Header Ads

MALAIKA MWEUSI SEHEMU: 01


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
MALAIKA MWEUSI.
Alikuwa amepiga goti pembeni ya mwili wa mama yake ambaye alikuwa amefariki muda mfupi tu kutokana na kipigo cha mumewe, ambaye ni baba wa kufikia wa msichana Thereza. Huku akiwa analia kwa uchungu alimuahadi mama yake kuwa lazima atalipa kisasi kwa wale waliomtendea unyama. Kwa kusoma kwa bidii ili siku moja awe hakimu au mwanasheria awafunge wote wanaonyanyasa wanawake na kuwabaka. Lakini dhamira yake ilikatishwa kwa kuachishwa shule akiwa darasa la sita na kuuzwa kwa mtu ili awe mtumishi wa ndani! Je, msichana Thereza atatimiza ahadi yake aliyo ihaidi mbele ya mwili wa marehemu mama yake? Ungana na mtunzi mahiri Ally Mbetu katika riwaya hii ya kusisimua.

****
MLIO wa simu ulimshtua mkuu wa upelelezi aliyekuwa katikati ya usingizi. Aliyatupia macho yake kwenye saa ndogo iliyokuwa juu ya droo ya kitanda, ilimuonyesha kuwa ni saa 10:15 za usiku nusu saa tangu amsindikize rafiki yake wa kike aliyembatiza jina la Black Angel, yaani Malaika Mweusi.
Aliinyanyua simu yake iliyokuwepo pembeni ya mto aliokuwa ameulalia, alipoichukua simu ilimuonyesha ni simu maalumu kutoka ofisini. Mara nyingi simu hiyo hutumika kwa ajili ya dharura tu. Hasa pale panapotokea matatizo yasiyokuwa ya kawaida.
Alibofya kifute cha kupokelea simu na kuzungumza kwa sauti ya uchovu, kutokana na shughuli ya usiku haikuwa haba, ilimnyong’onyesha mwili.
Shughuli ya Malaika Mweusi ilimfanya atangaze ndoa na msichana huyo aliyetokea kumuamuni kupita kiasi, hasa kutokana na tabia yake ya upole, ucheshi na roho ya huruma. Vitu ambavyo wanawake wengi hawana zaidi ya kuwa na kimojakimoja, pia Malaika Mweusi alijaliwa sura na umbile la kuvutia.
Mwanaume yeyote asingeweza kujizuia kutangaza ndoa kwa binti huyo aliyeonekana kutoka kwenye familia ya kitajiri. Akizungumza kwa sauti ya kivivu, Mkuu huyo wa upelelezi bwana Anderson:
“Ndiyo nakupata, lete habari.”
“Afande, mambo yameharibika,” sauti ya upande wa pili ilisema.
“Wapi tena?” Aliuliza huku akiiweka sawa akili yake.
“Yule hakimu.”
“Ooh! Mungu wangu, hii sasa inatisha nakuja sasa hivi ofisini.”
Bwana Anderson alikwenda bafuni kuoga haraka haraka na kubadili nguo, wakati alitoka nje aliona mkoba wa Malaika Mweusi ukiwa juu ya kochi. Aliwaza sana kuhusu ule mkoba wa Malaika Mweusi na kusema kwa sauti ya chini:
“ Aah! Kumbe jana aliacha mkoba wake, siyo mbaya ataufuata jioni.”
Alikwenda hadi kwenye banda la gari na kulichukua tayari kwa safari ya ofisini. Saa yake ya mkononi ilimuonyesha kuwa ni saa 11:35. Akiwa njiani akiwaza mambo mengi kuhusu vifo vya kutisha vya mfululizo, vifo ambavyo vimemchanganya yeye na vijana wake. Alipofika ofisini alimkuta maofisa upelelezi na vijana wake wakiwa wameshafika ofisini. Alipoingia ofisini wote walinyanyuka, baada ya kukaa aliwaamuru nao wakae chini.
“Mnaweza kukaa,” baada ya kuketi alisema.
“Ndiyo, leteni habari,” alisema huku akitembeza macho kila kila mmoja aliyekuwemo mule ndani.
“Afande kama ulivyosikia yule hakimu ameuawa, inavyoonekana ameuawa si chini ya saa sita zilizopita.” Alisema afisa upelelezi.
“Saa sita! Ilikuwaje akachelewa kujulikana?”
“Inavyosemekana amekutwa amekufa katika gari lake ambalo lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara.”
“Nani aliyegundua mwili wa marehemu kwenye gari?”
“Askari wa doria ambao walikuwa wanalipita kila mara ile gari, walipoamua kulichunguza ndipo walipogundua mwili wa hakimu.”
“Lazima tukubali tumefanya uzembe wa hali ya juu kutokana na kifo cha hakimu.”
“Bosi sidhani kama tumehusika, pamoja na muuaji kutoa vitisho miezi miwili iliyopita. Nina imani tulimpa Hakimu tahadhari na kumweleza sehemu na muda anaotakiwa kuwa nje ya nyumba yake. Kwa kukiuka masharti yetu kifo chake amekitengeneza yeye mwenyewe.”
“Mmh! Sasa muuaji ni nani, hivi vifo vinafanana? sidhani lakini la muhimu tuwahoji wale ndugu wa yule bwana aliyefungwa na kusababisha vitisho vya muuaji. Maelezo ya awali yalionesha Hakimu alipindisha sheria na mwisho wa siku ilimuhukumu mwenyewe.”
“Lakini si tuliwahoji mapema wao wakasema hawana uhusianao wowote wala taarifa yoyote kutoka kwa muuaji.”
“Unajua hii inatisha, eti muuaji anajiita mtetezi wa haki za binaadamu.”
“Kwani kwa mara ya mwisho hakimu alikuwa wapi?”
“Job Pub.”
“Okay, kuna umuhimu wa kuwahoji watu waliokuwepo pale Job Pub ili kujua kuwa aliondoka saa ngapi na aliongozana na nani.”
“Sawa bosi, tutaifaanya kazi hiyo.”
“Haya majibu niyapate kabla ya saa moja usiku, sawa jamani?”
Mkuu wa upelelezi Anderson aliagana na vijana wake na kuondoka kurudi nyumbani huku akiwa amejawa na mawazo mengi kuhusu mauaji ya kutisha yaliyokuwa yakiendelea huku muuaji akionekana ni mtaalamu wa hali ya juu. Alijiuliza muuaji ni nani? Kama kamuua hakimu kwa ajili ya kupindisha sheria na hao wengine vifo vyao vimetokana na nini? Kikiwepo cha mkewe na mwanaye kipenzi Gift?
Alijiapiza kuwa siku atakayomtia mikononi huyo muuaji ama zake au za muuaji. Alipofika nyumbani alikuwa amechoka akili na mwili, alijitupa kwenye kochi na usingizi mzito ukamchukua.
Anderson alishtuka usingizini majira ya jioni na kujiona amelala kipindi kirefu, muda uliobaki ilikuwa nusu saa akutane na vijana wake kumpa taarifa ya hakimu hiyo. Kama kawaida alikwenda kuoga na kubadili nguo tayari kwenda ofisini.
Wakati anataka kutoka mkoba mweusi wa Malaika Mweusi ulimgusa na kuhisi kuna kitu cha muhimu kukiangalia kwenye mkoba wa binti anayeonekana mtoto wa tajiri. Aliangalia saa yake ilimuonyesha bado dakika ishirini akijua ni muda wa dakika tano hivi kwa mwendo wa gari atawahi ofisini. Hamu ya kujua kuna nini katika mkoba ule ilimfanya kuupekua ili ajue kuna vitu gani. Aliamini huenda angegundua siri yoyote ya msichana huyo kutoka familia ya kitajiri. Kwa dakika kumi alijua zinatosha kufanya upekuzi wa haraka haraka.
