamini kama nimeweza kuiona harusi ya Cecy na Colin,” alisema mama Cecy.
“Si wewe yaani mpaka sasa naamini Mungu akiamua kitenda hutenda jambo.”
“Kwangu naona kama muujiza siamini... siamini kama kuna siku nitamuona mwanangu akitabasamu lazima nimshukuru Mungu asante Mungu kwa kila unitendealo.”
“Kweli naamini Colin na Cecy wanapendana mapenzi ya dhati.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Mwanzo niliamini labda Cecy anampenda mwanangu kwa ajili ya utajiri wake lakini alinionesha hamuhitaji kwa ajili ya mali zake bali mapenzi ya dhati, Pia Colin alinihakikishia hataoa mwanamke mwingine zaidi ya Cecy na alikuwa radhi kuioa maiti na Cecy kama angekufa.”
“Ni jambo la kushukuru watoto wetu kupendana ni mwanzo wa kutengeneza familia yenye upendo.”
Wazazi wakiwa wanabadilisha mawazo ndani ya ndege jijini Port Elizabeth ndani ya chumba cha VIP katika hoteli ya The Beach, Cecy alikuwa akimuangalia Colin kwa muda mrefu na kuanza kutokwa na machozi kitu kilichomshtua Colin na kuhoji.
“Vipi mpenzi wangu mbona unalia?”
Cecy hakujibu machozi yaliendelea kumtoka kama maji na kuzidi kumweka mumewe kwenye wakati mgumu.
“Mke wangu kuna nini tena? Leo ni siku ya furaha baada ya kufika nusu ya safari yetu kutokana na mitihani mingi. Badala ya kufurahi mke wangu unalia, kipi kimekusibu mpenzi wangu au kama kuna nilichokukosea nipo radhi kwa adhabu yoyote,” Colin alisema huku akisogeza mbele ya Cecy kumpigia magoti.
Kabla hajapiga magoti Cecy alikurupuka alipokuwa amekaa na kumuwahi mpenzi na kumvamia na kuwafanya wote waanguke mweleka.
“Colin machozi haya si maumivu bali furaha iliyopitiza nashindwa... nashindwa mume kuvumilia. Siamini kama ndoto niliyoota mchana imekuwa kweli, leo hii mimi ni mke wa Colin, asante Mungu asante kwa kila jambo sitaacha kukushukuru usiku na mchana siku zote za pumzi zangu.”
“Cecy mpenzi wangu nilikupenda toka siku ya kwanza nilipokuona lakini nilikuta chaguo lingine la mama yangu. Lakini amini uliingia moyoni mwangu toka siku ya kwanza jicho langu lilipokuona. Naamini kabisa jicho la mwanzo lilikuwa sahihi kuliko mtu niliyechaguliwa.
“Umekuwa kiumbe wa ajabu ambaye siwezi kumfananisha na kiumbe wa kawaida, umewaze kunipigania japo katika hali yako ya umaskini, lakini ulikuwa radhi ukose kitu chochote chini ya jua ili unipate mimi. Nakuahidi lile jicho lililokuona mara ya kwanza na kukufungulia mlango moyoni mwangu ndilo hilohilo linalokuona ua zuri lililochanua mbele yangu.
“Wewe ni mwanamke niliyepewa zawadi na Mungu, nimeamini bundi hawezi kukaa kundi moja na njiwa.”
“Una maanisha nini?”
“Mage hakuwa njiwa katika safari ya maisha yangu, naamini mbeleni lazima angenitenda, Mungu alilijua hilo ndiyo maana alikuleta wewe wakili wa moyo wangu bila wewe nina wasiwasi ningekuwa nimeisha kufa kwa vile aliuhukumu moyo wangu kifo, lakini umeweza kuutoa moyo wangu kwenye adhabu nzito niliyopewa na Mage sijui usingekuwepo ingekuwaje?”
“Colin niliyafuatilia maisha yako kila hatua ni moyo wa upendo ulinisukuma, niliamini kabisa wewe ndiye mume wangu. Nilikupenda sitachoka kukupenda kwa vile kila siku unakuwa kiumbe kipya moyoni mwangu.”
“Hata mimi mke wangu.”
Walikumbatiana kwa furaha kuifurahi fungate yao iliyokuwa na raha ya aina yake baada ya safari ndefu yenye misukosuko.
****
Nchini Tanzani taarifa za mama Colin kwenda afrika ya kusini zilimshtua sana Mage, alijikuta akiwaza huenda Cecy amezidiwa na hivyo amekwenda kuangalia hali yake inavyoendelea. Aliomba kama ni hivyo basi akute Cecy amediziwa na kufariki dunia, lakini bado alibakia na akiba ya mpango wake wa kumfanyia kitu kibaya Cecy kama atakuwa hai ili kuhakikisha ndoa haifungwi.
