Header Ads

Kanga Moja Kiunoni...Mbengembenge -3

 
ILIPOISHIA : “Baba Hawa hiyo mizigo unaipeleka wapi mume wangu? Sikuelewi,” sauti ya mkewe, mama Hawa ilimshtua kwa nyuma akiwa anapanda Bajaj... 
JIACHIE MWENYEWE SASA... “Ohoo! Ni mzigo wa baba Kabweka, kaniambia aliacha hapo sokoni, sasa kwa vile mimi nakwenda kule kwake kaomba nimbebee,” alipiga uongo Jombi... “Sawa mume wangu.” Jombi alipona, alipeleka mizigo hiyo hadi nyumbani kwa mzee Hewa na kukutana na mzee huyo nje. Alishangaa kumwona Jombi anaingia na Bajaj tena na mizogo wakati dakika chache nyuma, alikaa naye hapo... “Imekuaje tena kijana wangu? Mbona natoka na gazeti sikuoni?” Huyo dada mpangaji wako aliniagiza sokoni.” 

Mara, mama Mei mwenyewe alitokea huku akimshukuru sana Jombi... “Jamani anko yaani sijui nikupe zawadi gani? Yaani nashukuru kama nini...yaani eee...na jua hili nilikuwa najifikiria sana yaani...” alisema mama Mei huku akijifunga kanga vizuri kwani alitoka na kanga moja tu... “Si unipe mimi mwenyewe nafasi ya kuchagua zawadi anti,” Jombi alijisemea moyoni...Usijali anti...sisi ni wamoja mbona,” alisema Jombi. Baada ya Bajaj kuondoka na mama Mei kuzama ndani na mizigo yake, mzee Hewa alimtupia jicho Jombi... “Kijana,” aliita... “Naam...” “Kuna kitu...” “Kuhusu nini mzee Hewa..?” “Huyu mama wewe unajuana naye?” “Wala! Ametoka tu hapa akasema anasikia jua kwenda kununua vyakula nikamwambia lete hela nikakununulie.”

 “Basi, umejishindia kijana wangu....maana kama ni mke wa mtu na anajitambua halafu anafikia hatua ya kukuamini wewe kijana mkubwa ukamfanyie manunuzi, mshukuru Mungu maana wenzako wengi wanapitapita hapa kila siku kufukuzia,” alisema mzee Hewa. Moyoni, Jombi aliamini yeye ni mshindi kama kweli kuna wenzake wanapitapita kufukuzia halafu yeye kafikia levo ile, basi yupo juu... “Yes! Mshindi mimi bwana,” alisema moyoni Jombi... “Hapana mzee Hewa mimi binafsi sina lengo baya na mke wa mtu...kwanza mimi ni muoga sana na wake za watu,” alisema Jombi huku akilichukua gazeti kwa mzee Hewa na kusoma habari aliyoambiwa. Mama Mei akatoka tena, safari hii alikata kona kwenda kwenye kiduka cha jirani. Alikuwa ndani ya kanga moja tu, sasa ile tembea yake na mtingishiko wa wowowo, mzee Hewa alijishika kichwa licha ya umri wake mkubwa, Jombi yeye alijiinamia.

 Walinyamza kimya! Kimya kabisa!! Wakati anarudi sasa, macho yake yalikutana na macho ya Jombi yakiwa yameoneka kuumizwa, mama Mei akaachia tabasamu pana kwa maana ya kuweka ukaribu wa kibinadamu kwa vile alimsaidia jukumu la kununua mahitaji. Jombi naye aliachia tabasamu la woga, akamwangalia kwa kumsoma kuanzia juu kwenda chini, mama Mei akazama ndani kwake. Safari hii, mpaka Jombi anaondoka zake, mama Mei hakuwa ametoka tena. Mbaya zaidi, hatua chache mbele, Jombi alipishana na mume wa mama Mei akiwa anarejea nyumbani kwake. Walikutana macho, baba Mei alionekana kummaindi sana Jombi. *** Siku ya tatu, jioni, Jombi alishatoka kazini sasa alikuwa akirandaranda mitaani, akaibukia mtaa wa jirani na kwa mzee Hewa ambapo pana baa.

 Alikaa hapo. Katika kutupia macho, akamwona mama Mei amekaa sambamba na mume wake, alishtuka... “Ohoo! Jamaa si atajua namfukuzia mke wake, maana nabanana naye sana,” aliwaza moyoni. Mama Mei naye, katika kupitishapitisha macho, akamwona Jombi, akafurahia moyoni kwani alikumbuka alivyomtuma sokoni... “Wanaume wengine jamani, wakarimu kweli. Baba Mei umtume vile sokoni, mbona atakung’oa meno,” alisema moyoni mama Mei. Kuna wakati baba Mei alikwenda chooni, mama Mei akatumia nafasi hiyo kulisisitiza jicho lake kwa Jombi ambapo yalikutana, mama Mei akaachia tabasamu na kupunga mkono, Jombi naye akapunga mkono, wakaachiana tabasamu.

Baba Mei alipotoka chooni, hakukaa, aliondoka na mkewe huku baa yote wakimtupia macho, wake kwa waume. Baadhi yao walionesha kutingisha vichwa vyao kutokana na umbo la mama Mei. Jioni hiyo, alivaa suruali ya kubana na t-shirt pia ya kubana, sasa wakati anakanyaga chini ili mguu uende mbele, looo! Wanaume walionekana kuumia ndani kwa ndani, wengine walisemezana kwenye meza. Kwa upande wake, Jombi alionekana kuumia zaidi kwani alimkodolea macho mwanamke huyo mpaka anapotea na mume wake huku moyoni akiumia kama vile mwanamke alikuwa wake sasa ameporwa na mwanaume mwenye fedha zake. 

Saa mbili usiku, Jombi aliondoka kwenye baa hiyo kurudi kwake, lakini akaamua kupitia njia ya kwa mzee Hewa akiamini anaweza hata kusikia sauti ya mama Mei... “Yule saa hizi atakuwa ameshalala,” alisema moyoni Jombi. Alipita nje ya nyumba hiyo huku macho na masikio yakiwa hapo. Ghafla alisikia mlango mkubwa ukifunguliwa kwamba kuna mtu anatoka. Jombi alisimama na kukazia macho mlangoni, moyoni alimwomba shetani wake amsaidie kwamba, anayetoka awe mama Mei... “Yaani akinipa dakika tatu tu ya kunisikiliza atajua mimi ni nani na naamini ataingia laini,” alisema moyoni Jombi huku macho yake yakitamani sana kumwona anayetoka.Je, nini kilitokea hapo? Aliyetoka ndani ni nani? Usikose kusoma SIKU YA JUMATATU

No comments