Alipofungua pochi, ndani alikutana na cheni isiyopungua thamani ya shilingi milioni moja na nusu na simu ya mkononi aina ya Sum sung yenye thamani ya shilingi milioni moja na laki saba, lakini ilikuwa haina line. Katika mfuko mdogo wa ile pochi alikuta kijitabu kidogo “note book.”
Alikifungua na kuanza kukisoma karatasi moja baada ya nyingine, ilionyesha kuwa ni msichana mwenye miradi mingi ya mamilioni ya shilingi. Aliendelea kusoma karatasi za mbele alikutana na majina yameandikwa majina ya bluu.
Lakini asilimia kubwa ya majina hayo yalikuwa yamezungushiwa wino mwekundu na majina mawili tu ndiyo yalikuwa hayajazungushiwa wino mwekundu.
Majina yale yalimshtua moyo wake na kusababisha mwili kusisimka na jasho jembamba kumvuja juu ya paji la uso. Aliyarudia zaidi ya mara tano na jibu lilikuwa lilelile, alichokisoma machoni mwake kilikuwa sahihi.
Yalikuwa ni majina ya baadhi ya watu waliouawa katika matukio yaliyomchanganya akili na kushindwa kumtambua muuaji. Mbele ya majina yale yalikuwa na tarehe sahihi ya mauaji yaliyofanyika. Ndani ya majina yale lilikuwepo jina la marehemu mama yake mzazi, siku na tarehe aliyouawa, japo mama yake alijua amekufa kwa ajali ya gari.
Jina lingine lilikuwa la mdogo wake aliyeuawa kwenye mazingira ya kutatanisha. Mwili wake ulikutwa kwenye bwawa la mji machafu chuo kikuu. Pia tarehe ya kifo cha mkewe na mwanaye ilionekana siku moja na tarehe ilikuwa ileile. Kifo kilichomuuma sana na kumchanyanya akili.
Mkewe aliuawa kikatili kwa kuchunwa ngozi sehemu za siri na kisha kupigiliwa kipande cha mti. Kilikuwa kifo cha mateso makubwa, maiti yake ilikatwa ikiwa imelaliwa na mwanaye ikiwa inavuja damu mwili mzima.
Vifo vya mkewe na mwanaye vilimuuma sana hasa alipouona mwili wa mkewe livyoharibika vibaya hasa sehemu za siri. Aliapa mbele ya ya mwili wa mkewe na mwanaye siku ya kutoa heshima za mwisho kwamba atamfafuta muuaji na kumtia hatiani kwa mkono wake mwenyewe.
Alijikuta katika mawazo mengi kuhusu kile kitabu cha majina na Malaika Mweusi kina uhusiano gani? Alijiuliza kama atakuwa amehusika na vifo vile au la. Hakukubaliana na akili yake kuwa Malaika Mweusi ndiye muuaji.
Alimuamini na kumwona ndiye atakayeziba pengo la marehemu mkewe hadi akafikia hatua ya kumtambulisha kwa wazazi wake ambao nao wakawapa baraka zote ili wafunge ndoa.
Kile kitabu kilimchanganya sana akili yake, Mama yake kabla kifo chake alionyesha mapenzi mazito kwa Malaika Mweusi na alimsifia mwanaye kwa chaguo lake zuri la msichana mzuri mwenye tabia njema.
Alijikuta akisema kwa sauti:
“Hapana haiwezekani Malaika Mweusi kuwa muuaji, lazima atakuwa anamjua muuaji, lazima nipate ukweli kupitia kwake.”