Aliwaandaa watu kwa ajili ya kufanya utekaji na kumfanyia vitendo vichafu, walikubalia kuifanya kazi baada ya Cecy kurudi nchini kutoka Afrika ya kusini. Vijana walimuahidi kumfanyia kazi vizuri kwa vile walikuwa na uzoefu wa kazi zile. Aliwahidi kuwaongeza mara mbili ya malipo waliyokubaliana kama watafanikisha kazi ile.
“Sister mbona utakubali kazi yetu, hata ungetaka kichwa chake tungekuletea,” alijisifia wakora.
“Sasa damu yenye virusi tutaipata wapi?”
“Hilo dogo mbona kuna mshkaji wetu mmoja ameumia tutachukua damu yake kidogo na kumdunga mtu wako.”
“Nawaamini msiniangushe.”
“Hatujawahi kuharibu kazi hata siku moja, hata kama kuna kazi nyingine we tupe tukufanyie tena tutakupunguzia kwa vile wewe mtu wetu.”
“Picha nimewapa?”
“Ndiyo sister, tumemcheki vizuri mbona huyu amekwisha.”
Baada ya mipango yake kwenda sawa Mage alijipanga kuhakikisha Colin hamuoi Cecy, alipanga baada ya tukio hilo la kumteka Cecy na kumduga damu yenye virusi atumie laini mpya ya simu na kumtumia picha za Cecy akibakwa na ujumbe kuwa ameathirika.
Baada kuwaza yote yale alitabasamu na kuamini kila kitu kipo vizuri anachosubiri utekelezaji tu. Akiwa amejipumzisha alipata taarifa toka kwa mama yake kuwa mama Colin amerudi toka Afrika ya kusini.
“He! Mbona hajakaa sana, karudi na Colin?”
“Hapana karudi peke yake.”
“Mbona karudi peke yake kwani alikwenda kufanya nini?”
“Kwa kweli sikumuuza.”
Mage hakutaka kuuliza swali lingine alinyanyuka na kutoka kuelekea kwa mama Colin kutaka kujua sababu ya safari yake ya Afrika ya kusini na kwa sababu gani hakurudi na Colin. Alitoka hadi kwenye gari na kuchukua aina ya Toyota Harrie na kuelekea kwa mama Colin, aliendesha kwa kasi ili kuwahi kupata taarifa.
Alipofika alipaki gari kwenye maegesho, kwa shauku ya kuyajua ya Afrika ya kusini hakufunga hata mlango wa gari. Alitembea mwendo wa haraka hadi mlangoni wa kuiingia ndani. Alibisha hodi na kukaribishwa na mama Colin aliyekuwa amekaa na mama Cecy wakiangalia mkanda wa video huku wakinywa vinywaji.
“Karibu ma mkwe,” mama Colin alisema.
“A..a..sa..”
Alishindwa kumalizia sentesi ambayo ilikatikia njiani baada ya jicho lake kutua kwenye kioo cha runinga alichokiona mbele yake. Ilikuwa vigumu kuamini kama ni kweli au alikuwa akiangalia ni maigizo. Alimuona Cecy katika vazi la harusi akiwa na Colin katika suti ya gharama, alikaza macho kama yanataka kudondoka.
“Maa..a..ma.”
“Vipi mkwe?”
“Huyu si Colin?” alisema huku akinyoosha kidole.
“Ndiyo.”
“Na..na..huyu si Cecy?”
“Ndiyo.”
“Hii si..si..harusi?”
“Ndiyo.”
“Wameoana lini?”
“Leo ni siku ya nne toka waoane na sisi tumerudi jana usiku kutoka huko.”
“Mmh! Si kweli, haya ni maigizo tu ili kuniumiza roho.”
“Kukuimiza roho ili iweje? Na picha zao hizi hapa.”
Mage alizichukua albam akiwa haamini anachoambiwa, aliifungua na kuanza kuangalia picha mojamoja huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio. Kila ukurasa alioufunua uliupasua moyo wake alijikuta machozi yamefunika macho na kushindwa kuona picha.
Alihisi mapigo ya moyo yakiongeza kasi pumzi zikamjaa na kutoka kwa shida, kiza kizito kilitanda mbele yake kilichoendelea hakukijua. Mage alianguka kama mzigo akiwa amepoteza fahamu, kitendo kile kiliwashtua sana. Walijikuta wakitaharuki ilibidi wamchukue na kumkimbiza hospitali kisha kumjulisha mama yake.
ITAENDELEA

No comments