Header Ads

Huu mgogoro wa Wabunge na Naibu Spika utatuliwe haraka

 
Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.
Tumsifu Mungu kwa kutupa uhai na afya tele leo. Baada ya kusema hayo niingie moja kwa moja katika mada ya leo kuhusu mgogoro unaoendelea kufukuta ndani ya bunge letu tukufu hivi sasa.
Mgogoro huo ni msuguano kati ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na wawakilishi wa wananchi wa kambi ya upinzani. Kiini cha mtafaruku huo kimeelezwa kuwa naibu spika amekuwa akitumia vibaya kanuni ili kuwanyima haki, uhuru na demokrasia wabunge wa kambi hiyo.
Msuguano huo umekuwa mkubwa na si wa kuuangalia na badala yake nashauri vikao vya uongozi wa bunge vifanyike au Spika Job Ndugai aingilie ili kuondoa tofauti za pande mbili hizo.
Vikao hivyo vikifanyika viangalie malalamiko ya wabunge kama kweli wao wanaambiwa wanatumia lugha ya kuudhi ama la na kama wana hoja kuhusu madai yao ya kung’ang’ania Bunge kuoneshwa ‘laivu’, haya yalikuwa yafanyike haraka.
Nasikitika kusema kwamba mpaka naandika maoni haya hayo hayajafanyika na matokeo yake wabunge wa upinzani sasa wamekuwa wakitoka bungeni kila anapoingia Dk. Tulia kuendesha Bunge.
Mtindo huo umewafanya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba mwongozo wa spika kwamba wabunge hao wa upinzani wanaosusia vikao wawe wakikatwa posho yao ya siku, mwongozo ambao awali ulijibiwa na Dk. Tulia kuwa haiwezekani mpaka sheria zibadilishwe lakini mwishoni mwa wiki iliyopita alibadili msimamo huo, akatoa uamuzi wa kukata posho za wanaosusia.
Sakata zima Dk.Tulia ndiye anayelalamikiwa na wasusiaji vikao na ndiye aliyepokea hoja za wabunge wa CCM namna ya kuwashughulikia wapinzani na ndiye aliyetoa hukumu ya kukatwa posho wapinzani.
Kwa maoni yangu nadhani haki ya msingi (matural justice), haikuzingatiwa.
Haki ya msingi inataka walalamikaji kupewa haki ya kusikilizwa malalamiko yao pili uamuzi kuhusu hoja zao ufanywe na mtu huru ambaye hahusiki na tatizo, tatu uamuzi utolewe kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na uwe wazi.
Nikirudisha nyuma mawazo yangu, nadiriki kusema kwamba maspika waliopita, Samwel Sitta na Pius Msekwa katika uongozi wao walikuwa wakijali sana haki na wamekuwa tochi na kielelezo katika uendeshaji wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Kwa mfano, kuna wakati Spika Pius Msekwa ilipokuwa ikifika zamu ya kujadili Wizara ya Afya, iliyokuwa ikiongozwa na mkewe, Anna Abdallah, alikuwa anakaa kando na kiti kuongozwa na mtu mwingine na hata Samwel Sitta alipokuwa Spika ilipokuwa inafika zamu ya mjadala wa Wizara ya Elimu ambayo ilikuwa ikiongozwa na mkewe, Magreth Sitta, alikuwa anakaa kando.
Wote kwa nyakati tofauti walikuwa wakisema wanafanya hivyo ili kuwapa uhuru zaidi wabunge kuzijadili wizara hizo kwa uwazi na bila woga kwa kuwa wanaoziongoza ni wake zao.
Kutokana na mifano hiyo, nashauri kiti cha naibu spika kizingatie haki ya kusikilizwa wanaokilalamikia kwa sababu yupo spika na hata kamati ya uongozi ambao wanaweza kusikiliza shauri hili ili kuondoa tatizo hili ambalo naamini wananchi wamechoka nalo.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli. 

No comments