Jasho lilikuwa linamvuja chapachapa kama aliyefungiwa kwenye chumba cheye joto kali. Aliendelea kusoma kitabu majina ya mwisho mawili yaliyobaki ambayo hayakuwa yamezungushiwa wino mwekundu. Katika majina hayo lilikuwepo jina la baba yake mzazi, yalizidi kumchanganya, alijikuta akibwatuka:
“Ha! Na babaa, nooo..nooo.”
Tarehe iliyokuwa mbele ya jina la baba yake ilikuwa ni siku ileile, alisema tena kwa sauti:
“Hapana haiwezekani na baba tena, hapana.”
Alitoa simu yake ya mkononi na kubofya namba ya baba yake ili kumjulisha awe makini kwani kifo kilikuwa kinamnyemelea. Lakini alipopiga ilikuwa inaita tu bila kupokelewa mpaka ikakatika. Alijikuta akitoka ndani kwa mwendo wa kuruka hadi katika gari lake na kuliondoa katika mwendo wa kasi mithili ya ndege za kivita kuwahi kwa baba yake.
Ndani ya dakika tano alikuwa anaelekea kwa baba yake, aliiacha barabara kuu na kuingia ndogo inayoelekea kwa baba yake, mbele yake kulikuwa na gari limeharibika.
Kwa haraka aliteremka kwenye gari bila ya kuchomoa funguo wala kufunga mlango na kuanza kukimbia kuelekea kwa baba yake.
Njiani alikutana na mwanamke kama Malaika Mweusi, lakini hakumjali zaidi ya kuwahi kuokoa maisha ya baba yake. Nyumba ya baba yake ilikuwa giza, aliingia ndani ya geti na kwenda moja kwa moja hadi ndani. Alimwita baba yake kwa sauti ya juu, lakini hakukukuwa na majibu lolote. Sebule ilikuwa kimya pia giza.
Alipowasha taa alishangaa kukuta ukumbi mtupu hakukuwa na mtu yeyote, alielekea chumbani kwa baba yake. Mlangoni alikutana na michirizi ya damu lakini chumbani kwa baba yake kulikuwa na giza. Ile damu ilimfanya aione hali ya hatari mbele yake
Alitoa bastola na kuingia kwa tahadhari kubwa alipapasa ukutani na kufanikiwa kuwasha taa.
Hakuamini macho yake, alishuhudia mwili wa baba yake ulikuwa umelazwa kitandani ukiwa mtupu kama alivyozaliwa. Sehemu zake za siri zilikuwa zimetenganishwa na kisu kilikuwa kimemchoma katikati ya moyo wake, macho yalikuwa yamemtoka akionyesha amekufa kwa mateso makali.
Damu ilikuwa mbichi na mwili wake ulikuwa bado una joto. Chumba chote kilikuwa kinanuka damu mbichi. Anderson aliuvamia mwili wa baba yake na kuukumbatia huku akiendelea kuapa atamshikisha adabu aliyetenda kosa lile.
Alitoka harakahara ili aanze msako wa Malaika Mweusi ili apate ukweli a vifo vyote. Lakini alikataa katakata muuaji anaweza kuwa Malaika Mweusi. Kwa vile nguo zake zilikuwa zimetapakaa damu ya baba yake alipapigia simu vijana wake waje kuchukua mwili wa marehemu baba yake kuupeleka hospitali.
Akiwa njiani aliwaza sana uhusu vifo vyote hasa vinavyoihusu familia yake kama wameuawa wote aliyebaki ni yeye na kama asipomuwahi muuaji basi atamuua yeye.
“Hivi Malaika Mweusi anaweza kuwa muuaji?.....inawezekana maana nimemuona eneo la tukio sasa hivi, kwani ana siri gani inayomfanya afanye hivyo?” Mr. Anderson alijikuta akizungumza peke yake. Hakuamini mtu aliyemuamini na kumbatiza jina la Malaika Mweusi awe muuaji, kama ni kweli alihusika hakuwa Malaika Mweusi bali Shetani Mweusi.

ITAENDELEA KESHO

No comments