Header Ads

HADITHI: WAKILI WA MOYO SEHEMU: MWISHO -31


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIP{OISHIA:
Alihisi mapigo ya moyo yakiongeza kasi pumzi zikamjaa na kutoka kwa shida, kiza kizito kilitanda mbele yake kilichoendelea hakukijua. Mage alianguka kama mzigo akiwa amepoteza fahamu, kitendo kile kiliwashtua sana. Walijikuta wakitaharuki ilibidi wamchukue na kumkimbiza hospitali kisha kumjulisha mama yake.
SASA ENDELEA...
Mama Colin alijua kilichokuwa kikiendelea aliamini Mage alipatwa na mshtuko baada ya kuona Colin amemuoa Cecy. Mama yake alifika mara moja hospitali na kukuta tayari mwanaye kaingizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Baada ya vipimo ilionesha alipatwa na mshtuko na kusababisha mishipa ya damu kupasuka na kusababisha apooze upande mmoja.
Kwa vile huduma ile haikuwepo alitakiwa kupelekwa Afrika ya kusini haraka kwani walisema ugonjwa ule ikiwa kupata matibabu ya haraka anaweza kupona. Siku ya pili alipelekwa Afrika ya kusini kwa ajili ya matibabu ya haraka katika hospitali ya Mil park.
***
Mage alisafiri na mama yake mpaka Afrika ya kusini katika hospitali ya Milpark iliyopo katika jiji la Johannesburg. Alipokelewa na kuanzishiwa matibabu mara moja, madaktari walifanikiwa kufanya upasuaji uliochukua saa tatu kuondoa damu zilizovuja baada ya mshipa kupasuka.
Baada ya upasuaji kwenda vizuri alirudishwa kwenye chumba maalumu chini ya uangalizi ya madaktari bingwa. Taarifa za Mage kuumwa zilimfikia Colin aliyekuwa katika mji wa Port Elizabeth.
“Mpenzi nasikia Mage anaumwa ameletwa hospitali ya Milpark, Johannesburg,” Colin alimwambia Cecy aliyekuwa akicheza game kwenye Ipad.
“Maskini mke mwenzangu nini kimemsibu?”
“Nasikia kapata mshtuko baada ya kuona video na picha zetu za harusi.”
“Maskini, Mage alikuwa kama fisi aliyeamini siku moja mwanadamu atadondosha mkono.”
“Namshangaa kutaka kufa wakati anajua mimi ni wa nani.”
“Wa Cecy.”
“Najiuliza bila Cecy, Colin leo ningekuwa wapi?”
“Anajua Mungu si sisi wanadamu ambao hupokea matokeo.”
“Asante mpenzi wangu kwa kuyaokoa maisha yangu, huwezi kuamini baada ya kuachwa ghafla na Mage nilijaa mawazo mengi na kujiona nina mapungufu.”
“Asante niseme mimi uliyoyapa majibu mswali yangu kama kuna siku maji yatapanda mlima.”
“Nina imani huu ni muda muafaka wa ku-renew mkataba wako na makapuni yote ya mavazi ya majarida. Waliniuliza afya yako nikawaambia hujambo kabisa hivyo wameomba tupange siku ya wao kuja ili uendelee na kazi yako.”
“Mpenzi moyoni mwangu nimepanga kwanza nikae na mume wangu kwa mwaka mzima ndipo nifanye kazi nyingine.”
“Cecy si tumeishafinga ndoa wasiwasi wako nini?”
“Sijaifaidi raha ya ndoa kazi ipo tu, kama wameweza kunisubiri muda wote waendelee kusubiri.”
“Makubaliano ya awali ni kwamba tutakuwa tupo pamoja katika kazi zako zote kwa vile mimi ndiye meneja wako.”
“Mmh! Kama hivyo sawa.”
“Mmh! Bado tu una wasiwasi wa kuibiwa?” Colin alimtania.
“Si umesikia mtu kataka kufa baada ya kusikia umeoa, vipi niwe mbali nawe? Nikisikia upo na Mage ningekufa mimi.”
***
Baada ya kuwajulisha siku ya kuonana kampuni ya Ebony walifika katika hoteli ya The Beach na kuingia mkataba mpya wa miaka miwili. Pia kampuni ya maonesho ya mavazi na urembo nayo iliingia mkataba mpya na makubaliano ya kuanza kazi baada ya miezi mitatu.
Mage naye alitoka hospitali akiwa na afya njema, mama yake alipotaka kujua sababu ya mshtuko ule, alimweleza ukweli kuwa baada ya kuona harusi ya Colin na Cecy alipata mshtuko wa ajabu kilichoendelea hakujua mpaka alipozindukia Hospitali Muhimbili akiwa amepooza upande mmoja.
“Unasema nani kaoa? Sijakuelewa vizuri,” mama Mage alishtuka kusikia Colin kaoa.
“Colin, mama.”
“Muongo! Hiyo harusi imefanyika lini mbona sina habari?”
“Ilikuwa ya siri imefanyikiwa Afrika ya kusini.”
“Kama ni kweli basi mwanangu achana na mawazo ya Colin, Mungu atakupa mume wa kweli.”
“Mama hata mimi nimejifirikia hivyo lakini Colin nilimpenda sana.”
“Si kweli, ulimpenda Hans, Colin anapendwa na Cecy kwa hiyo waache na ndoa yao.”
“Ndiyo mama, japo nilikuwa na nia mbaya kwa Cecy, lakini kuanzia sasa sitashughulika na Colin wala Cecy nami nasubiri ndoa yangu.”
“Hilo ndilo neno la kujasiri mwanangu.”
Baada ya Cecy kumaliza mapumziko alianza kazi rasmi, mwaka mmoja baadaye alishika ujauzito na kusubiri muda wa kujifungua. Mage naye alipata mchumba na mambo yalikwenda kama yalivyopangwa. Siku ya harusi akiwa anajiandaa kwenda kanisani anapata habari zilizo mshtua moyo na kufanya apoteze fahamu kuwa mpenzi wake Hans yupo huru baada ya kushinda rufaa yake.
MWISHO

1 comment: